Luqman Maloto
(+255 713
355 717)
MOSHI mweusi
umefunika Zanzibar, nuru haipo. Kila anayejaribu kufumbua, unajaa machoni,
machozi yanamtoka. Ni nyakati za tafakuri, zile hasa zinazolazimisha kuusujudia
ukweli.
Mwanafasihi
Shannon Alder angesema: “The moment you realize that no one is your enemy,
except yourself.”
Kiswahili:
Nyakati za kuukiri ukweli kuwa hakuna adui yako, isipokuwa wewe mwenyewe.
Huu siyo
wakati wa mapambio. Ni muda wa kushughulika na uhaini. Ajulikane mhaini nani,
Dk Ali Mohamed Shein anayeitwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi wakati hana
serikali?
Je, ni Seif
Sharif Hamad aliyejitangaza mshindi katika kipindi ambacho hata Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec) ilikuwa hata haijakamilisha majumuisho?
Je, mhaini
ni Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Zec, aliyetangaza kufuta matokeo ya
Uchaguzi wa Rais Zanzibar kisinema-sinema?
Tusiache
kuuomba ukweli; Seif alifanya maandalizi gani ya haraka mpaka kukamilisha
majumuisho ya kura kabla ya Zec? Ana rasilimali kuliko Zec?
Jecha ni
marehemu Samuel Kiviutu? Yule aliyekuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Uchaguzi Kenya, aliyemtangaza Mwai Kibaki mshindi Desemba 2007 wakati alizidiwa
kura na Raila Odinga.
Je, Jecha
aliogopa kutangaza matokeo yenye kuonesha Shein ameshindwa ndiyo maana alifuta
matokeo? Au aliyafuta kwa shinikizo la Shein mwenyewe?
Lazima jipu
litumbuliwe; Kuna usahihi upi kuhusu idadi ya kura za Pemba kuwa nyingi kuliko
idadi ya kwenye daftari la Zec? Mchezo umefanywa na nani?
Jecha
alipotangaza kufuta matokeo na kutaka uchaguzi urudiwe, hizo gharama za marudio
zinalipwa na nani? Mfukoni kwake? Serikali tena?
Suala la
dosari za uchaguzi Zanzibar halihitaji kufikirishana, linatakiwa lionekane na
lidhihirike kwa kila mtu. Vigezo vizingatiwe.
Pamoja na
kuonekana, vema ijulikane akina nani wamesababisha madudu. Wachukuliwe hatua.
Watanzania waoneshwe kila kitu na wajue, siyo kukaririshana.
Jecha
ameshindwa kuwafanya Watanzania na pengine dunia yote ielewe kuwa Zanzibar
zilitokea dosari nyingi na kubwa mpaka kusababisha matokeo ya uchaguzi kufutwa.
Tusiache
kujiuliza na maswali haya; Kwa nini Chama cha Wananchi (Cuf), hakitaki kusikia
habari ya marudio ya uchaguzi? Je, kinaona kinadhulumiwa? Haki yake itapotea?
Kilifanya uhuni wa kura ambao kinajua hakitaweza kuurudia? Tuchekeche ubongo
hapa.
Kama kweli
wapigakura ni walewale, Cuf hofu yake inatoka wapi? Si uchaguzi ukirudiwa
walewale watapiga kura? Je, CCM na Shein kama kweli wameshindwa, wanataka
kulazimisha utwala usio na ridhaa ya asilimia kubwa ya wananchi?
Katika somo
la Sayansi ya Siasa (Political Science), legitimacy ni ridhaa ya wengi katika
kuikubali mamlaka. Je, Shein na Seif nani ambaye haheshimu legitimacy? Ni Shein
mwenye kukaa Ikulu kwa mabavu? Ni Seif anautaka urais kwa udanganyifu?
Mwandishi Malcolm
Gladwell, raia wa Canada anaielezea legitimacy kuwa hushamirishwa na mambo
matatu. Mosi ni watu wenye kutakiwa kutii mamlaka, wao wenyewe wajione wanayo
sauti, kwamba wakizungumza wanasikika.
Pili ni
sheria iwe wazi na itabirike, kusiwe na konakona katika masuala kuhusu haki na
sheria. Huyu hukumu yake ni hii mwingine ni ile wakati jambo ni la aina moja.
Tatu ni mamlaka kufanya mambo yake kwa usawa.
Zanzibar
legitimacy inachezewa. Ni jambo lisilo na heshima kwa mtu asiye na legitimacy
kuongoza. Ni utovu wa demokrasia!
Shida kubwa
ambayo imekuwepo Zanzibar ni haki kutoonekana ikitendeka. Tangu mwaka 1995,
kumekuwa na mgawanyiko, Cuf wamekuwa wakidai kushinda uchaguzi kisha kuporwa na
CCM.
Anza na
muhula wa pili wa Dk Salmin Amour (1995-2000), kisha mihula yote miwili ya Dk
Aman Abeid Karume (2000-2010), lipo kundi la Wazanzibar waliona tawala hizo ni
za mabavu.
Ni Shein
kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 ndiye angalau aliheshimika kisawasawa kwa sababu
utawala wake uliridhiwa na Cuf, kisha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
ZANZIBAR
IMEFIKAJE HUKU?
Kiswahili
kinafanya yake, kwamba bandu bandu humaliza gogo, kisha Kiingereza kinajibu, cutting
small chips finishes the log, ni sawa tu na msemo mzaha mzaha hutumbua usaha.
Mwandishi wa
Marekani mwenye asili ya Ukraine, Charles Michael Palahniuk, maarufu kama Chuck
Palahniuk, anasema: “When we don't know who to hate, we hate ourselves.”
Kiswahili:
Tunapokuwa hatujui mtu wa kumchukia, huchukiana sisi wenyewe.
Shida kubwa
iliyopo Zanzibar ni chuki ya “sisi kwa sisi”, na katika eneo hili Cuf na CCM
kwa pamoja wanao mzigo wa lawama ambao lazima waubebe.
Pemba kila
uchaguzi, huubeba kama mchakato wa kudai uhuru wao. Wanajiona kama wanakaliwa
kwa mabavu. Ni kwa nini imekuwa hivyo?
Sasa
jiulize; Ni kwa nini Pemba hupiga kura ya upendo kwa Cuf na chuki kwa CCM?
Wapemba wana nini ndani ya mioyo yao?
Ni kwa nini
misimamo ya Wapemba ipo wazi kabisa kuwa bora kupigia kura jiwe kuliko mgombea bora
wa CCM?
Ni kwa vipi
siasa Pemba zinabebwa kama imani kutoka mbinguni? Kwamba kuwa Cuf ndiyo njia ya
Mungu na CCM ni upagani.
Mwisho sasa
jiulize ni kwa nini dosari za uchaguzi zimetokea Pemba ambako siku zote CCM
hawana chao? Je, Cuf walitumia kiburi kuwa wenyewe ndiyo wanaoshikilia mamlaka
zote za kisiwa hicho kuongeza kura za wizi?
Je, Cuf
walijua kuwa hawawezi kuongoza kwa kura nyingi Unguja hivyo kujijazia kura
Pemba ili zifidie upungufu wa Unguja na kushinda? Au CCM wanaamua kutafuta
kisingizio kama ilivyo mfa maji na kutapatapa?
Ni kwa nini
Jecha hakufuta matokeo haraka baada ya kugundua dosari na kusubiri dakika za
mwishoni? CCM wenyewe ndiyo wataalam wa mizungu ya uchaguzi, ilikuwaje wakaibiwa
kura na Cuf ambao wamejifunzia siasa kutoka kwao?
Zanzibar
isitazamwe kwa jicho la siasa peke yake. Acha mhemuko, achana na siasa za Cuf
na CCM, kisha itazame kwa jicho dadisi, dodosa historia, mwisho utapata jibu
kuwa hatari iliyopo ni zaidi ya inavyonenwa.
Watu
hawajiulizi ni kwa nini Uchaguzi Mkuu 2015, wimbo ulioimbwa sana ulihusu
Zanzibar na Mamlaka Kamili? Nini kilichokuwa kinatafutwa? Mamlaka kamili kutoka
wapi kama siyo Tanganyika?
Ni kwa nini
wapo Wazanzibar wanaishi nje na hawataki kurudi nyumbani kwa madai kuwa nchi
yao imekaliwa kwa mabavu na Tanganyika?
Chuki hii
dhidi ya muungano nani aliianzisha? Na kwa nini Seikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa muda mrefu imepoteza umaarufu (popularity) Zanzibar, hususan
Pemba?
Nani hajui?
Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya kuundwa kwa Katiba Mpya, Zanzibar
kulikuwa na harakati za kutaka sauti ya Wazanzibar isikike kuhusu uhai wa
muungano.
Walitakiwa
kuchagua miongoni mwa mambo matatu. Mosi muungano uendelee kama ulivyo. Pili
muungano uwepo wa mkataba. Tatu waachwe wapumue. Kwa kunukuu “watuache
tupumue.”
Wenye kauli
“watuache tupumue” ndiyo hao waliomzunguka Seif. Mpaza sauti mkuu alikuwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Cuf, Ismail Jussa Ladhu.
Je, hili
nalo ni la kupuuzwa? Wanawezaje kusema waachwe wapumue kama hawajioni
wanaminywa mpaka wanashindwa kupumua? Lazima chuki ya Zanzibar ishughulikiwe
kwa viwango vyake.
Wala Zanzibar
shida siyo maendeleo. Katika miaka 20 ya CCM kutokukubalika Pemba, kumekuwa na
jitihada nyingi za kupeleka maendeleo yenye kuonekana kisiwani humo. Shein pia
kwa miaka yake mitano amejitahidi mno.
Kuna zaidi
ya siasa, na ndiyo inayotakiwa imulikwe. Mchezo wa kuzunguka kichaka hautakiwi.
Ni lazima kuingia katikati na kumkabili adui.
Zanzibar
ilipofikia na kule iendako haipaswi kutazamwa kwa jicho la siasa za kawaida.
Taswira yake inatakiwa iangaliwe katika macho yenye kuona mbali. Macho yenye
tiba na suluhu ya ukakika. Maana Zanzibar hakuna mgogoro wa kisiasa, kuna
chuki.
Siyo
kuitazama kwa jicho la uchaguzi kurudiwa au Seif kutangazwa kuwa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hali halisi inataka Zanzibar iangaliwe kwa
jicho la tiba. Tiba mahsusi, tiba ya kudumu!
Hali ilivyo
sasa ni kuwa unapoiondoa Tanganyika, hutaikuta Zanzibar, bali vitakuwepo visiwa
vya Unguja na Pemba. Kama watu hawathubutu kuwaza hili basi wanafanya kosa
kubwa mno la kiufundi.
Unapoutazama
ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unapata jawabu kuwa ipo kazi ya
kufanya kuhakikisha kuwa Wazanzibar na Watanganyika kwa pamoja wanaufurahia
muungano wao.
Lipo jukumu
la kutekeleza kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna kazi ambayo
haihitaji kupuuzwa. Hii inahusu maoni ya walio wengi kuhusu kuendelezwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wachache pia
wasikilizwe, nini kinachowauma? Mbegu ipi imepandikizwa kwenye nyoyo zao? Mbona
Shein ni Mpemba mwenzao lakini hiyo haijawafanya wakikumbatie Chama Cha
Mapinduzi?
Hapo unapata
jawabu kuwa hoja siyo Upemba, sasa kuna nini kingine? Tuzame katikati ya
kichaka! Tusikariri majibu wala hatutakiwi kuongozwa na dhana.
Tusipuuze
ile hoja ya kuwa kuna malodi Uarabuni wanaifuatilia Zanzibar mithili ya fisi
anavyoumendea mkono wa binadam kwa nyuma akiamini utaanguka ale kitoweo.
Kwamba
malodi waliopo Uarabuni shida yao kubwa ni kuona muungano unavunjika na
Zanzibar inakuwa jamhuri kamili. Baada ya hapo ndipo waanze kufaidi rasilimali
za Wazanzibar.
Inaelezwa
kuwa sasa hivi wanashindwa kuzifikia mali za Wazanzibar kwa sababu visiwa hivyo
vimeatamiwa na Tanganyika. Kila hoja itazamwe kwa upana wake. Na hapa ukweli
upo wapi?
Je, ni kweli
kuwa chuki za Wapemba kwa CCM nyuma yake kuna mkono wa malodi wa Uarabuni?
Hawalitaki zimwi linalowajua, wanataka jipya.
Hoja ya
ugaidi inazungumzwa pia, nayo ipewe nafasi. Eti Zanzibar ikiachwa peke yake,
magaidi watavifanya visiwa hivyo kuwa ngome yao ya kujitanua, hivyo kutanua
wigo wa magaidi katika Pwani ya Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa jumla.
Hofu hii
inathibitishwaje? Kwa nini yawe maisha kama unajimu wa marehemu Sheikh Yahya
Hussein?
Na kama ni
kweli hofu hiyo ipo na CCM wanaogopa kuwapa Cuf Zanzibar waitawale, sasa
uchaguzi unafanyika wa nini? Kutumia fedha za walalahoi kufanya uchaguzi ambao
matokeo kinzani kwa CCM hayataheshimiwa ni ufisadi.
Je, ni
uchaguzi wa marembo kuzionesha jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania kuna
demokrasia? Tiba mahsusi ni ile ambayo inatolewa baada ya mgonjwa kupimwa na
kugundulika anachoumwa. Zanzibar inahitaji vipimo.
Usifanye
kosa kubwa kwa kusahau kuhusu uwepo wa hofu ya kutaabika baada ya matokeo
(aftermath). Kwamba Waunguja wamekuwa wakifaidi zaidi keki ya Zanzibar kuliko
Wapemba tangu Muingereza na Sultan wake walipotimuliwa.
Kwamba
Waunguja wameshawafanyia mambo mengi ya hovyo Wapemba. Kwa maana hiyo wanahofia
kisasi baada ya Seif kukabidhiwa nchi.
Kwamba
malodi (elites) wa Unguja ndani ya CCM, wameshafanya matukio ya kuwafunga jela,
kuwadhalilisha vigogo wa Cuf, wapo waliopata ulemavu wa maisha na hata baadhi
kufariki dunia, hofu ipo kuwa je kisasi kitalipwa?
Seif
alitamka kuwa hakuna kisasi kwenye misamiati yake kichwani lakini nani anaamini
kuwa hatageuka baada ya kukabidhiwa rungu? Kila dhana itazamwe kwa uzito wake.
Lingine ni
kuhusu afya ya muungano, inadaiwa kuwa hofu kubwa ni kuwa Seif akipewa Zanzibar
ataleta usumbufu wa kutaka muungano ufe. Tunapaswa kushiba hoja nyoofu. Je,
hili lina uzani gani katika uhalisi wa jambo?
KUHUSU
MUUNGANO
Kila upande
hautakiwi kuwa kipofu, moja ya tunu bora kama Watanzania ni uwepo wa muungano
kati ya Tanganyika na Zanzibar. Matatizo yashughulikiwe kinagaubaga.
Hata hivyo, hatutakiwa kusahau kuwa zipo dola
zilizoungana, zilizokuwa na nguvu kubwa ya kijeshi, kirasilimali na kimamlaka
lakini ziligawanyika vipandevipande. Upo wapi Muungano wa USSR, yaani Jamhuri
za Kijamaa za Sovieti?
USSR
walifikia uwezo mpaka wa kumiliki nyuklia. Urusi haikuwa yenye kukamatika
ulimwenguni. Ni USSR na Marekani pekee zilizotamba kiuchumi na kijeshi duniani baada
ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Urusi kama
baba mwenye nyumba wa USSR, inabaki kulaumu kuwa iliangushwa kwa sababu ya vita
ya ubebari na ujamaa. Marekani bepari mkuu na Urusi baba wa ujamaa.
Ukweli upewe
heshima yake kuwa hata kama Marekani ilihusika kuiparanganyisha USSR lakini
sababu ni matundu ambayo Urusi iliyatengeneza yenyewe. Kwamba dola nyingi
ziliona zinapunjwa, kwamba Urusi ilizitumia kujiimarisha.
Hii dhana ya
Tanzania Bara kuonekana kama inaitumia Zanzibar kujiimarisha haipaswi kuachwa
ikatawala kwenye vichwa vya watu. Ni tatizo kubwa!
Wanandoa
wenye maelewano huwa hawafarakanishwi na maneno ya pembeni. Ila neno la
uchonganishi hupata nguvu kwenye ndoa ya watu wenye migongano. Marekani
walifanikiwa kuiua USSR kwa sababu wao wenyewe ndani kwa ndani walikuwa na
migongano.
Ulikuwepo
muungano mzuri wa kijamaa wa Czechoslovakia, ulikwenda na maji kisha kuacha
nchi mbili Jamhuri ya Czech na Slovakia, sababu ni kama zinazosemwa kuhusu
Zanzibar na Tanganyika. Slovakia iliona Czech inanufaika kuliko yenyewe.
Rejea kwenye
kifo cha muungano wa Dola ya Yugoslavia kisha uone kuwa Tanganyika na Zanzibar
inaweza kuifanya Tanzania isiwepo. Muhimu ni kutambua kuwa heshima ya muungano
lazima izingatie mahitaji na matakwa ya kila upande.
Naiona hofu
kuu kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi katika kuifanya
Zanzibar iwepo kama dola moja. Kinyume chake zitakuwepo dola mbili, ile ya
Unguja na Pemba. Maana hawaaminiani kwa sababu hawapendani, na wasiopendana
huchukiana.
Mimi ni
mjumbe tu, nafikisha, maana atangazaye mirimo si mwana wa ruwari (mjumbe
hauawi). Mvumo wa Zanzibar unanipa hofu. Tusiache kukumbuka matukio ya Januari
26 na 27, 2001. Watu walikufa, wengine wakawa wakimbizi. Chanzo kilikuwa
uchaguzi. Atambaaye na nyasi, mtambulie ni nyoka!
Baada ya
Mwafaka wa Zanzibar wa mwaka 2001, wengi walisema “tusahau yaliyopita tugange
yajayo” lakini aliyekuwa Mwenyekiti wa Cuf, Prof Ibrahim Lipumba alisema:
“Tunasamehe lakini hatupaswi kusahau, tukisahau yatajirudia.” Naona kweli watu
wamesahau, na yapo njiani kujirudia!
Rais wa
Urusi Vladimir Putin anasema: “Whoever does not miss the Soviet Union has no
heart. Whoever wants it back has no brain.”
Kiswahili:
Yeyote ambaye haukumbuki wa Umoja wa Soviet hana moyo. Yeyote anayetaka umoja
huo urejee hana ubongo.
Tusipoona
mbali Tanzania itafika zama hizo za kutoa matamshi kama ya Putin, nyakati
ambazo haitwezekana tena kuuhuisha Umoja wa Tanganyika na Zanzibar. Umakini
unahitajika. Upendo uishi ndani yetu, haki iheshimiwe.
0 comments :
Post a Comment