NA LUQMAN
MALOTO
TUNALALAMIKA
matokeo, eti wanafunzi wengi wameanguka! Hatujui tatizo. Tuache kudanganyana!
Shida za
walimu zinajulikana? Mwalimu na mwanafunzi wanacheza kamari ya kutabiri matokeo
ya soka. Asubuhi wakikutana, mwanafunzi anamuuliza mwalimu wake: “Ticha vipi,
mkeka wako jana ulisoma?”
Tunataka
elimu ipande kweli? Shida za walimu zimetatuliwa? Walimu wamejaa dhiki mpaka
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda anawaombea wapande daladala bure. Eti
tunataka ufaulu ufande!
Mwalimu na
mwanafunzi wanakutana kwenye kibanda cha kuangalia mpira, tena mwanafunzi
anamlipia kiingilio mwalimu. Kesho tunataka mwanafunzi awe na nidhamu kisha
afaulu. Hii tabia ya kuitania elimu yetu tutaacha lini?
Mwalimu na
mwanafunzi wana uhusiano wa kimapenzi. Mwalimu na mwanafunzi wana vita ya
kugombea mpenzi. Jamani jamani jamani!
Mwalimu na
mwanafunzi wamegawanywa na Team Diamond na Team Kiba. Wakikutana wanaanza
kubishana, mwanafunzi: “Diamond Platnumz wa kimataifa, yule ndiye Dangote.”
Mwalimu
anajibu: “Anaitwa King Kiba, jamaa fundi sana. Mwite Ali K For Real.”
Katikati ya
masomo, inaingia michapo ya Wema Sepetu na Zari The Boss Lady. Mwanafunzi
anamuuliza mwalimu wake: “Eti mwalimu kati ya Zari na Wema nani mzuri?”
Mwalimu
kabla ya kujibu anamuuliza mwanafunzi wake: “Anza kujibu kwanza wewe, nani
mkali kati yao?”
Mwanafunzi:
“Zari noma, ana watoto wanne lakini kama vile hajazaa. Mweupe, ana mguu umejaa,
umenona kama chupa ya Dompo. Yote tisa, 10 ana pesa, mwite Zari The Boss Lady.
Yule Wema anapumua kwa nguvu ya wanaume tu!”
Mwalimu naye
anajibu: “Acha kujishaua, Madam Sepetu ndiye homa ya nchi. Anaitwa Beautiful
Onyinye. Kale kasauti kake huwa kanamliza Diamond, halafu ana mwanya fulani
hivi mwembamba, sura yake haizeeki.”
Mtihani wa
mwisho kitaifa ukiwadia, hakuna swali la kuhusu Diamond, Ali Kiba, Wema wala
Zari, unadhani nani atafaulu? Siku tukiweka utani pembeni elimu itapanda na
viwango vya ufaulu tutaviona.
Tatizo siyo
wanafunzi kuwa hawana akili, ni kizazi cha sasa na aina ya walimu wanaoshika
chaki kuingia darasani, hali zao za kimaisha, nidhamu yao ya ufundishaji, wito
wao kwenye kazi na maadili ya ualimu kwa jumla.
Mwalimu
kamtaka mwanafunzi, wakishakubaliana kimapenzi basi anahakikisha kila mtihani
anapata A. Mwanafunzi anabweteka, anasahau kuwa mtihani wa mwisho mwalimu wake
hatakuwepo kwenye chumba cha usahihishaji wala cha utungaji wa mitihani. Mwenye
A nyingi shuleni, anapata Sifuri kitaifa.
Mwalimu
anawakuta wanafunzi wawili wanajisomea, wakiwa mvulana na msichana, anawaambia:
“Inaonekana mnapendana sana, wewe Mage mwangalie huyo Mudi atakuja kukupa
mimba.” Wanafunzi wanacheka, kisha Mudi anasema: “Mwalimu bwana kwa madongo!”
Mwalimu
akiwakuta wanafunzi wawili wa kike wanajisomea au wanaongea peke yao, anawaambia:
“Nina wasiwasi nyie mnasagana, huu ukaribu wenu siyo wa kawaida.”
Mwanafunzi
mmoja anauliza: “Mwalimu kusagana ndiyo nini.”
Mwalimu
anasema: “Mnajifanya hamjui eeeh!”
Mwanafunzi:
“Kweli tena mwalimu, hatujui.”
Mwalimu:
“Kama kweli hamjui basi nyie ni washamba. Fuatilieni mtagundua.”
Halafu
wakubwa wanapokutana, baada ya kuanza kutafuta kiini, eti wanajikita kwenye
vitu vidogo-vidogo. Mara GPA, mara Division! Ndiyo maana kwenye suala la elimu
yetu, nimekataa kabisa utani na Profesa Joyce Ndalichako.
Walimu
wakiwa ofisini, wanateta, anaanza Mwalimu Kimpomo: “Mimi Mwaija, Sikudhani,
Sikitu, Chausiku na Kaundime wote tayari.”
Mwalimu
Mong’o anadakia: “Kuanzia form IV na III, nimewazunguka kama sina akili nzuri.
Maslahi yenyewe ya ualimu ubabaishaji mtupu, tutafanyaje zaidi ya kujilipa
mapenzi ya wanafunzi wazuri?”
Mwalimu
Chongo anaunga mkono: “Kweli bwana, inabidi tufidie machungu ya ukapa wa ualimu
kwa watoto wazuri. Ila washkaji tuwe tunapeana signal, isije tukagonganishwa
magari bure!”
Mwalimu
Mkweche anashusha nyepesi: “Hivi mnajua kuwa sasa hivi mwalimu Pili na mwalimu
Maria wana ‘bifu’? Kimenuka nawaambia!”
Mwalimu
Mkangafu anauliza: “Bifu la nini tena, wanagombea bwana?”
Mwalimu
Mbinuko anachangia: “Wewe upo wapi? Shule nzima watu wanajua. Wale wanamgombea
James, yule dogo bishoo wa Form IV anayeimba Bongo Fleva, dogo katembea nao
wote, wamejuana, sasa ni vita, kila mmoja anataka yeye ndiye awe mmiliki wa
penzi la James.”
Usiku
mwalimu Jessica anazungumza kwa simu na mwalimu Sudi, anamwambia: “Ndiyo nini
ulichonifanyia kunichanganya na Salome? Kile kisichana chako cha Fom III? Kwa
taarifa yako nimeshajua kila kitu.”
Asubuhi
mwalimu Jessica akiingia darasani anaamrisha: “Salome toka nje, na kuanzia leo
nisikuone darasani kwenye vipindi vyangu.”
Jioni Salome
anamwandikia SMS mwalimu Jessica: “Najua unanichukia kwa sababu nimekuzidi
ujanja kwa mwalimu Sudi. Tena nikwambie, Sudi hapa kwangu ndiyo kafika, wewe
utaishia kulia, humpati tena.”
Mwalimu
Jessica akiwa anatafakari, mara anapokea SMS nyingine ya Salome: “Utavimba
mpaka upasuke. Sudi hawezi kuwa na wewe tena, mwanamke huna vionjo wala
manjonjo!”
Kisha
mwalimu Jessica naye anajibu: “Sibishani na watoto wasiojua hata kuoga. Sudi
kwako anafanya utafiti tu, mimi ndiye malkia wake.”
Mwalimu
anakatiza mitaani, anakutana na kundi la watoto wakiwa wamevaa
kinyumbaninyumbani, Jose anampa ‘shua’ mwalimu wake: “Leo utakoma kuringa, si
huwa unajifanya mjanja kuniletea unoko shuleni!” Mwalimu anapigwa halafu
anaambiwa: “Usirudie tena kucheza na wahuni wa kitaa!”
Mwalimu mkuu
anafanya mapenzi ofisini kwake, wanafunzi wakiwa nje wanachungulia dirishani na
kuona kila kitu.
Wanafunzi
wakikaa wanasimuliana. Vicheko na simulizi zinakuwa nyingi, kuhusu tukio na
vitendo hatua kwa hatua. Jamani elimu yetu inapokwenda!
Mwalimu
Consolata anamwita Abbas ofisini kwake amwadhibu, Abbas anamchimba mkwara
mwalimu wake: “Thubutu, ukinikomalia kuniadhibu nitasema siri zako zote.”
Mara Abbas
anamwonesha mwalimu Consolata picha yake ya aibu. Mwalimu badala ya kuwa mkali
anambembeleza Abbas kwa zawadi na ahadi. Matokeo ya baadaye ni Abbas kuwa
mpenzi wa mwalimu Consolata. Ni mengi ya aibu kwenye shule zetu.
Mwalimu na
mwanafunzi usiku ‘wanachati’, maswali wanayoulizana: “Umelalaje? Eehhee, umevaa
nini? Hebu jipige selfie hapo kitandani unitumie picha kwa WhatsApp.” Eti
mwanafunzi na mwalimu, hapana jamani, hatukutakiwa kabisa kufika huku!
Wakati
mwingine mwalimu anawafanya wanafunzi wake makuwadi wa kumuunganishia wanafunzi
wa kike. Haya yanatokea jamani!
Mwalimu wa
kike anakuwa na mabwana zake hata watano. Anamtuma mwanafunzi amfuatie pesa kwa
wanaume wake, leo kaenda kwa Paul, kesho Seba, keshokutwa Mathew, mtondogoo
Sam, halafu jana alimtuma kwa Faridi.
Baadaye
mwalimu anakuwa anamuogopa mwanafunzi kuliko hata mwalimu mkuu. Na mwanafunzi
naye akikaa na wenzake anawaambia: “Mwalimu hawezi kufunua mdomo mbele yangu,
najua siri zake kibao na yeye anajua, ndiyo maana ananiogopa.”
Baba kaenda
shule kufuatilia maendeleo ya mwanaye, baadaye mwalimu anamwambia mwanafunzi:
“Baba yako handsome kweli.”
Mtoto naye
anafika nyumbani, anamwambia baba yake: “Daddy eeh, ticha Nuru amekufagilia
sana leo, anasema wewe ni bonge la handsome.”
Baba na
mwana wanaishi kisasa, Uzungu mwingi! Ndivyo walivyoamua iwe mtindo wao wa
maisha. Baada ya muda mtoto anakuwa anatumwa na baba yake kumpelekea zawadi na
fedha mwalimu Nuru. Tayari baba na mwalimu wameshakuwa wapenzi.
Mama naye
kwenda mara moja tu shuleni, tayari kawa mpenzi wa mwalimu. Uhusiano unakwenda
mpaka mtoto anajua. Tena mara kwa mara mama anakwenda shuleni.
Mengine
yanafanyika ofisni. Matokeo yake mtoto ananyimwa raha, wenzake wanamtania:
“Mama yako ni demu wa ticha.”
Wanafunzi
wanasasambua darasani, Mduara unachezeka, mwalimua anamwambia Jamila:
“Nakukubali sana kwa kusasambua, nilikuona darasani, itabidi tufanye kweli.”
Wazazi
wanawaruhusu watoto wao kwenda kwenye Vigodoro usiku, asubuhi darasani ni
mashindano, nani mkali wa kuyakata mauno. Tobaaaa!
Hatuwezi
kukimbilia matokeo bila maandalizi. Na jambo la kwanza na muhimu ni nidhamu,
bila hilo ni utani. Na kama tunataka kuendelea kutaniana sawa, ila ikiwa
tunahitaji mabadiliko, basi yaonekane.
Walimu
waache kuzifanya shule ni eneo la ‘nikamate nichinje’ kama mashindano ya Big
Brother Africa. Heshima ya kweli inahitajika kati ya walimu na wanafunzi ili dhana
ya ufundishaji ipate hadhi yake.
Wazazi
wajiheshimu. Watambue kuwa kuhusika kimapenzi na walimu kwa namna moja au
nyingine kunaifanya saikolojia ya mtoto iwe tenge.
Tukitaka
elimu ipae, lazima kwanza tupigie kelele kwa zingatio “Nidhamu… Nidhamu… Nidhamu.”
Ndimi Luqman
Maloto
Kwanza mfumo
wenyewe ubabaishaji mtupu! Anza darasa la saba, njoo kidato cha nne, ni kwa
nini mwanafunzi aliyekuwa anafanya vizuri darasani siku zote ndoto zake za
kielimu zinaweza kukatika kwa mchujo tu wa mtihani wa mwisho? Nasisitiza mfumo
ubadilike.
Sipingani na
mitihani ya mwisho, lakini lazima kuwepo na utaratibu wa alama za awali.
Mathalani, inakuwepo mitihani ya kidato cha kwanza mpaka cha nne yenye hadhi ya
kitaifa kila mwaka, lengo likiwa kupima maendeleo ya mwanafunzi hatua kwa
hatua.
Mathalan,
katika alama 100, 70 zinakuwa zimekusanywa kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha
nne na 30 ndiyo ambayo inapatikana katika mtihani wa mwisho. Yule ambaye
alikuwa na kawaida ya kufanya vizuri kila mwaka, anaweza kuokoka hata kama
mwishoni aliteleza.
Inawezekana
katika katika mitihani ya nyuma alikuwa na pointi 60, anapopata pointi 15
katika mtihani wa mwisho, anakuwa na jumla ya alama 75. Hata viwango vya ufaulu
vipimwe kwa pointi ambazo mwanafunzi anakuwa amekusanya kuanzia mwaka wa kwanza
mpaka wa mwisho.
Huko nyuma
mwanafunzi wa shule ya msingi alipimwa kwa mtihani wa siku moja tu. Yaani miaka
saba anatoka kwa kwanza darasani mpaka Juni kwenye mitihani ya Moko na nusu
muhula, anaongoza lakini Oktoba anaingia kwenye mitihani ya mwisho, siku
inamkataa. Anafeli. Ndoto zake kielimu zinapotea, anakwenda kukata mkaa!
Kuna watu
wengi ambao walimaanishwa kuwa wakombozi wa nchi hii, waliokuwa tishio darasani
hawakufika hata sekondari kwa sababu ya matokeo ya mwisho darasa la saba. Kama
aliingia kwenye chumba cha mtihani na kupaniki, basi ni tatizo.
Yapo pia
makosa ya usahihishaji. Hili tatizo la uwezo wa wasahihishaji lilishazungumzwa
sana. Wengi walisoma kwa kukariri, alishakariri jawabu kuwa Mnara wa Bismini
upo Mtaa wa Azikiwe, akikutana na jibu la mwanafunzi mwelewa zaidi,
anayefafanua kuwa Bismini ipo kwenye makutano ya Samora na Azikiwe,
anamwandikia kosa.
Ni rahisi
mwananchi wa kawaida kuwaza kuwa pengine kwa sababu watoto wa wakubwa wamekuwa
hawapati wakati mgumu kwenye maisha yao ya kutafuta elimu ndiyo maana matatizo
kama hayo yamekuwa hayazingatiwi.
Kweli watu
hawajiulizi tiba, yaani mitihani ya mwisho haifanywi kama chujio la mwisho,
inakuwa kama sadakalawe, anayepata apate, anayekosa akose. Ikawa sababu ya
wengi hawasomi, wanasibiri mitihani ya mwisho waibe na kukariri majibu ya
kuingia nayo kwenye chumba cha mtihani.
Matokeo yake
tumeshuhudia baadhi ya wanafunzi
wanaofaulu lakini hawajui kusoma wala kuandika. Katika nyakati ambazo hakujawa
na jawabu la kimsingi la wanaofaulu lakini hata majina yao hawawezi kuandika
vizuri, serikali ikashusha viwango vya ufaulu.
Ni janga
kubwa kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika katika zama hizi
zinazoitwa za sayansi na teknolojia. Ni lazima kuutazama vizuri mfumo mzima wa
elimu inayotolewa nchini, ubomolewe na kusukwa upya. Ni ngumu kwa kuwaza na
kujawa na nyoyo zenye kusitasita, ila ni rahisi kama dhamira ya dhati ipo.
Ukosefu wa
hali bora za kimaisha za walimu, maslahi duni, posho za kukijikimu na huduma
nyingine stahiki kama vile afya ya uhakika, ikiwemo suala zima la mishahara, ni mojawapo ya mchango mkubwa wa
elimu ya msingi na ya sekondari kuporomoka. Tunapokataa ukweli tunaichimbia
kaburini elimu yetu.
Kiwango duni
cha kimaisha walichonacho walimu, kinawafanya wafundishe mwanafunzi wakiwa
hawana molari ya kazi na kufanya bora
liende na matokeo yake ni kuwa na kizazi mbumbumbu kutokana na kufundisha bora
elimu kuliko elimu bora.
Lazima
serikali iwekeze kwa walimu kwanza kama tiba kuu ya kupanda kwa elimu,
vinginevyo wanafunzi wataendelea kufeli, kisha maskini watazidi kuangamia,
maana wao ndiyo hawana uwezo wa kupeleka watoto wao kwenye shule za kulipia.
0 comments :
Post a Comment