Luqman Maloto
HAYAMITHILIKI maumivu ya kuondokewa na mtu uliyempenda. Kuna
watu wamewahi kuanguka katika maisha yao kwa sababu ya kushindwa kuzoea
machungu na upungufu wa kufiwa na watu wao muhimu.
Celine Dion, mwanamuziki mkubwa duniani na mwanamke imara
nyakati zote kutokana na jinsi alivyobadili upepo wa maisha yake, kutoka
ufukara mpaka utajiri mkubwa, yupo kwenye majonzi makubwa.
Celine amefiwa mume wake, Rene Angelil, aliyefikwa na mauti
Januari 14, mwaka huu. Ni machungu kwa sababu siyo tu kwamba amempoteza mume,
bali pia baba wa wanaye na mshirika mkuu wa kazi zake.
Yatazame mafanikio ya Celine kwa upana kabisa, kisha tambua
kuwa Rene amekuwa na mchango mkubwa mno.
Rene amekuwa meneja wa Celina na msimamizi mkuu wa kazi za
mwanamuziki huyo, hususan kile kipindi chake cha dhahabu, alipouza mamilioni ya
nakala ulimwenguni kote.
RENE NI NANI?
Alizaliwa Januari 16, 1942 nchini Canada. Alianza kama
mwanamuziki kabla ya kugeuka meneja wa wanamuziki.
Rene na Celine walianza kufanya kazi pamoja lakini mapenzi
yaliwateka, na mwaka 1994 walifunga ndoa.
Mji aliozaliwa ni Montreal, Quebec, Canada. Asili yake ni
Mashariki ya Kati, kwani kiasili baba yake ni mtu wa Syria na mama yake
alitokea Lebanon. Walihamia Canada na kuchukua uraia wa taifa hilo la Amerika
Kaskazini.
Miaka ya 1960 Rene alifanya muziki wa Pop na aliwahi kuunda
kundi lililoitwa Les Baronets ambalo lilijihusisha na muziki wa pop rock.
Baada ya hapo, kuanzia mwaka 1981, Rene alianza
kujishuhughulisha na usimamizi wa kazi za wanamuziki mbalimbali (umeneja).
Mwishoni mwa mwaka 1980, Rene aligundua kipaji cha Celine na
uwezo mkubwa alionao baada ya kusikiliza demo yake.
Kipindi hicho, Celine alikuwa akitafuta watu ambao angeweza
kuingia nao mkataba wa muziki, ndipo alipopeleka demo kwa Rene.
Sauti ya Celine ilimtoa machozi Rene na ndipo aliamua kuwekeza
nguvu zake zote kuhakikisha mwanamuziki huyo anakuwa staa wa dunia. Na hakika
amefanikiwa.
Na ndiyo maana leo hii Celine anapoumia kuondokewa na mume
wake, maumivu yanaongezeka zaidi kwa sababu Rene ndiye shujaa wa mafanikio
yake.
Mwaka 1981, Rene aliweka rehani nyumba yake na kupata fedha
ambazo alizitumia kuwekeza kwenye kurekodi albamu ya kwanza inayoitwa kwa Lugha
ya Kifaransa, La voix du bon Dieu, ikiwa na maana Sauti ya Mungu Mzuri.
Baada ya kutoa albamu hiyo, Celine alivuma vilivyo Canada na
kufanya biashara kubwa. Vilevile muziki mzuri wa Celine kutoka kwenye albamu
hiyo, ulivuma mpaka Marekani na maeneo mengine duniani.
Mwaka 1982, alishinda tuzo Tokyo, Japan, mwaka 1983, alikuwa
mwanamuziki wa kwanza mwenye asili ya Canada kufikisha mauzo ya kiwango cha
dhahabu (nakala zaidi ya 500,000), kupitia wimbo wake D'amour ou d'amitiƩ ukiwa
na maana ya Kwa Mapenzi au Kwa Urafiki (Of Love or of Friendship).
Kupitia mafanikio ya Celine, Rene aliweza kushinda tuzo
mbalimbali kama meneja bora wa muziki.
Hivyo, kwa sasa Celina anapotajwa kuwa na utajiri unaofikia
dola milioni 630, ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.37, nguvu kubwa ya
kufikia hapo, imetoka kwa Rene.
Ni Rene aliyemtoa Celine Canada mpaka Marekani na
kumbadilisha kutoka kuimba nyimbo za Kifaransa mpaka za Kiingereza, hivyo
kumuwezesha kufanya biashara kubwa zaidi.
Rene ameacha utajiri unaokaribia kuzidi dola milioni 400
ambazo kwa sarafu ya Tanzania ni shilingi bilioni 875.
Hii ina maana kuwa kwa kuunganisha utajiri wa Rene na
Celine, unaipata familia inayomiliki dola bilioni 1.03 ambazo ni sawa na
shilingi trilioni 2.25.
Celine na Rene wana watoto watatu lakini Rene anao watoto
wengine watatu ambao aliwapata kwa wake zake wengine wawili aliokuwa nao kwa
vipindi tofauti kabla hajafunga ndoa na Celine,
CELINE ALIVYOPAMBANA KWA AJILI YA AFYA YA RENE
Rekodi za afya ya Rene zinaonesha kuwa alipata shambulio la
moyo mwaka 1992, kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 51.
Mwaka 1998 Rene aligundulika kuwa na kansa ya koo kisha
ikaripotiwa amepona kabisa. Kipindi hicho, Celine alikuwa bega kwa bega na
mumewe kuhakikisha anapata matibabu ya kimsingi, na kwa hakika walifanikiwa.
Mwaka 2009, aligundulika kuwa na matatizo ya moyo lakini
tatizo la kansa ya koo lilijidhihirisha tena na mwaka 2013 alifanyiwa upasuaji.
Mwaka 2014, Rene alijiuzulu umeneja wa Celine ili
ashughulikie zaidi afya yake. Hata hivyo, alibaki kuwa sehemu ya washauri wa
kazi za kile siku za Celine.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
0 comments :
Post a Comment