Mwandishi Wetu
DAIMA tuendelee kukumbushana kuhusu umuhimu wa uaminifu.
Tuzingatie na kukiri kuwa usaliti siyo kosa la bahati mbaya ni uamuzi wa
makusudi. Hajapata kutokea msaliti akatenda dhambi hiyo pasipo kujua, eti baada
ya tendo ndiyo akagundua, hiyo haipo!
Ongeza kitu kichwani kwa stori ya Sarah Johnson. Baada ya
kutenda dhambi ya usaliti na mumewe kujua, alianza kuteseka ndani kwa ndani,
akijilaumu na kujilaumu.
Pokea ukweli huu; Mtu anapotenda usaliti hujidanganya kuwa
itabaki kuwa siri. Mbaya zaidi hujiaminisha kuwa ‘usaliti’ wake hautajulikana.
Hakuna maandalizi ya kisaikolojia ambayo unaweza kuyafanya
na yakakusaidia pindi tendo lako la usaliti litakapogundulika. Kila
aliyegundulika, aibu ilimshika na akaishia kujuta.
Sarah, mwanamke msomi mtaalam wa sheria, yeye baada ya tendo
lake la usaliti kugundulika, aliona mambo ni mazito, akaishi kwa mateso kwa
takriban miezi minne, mwisho akaona afadhali kukatisha maisha yake.
Hakuna anayeweza kufurahia kifo cha mwingine, ila haipingiki
kuwa Sarah alijipeleka mwenyewe kwa Mungu baada ya kuona dunia imegeuka mzigo
mzito kichwani kwake, kisha Mfalme wa Mbingu na Ardhi naye akampokea.
Sarah, wakili tajiri, aliyekuwa akiishi kwenye nyumba yenye
thamani ya shilingi bilioni 30 (pauni milioni 12), unaweza kuwaza alikuwa
kwenye wakati mzuri kiasi gani wa kufurahia maisha. Halafu katika tafakuri yako
ongezea kuwa amejiua mwenyewe.
Alikuwa mwanamke tajiri, aliyepata kila alichotaka. Jumba
lake lililopo Chester Square, ndani ya Wilaya ya Belgravia, Jiji la London,
Uingereza, lilikuwa na kila aina ya burudani. Aliendesha magari ya kifahari
jinsi alivyotaka.
Mume wa Sarah, David Johnson, ni mtu mwenye uwezo pia. Na
David hakuwa akimbughudhi wakili huyo ila tu mwenyewe alishindwa kupata utulivu
tangu kitendo chake cha usaliti kilipogundulika.
Baba yake Sarah, Graham Parr, ni mfanyabiashara mkubwa.
Alikuwa karibu na binti yake kumpa chochote kile ambacho angekihitaji yeye
binafsi na familia yake lakini Sarah hakuona kama kuna kingine kinachoweza
kubeba thamani ya heshima yake baada ya mumewe kuubaini usaliti wake.
Sarah, alimweleza mara kwa mara daktari wake wa saikolojia,
aliyejitahidi kumtibu kwa miezi minne: “Mimi siyo mama bora, siyo mke bora.”
Dk Shirley Radcliffe, mtaalamu wa saikolojia aliyekuwa
akimtibu Sarah, alisema: “Ugonjwa wa Sarah ulitokana na kujiona mwenye hatia
ndani yake. Baada ya yote kutokea, alikuwa akisema kwa msisitizo kuwa yeye siyo
mama bora. Aliona heshima yake yote imetoweka. Na ukiniuliza maoni yangu,
nitakujibu kuwa hiyo inaweza kuwa sababu ya yeye kujiua.”
Sarah ambaye mpaka anajiua alikuwa na umri wa miaka 36,
inaelezwa kuwa tangu mumewe alipojua kuhusu usaliti wake, alijiingiza kwenye
vitendo vya ulevi na zipo nyakati alilewa mpaka kuzimika. Rekodi zinaonesha
kuwa alianza ulevi Januari mwaka huu.
Daktari wake alimtibu mpaka akaonekana kama anaelekea kupata
nafuu, lakini Aprili 27, mwaka huu, alijirusha mbele ya treni , ilipokuwa
kwenye mwendo, Stesheni ya Victoria, London.
Zaidi, Sarah aliwahi kulazwa kwenye hospitali ya matatizo ya
akili, The Priory, ambayo huhudumia watu mashuhuri na matajiri kutokana na
gharama zake kuwa kubwa. Pamoja na hivyo, hakuweza kupona.
Mataabikiko ya usaliti ni mbaya mno; Madaktari bingwa
Uingereza hawakumsaidia, pombe zikazidi kumvuruga akili. Kila alipokumbuka
dhambi aliyotenda ya kusaliti ndoa alijiona mwenye hatia, mwisho akaona bora
kuutanguliza mwili wake kaburini.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya familia, Sarah alianza
kunywa pombe saa 5 asubuhi, alitumia vodka na kila jioni aligeukia bia.
Sarah, aliamini pombe ndizo zinaweza kumsaidia kwa maelezo
kuwa kugundulika kwake kwa mambo aliyokuwa anayafanya kwa siri, kulisababisha
furaha yake yote ya maisha kutoweka.
Ukiachana na Dk Radcliffe, ndani ya Hospitali ya The Priory
alilazwa mara mbili, Februari na Aprili 2015. Na alijiua akiwa hajamaliza siku
nyingi tangu alipotibiwa.
Daktari wa saikolojia ya akili katika Hospitali ya The
Priory, Dk Neil Brener ambaye ndiye alikuwa anamhudumia Sarah, alisema: “Tatizo
lake kubwa lilihusu masuala binafsi ndani ya familia, na alikuwa akitumia pombe
kwa wingi ili kutuliza mawazo.
“Hakuwahi kuwa na matatizo ya kisaikolojia huko nyuma.
Mawazo pekee yaliyomsumbua ni kwamba alimwangusha kila mmoja ndani ya familia
yake, mume wake na watoto wake. Kwa maana hiyo sababu ya kujiua itakuwa hiyo.”
Dk Brener alisema kuwa siku ambayo Sarah aliruhusiwa kutoka
Hospitali ya The Priory, alifurahi kwa sababu alimuona mgonjwa wake akiwa
kwenye maendeleo mazuri ya kiafya.
Daktari huyo aliongeza: “Siku tunamruhusu hakuwa na mawazo
ya kujiua, alikuwa na maendeleo mazuri kabisa kiakili, na alikuwa mzungumzaji
sana.”
Inaelezwa kuwa Aprili 26, 2015, Sarah alikuwa na ahadi ya
kumuona Dk Brener lakini hakwenda, wala hakutoa sababu yoyote.
Asabuhu ya siku iliyofuata (Aprili 27), mume wa Sarah,
David, aliamka na kukuta mkewe hayupo na aliona karatasi aliyoacha ujumbe
kwamba anakwenda kujiua kwa sababu ya kuzidiwa na mzigo mzito wa mawazo ya
kujiona mwenye hatia.
Kwa karatasi hiyo, David, 37, aliwahi polisi kutoa taarifa
ya kutoweka kwa mkewe na kuhusu uwezekano wa kufanya jambo baya, lakini hakuna
kilichosaidia kuokoa maisha ya Sarah, kwani muda huo tayari roho ilikuwa
imeshatengana na mwili.
Ilibainika kuwa Sarah aliwasili Stesheni ya Victoria saa
11:30 asubuhi, na alishangaashangaa kwa takriban dakika 50 kabla ya kujirusha
saa 12:20 asubuhi mbele ya treni ya ardhini inayotumia umeme, iliyokuwa
inatembea.
Mpelelezi Steve Tucker alisema, kabla Sarah hajafariki
dunia, alionekana akijiandaa kujirusha, kwa hiyo hivyo ni wazi dhamira yake
alitembea nayo kwa muda mrefu.
Tucker alisema: “Picha ya kwanza inayomuonesha Sarah kupitia
kamera za usalama (CCTV), ilikuwa saa 11:37 asubuhi. Alikuwa akizunguka zunguka
kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
“Saa 12:00 asubuhi alionekana kwenye kamera katika sehemu ya
kupandia abiria ya kaskazini. Kwa kufuatilia hatua zake, niliingiwa na wasiwasi
kuwa kuna kitu anataka kufanya. Nilipata hisia hizo kwa sababu alikuwa
anakwenda mbele kisha kurudi nyuma kwa mtindo wa kushangaza.
“Saa 12:20 asubuhi, kamera zinamuonesha anatazama upande
ambao treni inapita.”
Taarifa za Kitengo cha Ambulance zinasema kuwa Sarah
alichukuliwa stesheni akiwa na majeraha makali na ilionekana wazi kuwa
asingeweza kupona.
Kwa upande mwingine, taarifa za simu yake aina ya iPhone,
ilikutwa na historia ya intaneti, zilizoonesha kuwa Sarah kupitia mtandao wa
Google, kwa mara ya mwisho alitafuta ‘idadi ya vidonge vya paracetamol ambayo
mtu mzima akimeza anaweza kufariki dunia.’
Uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionesha kuwa Sarah hakuwa
na kiwango chochote cha pombe, kuonesha kuwa kujiua kwake hakukutokana na aina
yoyote ya kilevi.
UNACHOPASWA KUCHUKUA
Kifo cha Sarah kiwe na mambo mawili yenye kufundisha. Kwanza
ni usaliti, athari yake ni kubwa mno baada ya kugundulika.
Usiseme itakuwa siri, amini usiamini kuwa ipo siku
itajulikana na wewe utakosa mahali pa kuiweka sura yako kwa aibu.
Usisubiri majuto ya baadaye na hata kufikia uamuzi mgumu na
uliojaa maumivu makali kama wa Sarah, jenga utaratibu wa kujikosoa kila Shetani
anapokuvuta kwenye njia yake.
Mfumo wa kuukataa usaliti ni kuzishtukia dalili zote
zinazoletwa na Shetani. Usingoje kusema “Shetani alinipitia.” Fanya kumzuia
asiingie kabisa kwenye anga zako.
SAMEHE ANAYEJUTA
Kama mwenzio amekusaliti na unajiridhisha kuwa anajuta kwa
alichokifanya, jaribu kuyatibu maumivu uliyonayo kisha umsamehe.
Usisamehe kama hujapona. Matokeo yake leo utamwambia
umemsamehe kesho unalianzisha tena. Pona majeraha kwanza na baada ya hapo toa
msamaha wa kweli.
Kikubwa ni kwamba ni heri kumsamehe anayejuta kwa kosa
alilofanya, maana atakuwa mwangalifu siku zijazo, kuliko kwenda kumvamia
mwingine ambaye anaweza kukuibulia maumivu mapya.
MASKINI SARAH KAACHA MTOTO MDOGO KABISA
Sarah amekwenda, amemwacha mumewe na watoto wake wakiwa
kwenye ukiwa mkubwa. Maumivu makubwa ni kwamba mwanaye wa mwisho ndiyo kwanza
alimwacha akiwa ametimiza umri wa miaka mitatu.
David (mume wa Sarah), hajatoa tamko lolote au kuelezea kile
hasa ambacho marehemu mke wake alikosea, yupo kimya, anasitiri aibu ya mwandani
wake lakini ndani yake kuna donda kubwa, kusalitiwa na kumpoteza mke. Labda
alimsamehe lakini Sarah hakujisaheme kabisa. Tuwe waaminifu siku zote!
0 comments :
Post a Comment