Na Luqman
Maloto
MUNGU akiamua
huifanya ngumu ionekane nyepesi na laini yaweza kuwa yabisi. Ni yeye aliye juu hubatilisha
mipango ya binadamu kwa namna anavyotaka. Ndiyo maana ikasemwa jitihada
hazishindi kudura.
Ni kwa ukuu
wa Mungu, Bikira Maria, mwanamke ambaye alikuwa hajamjua mwanaume, alibeba
mimba ambayo ilimleta duniani Yesu Kristo (Isa bin Mariam).
Hapa ngoja
niweke kituo, kisha nikuhoji, ni kipi hasa kinachoweza kukufanya ukimbilie
kutoa mimba? Unamjua aliye tumboni mwako amepangwa na Mungu awe nani hapa
duniani?
Wewe
mwanamke unayenyonga kichanga, ni kwa nini unawahi kukata tamaa mapema na
kupitisha hukumu kuwa huwezi kumlea mwanao? Je, unatambua ni sahani gani ambayo
Mungu amempa aje nayo hapa duniani?
Umewahi
kujiuliza, hivi kama Mark Zuckerberg angetolewa akiwa mimba na mama yake wakati
huo, ni nani angeleta mapinduzi ya matumizi ya mtandao kupitia Facebook?
Vipi Bill
Gates na Microsoft yake, angewezaje kuyafanya maisha yetu ya kila siku kikazi
kuwa rahisi kama mama yake angemnyonga akiwa kichanga?
Ni kwa
kufikia hoja hiyo ndipo unaweza kuona kuwa wapo watu wengi ambao walimaanishwa
kuifanya dunia kama peponi lakini safari yao ilibaki njiani kwa sababu wazazi
wao hawakuwapa nafasi ya kuishi.
Ngoja nikwambie
ndugu yangu, fursa ya kuishi anaitoa Mungu na ni yeye mwenyewe huyakatisha
maisha ya mja wake kwa wakati na namna atakavyo. Juhudi zozote za kukatisha
maisha ya mtu ni kuingilia mamlaka ya Muumba!
Mimba
inapoingia tumboni, hebu hakikisha unaitunza, maana Mungu ametoa fursa kwa mja
wake mwingine kuja duniani. Harakati zako za kwenda kwa madaktari kuichoropoa,
kwanza unashindana na mamlaka ya Mungu, pili unapiga teke sahani la almasi.
Je, hupendi
kuwa mzazi wa Lionel Messi wa soka? Hutajisikia fahari endapo Steven Curry wa
kikapu NBA atakuwa mwanao? Huwezi kufikia hatua hiyo muhimu ya heshima kama
hutatii amri ya Mungu, anapoelekeza kiumbe chake ndani ya tumbo lako.
Mwanamke
anaweza kutoa mimba kadhaa, kumbe hizo ndizo za wanasayansi wengine kama Neil
Armstrong na Buzz Aldrin, waliotangulia kufika mwezini na kufanya ugunduzi
mkubwa.
Ungependa
mwanao awe mgunduzi wa kihistoria kama Thomas Edison, aliyetengeneza kwa mara
ya kwanza taa za umeme, vifaa vya kurekodia sauti na kamera za video, lakini wakati
watoto wenye akili kubwa umewanyima fursa ya kuishi.
Lea mimba
kwa unyenyekevu wa hali ya juu ikiwa unatamani kuwa na watoto wenye sifa bora
kama The Wright brothers, yaani Orville na Wilbur Wright, waliotengeneza na
kurusha ndege kwa mara ya kwanza, hivyo kuwa waanzilishi wa usafiri huo wa
anga.
Amini kuwa
Mungu anapoleta kiumbe chake, anakuwa analeta na sahani yake. Usiogope
changamoto za maisha. Endapo utazivumilia si ajabu ukamleta duniani Nikola
Tesla, aliyegundua mfumo wa kisasa wa umeme au mwanasayansi Marie Curie ambaye
ni mwanamke wa kwanza duniani kutunukiwa Tuzo ya Nobel.
Kuja kuitwa
mama wa mfalme, zipo gharama ambazo hutakiwi kuzikimbia. Nyingine ndiyo kama
hizo kwamba uwe tayari kubeba mimba katika kipindi ambacho unaona kabisa maisha
yako ni magumu.
Mungu ana
kawaida ya kuruhusu majaribu yakufike ili yakikuzidi nguvu upotoke. Na
mpotokaji anakuwa amechagua njia ya Shetani. Mungu huwapa akili nzuri waja wake
pamoja na utashi unaojitosheleza. Unapokosea kwa sababu yoyote ile, maana yake
umeshindwa kutumia akili yako ipasavyo.
Muhimu
kuzingatia ni kuwa unapopotoka, unakuwa umeshika njia ya Shetani. Mungu
aliyekuumba hutaka ubaki kwenye mstari wake hata unapokuwa kwenye wakati mgumu
kiasi gani. Muelekee yeye nyakati zote, kuwa na imani isiyoyumba.
Ni kwa imani
yako, ndipo unaweza kumleta duniani, Sandford Fleming ambye ni mgunduzi wa
majira, mwanzilishi wa stempu za barua, vilevile kiungo muhimu wa uwekwaji wa
njia za reli duniani. Usitoe mimba, pengine ukawa mama wa rais au waziri mkuu.
CRISTIANO
RONALDO ANGETOLEWA AKIWA MIMBA
Dolores
Aveiro ni mama wa staa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anaitwa mama wa
stadi huyo wa mpira wa miguu kwa kudura za Mungu. Matunda anayokula ku[itia
mwanaye hakika hakuyastahili. Maana anakula raha alizojaribu kuzihujumu.
Kama mipango
ya binadamu peke yake ingekuwa inatosha kutimiza mambo na maazimio, Dolores
asingeweza kuwa mwanamke maarufu duniani. Asingeitwa mama wa kijana gwiji wa
soka duniani, anayeichezea Klabu ya Real Madrid na Timu ya Taifa ya Ureno.
Dolores hakumtaka
Ronaldo wakati ikiwa mimba lakini sasa hivi anatamba huku na huko kwamba yeye
ndiye mama mzaa nyota. Mungu alimlinda Ronaldo.
Mama huyo,
alikusudia hasa kukatisha maisha ya Ronaldo akiwa bado mimba, kwani hata
madaktari walipomshauri asifanye hivyo, alitumia mpaka njia za kienyeji.
MAMA RONALDO
ANAKIRI
Dolores ameandika
kitabu na kukiita kwa Lugha ya Kireno, Mae Coragem (Mother Courage), maana yake
ikiwa ni Ujasiri wa Mama. Ndani ya kitabu hicho Dolores anasema: “Nililenga
kutoa mimba ya Ronaldo. Nilitumia njia nyingi bila mafanikio.”
Anaongeza:
“Madaktari waligoma kunisaidia kutoa mimba, uamuzi uliofuata baada ya hapo
ikawa ni kunywa pombe kali ili kutoa mimba. Lakini sikupata matokeo
niliyohitaji.
“Nilitumia
kila njia nikashindwa. Sikutaka kumzaa Ronaldo. Sikujua kama atakuja kuwa huyu
anayenifanya nijivunie kuwa mama.”
RONALDO
AMRUDI MAMA YAKE
Ronaldo
anajua hila za mama yake, na siku moja alimrudi, akamwambia: “Mama angalia,
ulitaka kunitoa nikiwa mimba na sasa mimi ndiye kinara wa nyumba yetu. Unanitegemea
na familia yetu yote inanitazama mimi.
“Tazama
jinsi ambavyo dunia inanitazama. Naitwa mchezaji mkubwa duniani. Kila klabu
kubwa ya soka duniani ingependa kupata huduma yangu. Unadhani hii ni fahari
yangu peke yangu? Inakuhusu na wewe mama yangu. Unapaswa kujivunia sana kuwa na
mtoto kama mimi.
“Hata hivyo,
usingenipata kama ungefanikiwa. Unaweza kuona somo unaloweza kutoa kwa wanawake
wengine kuhakikisha wanatunza mimba na kuwalea watoto wao ili waje kujivunia
uwepo wao. Pengine wakawa watoto wenye umashuhuri mkubwa duniani.”
Mume wa
Dolores, Dinis Averio ambaye ni baba wa Ronaldo, alishatangulia mbele za haki
kwa maradhi ya kuharibika kwa ini, ikiwa ni matokeo ya kuathirika na unywaji
pombe kupita kiasi.
Hata hivyo,
Ronaldo aliijua siri hiyo tangu akiwa mdogo lakini amekuwa akiitunza bila
kuitamka popote mpaka pale mama yake alipoamua kuvunja ukimya kwa kuandika
kitabu.
NINI SHABAHA
YA KUANDIKA KITABU?
Kwa mujibu
wa Dolares, shabaha yake ni kuwafanya wanawake wengine waone matokeo yake ili
wajifunze kwamba unaweza kutoa mimba na kujidanganya kuwa ni salama kumbe
umepoteza mkombozi.
“Ningefanikiwa
kumtoa Cristiano akiwa mimba, maana yake nisingekuwa mama mwenye thamani kubwa
kama nilivyo sasa. Nilikubali kumwacha Cristiano akue tumboni kwangu baada ya
kushindwa kumtoa. Nilisema basi tu acha nizae lakini siyo kwa mapenzi yangu.
“Wakati
mwingine mpaka huwa nashangaa kila nikikumbuka nilivyokuwa napigania kuitoa
mimba ambayo ndiyo imemleta Cristiano duniani. Nikimtazama Cristiano alivyo
mkubwa na anavyowika, najiona kabisa kuwa nilitaka kufanya jambo baya na
nilikaribia kukatisha maisha ya nyota ya dunia.
“Ananisuta
lakini najivunia, maana simuoni mama ambaye asingependa Cristiano awe mtoto
wake. Tumboni kwangu ameishi, nilimzaa na kumlea mimi mwenyewe. Ndiyo maana
nasema ananisuta lakini najiona mama mwenye fahari kubwa kupitia mwanangu
Cristiano,” anasema Dolares.
Anaendelea: “Ona
sasa, nimeandika kitabu na kuuza nakala nyingi kwa sababu nimemzungumzia mtoto
wangu ambaye ni maarufu sana duniani. Nimepata mafanikio makubwa, nimeingiza
fedha nyingi. Nafaidika sana kupitia kuwa mama wa Cristiano.
“Upande
mwingine, mimi sina wasiwasi juu ya maisha yangu. Cristiano ananiwezesha kwa
kila ninachohitaji. Nikipita barabarani naheshimika. Serikali ya Ureno inaniheshimu.
Nikiwa Hispania au popote, hata Uingereza naheshimika.
“Nafahamika
mimi ni mama wa Cristiano. Ni faida kubwa sana hii. Daima najivunia kuwa mama
wa Cristiano. Nampenda sana Cristiano, namshukuru Mungu kwa kuzuia mpango wangu
kutoa mimba yake.”
ANAFAIDI
UTAJIRI WA MWANAYE
Kwa sasa
Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mmoja wa wanamichezo wanaoingiza fedha
nyingi sana kupitia mshahara na mikataba ya matangazo.
Anatumia
gari apendalo na anaishi kwa ufahari mkubwa. Hayo ndiyo matokeo ya Mungu
kumlinda Ronaldo mpaka kufikia mafanikio yaliyopo kwa sasa. Na hiyo ni sawa tu
na ile bahati ya mtende kuotea jangwani.
WAPO WENYE
JUHUDI KUBWA ZA KUUA
Mtu anafanya
jaribio la kwanza, mimba haitoki, anarudia tena na tena. Hiyo ni dhamira ya
hali ya juu.
Mwingine
anafikisha mimba 10 mpaka 20, zote katoa. Kila mwaka anaweka rekodi ya
kuchoropoa tatu mpaka nne.
Unaweza
kujiuliza kuna nini ambacho mtu anakuwa anakitafuta. Hawezi kuwaza ni
wanasayansi wangapi, idadi gani ya wachumi, wanasiasa wakombozi wa nchi,
madaktari wenye karama kubwa, waandishi wamulika nchi na kadhalika.
Unakuta mtu
anafanya majaribio yote hayo, kisha analaumu kuwa katika uzao wake hajapata mtu
mwenye kipaji maalum.
Kila
mwanamke atambue kuwa ndani ya tumbo lake kuna tunu kubwa mno. Ni jukumu lake kuitunza.
Njia pekee ya utunzaji wa tunu hiyo ni kukilinda kiumbe kinachoingia ndani yake.
Zingatia uaminifu!
Kwa mfano
mmoja tu wa mama yake Ronaldo, tafakari ni idadi gani ya akina Ronaldo
wanapotea? Ndiyo sababu mimi huwa nawaambia watu kuwa Mtanzania aliyetakiwa
kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia (ballon d'or) kumzidi Messi, pengine
alitolewa akiwa mimba au alinyongwa akiwa kichanga.
Mwanamke
Mtanzania tishio wa tenisi duniani, mwenye viwango kuliko Serena William,
inawezekana naye alinyimwa fursa ya kuishi na wazazi wake, kwa ama kutolewa
akiwa mimba au alinyongwa akiwa kichanga au hata alitupwa chooni.
Chukua hii;
Kila siku kataa kuupofusha ubongo wako kwa sababu ya upeo wa mboni zako. Kila
uamuzi unaofanya hakikisha unatazama juu na mbali kabisa. Changamoto za leo
zisikunyime matunda ya kesho.
Hebu
nikuombe tuzungumze biashara nzuri na rahisi mno lakini yenye mtaji mkubwa na
faida yake inaweza kukufanya ufurahie maisha yako yote. Ukashangaa kila siku
unatabasamu, ukitembea unajivuna na watu wanakuheshimu bila shaka.
Kimsingi ni
biashara ambayo hata siku moja haiwezi kukupa majuto. Nakuhakikishia pasipokuwa
na chembe ya shaka kwamba haitatokea ikakufanya ujilaumu kuifanya.
Naomba
uniamini mimi, biashara yenyewe ni uwekezaji kwa mtoto. Wekeza kwa mwanao kisha
utaona jinsi maisha yanavyoweza kubadilika kwa kasi.
Weka mipango
safi kwa ajili ya mtoto wako na hakikisha unamwita jina zuri kisha umjenge
katika misingi iliyo bora.
Usiwe
mbinafsi, mpe anachohitaji kama kipo ndani ya uwezo wako. Mwoneshe upendo mpaka
yeye mwenyewe akiri kwamba anapendwa.
Watoto ni
wakoseaji mara nyingi, siyo yeye ni utoto. Muonye na umsahihishe kwa upendo.
Mkaripie na umuadhibu kwa upendo.
Kuwa mtu wa
shukurani kila siku. Usimkufuru Mungu. Amini kuwa kwa Muumba kuna neema nyingi
nje ya matarajio pamoja na maombi yako. Tambua kwamba aliyekuumba anakupenda
kuliko unavyojipenda wewe mwenyewe.
Tukubaliane
sasa; Endapo utapata mimba, furahi na useme kuwa hayo ni mafanikio. Usithubutu
kusema kuwa imekuja kinyume na matarajio.
Pengine mimba
unayosema imekuja kinyume na mipango, ndiye zawadi ya ukombozi. Ipokee na
uithamini. Nakuhakikishia hutajuta.
Kuna siku
ngumu inakuja, ambayo wengi watashindwa kujibu maswali ya Muumba na malaika
wake. Siku tamu kwa watu wema na ngumu kwa waovu. Inaitwa siku ya mwisho.
Siku hiyo
hukumu itatolewa. Na ikifika, wapo marais, wanasiasa wakubwa, wanasayansi
waliomaanishwa kuja kuikomboa dunia, viongozi wa kidini na kadhalika,
watasimamishwa kwenye uwanja wa hukumu, kisha kutangazwa kuwa ni mashujaa walionyimwa
fursa ya kuishi na wazazi wao.
Tuendelee
kukumbushana. Tunaweza kujenga kizazi kizuri kwa faida ya leo na kesho.
0 comments :
Post a Comment