Luqman Maloto
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni shamba la bibi,
fedha za mafao ya Watanzania zimekuwa zikifyonzwa kienyeji bila woga wa sheria
za nchi, huruma kwa wanachama wachangiaji walalahoi na pasipo uzalendo hata
chembe.
Ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na taasisi ya kimataifa ya ukaguzi ya
Ernst and Young, umebainisha ufisadi mkubwa kutendeka katika mwaka wa fedha
2014-2015.
www.luqmanmaloto.com inayo ripoti hiyo na kilichobainishwa
ndani yake ni ufisadi mkubwa wa ama kwa uzembe au makusudi kwa kila mradi ambao
NSSF ilifanya katika mwaka husika, hivyo kuusababishia mfuko hasara ya trilioni
za fedha.
Uchambuzi wa taarifa hiyo ya ukaguzi umebaini kasoro za
jumla kama ifuatavyo;
MOSI: NSSF iliridhia manunuzi ya kiwanja ekari moja kwa
zaidi ya shilingi milioni 800 Kigamboni, Dar es Salaam, na zaidi ya shilingi
bilioni 1.8 Arumeru Arusha.
PILI: Kampuni yenye mtaji mdogo pamoja na kiwango kidogo cha
uwekezaji, kupewa zabuni ya mradi wenye thamani ya kuzidi uwezo wa kampuni
husika.
TATU: Kampuni yenye kupewa tenda ya mradi, kulipwa asilimia
20 ya gharama kamili ya mradi kabla ya mkataba rasmi kusainiwa.
NNE: Menejimenti ya NSSF kufanya malipo ya miradi nje ya sheria
za manunuzi pamoja na mpango wa mwaka wa manunuzi.
TANO: Menejimenti ya NSSF kuizunguka Bodi ya NSSF pamoja
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya malipo ya miradi mikubwa, kinyume na
sheria ya manunuzi pamoja na utaratibu wa kawaida wa kiutendaji.
SITA: Uzembe wa menejimenti ya NSSF kufanya uchunguzi wa
kujiridhisha (due diligence) kabla ya kusaini mkataba na mwekezaji binafsi katika
miradi yake.
SABA: Kinyume na sheria ya manunuzi inavyotaka, menejimenti
ya NSSF ilitoa upendeleo kwa kuipa kampuni zabuni wakati ilikuwa ikidaiwa mradi
mwingine na mfuko.
UFISADI NAMBA MOJA
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukakasi mkubwa upo kwenye miradi
ya ujenzi wa miji ya kisasa (satellite towns), Kigamboni, Dar es Salaam na
Arumeru, Arusha uliosainiwa Novemba 15, 2013 kati ya Bodi ya NSSF na kampuni ya
Azimio Housing Estates Limited (AHEL).
Katika mkataba huo, udanganyifu mkubwa umebainika kuhusu
gharama ya ardhi katika maeneo ya mradi, bei ikiwa kubwa mno kinyume na
uhalisia lakini NSSF ikaridhia hivyohivyo na kudhihirisha makusudi ya ufisadi
kutendeka.
Wakati wa makubaliano hayo, AHEL ilijieleza kuwa ardhi ekari
20,000 Kigamboni, ekari 655.3 Arumeru, Arusha, ekari 7,832.7 Pwani, ekari 200
Mwanza, ekari 5,723.6 Mtwara, kwamba maeneo yote yanakidhi mipango ya kuwa satellite
towns.
Katika makubaliano ya pamoja, NSSF ilikubaliana na AHEL
kushirikiana katika ujenzi wa miji hiyo ya kisasa, Kigamboni ekari 300 na thamani
yake ni dola 653,436,675 na Arumeru dola 3,340,589,543 mpaka kukamilika kwake.
Makubaliano hayo, yaliitaka AHEL kuwekeza ardhi ekari 300
Kigamboni ambayo ni sawa na asilimia 20 ya mradi, ambayo ni dola 108,906,113 na
ekari 655.3 Arumeru dola 556,764,924, hivyo kufanya jumla ya ardhi kutoka AHEL
kuwa na thamani ya dola 665,671,037.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NSSF iliingiza fedha kwenye
mradi, pasipo kujiridhisha uhalali wa ardhi kutoka serikalini kama kweli
viwanja vilivyotajwa vinamilikiwa na AHEL au la!
Ukaguzi ulibaini pia kuwa AHEL hawakuonesha nakala zozote za
umiliki wa ardhi tajwa, hivyo kuonesha kuwepo kwa uzembe ambao umesababisha
hasara kubwa kwa mfuko.
“Inashangaza kwa
NSSF kuingia makubaliano ya aina hii, mfuko una viwanja vingi ni kwa nini
haukutumia viwanja vyake mpaka kwenda kuwekeza fedha kwenye viwanja vya mbia
ambaye umiliki wake unatia shaka?” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti inasema
kuwa NSSF imepata hasara kubwa kwa uwekezaji huo, kwamba imepoteza kiasi cha
shilingi bilioni 179 Kigamboni na shilingi trilioni 1.165, hivyo hasara
ya jumla kuwa shilingi trilioni 1.344.
Katika ukokotoaji wa mahesabu, ukaguzi umebainisha kuwa
ardhi kubeba thamani ya asilimia 20 ya mradi wote, maana yake ekari 300 za
Kigamboni ni shilingi trilioni 1.254, hivyo thamani ya ekari moja ni shilingi
milioni 835.96.
Thamani hiyo ni kubwa mno kutokana na bei halisi ya Manispaa
ya Temeke, ambayo Juni 29, 2012, ilitangaza kuuza viwanja kwa bei ya shilingi 8,000
kwa mita za mraba, kwa hiyo ekari moja ni shilingi milioni 39.
Ripoti hiyo pia inashangazwa na uamuzi wa NSSF kuwekeza
kwenye ekari 300 za AHEL, wakati mfuko ulikuwa na ekari 267 kutoka Kampuni ya
Georgia Homes (T) Ltd, ambazo kila ekari moja thamani yake ilikuwa shilingi
milioni 4.5.
Wakati hali ikiwa hivyo, katika mradi huo wa Kigamboni,
tayari NSSF ilishaingiza zaidi ya shilingi bilioni 205, wakati AHEL haijawekeza
chochote zaidi ya ardhi ambayo thamani yake ni ya kuhoji na wakati huohuo, hata
uhalali wa kampuni hiyo ni wenye kutia shaka, kwani hakuna nyaraka za karibuni
zilizosainiwa kwa msajili wa makampuni (Brela) kuonesha inaendelea na kazi.
Mapendekezo ya ripoti hiyo ni kuwa wahusika waliouingiza
mfuko kwenye matatizo hayo, wanapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
“Watu ambao kwa uzembe, waliushauri mfuko kuingia kwenye
matatizo haya na kuhatarisha fedha za wanachama lazima wawajibishwe ili
kuepusha matatizo mengine yajayo kwa fedha za wanachama wa mfuko,” ilisema
ripoti hiyo.
Kwa mujibu ripoti, uchunguzi uliofanywa Brela umeonesha kuwa
AHEL ni kampuni ambayo mtaji wake ni shilingi milioni 10 tu.
Ilieleza kuwa kampuni hiyo ilisajiliwa Mei 25, 2006, kwa
nambari 56321, ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni moja.
Wanahisa waliotajwa ni Mohamed Ikbal Haji Mohamed hisa 70,
Zarina Mohamed Ikbal hisa 15 na Hassanat Mohamed Ikbal hisa 15, ofisi yao ikiwa
kiwanja nambari 2080, kitalu 148, Mtaa wa Jamhuri, Dar es Salaam.
Hata hivyo, ripoti ya
mwaka ya Brela, Mei 21, 2013, inaonesha kuwa idadi ya hisa za AHEL zilikuwa
zilezile 100 lakini thamani yake ilikuwa shilingi milioni 10, huku wanahisa
wakiwa walewale, Mohamed Ikbal Haji Mohamed, Zarina Mohamed Ikbal na Hassana
Mohamed Ikbal.
Kuhusu mradi wa Arumeru, thamani ya ardhi kuwa asilimia 20
ya mradi wote, maana yake ni kuwa ekari moja ni dola 849,633,639.8 sawa na shilingi bilioni 1.8 (kwa kutumia
mabadilishano ya sarafu dola moja kwa shilingi 2,150).
Thamani hiyo ya ekari moja kuwa shilingi bilioni 1.8
(bilioni 2 kasoro milioni 200), ni kinyume na thamani halisi ya viwanja kwenye
eneo la mradi ambalo lipo kilometa 30 kutoka Jiji la Arusha.
Ukaguzi umeonesha kuwa eneo husika limezungukwa na wakulima
wa mahindi na maharagwe na wenyeji walipoulizwa walisema kwa kawaida ekari moja
huuzwa kwa bei ya kati ya shilingi 500,000 mpaka milioni moja.
Kasoro nyingine ni kwamba NSSF ilisaini mkataba na AHEL
kabla hata upembuzi yakinifu haujafanyika, kwamba nyaraka za kiofisi zinaonesha
kuwa baada ya mkataba kusainiwa ndipo upembuzi yakinifu ulifanyika.
Kasoro nyingine ni kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
hakushirikishwa na NSSF ili afanye uchunguzi wa kitaalamu (vetting) kuhusu
kampuni ya AHEL, uhalali wa mradi na uwezo wa pande zote mbili kutekeleza mradi
husika kama Sheria ya Ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2010
inavyosema.
UFISADI WA PILI
Ripoti imeonesha kuwa NSSF ilitangaza zabuni ya ujenzi wa
jengo la biashara la Mzizima Tower, Dar es Salaam, na kampuni za Atlas kupewa zabuni
yenye thamani ya shilingi bilioni 6.5, Ginde shilingi bilioni 8.7 na Jandu
shilingi bilioni 8.3.
Hata hivyo, ukaguzi ulionesha kuwa zabuni ya Jandu
ilirekebishwa na kamati ya tathmini, kutoka kiasi cha shilingi 8,346,155,654
mpaka shilingi 8,340,700,710.94 ikiwa pamoja na VAT, kisha kampuni hiyo
ilikubali masahihisho hayo.
Pamoja na masahihisho hayo kufanyika, bado mkataba ulisainiwa
kwa kiwango kilekile cha shilingi 8,346,155,654, hivyo kuungizia mfuko hasara
ya shilingi 5,454,943.
“Tunapendekeza kuwa kiasi kilichosainiwa kirejewe upya kwa
kiwango kilekile kilichokubalika baada ya tathmini ambacho ni shilingi 8,340,700,710.94,”
ilisema ripoti hiyo.
UFISADI WA TATU
Ripoti hiyo imeonesha pia ufisadi wa shilingi bilioni 16.98,
katika ujenzi wa hoteli ya kitalii, Mwanza, mwaka 2013.
Imeelezwa ndani ya ripoti hiyo kuwa Februari 4, 2013,
kampuni tatu ziliomba zabuni lakini mwisho, Kampuni ya China Railway Jianchang
Engineering Co.(T) ilishinda na mkataba ulisainiwa Septemba 9, 2013 kwa thamani
ya shilingi bilioni 72.85.
Katika mkataba huo, ilijumuishwa pia uwekaji wa umeme,
viyoyozi, vifaa vya usalama na mawasiliano ya simu.
“Hata hivyo, tumegundua kuwa NSSF iliingia mkataba mwingine
kwa ajili ya kufanya kazi hizohizo zilizopo kwenye mkataba wa China Railway
Jianchang Engineering Co.(T) kwa thamani ya shilingi 16, 980,840,809 ambazo ni
sawa na asilimia 23 ya mradi wote,” ilisema ripoti hiyo.
Mapendekezo yametolewa ndani ya ripoti hiyo kuwa uongozi wa
NSSF lazima ufanye uchunguzi ni kwa nini fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni
16.98 zililipwa, wakati mkataba wa awali, uliitaka kampuni ya Kichina ya China
Railway Jianchang Engineering Co.(T), ifanye majukumu yote hayo kwa fedha
zilezile za makubaliano ya msingi.
UFISADI WA NNE
Ripoti imeonesha pia kuwepo kwa ufisadi mkubwa kwenye zabuni
ya manunuzi ya sare za wafanyakazi ambayo NSSF iliipa Kampuni ya Pink Diamond.
Imeelezwa ndani ya ripoti kuwa NSSF ilisaini na Pink Diamond
mkataba wenye nambari PA/004/2014-2015/HQ/G/04 na bei ya manunuzi ya sare za
wafanyakazi katika mkataba huo ni shilingi bilioni 1.078.
Hata hivyo, katika kuichambua zabuni na mkataba husika,
wakaguzi walibaini kuwa kabla ya mkataba kusainiwa, NSSF iliilipa Pink Diamond
shilingi milioni 215.4, sawa na asilimia 20 ya thamani ya mkataba.
Ripoti imeeleza kuwa malipo hayo kufanyika kabla ya mkataba ni
uvunjaji wa sheria ya manunuzi, kwani malipo ya awali kwa ajili ya kazi
serikalini, yanapaswa kufanywa baada ya mkataba kusainiwa.
Wakaguzi walibaini pia kuwa hata mkataba wenyewe ulisema
baada ya kusaini ndipo Pink Diamond wangestahili kulipwa asilimia 20 ya zabuni
lakini walilipwa kabla ya kusainiwa kwa mkataba.
Kingine ambacho wakaguzi walikibaini ni kuwa baada ya
mkataba kusainiwa Machi 4, 2015, Pink Diamond waliandika barua yenye kumbukumbu
nambari PD/NSSF/UNI/095/14/15, kwenda NSSF wakiomba nyongeza ya asilimia 20 ya
zabuni ili waweze kufanya kazi.
Imebainishwa ndani ya ripoti hiyo kuwa Machi 13, 2015 mfuko
ulithibitisha malipo mengine ya shilingi milioni 215.4 kwenda Pink Diamond,
kama asilimia 20 ya zabuni, hivyo kufanya jumla ya shilingi milioni 431
kulipwa, sawa na asilimia 40 kabla ya kazi kufanyika.
Wakaguzi wameonesha kwenye ripoti yao kwamba Machi 31, 2015,
ndiyo nyongeza hiyo ya asilimia 20 ilifanywa, hivyo kutengeneza malipo ya jumla
asilimia 40 kama malipo tangulizi na kabla kazi haijafanyika.
Ripoti imeeleza kuwa Pink Diamond ilipaswa kuipa NSSF dhamana
ya usalama wa kazi ili kuthibitisha uaminifu katika kazi na kwa mahesabu,
dhamana hiyo ilipaswa kuwa na thamani ya shilingi milioni 215.52.
Hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya 29 ya Manunuzi ya mwaka
2013, lakini kilichotokea ni kuwa NSSF ilipokea dhamana yenye thamani ya
shilingi milioni 107.8, sawa na asilimia 10.
Kitendo cha kupokea kiwango kidogo cha dhamana ya usalama wa
kazi, kimeelezwa kwenye ripoti ya ukaguzi kama hali yenye kutia shaka kubwa na
inahatarisha fedha za wanachama wa mfuko.
Wakaguzi walibaini pia kuwa hata muda wa dhamana ya usalama
wa kazi kama ulivyodhaminiwa na Benki ya Equity Tanzania Limited, ulikwisha
kabla ya Pink Diamond kukabidhi mzigo wowote.
Mapitio ya dhamana ya Benki ya Equity katika mkataba
uliosainiwa Januari 20, 2015, yanaonesha kuwa dhamana ya benki hiyo kwa Pink
Diamond, iliisha muda wake kuanzia Mei 28, 2015.
Ukaguzi umegundua pia kuwa NSSF ilishindwa kuikata Pink
Diamond kiasi cha shilingi milioni 137.4 baada ya kushindwa kukabidhi sare za
wafanyakazi ndani ya siku 90, kama mkataba ulivyotaka, kipengele cha 25, Hali
ya Mkataba.
Mkataba ulitaka Pink Diamond kukabidhi sare za wafanyakazi
kabla ya Aprili 23, 2015 lakini NSSF ilipokea sare hizo Julai 21, 2015 nje
kabisa ya muda wa mkataba.
Kipengele cha 21 katika mkataba huo, kilitaka malipo ya
fidia kwa NSSF kwa kwenda kinyume na mkataba na kwa ucheleweshaji, kila siku
moja iliyochelewa thamani yake ilipaswa kuwa asilimia 0.15 ya mkataba.
Wakaguzi walibaini kuwa Pink Diamond walichelewa kwa siku
85, hivyo asilimia 0.15 ya shilingi bilioni 1.078 kwa siku 85 ni shilingi milioni 137.4 ambazo
NSSF ilipaswa kuzikata kwenye malipo.
Wakaguzi wanahoji ni kwa nini NSSF haikukata kiasi hicho cha
fedha kama mkataba ulivyotaka? Na kwa nini mfuko ulilipa fedha kabla mkataba
haujasainiwa? Na ni kwa nini ililipa asilimia 40 katika malipo ya awali pasipo Bodi ya NSSF kuwa na
taarifa?
UFISADI WA TANO
Wakaguzi walibaini kuwa NSSF ilikwenda kinyume na utaratibu
wa manunuzi katika kumiliki ardhi yenye thamani ya shilingi bilioni 15.159
katika maeneo ya Madale, Kinondoni, Dar es Salaam, Mataya, Bagamoyo, Misugusugu, Kibaha na Ngarambe, Mkuranga,
Pwani.
Shaka ambayo imeelezwa na wakaguzi ni kuwa NSSF iliegemea
kwenye chanzo kimoja kinyume na utaratibu wa manunuzi unavyotaka.
Imeelezwa kuwa umiliki wa kiwanja chenye thamani ya shilingi
bilioni 13.559 ulifanyika nje ya utaratibu wa manunuzi ya mwaka, na
haukuthibitishwa katika mpango wa manunuzi ya mwaka fedha wa fedha 2014/2015.
Wakaguzi wamebaini kuwa shilingi bilioni 1.6 ziliwekwa
pembeni katika mpango huo wa umiliki wa kiwanja lakini hesabu za jumla
zilionesha kuwa mfuko ulitumia shilingi bilioni 15.159.
Ripoti ilimtilia shaka mshauri wa NSSF, Suphian Rashid
Lugendo ambaye ushauri wake kwa mfuko kumiliki ardhi ulikwenda kinyume na
Sheria nambari 312 ya Manunuzi.
Aidha umiliki huo wa ardhi, ulifanyika bila kufuatilia
Wizara ya Ardhi kuhusu uhalali wa umiliki huo, hivyo kuziweka fedha za
wanachama katika hatari.
UFISADI WA SITA
Wakaguzi pia walibaini kuwa mshauri wa mradi wa mji wa
kisasa wa Arumeru, alilipwa zaidi ya shilingi bilioni 400.
Nyongeza kuhusu utata wa mradi wa mji wa Arumeru ipo kwenye
thamani, kwamba ni mradi ambao ukamilikaji wake utaigharimu shilingi trilioni
7.18.
Wakati huohuo, NSSF ipo kwenye ubia na kampuni (AHEL) ambayo
mtaji wake ni shilingi milioni 10, kama taarifa za Brela zilivyoonesha.
Ripoti inaweka shaka kuhusu ukweli wa rasilimali za NSSF kwa
sababu ripoti ya mali zake kwa mwaka ulioisha Juni 30, 2015 ni shilingi
trilioni 2.98, wakati kwa mwaka wa fedha 2014 ilikuwa shilingi trilioni 2.58.
Swali katika ripoti hiyo ni vipi NSSF yenye rasilimali za
shilingi trilioni 2.98 na AHEL yenye shilingi milioni 10, inaweza kumudu mradi
wa shilingi trilioni 7.18?
Ripoti itaendelea
0 comments :
Post a Comment