Na Luqman
Maloto
Mpokee na
umkarimu aliyetoka kutendwa na mwenzi wake aliyempenda sana, kisha umsaidie
kuhamisha maumivu aliyokuwa nayo yatoke kwake yaje kwako.
Mapenzi yana
tabia mbaya sana! Kipimo chake kimapenzi siyo upendo wako kwake wala jinsi
unavyomuonesha uhusika bora wa kimapenzi. Kipimo ni utashi wa moyo wake.
Je,
amekupenda na kuridhia kuwa na wewe? Au ulimpata katika kipindi ambacho alikuwa
na masumbuko ya moyo baada ya kutendwa?
Alikupenda
au alitua kwako baada ya kuponyokwa na hifadhi aliyoitarajia? Je,
alikukaribisha na kukuingiza moyoni au alikwambia “sawa” baada ya aliyemwamini
kumtenda ndivyo sivyo?
Chukua hii;
Mapenzi huongozwa na moyo. Na kwa kawaida moyo hujielekeza kwa mtu na
kujifikisha ‘mazima’. Wakati mwingine hujielekeza na kujifikisha bila
kupokelewa. Matokeo yake unakuwa unaonekana unalazimisha mapenzi. Mwenye
kupendwa hataki!
Moyo wa
binadamu una king’ang’anizi cha ajabu. Jinsi mtu anavyotendwa, ndivyo
anavyozidi kuumia na kulihitaji zaidi penzi la anayemtenda.
Ona moyo wa
binadamu usivyo na shukurani; Wakati akilalamika kutendwa, pale alipo kuna mtu
anayemwonesha mapenzi yote ya ndani ya moyo. Anapewa zawadi na kupelekwa maeneo
mazuri yenye mandhari ya kimapenzi lakini haiwi liwazo.
Pokea hii;
Usimlaumu mtu asiyekupenda pamoja na upendo wote unaomuonesha. Huwezi kujua
ndani yake kuna maumivu kiasi gani juu ya yule anayempenda lakini hapati
anachokitaka. Siyo yeye, ndivyo moyo wa binadamu ulivyo.
Tatizo ni
moja, moyo wa binadamu haukuumbwa na macho. Haumuoni anayestahili kupendwa na
ambaye hastahili. Moyo ukishampokea mtu na kumkubali, yanakuwa mateso makubwa
kwa mwenye moyo. Moyo una tabia ya kulazimisha matakwa yake hata kama
hayawezekani.
Mtu anaweza
kukuonesha dalili zote za kukukataa. Akakufanyia vitimbi vya kila aina. Akakusimanga
na kukupeleka kwenye jumba la maonesho ya mabwege kama siyo mazuzu wa mapenzi.
Pamoja na yote hayo, moyo unakushinikiza kuwa na huyohuyo anayekutesa.
Binadamu
ameumbwa na macho, kwa hiyo anamuona anayefaa na asiyefaa lakini moyo hauna
macho ndiyo maana hung’ang’aniza. Binadamu huchoshwa na mateso ya mapenzi na
kukata shauri la kufanya mabadiliko lakini moyo huyakataa mabadiliko hayo.
Mtu katili
ni yule anayemtesa mwenzake na kumwambia maneno makali: “Wewe mbona
king’ang’anizi? Nimeshakwambia sikutaki.”
Anashindwa
kuelewa kuwa huyo ni binadamu mwenzake, ana moyo kama yeye. Na tatizo siyo
yeye, ni moyo ambao siku zote umekaa kihafidhina. Moyo haupendi mabadiliko!
Anayetamka
maneno makali kama hayo, anajisahaulisha kwa sababu naye kwa wakati wake
aliwahi kukumbana na kibano cha kumpenda asiyempenda. Na kama hayajamfika, naye
ipo siku yake. Ahadi hiyo ni kwa sababu naye ana moyo na tabia za moyo duniani
kote zinafanana. Avute subira!
Mtu mjinga
ni yule anamyemcheka mwenzake anayebembeleza mapenzi. Anampigia magoti
ampendaye, anaomba msamaha hata kama ni yeye aliyekosewa. Ni mjinga kwa sababu
hajui kuwa mwenzake ana moyo ambao ukitaka lake ni lazima litimie.
Hata huyo
anayemcheka mwenzake, siku ikimdondokea ataona matokeo. Anaweza kupitisha usiku
mzima bila kupata japo usingizi wa mang’amng’amu. Siku itapita na asiwe na hamu
ya kuingiza chochote tumboni. Kwa vile ana moyo, basi na asubiri.
Binadamu
kama angeweza kuishi bila moyo, maisha yake yangekuwa mazuri mno. Maumivu ya
mapenzi yasingekuwepo. Ingekuwa watu wakiachana, mmoja anasema “poa” na
mwenzake anajibu “poa”, kisha kila mtu anashika hamsini zake. Kusingekuwa na
kung’ang’aniana wala kupigiana simu usiku wa manane na kuombana misamaha.
Shida kubwa
ni kuwa binadamu hawezi kuishi bila moyo. Moyo ndiyo injini ya mwili wa
binadamu. Bila moyo hakuna maisha. Tuzingatie pia kuwa moyo ndiyo husababisha
upendo wa dhati uwepo. Mgogoro unaletwa na wapendao kwa wapendwao.
MAPENZI
YANATAKA UELEWA
Utampenda
sana mtu, kwa bahati mbaya yeye anakuwa anampenda mwingine ambaye anamuumiza.
Usipokuwa mwelewa, utajikuta unaumia kila siku. Yaani yeye anaumizwa na anayempenda
kisha anakuumiza wewe ambaye huambiwi kitu kwa jinsi unavyompenda.
Lazima
kufahamu kuwa mapenzi ya kweli hayakatishwi mara moja. Wewe mwenyewe ukipenda
mahali kwa viwango vya kweli vya kupenda, ukikatishwa hutakuwa sawa. Utaumia
mno!
Hivyo
mwelewe mwenzako kuwa anashinikizwa na moyo wake. Usiseme: “Mimi nakujali na
kukuonesha mapenzi yote, wewe unamng’ang’ania mtu wako.” Hizo ni kauli za
kumuongezea maumivu. Zaidi uking’ang’ania, mtakosa wote. Wewe utamkosa yeye,
naye atamkosa anayempenda.”
Kama kweli
unampenda, msaidie aachane na huyo anayemtesa kwa utaratibu. Kuwa sehemu ya
maumivu yake, labda mbeleni ukawa tiba yake, kisha moyo wake ukakupokea.
Amini kuwa
moyo na hulka zake, huyo anayeng’ang’ania, siku akichushwa, yaani moyo ukisema
basi, ndipo utaona kimya. Yuleyule aliyekuwa anapendwa anaweza kurudi
kubembeleza na asipokelewe. Moyo wa binadamu ukishahama ni vigumu kurudi nyuma.
Moyo wa
binadamu ukishageuka, kurudia mapenzi huwa sawa na mtu kubeba punda mkubwa
begani. Wanaorudiana mara nyingi ni wale waliokuwa wanapendana ila wakawa
wanajishaua na kudenguliana. Waliokataana kutoka moyoni huwa hawakaribishani
tena.
MAPENZI
HAYATAKI MASHINDANO
Nimeshaeleza
kwa upana kuhusu moyo wa binadamu unavyofanya kazi na ubishi wake wa kuhamisha
mapenzi. Hivyo basi, ni vizuri kwako kutambua hali halisi na kushika njia
ambayo inakubalika.
Ni ukweli
kuwa haiwezekani ukawa na amani pale unayempenda na kumfanyia kila unaloona ni
zuri lakini yeye akawa hajali, na badala yake umakini wake wote anauelekeza kwa
mtu mwingine.
Na asili ya
moyo wa binadamu, humlazimisha mtu kutamani kupokea zaidi ya anachotoa. Siyo
kwa maana ya zawadi kuwa akikupa simu, anakuwa anatarajia kupokea televisheni,
la hasha!
Anayetoa
anaweza kuelewa kabisa kuwa mwenzi wake hana uwezo wa kutoa vitu vikubwa. Ila
anakuwa anahitaji kupewa shukurani za kimatendo kuliko maneno.
Mtu ambaye
anashukuru kwa mazuri anayofanyiwa hujulikana. Ile hali ya unyenyekevu ambayo
mtu anayepewa kitu huionesha, ndivyo ambavyo hutakiwa kuonekana kwa wapenzi,
aliyepewa kwa aliyempa.
Hata hivyo,
tabia ya kutaka kupokea kadiri anavyotoa ndiyo huzalisha malumbano na maumivu
ya upande mmoja. Mapenzi yanahitaji uvumilivu hasa wakati wa kutoa, maana sivyo
utakavyopokea.
Suala la
kutoa na kupokea halipo kwenye vitu vya kuonekana, lina rangi nyingi. Mfano,
unaweza kuwa unampigia sana simu mwenzi wako lakini yeye hakupigii. Na ukipiga,
unaweza kukuta anaongea na mtu mwingine kwa muda mrefu.
Anaweza
kukuomba umtumie muda wa maongezi na ukafanya hivyo lakini asikupigie hata mara
moja. Ukimtumia SMS, anaweza kukujibu kwa kujisikia. Hali hiyo inaumiza lakini
haipaswi kuutesa moyo wako.
Tambua kuwa
ninyi wote mna jukumu la kupigiana simu na siyo lazima nani aanze. Usiseme:
“Yaani kila siku lazima nianze mimi kukupigia.” Mapenzi hayajengwi kwa
mashindano. Ukiliweka hilo kichwani litakuumiza zaidi.
Unaweza kuwa
mshindi kwenye mapenzi na usiumie, endapo utasema na nafsi yako: “Mwenzangu ni
mzito kupiga simu, sasa mimi nitampigia kila wakati.” Kisha ukajiwekea
utaratibu wa kumzindua kwa kumpigia mara kwa mara.
Wewe ni
mwepesi kumsifu mwenzi wako kwa mambo mbalimbali lakini yeye hafanyi hivyo.
Usikasirike na kuacha! Mathalan kumwambia amependeza au anafanya vizuri kazi
zake.
Ajabu ya
moyo ni kuwa wakati wewe unamwambia amependeza kisha anaishia tu kusema
“asante” au “uzuri nao unachangia”, kisha hakwambii hata mara moja, naye
akikutana na mtu fulani anammwagia sifa kemkemu za kupendeza na uhodari wa kazi
lakini anaishia tu kushushuliwa au kusemwa pembeni kuwa anajigonga!.
Hata wewe,
yupo ambaye hukupongeza kwa kazi nzuri na jinsi unavyopendeza lakini humjali.
Utashangaa kuwa huyo anayekupa sifa nyingi, naye hupewa na mtu mwingine lakini
hajawahi kuzingatia hata mara moja. Moyo haujawahi kupewa mtihani ukafaulu.
Moyo una rekodi ya kufeli tu!
SASA
TUKUBALIANE
Mapenzi yana
tabia mbaya mno. Unaweza kumhangaikia mtu ambaye anahangaika na mwingine.
Anayekuumiza, kumbe yupo anaumizwa na mwingine.
Huwezi kujua
moyo wake unatatizika na nini wakati wewe unalalamika anakuumiza. Pengine yeye
anaumia zaidi.
Mwenzi wako
anaweza kuwa karibu na wewe, mnazungumza kwa ukaribu kabisa, lakini akawa
anakutesa vilevile.
Akawa anakupa
muda wake wote, mnalala kitanda kimoja na bado akakutesa. Ni kwamba mapenzi
yanapatikana moyoni. Utakuwa naye kimwili lakini moyo wake upo kwa mwingine
ambaye naye pengine muda muda huo amelala na mwingine.
Kwa ukaribu
ambao mtakuwa nao, utapenda akuhudumie lakini hutapata huduma ambazo ungependa
upewe na mwenzi wako. Ni kwamba hamu ya utoaji huduma inatoka moyoni, nawe kwa
wakati huo moyoni mwake haumo.
Mtu anaweza
kutoka kuumizwa na mtu, akaachwa vibaya lakini baadaye akaanzisha uhusiano
mwingine ambao utaisha kwa kumuumiza mwenzake. Huo ndiyo ukatili wa mapenzi!
Unadhani
aliyeumizwa kisha akaumiza anastahili lawama? Hapana hata kidogo! Siyo yeye, ni
moyo. Moyo hauna macho, hauoni penye mapenzi ya kweli. Upofu wa moyo ndiyo
unaosababisha mapenzi yawe na tabia mbaya.
Kila siku
omba Mungu akufunulie mwenzi wa kweli na umtambue. Usije kabisa kuamini moyo.
Maana moyo wenyewe haujielewi. Unajiendeaendea tu! Moyo umenyimwa macho, basi
imekuwa shida kubwa katika mapenzi.
Ndimi Luqman
Maloto
0 comments :
Post a Comment