MALKIA Mary I,
alizaliwa Februari 18, 1516, alikufa Novemba 17, 1558. Huyu alikuwa Malkia wa
England na Ireland kuanzia mwaka 1553 mpaka kifo chake.
Ni mtoto wa
Mfalme Henry VIII na Catherine wa Aragon. Malkia Mary alibatizwa jina la Mary
wa Damu (Bloody Mary). Alikuwa Mkatoliki na kipindi cha utawala wake, aliua
viongozi wote maarufu wa madhehebu ya Protestant, hivyo kusababisha waumini
wengi kukimbia nchi.
Naam! Chuki
ukiipanda, utaivuna na kuizalisha! Mary alitenda ukatili huo kama sehemu ya
kulipiza yale ambayo mama yake mzazi, Catherine wa Aragon alitendewa.
Ukatoliki na
madhehebu yenye kuupinga Ukatoloki (Uprotestant), kwa pamoja uliyagharamu
maisha ya Catherine wa Aragon (mama wa Malkia Mary I), na sababu kuu ni baba
yake mzazi, yaani Mfalme Henry VIII.
Pokea
simulizi hii uone jinsi ambavyo chuki inapopandwa, huvunwa na kuzaa.
Ni kwamba
Henry asingekuwa Mfalme wa Uingereza kama asingemuua kaka yake, Arthur Tudor,
ambaye alikuwa anangoja tu baba yake Mfalme Henry VII afariki dunia kisha yeye
atawazwe ufalme.
Arthur
alikuwa Prince wa Wales na mkewe, Catherine wa Aragon ndiye alikuwa Princess wa
Wales.
Henry VIII
alimuua Arthur, na ili atawazwe kuwa Mfalme wa Uingereza, ilibidi atimize
sharti la kumuoa Catherine wa Aragon ambaye alikuwa anasubiri wakati ufike awe
malkia (The Waiting Queen).
Baada ya
kufunga ndoa na Catherine, alitawazwa kuwa mfalme, kisha Catherine akawa malkia
wa Uingereza.
Tambua kuwa
Henry VIII alimuoa Catherine kwa sababu tu ya ufalme, hivyo hakuwa na mapenzi
naye ya dhati.
Basi baadaye
akatokea mtumishi wa Catherine, anayeitwa Anne Boleyn. Mfalme Henry akampenda
Anne, akamfanya kimada wake, na aliponogewa na penzi akataka kumtaliki
Catherine ili amuoe Anne.
Mfalme Henry
VIII kwa kutumia ufalme wake, akadhani inawezekana kupindisha sheria za
Kikatoliki, kwamba ndoa ni moja. Hivyo basi, alimuomba Kiongozi wa Kanisa
Katoliki wakati huo, Papa Clement VII, amruhusu amtaliki Catherine kisha amuoe
Anne.
Papa Clement
VII alikataa ombi hilo, akamsisitizia kuwa ndoa ni moja kisheria na kwamba
talaka haikubaliki.
Kwa hasira,
Mfalme Henry VIII alimkashifu Papa Clement VII, kwamba siyo kiongozi wa Kanisa
duniani, bali ni askofu tu wa Roma.
Baada ya
hapo Mfalme Henry VIII alianzisha madhehebu ya Anglikana. Ukatoliki ukapigwa
marufuku Uingereza. Kisha Mfalme Henry VIII alimtaliki Catherine na kumuoa Anne
chini ya Uanglikana.
Maisha ya
Catherine yakawa magumu mno, aliteswa mno na Mfalme Henry VIII na Anne. Mfalme
Henry VIII hakutunza heshima ya Catherine kama mwanamke aliyemfanya awe mfalme,
vilevile mama wa watoto wake.
Mateso yote
ambayo Catherine alitendewa, Mary aliyaona. Akamuona baba yake adui, kwani
hakumpenda mama yake na alishuhudia. Aliwachukia wapinga Ukatoliki kwa sababu
aliwaona kama maadui wa mama yake.
Baadaye
Catherine alifariki dunia. Kifo kilijaa utata mkubwa. Anne alidaiwa kumuua
Catherine kwa jeuri aliyokuwa anapewa na Mfalme Henry VIII. Yote hayo Mary
aliyaona!
Chuki
ukishaipanda lazima uivune; Unafiki wa Anne na ubaya wote aliomtendea
Catherine, ulimrudia baada ya kila kitu kujidhihirisha kwa Mfalme Henry VIII.
Anne Boleyn akahukumiwa kuuawa, hivyo kuvuna ile chuki yake kwa Catherine.
Mfalme Henry
VIII kwa shingo upande alilazimika kukubali mke wake kipenzi auawe. Alivuna
chuki ambayo aliipanda kwa kumuua kaka yake, kisha kumtesa Catherine.
Mfalme Henry
VIII alizalisha chuki; Kwani mwanaye Mary baada ya kutawazwa kuwa malkia wa
Uingereza, kumbukumbu za mateso ya mama yake zilimjia na kuanza kumwaga damu
ovyo kwa Waprotestanti.
Alitaka watu
wote wawe Wakatoliki. Na hiyo ndiyo ikawa sababu ya ukatili wote alioufanya. Na
hayo ndiyo matunda ya chuki, iliyoanzia kwa baba yake.
Chuki ni
kama tindikali, ukiimwaga juu ya kabati, baada ya muda utakuta imefika
sakafuni, yaani kabati lenyewe na nguo, vitakuwa vimetafunwa na makali yake.
Daud alianza
chuki kwa kumtwaa Bathsheba ambaye ni mke wa askari wake, Uriah. Chuki ya Daud
haikuishia hapo, akaagiza Uriah auawe, na kweli, kijana asiye na hatia akauawa.
Kisa mke wake ni mzuri, amependwa na Mfalme Daud.
Ona jinsi
Daud alivyovuna na kuizalisha chuki kwenye familia yake; Kwanza kabisa Amnon
ambaye ni mtoto wa kiume wa Daud, alimbaka dada yake Tamar. Watoto wa mfalme,
yaani mtu na dada yake, kutenda dhambi ya ngono, tena katika njia ya ubakaji.
Haikuishia
hapo; Absalom, mtoto wa kiume wa Mfalme Daud, alifanya mapenzi na wake wa baba
yake. Zaidi, akamuwinda baba yake amuue.
Absalom
alitengeneza jeshi lake la kumkabili baba yake. Ukisoma Biblia 2 Samuel, utaona
Daud akiumizwa na jinsi mwanaye alivyogeuka adui yake, hadi kuutaka uhai wake.
Mwisho, ilibidi
askari waaminifu wa Daud wamuue Absalom. Japo Daud aliumia sana mwanaye kuuawa
kiasi cha kutamani bora angekufa yeye Absalom abaki, lakini matokeo yalikuwa
hivyo. Chuki ina tabia kustawi na kumlazimisha aliyeipanda aivune na
kuizalisha.
Mary Ann
Cotton, alizaliwa Oktoba 1832, alikufa Machi 24, 1873. Wakati akiwa mdogo,
alijifunza kuwachukia wanaume kutokana na jinsi mama yake alivyopata mateso.
Matokeo
yake, mwanamke huyo raia wa Uingereza, aliwaua watoto wake nane kwa nyakati
tofauti, wote kwa kuwawekea sumu. Aliolewa mara mbili na waume zake wote
aliwaua kwa sumu. Vifo vya watoto na waume zake, vinafanana. Alinyongwa baada
ya kukutwa na hatia ya kutenda unyama huo.
Usizalishe
chuki ndugu yangu, gharama yake ni kubwa. Inaweza kukukuta wewe mwenyewe au
hata kizazi chako.
Chuki ina
tabia ya kusafiri. Ukimchukia mtu fulani na kizazi chake kinapokea. Unaweza
kujikuta unazalisha watoto maadui, baada ya wazazi kupanda chuki na kuondoka
duniani kabla ya kupata suluhu.
Ni chuki za
kurithi ndizo zilizosababisha Isabella wa Castile aingie kwenye orodha ya
wanawake katili kuwahi kutokea duniani.
Isabela
ambaye alizaliwa Aprili 22, 1451 na kufariki dunia Novemba 26, 1504, alikuwa Malkia
wa Hispania.
Utawala wake
ulikuwa wa kiimla hasa. Pamoja na udikteta wake, Machi 31, 1492, alianzisha
mpango wa kudhibiti uasi Kanisa Katoliki (Inquisition).
Alimteua
Tomas de Torquemada kuwa kamanda wa kusafisha watu ambao siyo Wakatoliki nchini
humo. Kipindi hicho, watu wengi wasio Wakatoliki walipoteza maisha, huku
Waislam na Wayahudi wapatao 200,000 wakiikimbia nchi hiyo.
Chuki ni
ugonjwa mbaya mno na unaambukiza (communicable disease), tena huwezi kuuweka
katika kundi moja na magonjwa yasiyoambukiza (non communicable diseases) kama
ilivyo presha au kisukari.
Wapo
wafanyabiashara walikuwa na uhasimu mkubwa, na matokeo yake watoto wao
wakarithi chuki na hata kuuana.
Walioanzisha
uhasama kati ya Wahutu na Watutsi walifariki dunia miaka mingi kabla ya vita ya
kimbari, iliyogharimu maisha ya watu zaidi ya watu milioni 1.2 nchini Rwanda
mwaka 1994. Hii ina maana kuwa wanaorithi chuki, huivalia njuga kuliko
walioianzisha.
Chuki kati
ya Palestina na Israel, walioianzisha walishatangulia mbele ya haki miaka
dahari na dahari iliyopita, lakini mpaka leo watu wanauana. Chuki ina kawaida
ya kuishi na kuhama kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Walioanzisha
chuki ya wakulima na wafugaji wala wao hawakuuana, walinuniana na kutishana tu
lakini waliorithi wanauana na kuchomeana nyumba. Chuki ina hulka kama risasi,
inapoingilia kuna tundu padogo, ila inapotokea tundu lake ni kubwa.
Acha
kutengeneza chuki na mtu leo, maana huwezi kujua mbeleni athari zake ni kubwa
kiasi gani.
Usipende
kutangaza chuki na watu wengine, pengine wanaokupenda wakaichukulia kwa uzito
kuliko wewe mwenyewe.
Labda
nikufahamishe kitu, kwamba hata upendo na undugu huambukiza. Ukiwapenda watu,
na kizazi chako kitakuja kuwapenda. Ruhusu upendo usambae.
Huwezi kujua
kuwa chuki zako zinaweza kuwapa wakati mgumu watoto au ndugu zako kwa kiasi
gani.
Hujawahi
kuona mtu anagombana na hasimu wake, lakini anakwenda kulipiza kwa mtoto wa
adui yake? Au mkewe? Au hata wazazi?
Inawezekana
kuwa na maisha bila chuki. Yafanye maisha yako yawe rahisi, vilevile
warahisishie watoto au ndugu zako maisha yao, kwa kutowaachia urithi wa chuki.
Chuki ni mzigo haramu, usiwabebeshe.
Ishi na watu
vizuri kisha hata baada ya kuondoka kwako, kizazi chako kitafaidi matunda mema.
Maisha yenye kujengwa na upendo ni ulinzi kwako binafsi na familia yako. Ni
msaada kwa kizazi chako utakapokuwa umeondoka.
Wapo watu
watalazimisha chuki, wewe tabasamu mbele yao. Usiwape nafasi ya kustawisha
chuki zao. Wewe siyo shamba lenye rutuba ya kustawisha chuki.
Ndiyo, kama
mtu anakuchukia kisha akafanikiwa kuifanya chuki yake istawi juu yako, maana yake
wewe ni shamba bora lenye kustawisha chuki. Usikubali. Ladha ya maisha bila
chuki ni tamu asikwambie mtu.
Akijitahidi
kupandikiza chuki kwako, wewe pandikiza upendo kwake, ongeza zaidi na kwa
wengine. Ifanye chuki yake ikose nguzo kwenye maisha yako. Ni kawaida kwamba
chuki ikikosa nguvu kwa mkusudiwa, humrudia mwenye nayo.
Asante.
Ndimi Luqman
Maloto
0 comments :
Post a Comment