ads 728x90 B

WASANII HAWAFI ILA KANUMBA, NGWAIR WAMEKUFA!

NA LUQMAN MALOTO
JANA (Machi 9), nilipigiwa simu na mtangazaji wa Clouds Media Group, Soud Brown ambaye ni mtayarishaji mkuu wa kipindi cha XXL, akitaka maoni yangu kama mwandishi wa habari, vilevile mchambuzi wa masuala ya sanaa.
Mada aliyotaka nichambue ni namna ambavyo familia za wasanii zinaweza kuendelea kunufaika kupitia sanaa ya ndugu yao hata baada ya msanii mwenyewe kuwa ameshafariki dunia.
Nikiri kuwa ni mada nzuri na ya kikubwa. Kupitia kwenye simu sikuweza kumpongeza Soud kwa mawazo mazuri, vilevile sikumshukuru kwa kunishirikisha, maana wachambuzi wapo wengi na wenye viwango vikubwa kabisa. Ila hapa naomba nimpongeze na kumshukuru.
Nilichokizungumza na Soud, nimeona bora pia nikiweke kwenye maandishi ili kusambaza ujumbe na maarifa kiduchu kwa wengine.
Kwanza msanii huwa hafi ila huipisha dunia baada ya wito wa Mungu. Duniani kote huwa hivyo, ni Tanzania na nchi chache ambazo hazithamini umuhimu wa sanaa na kuwekeza kwenye sanaa ndiyo wasanii hufa.
Mathalan, Steven Charles Kanumba ‘The Great’ amekufa. Ndiyo amekufa jumla. Sasa hivi wanasimuliana “Kanumba alikuwa fundi Bongo Movie”, tunasimuliana tu!
Kizazi cha sasa kitapotea na Kanumba atasahaulika jumla. Msanii kusahaulika ni kosa la jinai. Msanii huwa hafi, kwa hiyo haiwezekani asahaulike. Msanii hupokea wito wa kuagana na dunia kwa sababu ni agizo la Mungu kuwa binadamu lazima arejee mavumbini!
Msanii kwa kazi zake huendelea kuishi kila siku. Msanii huwa hafi jumla. Hapa Tanzania kwetu akina Marijan Rajab pamoja na ujabali wake wa muziki lakini ameondoka jumla. Tatizo siyo yeye, ni Tanzania yetu na mwamko mdogo wa sanaa.
Mbaraka Mwishehe, mpaka leo watu wanaimba Mtaa wa Saba. Matunda hayapo, kama nchi tuliamua aondoke na sanaa yake. Mara moja moja ndiyo nyimbo zake zinachezwa baa, “Shida haikosekani hata siku ya harusi”, kisha walevi wanagonga glasi na kusema: “Mzee alikuwa fundi.”
Mzee Kassim Mapili emeondoka hivi karibuni, hata akiwa hai thamani yake haikuonekana pamoja na Rangi Yake ya Chungwa! Na hivi kaondoka, basi ndiyo kabisa. Unamuuaje jumla Mzee Mapili?
TX Moshi William na uhodari wake wa kutunga pamoja na sauti yake nzuri, wapi alipo leo. Kifo kilipomchukua na bendi yake ya Msondo nayo ikapoteza hadhi.
Msondo ilimbakiza Kamanda Maalim Muhidin Gurumo ambaye TX Moshi alipofikwa na mauti yeye alibaki mgonjwa. Siku ikawadia Maalim Gurumo akaipa kisogo dunia. Wito wa Mungu haukwepeki!
Unawezaje kuwasahau Gurumo na TX Moshi? Tanzania tumekuwa na uthubutu wa ajabu mno. Eti hatuna mbinu bora za kuwafanya watu hawa adhimu waendelee kuishi hata baada ya kuingia kaburini.
Juma Kilowoko ‘Sajuki’ amesahaulika mapema pamoja na kuwepo kwa simulizi ya kuumiza kuhusu maradhi yake mpaka kifo.
Adam Kuambiana hata wasanii wenzake wanamtaja kwa kuvizia, tena pale wanapokuwa wamekwama maeneo fulani ya kikazi ndiyo wanasema: “Angekuwepo Kuambiana hapa hili lisingekuwa tatizo!”
Hakika inauma mno kumkumbuka Sharo Millionea na ubitozi wake. Aliitenda sanaa yake ya comedy vizuri kwa kuigiza usharobaro. Alitokea kuwa mashuhuri. Alizikwa kwa kishindo na kweli alizikwa jumla. Hakumbukwi tena!
Acha nishike tama! Eti hata Albert Mangweha ‘Ngwair’, naye ameondoka kimoja. Inakuwaje tena Mfalme wa Freestyle katika Bongo Rap?
Maskini Ngwair mwenye kichwa kama mgodi wa Tanzanite, kutokana na ufundi mkubwa aliokuwa nao wa kutunga na kurap, kweli imekosekana njia ya kumfanya aendelee kuishi?
Ifike mahali tuwe na aibu, yaani Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, yuleyule Mwalimu wa Walimu apotee jumla na tusimkumbuke kabisa? Vizazi vijavyo visiwe na taarifa kuwa ardhi ya Tanzania ilipatwa kukanyagwa na mwanafasihi huyu?
NGOJA TUSEMEZANE
Familia zina wajibu wa kuwafanya ndugu zao wasanii waliofikwa na mauti kuendelea kuishi.
Ni kwa vipi Tupac Shakur ‘Makaveli’, Christopher Wallace ‘Notorious BIG’, Elvis Presley ‘King of Rock’, Michael Jackson ‘King of Pop’, Marvin Gaye, Whitney Houston, Big Punisher, Ella Fitzgerald ‘Queen of Jazzy’ na wengineo wanaendelea kuishi?
Inakuwaje Kanumba, Ngwair, Gurumo, TX Moshi William, Sajuki, Kuambiana, Banza, Marijan Rajab, Mbaraka Mwishehe, Suleiman Mbwembwe, Hemedi Maneti na wengine wamekufa jumla?
Na hapa nifafanue kuwa kuishi kwa msanii haina maana ya nyimbo zake kusikika mara mojamoja redioni, kutazamwa kwenye video, kuwarusha watu klabu na maeneo mengine ya starehe, la hasha!
Kuishi kwa msanii ni kule kuondoka kwake lakini nyuma yake anawaacha watu wakiendelea kuwa ‘bize’, yaani jina lake linaendelea kutengeneza shughuli na matukio ya kila siku yenye kuingiza fedha.
Hapa sina maana ya maonesho ya kumbukumbu ambayo huandaliwa na wajanja kumkumbuka msanii fulani. Zipo namna kadhaa za kuwaenzi wasanii na kuwafanya waendelee kuishi.
VITUO VYA KUMBUKUMBU
Unaweza kujiuliza ni kwa nini mpaka leo, Flora Mtegoa ambaye ni mama yake Kanumba, hajaweza kufungua kituo cha kumbukumbu za mwanaye.
Je, hata wasanii wenzake wameshindwa kumsaidia mawazo Flora kutambua kiasi cha fedha ambazo anaweza kutengeneza kupitia kituo cha kumbukumbu za Kanumba?
Hapa Tanzania hakuna kituo cha Marijan Rajab wala Mbaraka Mwishehe, hakipo cha Gurumo wala hakijafikiriwa cha TX Moshi William.
Wasanii kwa kawaida wanakuwa na vitu vingi vya kuenziwa. Jamii inanyimwa kuvijua kwa undani wake, hivyo kusababisha wasahaulike na wakati huohuo, familia zinakosa fedha ambazo ingepata.
Hapa haina maana ya kufa kufaana, hapana! Ila ni ukweli kuwa wasanii wengi wanapoondoka huacha fedha nyingi nyuma yao lakini hazikamatiki kwa sababu ya familia zao kukosa ubunifu.
Lazima kuwafanya watu watoke kona mbalimbali za ndani na nje ya nchi kisha kutembelea vituo vya wasanii wao.
Mathalan, siku ya kuzaliwa na ile aliyokufa msanii, katika kituo cha kumbukumbu za msanii husika, kunakuwa na shughuli nyingi. Watu wanalipa fedha!
Muhimu ni jinsi ya kukifanya kituo kuwa na hadhi kwa kukitangaza na kuhakikisha mtu akifika hachushwi. Yaani huduma zisiwe za kuboa.
Afeni Shakur ambaye ni mama yake Tupac, yeye aliona fursa baada ya mwanaye kufariki dunia, ndiyo maana ‘ukimgugo’ utakuta utajiri wake unasoma zaidi ya dola milioni 50, yaani Kibongo-Bongo ni zaidi ya shilingi bilioni 100.
Mama yake Tupac pamoja na wingi wa nyimbo ambazo mwanaye aliziacha zinazoendelea kumpa fedha nyingi, mapema kabisa alifungua kituo cha sanaa (gallery) chenye picha na maelezo mbalimbali kuhusu maisha ya Tupac. Ni kuchangamkia fursa.
DOCUMENTARIES
Mathalan, maisha ya Maalim Gurumo yakipata simulizi nzuri na yenye ufasaha, ikatengenezwa documentary, nani ambaye asingependa kuitazama au kuisikiliza?
Waza pia kuhusu TX Moshi, maisha yake, ubishoo wake, ukuu wake kimuziki, ustaa wake, alivyokuwa mtu pendwa kwenye jamii kisha afya yake ilipoanza kutetereka baada ya ajali na hatimaye kifo!
Nyimbo zake zinasikika zikisindikiza simulizi nzuri yenye mengi ambayo jamii haijapata kuambiwa na mengine yaleyale yaliyofahamika lakini yanawekwa pamoja. Je, familia haioni kama hizo ni fedha na zipo nje-nje?
Watoto wa Marijan Rajab na Mbaraka Mwishehe mnashindwa vipi kuwafanya wazazi wenu waendelee kuwa hai kimaisha na kibiashara?
Na ieleweke kuwa kadiri mipango ya kutengeneza fedha inapokuwa kwenye mstari wake, ndivyo na jamii inapata fursa ya kutambua mengi. Kutahamaki, kizazi na kizazi Banza Stone hatasahaulika.
Leo hii James Dandu ‘Mtot wa Dandu’ au ‘Cool James’ hata hakumbukwi. Ni wachache wenye kutambua kuwa alikuwa mwanamuziki mkubwa nchini na ndiye mwanzilishi wa Tuzo za Muziki Tanzania, siku hizi zikijulikana kama Kili Music Awards. Familia ziamke!
Tatizo ndugu wengi wa wasanii waliofariki dunia wakiulizwa, utasikia wanalalamika kuwa serikali haiwasaidii. Dah, kudadadeki! Yaani hata kubuni njia ya kutengeneza fedha kupitia jina la ndugu yako unataka usaidiwe na serikali?
Wewe andaa mpango mzuri, kisha utaona mwenyewe jinsi serikali inavyoweza kuwa karibu na wewe. Itajileta tu, si itataka kodi yake?
Voleta Wallace ni mama wa BIG, ukimfuatilia utagundua ana utajiri unaokadiriwa kuwa dola milioni 40, zaidi ya shilingi bilioni 80.
Moja ya vitu ambavyo vimempa fedha nyingi Voleta ni documentary kuelezea maisha ya BIG.
Ni suala la kuiandaa vizuri na kuitengenezea njia bora za masoko. Mtaji mmoja mkubwa ni lile jina ambalo msanii husika anakuwa ameliacha.
MAANDISHI
Maisha ya msanii yakiwekwa vizuri katika kitabu kizuri, watu watapenda kusoma. Itasaidia kumfanya msanii aendelee kuishi na familia kutengeneza fedha.
Wasanii wengi huwa na vitu ambavyo havijulikani, na watu wenye uwezo wa kuvisimulia kwa ufasaha ni ndugu zake. Mathalan, mama yake Ngwair, anayo mengi ya kusimulia kuhusu mwanaye, na watu wangeyapenda.
Yapi hasa maisha ya Ngwair tangu akiwa mtoto? Vitabia vyake vya utotoni, alipoanza kuisumbua familia wakati akiwa na kiu kubwa ya kufanikiwa kimuziki. Kunakuwa na simulizi kutoka kwa marafiki zake kuhusu maisha yao ya ghetto.
Nakala za vitabu zinapelekwa Maktaba ya Taifa ili vizazi na vizazi, wakienda kujisomea, wanapata pia fursa ya kusoma maisha ya wasanii ambao kwa hakika wanastahili kuitwa mashujaa wa sanaa.
Vitabu vina maana kubwa. Pattie Mallete ni mama yake Justin Bieber, yeye alipoona mwanaye ana jina kubwa, aliandika kitabu kuhusu maisha yake ya kumlea Bieber kinachoitwa Nowhere but Up (The Story of Justin Bieber’s Mom).
Pattie aliweza kuuza kitabu hicho nakala nyingi na kumpatia fedha zaidi ya dola milioni 10 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 20.
Hata mama yake Diamond Platnumz, anaweza kuandika kitabu cha jinsi alivyomlea kwa tabu mwanaye na kutengeneza fedha nyingi kipindi hiki ambacho mwanaye anang’ara kila kona. Ni fursa!
Mimi mwenyewe ningependa sana kusoma kitabu kinachoeleza kwa ufasaha maisha ya Shem Kalenga lakini hakipo. Nahitaji mno kumsoma Dk. Remmy Ongala, sina pa kupata undani wa maisha yake. Fursa zinachezewa.
TUKUBALIANE
Kama wewe ni mwanafamilia wa msanii maarufu aliyefariki dunia na mnakaa pembeni kulalamika kuwa maisha magumu, basi tatizo lipo kwenu wenyewe.
Wazazi na watoto wa wasanii ndiyo wenye haki zaidi. Ni muda wa kufikiria mara mbili, kipi ambacho watu wangependa kukipata kuhusiana na msanii wao kisha wapewe. Watakuwa wanaihudumia jamii na wakati huohuo wanatengeneza fedha.
Wanaweza pia kutengeneza mfuko wa kuhudumia jamii kwa jina la msanii husika. Jinsi kazi zinavyofanyika ndivyo jina la msanii linaendelea kuwa hai na wakati huohuo fedha zinaingia.
Ni rahisi mtu kuchangia fedha kwenye mfuko wa elimu, afya na kadhalika, wenye jina la Sajuki kwa sababu anajulikana.
Muhimu kuzingatia ni kuwa leo hii tunao akina Lady Jaydee, Sugu, Prof Jay, Afande Sele, Juma Nature na wengine wengi, nao wataondoka, ila watakuwa wameipa kisogo dunia kama wataendelea kuishi, ikiwa wataondoka jumla kweli watakuwa wamekufa na hawatakumbukwa!
Ndimi Luqman Maloto
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment