ads 728x90 B

Katibu mkuu Chadema ana mzigo wa madeni




Na Luqman Maloto
MUNGU pekee anajua kilichokuwepo kwenye kichwa cha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kupendekeza jina la Dk. Vincent Mashingi kisha kuthibitishwa kuwa katibu mkuu mpya wa chama hicho.
Wapo watu kwa upeo wao waliamini uteuzi wa katibu mkuu Chadema ni jambo rahisi. Hali ya kisiasa kwa sasa na sura ya kuendelea kukibakisha chama kuwa taasisi imara, ilikuwa mtihani kwa Mbowe kuteua.
Ndani ya Chadema kuna viongozi maarufu vijana ambao mtaani wanaitwa masupastaa wa chama. Umpe Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), John Mnyika (Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara) anune?
Wapo akina Tundu Lissu, Halima Mdee, Ezekia Wenje, Peter Msigwa na wengine. Wote hao ni maarufu, na kila mmoja kwa nafasi yake anajiona ni roho ya chama na anatosha viwango vya kuwa katibu mkuu. Ampe nani, amnyime nani?
Ifahamike kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za chama. Anatakiwa mtu mwenye weledi, afya, busara na mvumilivu. Nani kati yao? Naweza kuhisi maumivu ya kichwa aliyokuwa nayo Mbowe!
Hapohapo lazima kutambua kuwa anayerithiwa ni Dk. Willibroad Slaa. Mwanasiasa mkongwe nchini, aliyejitengenezea haiba ya kupendwa na watu wengi katika kada mbalimbali.
Misimamo ya Slaa na kazi kubwa aliyopata kuifanya akiwa mbunge na kiongozi wa Chadema, ni thamani ambayo si rahisi kuilinganisha na mtu. Hivyo ilikuwa lazima kuwa na uhakika hasa wa anayeziba nafasi yake.
Jinsi Dk. Slaa alivyoondoka, alichafua hali ya hewa kuwa Chadema iliingia ubia na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, na kumfanya kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa ushirikiano na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Slaa alipakaza kuwa Lowassa aliingia Chadema kwa matumizi makubwa ya fedha. Maneno hayo kwa tafsiri ya karibu ni kwamba chama kilinunuliwa. Na CCM walitumia maneno hayo kwenye kampeni zao.
Kwa mantiki hiyo, siyo uongo kuwa chama kimesemwa vibaya, na kimekuwa kikishambuliwa kwa kupoteza ajenda ya ufisadi katika harakati zake za kuiondondoa CCM madarakani.
Nani wa kufaa kukipaka chama sabuni na kukiondolea uvundo wa mashambulizi yote ya nyuma? Mbowe alihitaji mtu mithili ya pafyumu nzuri, ambaye atakuwa manukato yenye kukifanya chama kinukie.
Kuelekea Mwanza kwenye uteuzi, yapo majina ambayo yalikuwa yakifikiriwa kuwa pengine yangepewa nafasi. Hata Profesa Mwesiga Baregu alitajwa, lakini haikuwa hivyo. Hatimaye Dk. Mashingi akawa moshi mweupe kwenye Mkutano wa Baraza Kuu. Zikapigwa kura za wazi!
Kwa hili suala la kura za wazi ni lazima tuliseme na liishe. Linaua demokrasia ndani ya vyama. Wakuu wameibuka na utaratibu wao wa kutotaka uamuzi wao usipingwe, kwa hiyo wanataka uchaguzi wa machoni. Kwamba “tukuone ukisema hapana.”
Mwanachama unawezaje kusema hapana mbele ya mwenyekiti na viongozi wote wakuu? Hii ndiyo sababu kura zote za wazi huwa na matokeo ya asilimia 100. Nani hajipendi? Hii ikome ili kukomaza demokrasia kwenye vyama!
Tukirejea kwenye muktadha wetu, ni kuwa uteuzi umeshafanyika na Dk. Mashingi ndiye katibu mkuu lakini ni vizuri kwa wakati huu kumkumbusha madeni yake.
Madeni hayo yanahusu nafasi aliyoteuliwa ili kukidhi viwango vya cheo chake, vilevile kutii kiu na matarajio ya wanachama wa Chadema.
DENI LA UMAARUFU
Dk. Mashingi ni mwanasiasa mpya. Siasa za nchi ndiyo kwanza zimepokea jina lake. Hajawahi kutajwa popote kabla, kwa hiyo watu ndiyo kwanza wanamtazama na kumchimba wapate kumfahamu kwa undani.
Siasa siku zote hutegemea mtaji wa umaarufu, na pointi hii siyo rafiki wa Dk. Mashingi kwa sababu hajulikani.
Ni ukweli kuwa chama chake ni maarufu, kwa hiyo atajulikana tu lakini umaarufu ambao unaohitajika ni ule wa ushawishi (influence). Awe na viwango vya kutengeneza maneno yenye nguvu kisiasa, kijamii na kihabari. Hili ni deni!
Ni deni kubwa kwa sababu anazungukwa na timu ya watu maarufu na yeye anatakiwa kuchanua katikati yao.
Zaidi, anatakiwa kufanya kazi ili kuupiku umarufu wa akina Lissu, Mnyika, Mwalimu na wengineo kwa sababu yeye ndiye anakuwa bosi na mtendaji mkuu wa chama.
Hatakiwi kabisa kutenda au kung’ara chini ya kiwango. Akifanya hivyo litakuwa kosa kubwa mno.
DENI LA VIATU VYA DK. SLAA
Nimeshaeleza kuwa Dk. Mashingi amepata nafasi hiyo baada ya Slaa kujiuzulu nafasi hiyo kisha kuachana na siasa, kutokana na kutokubaliana na uamuzi wa chama hicho kumpokea Lowassa na kumfanya kuwa mgombea urais.
Slaa ni mwanasiasa mwenye jina kubwa. Amefanya mengi kwenye siasa za upinzani. Chadema hakikuwahi kukua na kupata ukubwa wa kiwango cha sasa kabla ya Slaa kuwa katibu mkuu.
Kabla ya Lowassa kuondoka CCM na kujiunga Chadema, Slaa ndiye alikuwa nembo ya upinzani na kiongozi mwenye ushawishi mkubwa kuliko mwingine yeyote. Takwimu mbalimbali za kitaalamu zilimtaja hivyo.
Yapo maeneo Chadema imejulikana kwa sababu ya Slaa. Hili ni dhambi kulipinga. Kwa mantiki hiyo, Mashingi anatakiwa kucheza karata zake vema ili asiache pengo katika kiatu alichovua Slaa. Udhaifu wowote atakaouonesha, utaibua kelele nyingi za wanachama kwamba ameondoka mtu imara, amefuata dhaifu.
DENI LA SIASA ZA SASA
Mashingi ameingia kuwa mtendaji mkuu wa chama ambacho kina kiu kubwa ya kuchukua usukani wa nchi ifikapo mwaka 2020.
Ni kipindi ambacho siasa za upinzani zimepewa mazingira magumu ya kung’ara kutokana na mfumo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Tangu Dk. Magufuli alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, amekuwa akipita kulekule ambako wapinzani siku zote walipigia kelele, hivyo kuwafanya wapinzani kukosa ajenda yenye nguvu ya kusimamia.
Mtindo wa kutumbua majipu, udhibiti wa matumizi ya serikali na mambo mengine, vimekuwa vitu vinavyomfanya Dk. Magufuli ang’are, na kutazamwa zaidi kuliko harakati za upinzani.
Mfano mdogo ni kuwa baada ya jina la Mashingi kutangazwa usiku wa kuamkia Jumapili (Machi 13), tangu asubuhi yake, vijana wa Chadema wanaofahamika walikuwa ‘bize’ sana kusambaza wasifu wake ili kuonesha kuwa Mbowe amefanya kazi nzuri.
Sifa kubwa ambayo Mashingi alipewa ni kuwa ndiye katibu mkuu msomi kuliko makatibu wakuu wote duniani! Sijui kwa takwimu za wapi!
Walieleza kuwa Mashingi ana shahada ya Udaktari (MD), aliyosomea Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda kati ya mwaka 1995 mpaka 2001.
Wakasema anayo shahada ya pili ya Udaktari Bingwa (MMED Anesthesiology) aliyosomea Chuo Kikuu cha Muhimbili, Dar es Salaam kati ya mwaka 2003 mpaka 2005.
 Walimchambua kuwa mwaka 2004 alitunukiwa cheti (astashahada) katika Utafiti, Chuo Kikuu cha Muhimbili.
Wasifu wa Mashingi uliendelea kusambazwa kuwa kati ya mwaka 2008 na 2010, alisoma na kutukiwa shashada ya uzamili ya Uhusiano wa Umma (Public Relations) katika Chuo cha Evin School of Management, Dar es Salaam.
Sifa nyingine ya kielimu ni kuwa Mashingi kati ya mwaka 2007 na 2010, alisoma shahada ya uzamili ya Usimamizi wa Biashara katika Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge, Sweden.
Mwaka 2010, Mashingi alisoma Chuo Kikuu cha California, katika Shule ya Anderson, hapo alisomea stashahada ya Usimamizi wa Maendeleo.
Mwaka 2008 alisoma Chuo Kikuu cha Maryland, Marekani, Shule ya Dawa, akatunukiwa cheti cha Mfumo wa Wadudu Maradhi kwa Binadamu (Human Virology).
Kwamba kati ya mwaka 2010 mpaka 2016, alisoma na kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria Tanzania.
Uzoefu wa kazi ni kwamba amewahi kuwa daktari Hospitali ya Muhimbili, mtafiti wa kujitegemea, daktari bingwa Hospitali ya Regency, msimamizi wa miradi Shirika la Kimataifa la Afya (IMA World Health), vilevile mshauri wa tiba za kifua kikuu na Ukimwi wa Shirika la IMA.
Pamoja na sifa zote hizo, habari za katibu mkuu huyo kwenye mitandao ya kijamii, zilimezwa mara tu taarifa ya Ikulu kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa ilipotoka mchana wake.
Baada ya wakuu wa mikoa kutangazwa, kila upande habari zinazotamba ni majina ya wakuu wa mikoa, huyu kamzungumzia Paul Makonda kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, mwingine anajadili wanajeshi kupewa vyeo na kadhalika.
Hapa kwa hakika, Mashingi anayo kazi ya kufanya kipindi hiki ambacho upinzani unabanwa mbavu na serikali. Anatakiwa kuwa na ajenda zenye nguvu ili chama chake kipewe nafasi ya kutamba kwenye mzunguko wa habari na mitandao ya kijamii.
www.luqmanmaloto.com
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment