Na Luqman
Maloto
POKEA ukweli
huu kuwa yote yanawezekana, silaha kubwa ni juhudi zako bila kusahau sala kwa
Mungu wako ili akufanikishie malengo yako. Hakikisha unazo ndoto kisha uzifanye
ziwe hai kwa kujituma kuzitimiza.
Ukiwa na
ndoto hakikisha unakuwa na maono. Ndoto na maono (Dream and Vision) kwa pamoja
huzaa msisimko wa kuyaona matarajio, hivyo kuchochea juhudi ya kufikia malengo.
Unaota kuwa
nani? Jibu la swali lako ni juhudi zako. Utayari wa Mungu ni mkubwa siku zote
katika kufanikisha yale mahitaji mema ya waja wake. Wewe ni mja mwema,
unachokitaka ni kitu chema, basi usikate tamaa! Mbele za Mungu yote yatatimia!
Kingine
ambacho unatakiwa kuzingatia ni njia za kupita. Barabara ya mtu anayeota kuwa
mfanyabiashara mkubwa haifanani na ile ya mwanasiasa anayeutamani uongozi
mkubwa kwa nchi.
Kama malengo
yako ni kuwa mwandishi mkubwa vema sasa utaratibu wako wa kuenenda ufanane na
uandishi. Haiwezekani mtu anayetaka kuwa rubani au daktari bingwa, akawa
anatumia muda mwingi wa ujana wake katika harakati za kisiasa, huko ni kupoteza
muda.
Somo
hilohilo liendane pia wanamuziki, waigizaji, wanamichezo na fani nyingine zote.
Ukitaka kufanikiwa katika eneo lako ambalo unaliota, vema kuzitambua njia zake
na uzipite. Usichanganye utaratibu!
Felix
Mkosamali alikuwa kijana maskini, mdogo kabisa akiwa na umri wa miaka 24 tu.
Akiwa bado anasoma shahada ya kwanza ya sheria Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustine (Saut), Mwanza. Aliona hiyo haimzuii kutimiza ndoto zake.
Mwaka 2010, Mkosamali
aligombea ubunge Jimbo la Muhambwe, Wilaya ya Kibondo, Kigoma (NCCR-Mageuzi) na
kushinda. Siyo yeye wa kwanza, wapo wengi tu na umaskini wao wameweza kushika
nafasi za juu za uongozi. Hata Barack Obama aliwezaje kuwa Rais wa Marekani?
Sema hata kwako inawezekana!
Wewe ni
mwanamke na unataka uongozi? Mtazame Wendy Russell Davis kama kioo chako.
Tambua kuwa mtu kuibuka mpaka kuwa mashuhuri katika siasa za Marekani siyo kitu
kidogo. Wendy ameweza!
Sifa ya
Wendy kuwa kioo cha mwanamke anayesaka uongozi wa kisiasa, haitokani na kwamba
amefanikiwa katika taifa kubwa la Marekani, hapana hata kidogo! Utukufu wa
Wendy ni jinsi alivyoibadili sura ya Kutowezekana kuwa Inawezekana (the
impossible getting done).
Wendy ni
binti wa kimaskini, akiwa na umri wa miaka 19 alipewa mimba akawa mama wa
watoto wawili. Hakuweza kufika chuo. Alijitahidi kujisomesha lakini maisha
yalimchapa na chuo aliacha. Ila hakupoteza njia yake.
Imewatokea
wengi kujikuta wakipoteza uelekeo pale mambo yanapowaendea ndivyo sivyo.
Alitaka kuwa mtaalam wa sayansi ya kompyuta (computer science), baada ya
kukutana na changamoto za maisha, anaamua kusaliti ndoto zake, anaamua kuwa
dereva wa malori.
Usipoteze
ndoto! Wendy alitaka kuwa mwanasiasa mkubwa Marekani lakini kufika kiwango
alichotaka haikuwa kazi rahisi. Muhimu kushika ni kuwa dhamira inalipa. Amini
kuwa chochote unachokidhamiria ndani kabisa ya maisha yako, kitawezekana kama
tu hutayumba.
Ni msemo
wenye kunyooka kuwa penye nia pana njia. Tambua kuwa inaanza nia kisha njia
ndiyo inapatikana. Wendy aliona kila ugumu katika nyakati za ugumu wa maisha
yake. Ni kweli maisha yake yalikuwa gizani, akawa hauoni mlango wa kutokea,
lakini alipambana kuutafuta mlango muhimu kwa ajili ya ndoto zake.
Mlango wa
kupita kuelekea kwenye mafanikio yake. Na hapa ndipo nguvu ya ndoto
inapothibitika. Uwezo wa maono. Kipawa cha mwenye dhamira kinapodhihirika.
Vilevile ukubwa anaoweza kuwa nao yule muota ndoto.
WENDY
AMEFANIKIWA VIPI?
Ni ukweli
kuwa maisha ya kisiasa ya Wendy, ndani ya chama chake cha Democrats na Marekani
yote kwa jumla, yana heshima kubwa. Ila nyakati zake za utoto, aliteseka mno.
Si rahisi kuamini kuwa ameweza kufika alipo sasa.
Wendy
alikuwa mmoja wa watoto wanne. Wazazi wake walipotengana, mama yao alilazimika
kuwalea katika hali duni aliyokuwa nayo. Mama yake alifanya vibarua vya hapa na
pale ili kupata fedha za kuwahudumia watoto wake, akiwemo yeye mwenyewe Wendy.
Kutokana na
ugumu wa maisha uliokuwepo nyumbani kwao, Wendy alijikuta anapoteza umakini
katika masomo yake. Akiwa high school, alifeli. Alipokuwa na umri wa miaka 18,
aliolewa. Alikimbilia ndoa ili kujaribu kupata nafuu ya maisha, maana nyumbani
kwao palikuwa ‘pangu pakavu’ kwelikweli.
Baada ya
kufunga ndoa alijifungua mtoto wake wa kwanza lakini Wendy akiwa na umri wa
miaka 19, alitengana na mumewe. Hapo maisha yakawa magumu zaidi. Maana akawa
mama wa mtoto, bila kazi. Afadhali mwanzoni alipokuwa bila mtoto.
Kitendo cha
kurejea nyumbani, kulimfanya mama yake ayumbe kwa kiasi kikubwa. Maana Wendy
alihudumiwa yeye pamoja na mtoto wake. Zingatia kuwa makazi pia hayakuwa ya
uhakika. Mara leo wanaishi hapa, siku nyingine kwingine.
Wendy
mwenyewe anasema: “Yalikuwa maisha yenye kuumiza sana. Sikuwa na uhakika wa
kuiona kesho yenye uzuri wake. Niliumizwa sana na mtoto wangu, na nilitamani
sana kuona kunakuwa na mabadiliko katika maisha yetu. Imani yangu ni kuwa
kwenye kila giza, nuru hutokeza baadaye.
“Niliamini
kuwa ipo nuru kwa ajili yetu, kama familia, mama yangu na ndugu zangu.
Niliamini kuwa ipo nuru kwa ajili yangu, mimi binafsi na mtoto wangu. Kama kuna
kitu ambacho naweza kujisifu ni kutoka tamaa. Niliamini ushindi upo.”
Wendy
anasema: “Niliamini ipo siku nitakuja kuwa kiongozi, sikujua nitafikaje, maana
wingu mbele yangu lilikuwa zito. Bado niliamini kuwa ipo siku, kisha nikawa nayatazama
maisha yangu huku nikidhamiria siku nikipata fursa lazima nirudi kusoma.”
Elewa kuwa
magumu hayakumfika Wendy mara tu alipojifungua mtoto wake au baada ya
kutalikiwa na aliyekuwa mume wake wa kwanza, kwani historia yake inaonesha kuwa
alipokuwa na umri wa miaka 14, alilazimika kuuza magazeti mitaani angalau apate
fedha za kujikimu na familia yake.
Inaelezwa
kuwa ugumu huo wa maisha ndiyo sababu ya Wendy kuanza mapenzi akiwa na umri
mdogo. Kipindi yupo high school, wakati alipofikisha umri wa miaka 17, Wendy
alihamia nyumbani kwa boyfriend wake, Frank Underwood ambaye alikuwa mfanyakazi
wa masuala ya ujenzi.
Ni huyohuyo
Underwood ambaye baadaye walifunga ndoa, wakazaa mtoto ambaye walimpa jina la
Amber. Ndoa yao ilifungwa Januari 24, 1982. Baada ya kutengana, Wendy na Amber
kwa pamoja wakawa mizigo ya mama yake Wendy.
“Nilijitahidi
sana nisiwe mzigo kwa mama, nilipambana sana na maisha nikiwa na mwanangu Amber
lakini hali ilipozidi kuwa ngumu sikuwa na jinsi zaidi ya kuhamia kwa mama,
ilibidi iwe hivyo kutokana na hali halisi, sikuwa najiweza kabisa,” anasema Wendy
na kuongeza:
“Kurejea
nyumbani kwa mama ilikuwa muhimu zaidi kwa ajili ya ustawi wa mtoto wangu.
Nisingeweza kumpa huduma bora za kimaisha, ikiwemo matibabu kama
ningeng’ang’ania kusimama peke yangu. Ukweli ni kuwa sikuwa na chochote ambacho
niliona naweza kufanya kumpa mtoto wangu maisha yenye afadhali.”
Zingatia
kuwa alipata matokeo mabaya high school, kwa hiyo hakuwa na sifa za kudhaminiwa
na Serikali ya Marekani kusoma chuo kikuu. Naye aliamini kuwa elimu ya daraja
hilo ndiyo pekee inayoweza kumfanya afanikiwe kwa urahisi katika maisha yake.
Alijichangachanga
kwa muda kisha akaanza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Texas, mjini Arlington.
Bahati ikawa mbaya kwake, alimudu kusoma kwa muhula mmoja tu, fedha ilikosekana
ya kuendelea. Ikabidi aache.
Kipindi
hicho, baba yake alikuwa amefungua duka la sandwich na piza, katikati ya Jiji
la Fort Worth, Jimbo la Texas. Siku moja Wendy alimtembelea baba yake dukani
kwake ndipo aliweza kukutana na Jeffry R. Davis ambaye ni mwanasheria, vilevile
alipata kuwa mjumbe wa halmashauri ya Jiji la Fort Worth.
Jeffry Davis
ndiye baadaye alikuja kuwa mume wa pili wa Wendy. Na Davis inayotumika kama
ubini wa Wendy imetokana na Jeffry, kwani Wendy majina yake halisi ni Wendy
Jean Russell.
Kuna kipindi
Wendy alifanya kazi kama katibu muhtasi wa daktari katika hospitali moja
binafsi kwenye Jiji la Fort Worth. Ni katika nyakati hizo ndipo mmoja wa manesi
katika hospitali hiyo aliyokuwa anafanya kazi alipomuonesha kipeperushi kuhusu
Chuo cha Tarrant County.
Kupitia
kipeperushi hicho, alijiunga na masomo ya program ya awali ya shahada ya sheria
(paralegal program) katika Chuo cha Tarrant Count. Ni kipindi hicho alianza
uhusiano wa kimapenzi na Jeffry.
Mwaka 1986
baada ya kumaliza program yake, alijiunga na Chuo Kikuu cha Texas Christian,
kipindi hicho aliweza kupata ufadhili wa masomo yake kutoka Serikali ya
Marekani.
Mei 30, 1987,
baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa miaka miwili, Jeffry na Wendy walifunga ndoa.
Maisha ya Wendy yalibadilika, waliishi kwenye nyumba yao nzuri, iliyopo Mistletoe
Heights, nje kidogo ya Jiji la Fort Worth.
Pamoja na
kuhamia kwenye nyumba bora, unafuu wa maisha ya Wendy ulikuwa mkubwa, kwani
kipindi hicho Jeffry alikuwa anamhudumia mkewe, akimpa mahitaji yote muhumu,
hususan yale yaliyohusu elimu yake.
Septemba 1988,
Wendy alijifungua mtoto wake wa pili, Dru. Lakini wa kwanza kwa mume wake
Jeffrey. Hata hivyo, Jeffrey baadaye alimuasili Amber, hivyo kuwa mtoto wake
rasmi, kisha akawa anaitwa Amber Davis.
Mwaka 1990,
alihitimu shahada yake ya kwanza ya Kiingereza. Baada ya hapo alihama na wanaye
mpaka Lexington, Massachusetts, ambako alijiunga na Chuo Kikuu cha Harvard.
Chuo bora kabisa duniani katika masomo ya sheria. Chuo ambacho hata Obama
alisomea.
Maisha ya
malezi na shule hayakuwa rahisi. Ilibidi mama yake awachukue wajukuu zake,
aishi nao kipindi ambacho Wendy alikuwa anapambana kutafuta shahada yake ya
sheria.
Akiwa Harvard,
Wendy alianza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii. Tayari alishaona mlango
wake wa elimu umefunguka, kwa hiyo akawa anaundaa mwingine kuhusu siasa. Alijua
asingeweza kupata mafanikio ya kisiasa bila elimu.
Baada ya
kumaliza Harvard kisha kusoma uwakili, Wendy alianza kazi kama karani wa Jaji
wa Wilaya. Jeffry baadaye alianzisha kampuni inayoitwa Safeco Title Co.
ikijihusisha na masuala ya bima, Wendy akawa mmoja wa wamiliki.
ALIVYOANZA
KUCHOMOZA KISIASA
Mwaka 1996,
aligombea ujumbe wa Halmashauri ya Jiji la Fort Worth akashindwa kwa tofauti ya
kura 90. Mwaka 1999, aligombea tena ujumbe huo na kushinda. Alikuwa mjumbe kwa
miaka tisa na katika kipindi chake amekuwa mtetezi hasa katika sekta ya
usafiri, maendeleo ya uchumi na ujirani mwema.
Kipindi
akiwa mjumbe wa Halmashauri ya Jiji la Fort Worth, Davis alikuwa mwanachama wa Republican.
Anasema alipenda Republican kwa kuvutiwa na mbunge mwanamke (Congresswoman), Kay
Granger aliyekuwa akitokea Fort Worth.
Alikichagua
Republican na kuchanga fedha kwa wagombea wa chama hicho. Mwaka 2006
alimchangia Granger dola 1,500. Aprili 1999, alimchangia Rais wa 43 wa
Marekani, George W. Bush dola 2,500 wakati alipokuwa anawania urais kwa tiketi
ya Republican.
Michango hii
ina maana gani? Kwamba tayari uchumi ulishakuwa vizuri. Dola 2,500 kwa chenji
ya shilingi ni zaidi ya milioni 5. Huwezi kutoa mchango wa fedha hizo kama
mambo yako bado hovyo. Mambo yalishamnyookea.
Kipindi
hicho hakuwa Wendy yule wa maisha ya kutangatanga, bali mwenye maisha ya
uhakika. Watoto wake wakisoma shule bora. Huduma bora zilitoka kwa mama. Kila
kitu kinakwenda vizuri, maana mama yupo vizuri. Hii inatosha kuonesha kuwa
maisha yanaweza kubadilika. Muhimu ni kushika njia yako.
Mwaka 2008,
akiwa na tiketi ya Democrats, alishinda Useneta katika Seneti ya Texas,
akiwakilisha Jimbo la District 10. Mwaka 2012 aligombea na kushinda tena, hivyo
kushikilia nafasi hiyo mpaka Januari 13, mwaka huu.
Sababu ya
kuachana na useneta wa Texas ni mbio zake za kuwania ugavana wa Texas katika
Uchaguzi Mkuu wa Texas mwaka 2014. Alishinda uteuzi ndani ya Democrats, akawa
mwanamke wa kwanza kupitishwa na chama hicho tangu mwaka 1994, alipoteuliwa Ann
Richards ambaye alishindwa na George Bush wa Republican.
Hata hivyo,
Wendy hakuweza kushinda ugavana wa Texas, kwani alishindwa na aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Greg Abbott, aliyegombea kupitia Republican.
Pamoja na
kushindwa ugavana, Wendy amebaki kuwa mwanasiasa maarufu, huku akitarajiwa
kuendelea kufanya vizuri kisiasa katika nyakati zinazokuja.
Kikubwa
ambacho anakumbukwa ni jinsi alivyowasilisha muswada na baadaye kuwa sheria kuhusu
katazo la utoaji mimba.
Miswada na
mapendekezo yake ni mingi, vilevile ipo sheria ya uvutaji bangi ambayo
alipambana kuhakikisha inaanzishwa ili kudhibiti uvutaji wa mihadarati.
BADO
UNAAMINI HAIWEZEKANI?
Wendy na
Jeffry waliachana mwaka 2003 na baada ya talaka kutolewa rasmi mwaka 2005,
ilikubaliwa Wendy awe analipa dola 1,200, yaani zaidi ya shilingi milioni 2.4
kwa mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto.
Ni kipindi
ambacho maisha ya Wendy yameshakuwa juu, hivyo Jeffry alitaka alipwe fedha kwa
sababu mtoto alibaki kwake. Yote yaliwezekana pasipo usumbufu wowote.
Vyombo vya
habari vimekuwa vikimmulika na mafanikio yake ya kisiasa yamebeba mshangao wa
namna mwanamke huyu ambavyo hakuwahi kukatisha ndoto zake pamoja na ugumu
uliokuwa ukimkabili.
Jeffry alimkuta
Wendy anajiendeleza na masomo. Hata baada ya kufunga ndoa na kuuona urahisi wa
maisha, bado Wendy alisimamia maono yake, alijitahidi mpaka kufika Harvard.
Mwaka jana
wakati anawania ugavana wa Texas, aliushangaza ulimwengu alipochangisha fedha
dola milioni 12 (shilingi bilioni 25.9) ndani ya usiku mmoja ambazo zilimsaidia
wakati wa kampeni.
Anza na wewe
leo, usigeuke nyuma. Kufanya hivyo ni mwiko, kwani utasababisha matunda yako
yaliwe na wengine. Kila la heri muota ndoto!
0 comments :
Post a Comment