ads 728x90 B

Ukimuoa mwanamke kama Doris Fisher lazima utajirike




Luqman Maloto

JIWEKE karibu na Mungu unapotaka kufunga ndoa. Omba mwenzi sahihi ambaye ataleta msisimko wa mafanikio katika maisha yako.
Hata siku moja usije ukapuuza kuwa mwenzi wa maisha yako ni lazima aendane na maono yako. Hutakiwi kupishana na mwenzi wako katika maisha ya ndoa.
Ndoa bora ni ile yenye nuru. Ile iletayo mabadiliko ya kimaisha. Ulikuwa peke yako, kwa hiyo mnakuwa wawili, hivyo kipato kinaongezeka.
Mawazo ya wawili si sawa na wazo la mmoja. Na hiyo ndiyo imekuwa sababu ya mafanikio makubwa kwa familia ambazo mume na mke wanaishi kwa maelewano makubwa.
Chukua pointi hii; Kati ya sababu mbalimbali ambazo zinaweza kumfanya mtu ashindwe kufanikiwa maishani, kubwa zaidi ni kukosea kuchagua mwenzi wa maisha.
Unahitaji mwenzi mpenda maendeleo na aliye na nidhamu ya maisha. Mbunifu anayewaza mbali. Mwelewa na mwenye kukutia moyo ili uzidi kuyasogelea mafanikio.
Muhimu zaidi ni awe unaeyeendana naye. Maelewano yalete raha ndani ya ndoa na kila mmoja ajione yupo salama dhidi ya mwenzake.
Yote yanaweza kufaa lakini utamu wa ndoa hudhihirika pale mume na mke wanapokuwa marafiki wakubwa. Wanazungumza na kubadilishana mawazo vizuri. Wanafanya mizunguko yao pamoja. Kila mtu anakuwa huru kuzungumza neno lake kisha mwenzake anasikiliza na kupokea.
Doris Fisher ni mwanamke shujaa. Mawazo yake mazuri yameweza kuitetea familia yake na kuifanya isimame kifua mbele duniani.
Hata hivyo, asingefanikiwa au kupata heshima aliyonayo sasa hivi kama yeye na mume wake wasingekuwa na maelewano.
Doris ni tajiri, ni bilionea kwa dola na Kitanzania ni trilionea wa shilingi. Tumbo lake lilibeba watoto watatu ambao sasa ni mababa na wote ni matajiri wakubwa.
Jarida maarufu la Forbes ambalo linaheshimika kwa utafiti na utoaji wa takwimu mbalimbali ulimwenguni, linamtaja Doris kuwa mmoja wa wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani.
Doris ndiye mama wa Kampuni ya The Gap, Inc. ikizoeleka zaidi kama Gap Inc. ambayo ni maarufu ulimwenguni kwa utengenezaji na uuzaji wa mavazi kwa jumla na rejareja.
Toa heshima kwa Gap kama kampuni ambayo takwimu za mwaka 2014 ziliitaja kuwa na waajiriwa 135,000. Vilevile mtandao wake wa kutengeneza ajira ulimwenguni kote ni mkubwa mno.
Ipe heshima Gap kwa sababu takwimu zinaonesha kuwa mwaka jana, kampuni hiyo ilitengeneza mapato ya dola bilioni 16.148 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 34.377.
Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2015-2016 ni shilingi trilioni 23. Hivyo, mapato ya Gap kwa mwaka mmoja yanatosha kuendesha serikali ya nchi yetu na chenji ya kutosha.
Fanya hesabu ya harakaharaka, unapata shilingi trilioni 11.377 ambayo inabaki na hiyo inatosha kulifanya Jiji la Dar es Salaam kujaa barabara za juu (overpass) ambazo kwa lugha ya Kijumuiya ya Madola, zinatambulika zaidi kama flyover.
Kama Doris ameweza kufanikisha matokeo hayo, ni kwa nini asiitwe shujaa? Ongezea pointi hii kwamba mwanaume yeyote mwelewa anapompata mwanamke kama Doris lazima afanikiwe.
Ipo ile kanuni yangu kuwa Mke Bora + Mume Mwelewa = Familia Tajiri. Doris alikutana na mumewe mwenye uelewa hasa, hivyo kutengeneza utajiri ambao unaitikisa dunia hivi sasa.
Doris alikuwa mke wa Donald Fisher ambaye alifariki dunia Septemba 27, 2009. Walikuwa wakiishi kawaida tu. Lakini maisha yao yalitawaliwa na upendo wenye kuthibitika ndani ya mioyo yao na kuonekana machoni kwao.
Kutokana na upendo huo, walijadiliana aina ya mavazi na vipimo, vilevile walikwenda kwenye manunuzi pamoja.
Kwa vile walikuwa karibu mno, ilikuwa rahisi hata kujadiliana changamoto zao kwa ukaribu.
Walipokuwa wananunua nguo, waligundua kwamba kupata jeans ya vipimo vyao ni tatizo. Maana walikuwa wakihangaika sana.
Doris alifanya utafiti na kugundua kuwa tatizo la vipimo vya jeans halikuwa lao tu, bali liliwagusa wengine wengi.
Kupitia changamoto hiyo, Doris alipata wazo la kuanzisha kampuni ya kuuza mavazi yenye wigo mpana wa vipimo ili kila mtu aweze kuvaa nguo nzuri bila bughudha wala masharti.
Alikaa na mumewe (Donald), wakajadiliana kuhusu wazo hilo, wakakubaliana vizuri lakini mume akawa na wasiwasi, Doris akamwambia inawezekana.
Wazo kuu ambalo Doris alikuwa nalo ni kuhakikisha kampuni yao inakuwa na vitu mbalimbali vya mauzo ya nguo, vikiwa katika vipimo tofautitofauti ili kurahisisha kila mtu kupata vazi la ‘saizi’ yake.
Doris alikuwa na wazo la baadaye kwamba kampuni yao ikishakuwa watakuwa wanauza mavazi yenye nembo (chata) zao. Lakini kwa kuanzia, ilibidi waingize sokoni chata za wengine.
Kutokana na uwezo wao kuwa mdogo, walianza kudunduliza fedha ili wapate uwezo wa kufungua vituo vya mauzo ya Gap. Walifanikiwa kukusanya kiasi cha dola 63,000.
Walipopata fedha hizo, ndiyo ikawa mwanzo wa kuukimbilia utajiri kwa kasi ya juu mno. Kasi ambayo imesababisha mapinduzi makubwa kwa upande wa mauzo ya nguo ulimwenguni.
Agosti 21, 1969, Doris na Donald walifungua kituo cha kwanza cha mauzo ya mavazi ya Gap, eneo la Ocean Avenue, San Francisco, Marekani na kupata mafanikio ya harakaharaka.
Kwa vile hawakuwa na chata ya kuisimamia, walinza mauzo kwa kufanya makubaliano na kampuni ya Levi's pamoja na LP records. Katika mwaka wa kwanza tu, walipopiga mahesabu, waligundua kumbe walichelewa mno kuanzisha biashara hiyo, kwani inalipa vizuri kabisa.
Mwaka wa pili wa biashara, waliweza kufanya mauzo yenye thamani ya dola milioni 2, ambazo ukibadili kwa sarafu ya shilingi kutokana na thamani ya sasa, utapata zaidi ya bilioni 4.
Ikabidi waanze kujitanua. Mwaka 1970 baada ya kuuza mavazi kwa dola milioni 2, Gap iliongeza kituo cha pili mjini San Jose, California.
Mwaka 1971, Gap ilitambulisha makao makuu yake mjini Burlingame, California, ikiwa na wafanyakazi (waajiriwa) wanne tu. Hapa ni kuona namna ambavyo watu huanza mbali.
Mwaka 1973, tayari kampuni ilikuwa imeshakuwa zaidi, kwani iliweza kumiliki vituo zaidi ya 25. Kutanuka huko kuliweza kufika mpaka Pwani ya Mashariki (East Coast).
Ndani ya East Coast, walifungua kituo kikubwa kwenye jengo la biashara la Echelon Mall, Voorhees, New Jersey.
Ilipofika mwaka 1974, Gap ilianza kuuza mavazi yenye nembo yake yenyewe.
Kimsingi ukuaji huo wa Gap ni kutokana na juhudi za Doris. Kwamba hakuishia tu kutoa wazo, alihakikisha anashirikiana vizuri na mume wake, hivyo kuishinda shere ya umaskini.
Hapo unapaswa kuzingatia kuwa Doris ndiye hasa mbunifu wa wazo la kuuza mavazi. Hakuishia hapo, alishiriki kutafuta mtaji na walikuwa bega kwa bega kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.
Pointi hii inampambanua Doris kama mwanamke kichwa. Na ndiyo maana tumbo lake pia limebeba watoto matajiri leo hii. Baba na mama matajiri, watoto wanapita njia hiyohiyo, hakuna aliyetoka kwenye mstari.
Mafanikio ya wanaye, unaweza kuyachukua na kumjaza Doris kama mama mlezi bora. Familia nyingi hukosa msimamo kutokana na malezi ya watoto.
Hili liongezee kuwa Doris ni mama bora, msaka fedha mwenye kiu. Zaidi ya yote ni mama anayejitambua.
Doris akiwa mkurugenzi, Donald akiwa mwenyekiti wa Gap, walifanya kazi kubwa mno ambayo imewafanya wote wawe mashujaa.
Kama isemavyo Biblia Takatifu katika Mithali 13:22:  “Mtu mwema huacha akiba kwa wana wa wanawe.”
Mantiki hapo ni kuwa mtu mwema huwa anaacha urithi kwa wanawe na wana wa wanawe, yaani baraka za wema wake zinaweza kufikia hadi kwenye kizazi cha wanawe.
Huo ni muongozo wa maandiko kuwa kila mtu ni lazima atafute mali na aziache ili wajukuu wake waje kuziona. Huo ndiyo msingi bora wa maisha kwa kila mmoja.
Na kwa hoja hiyo, Doris ameweza kuwa mtu bora hata katika maandiko maana amefanikiwa kuacha utajiri mkubwa ambao wanaye na wajukuu zake wanaufaidi.
Gap ilikuwa chini ya Donald na Doris tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969 mpaka mwaka 2004, walipokabidhi mamlaka kwa mtoto wao mkubwa, Robert Fisher, akijulikana zaidi kama Bob Fisher.
Robert akiwa mwenyekiti wa Gap, Donald na Doris walibaki ndani ya bodi ya wakurugenzi, wakihusika zaidi katika ushauri, lakini masuala yote ya uongozi kiutendaji waliyaacha kwa Bob na watoto wao wengine.
USHUJAA WA DORIS
Kwa kuweka rekodi sawa, ushujaa wa Doris unaonekana katika mambo matatu, ambayo ni ubunifu wake, kufikiria kama tatizo walilokuwa nalo la kupata jeans zenye kuwatosha linaweza kuwa mtaji wa wao kugeuka wawekezaji wakubwa katika soko la mavazi.
Pili ni kusimama kwake kama mama, kwamba alitambua wajibu wake kama mke ni kumuweka mume wake karibu, kuwa marafiki na ndiyo maana waliweza kushauriana mambo hayo ambayo yamegeuka faida kubwa kwao.
Tatu ni usimamizi wa fedha na uongozi. Doris akisimama kama mkurugenzi mtendaji wa Gap, alikuwa kiungo muhimu kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kulingana na malengo.
Hata Donald kabla hajafariki dunia, aliwahi kukaririwa akisema: “Mafanikio ya Gap ni Doris, ni mke bora. Ni mama wa familia na ni mama wa Gap. Tusingepata mafanikio haya kama tusingekuwa pamoja kama mke na mume.”
Doris katika moja ya nukuu zake anasema: “Mwanamke mzuri na una akili nzuri unapompata mwanaume mzuri ni kwa nini usiwe bilionea? Bahati kubwa katika maisha yangu ni kwamba nimeolewa na mwanaume muungwana.
“Ningekuwa wa ajabu sana kama nisingefanikiwa wakati nipo na Donald. Hiyo pia ipo kwa Donald, angekuwa mtu wa hovyo kama asingetajirika wakati yupo na mimi. Hiyo ni kumaanisha kuwa mafanikio kwa familia yanatokana na aina ya wahusika.”
Kingine ambacho amewahi kukizungumza ni hiki: “Mume na mke lazima washirikiane, wazungumze mambo mbalimbali. Kila mmoja ajione yupo huru kusema chochote mbele ya mwenzake.
“Uhuru ambao watu hupeana ndiyo hurahisisha mafanikio ya pamoja, maana mtu akiwa na wazo anajisikia huru kumshirikisha mwenzake kama mtu wa kwanza kabla ya mwingine yoyote.”
CHUKUA HII
Mke na mume ambao hawatenganishwi na chochote katikati ni wale ambao  nyoyo zao zipo karibu. Mtu anaweza kuwa Bosnia na mwenzake Somalia lakini wakawa karibu sana moyoni.
Siku zote jitahidi kumuweka mwenzi wako karibu moyoni, siyo ukaribu wa miili. Kama hujamuweka moyoni, hata umuweke karibu kiasi gani, mafanikio hayatakuwepo.
Wanandoa na wapenzi ambao wamekuwa karibu moyoni wamekuwa na mafanikio makubwa kimaisha na kiuhusiano lakini wale wenye ukaribu wa viwiliwili, hupata usumbufu mkubwa kwenye maisha yao.
MIZIZI YA DORIS
Doris ana umri wa miaka 84 hivi sasa. Watoto wake wote ni watu wazima. Kila mmoja ana familia yake nzuri. Na hapo ndipo unapoweza kuona matunda ambayo Doris aliyaweka kwenye maisha yake na kizazi chake chote.
Mtoto wake wa kwanza, Bob ndiye bosi mkuu wa Gap. Amekuwa na mikoba ya usimamizi wa mali zote kwa niaba ya familia yao.
Kutokana na majukumu hayo, Bob amekuwa akipata mshahara mkubwa lakini wakati huohuo akibaki mwana hisa wa Gap, kama ilivyo kwa ndugu zake wengine.
Bob alizaliwa Agosti 26, 1954, ana umri wa miaka 61 kwa sasa. Na alianza kukuzwa kibiashara na uongozi wa kampuni na wazazi wake tangu akiwa kijana mdogo kabisa.
Mwaka 1990, Bob akiwa na umri wa 36 aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kampuni, kipindi ambacho Doris alianza kujipunguzia majukumu ya kiutendaji ili kuyakasimisha kwa watoto wake.
Wakati akiandaliwa kuwa mkuu wa kampuni baada ya wazazi wake, Bob aliteuliwa kushika nafasi mbalimbali. Na alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi kati ya mwaka 2004-2007 kabla ya kuwa mwenyekiti wa kampuni nzima kiutendaji (mwenyekiti mtendaji).
Mtoto wa pili wa Doris ni William Fisher, alizaliwa mwaka 1958, umri wake ni miaka 57. Ni mkurugenzi wa Gap tangu mwaka 2009. Kutokana na mafanikio ambayo ameyapata, aliamua kuanzisha kampuni nyingine inayoitwa Manzanita Capital Limited.
Katika kampuni hiyo ya Manzanita, William ndiye ofisa mtendaji mkuu. Hii inamfanya kuwa na majukumu makubwa, kwani Manzanita ni kampuni kubwa ambayo inajihusisha zaidi na uwekezaji wa masoko katika biashara mpya, utafiti na ushauri kwa wajasiriamali.
Mtoto wa mwisho wa Doris ni John Fisher ambaye alizaliwa Juni Mosi, 1961. Huyu naye ni mfanyabiashara. Ni mmoja wa wajumbe katika bodi ya wakurugenzi ya Gap.
Hata hivyo, John amekuwa akisaka mafanikio ya peke yake na kutokana na gawio ambalo hupata kutokana na biashara za Gap, ameweza kuwekeza kwenye michezo na kwa sasa ni mmoja wa wamiliki wa Klabu ya Oakland Athletics inayoshiriki Ligi Kuu ya Baseball nchini Marekani.
John pia ni mmoja wa wamiliki wa Klabu ya San Jose Earthquakes, inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Marekani. John vilevile ni mwanahisa mkubwa katika Klabu ya Soka ya Celtic inayoshiriki Ligi Kuu ya Scotland.
Ukiangalia umri wao wote, unaona kuwa watoto wa Doris tayari wana wajukuu. Hivyo, hata kesho Mungu akimchukua, atakuwa amefanikisha kuacha utajiri ambao umeweza kuonwa mpaka na wajukuu wa watoto wake.
Kwa maana hiyo, amezidi ule ubora ambao Mungu ameuweka kwa wanadamu kama ilivyoelezwa kwenye Mithali 13:22, kuwa mtu bora huwaachia urithi wana wa watoto wake, lakini yeye amefikisha mpaka wana wa wajukuu zake.
CHUKUA MTAJI HUU
Kutoka kwa Doris, unachotakiwa kushika ni kuwa hakikisha unatafuta mwenzi bora wa maisha yako ambaye mtasikilizana. Mfanye kuwa mshirika wako wa kwanza. Jadiliana naye mambo ya mafanikio pamoja na mawazo mapya.
Lile wazo ambalo mtaona linafaa, hakikisha mnalipa kipaumbele na mnashirikiana kufanikiwa. Mke bora siku zote huonekana ndani ya mafanikio yake binafsi na hata yale ya mume wake.
Iwe ni mafanikio binafsi au ya mume, au ya wote, hesabu ni mafanikio ya familia. Hivyo basi hakikisha mnashirikiana inavyotakiwa ili kujenga maisha yenye kuonesha ushujaa wako. Doris ni mama shujaa!

Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment