ads 728x90 B

Gloria James Anaendesha gari la milioni 450, anaishi jumba la bilioni 20, kisa ni mama LeBron





Luqman Maloto
MABADILIKO chanya katika maisha yana raha sana. Kutoka ufukara kwenda utajiri, daraja la chini kikazi na kupanda cheo, raia wa kawaida hadi kuwa kiongozi, upweke na kupata mwenzi au mtoto. Hayo na mengine mengi ni mambo yanayosimulika kwa urahisi sana!
Mabadiliko hasi ni maumivu na simulizi zake kwa kawaida siyo zenye kutoka kwa wepesi. Fikiria tajiri mjivuni aliyegeuka fukara, bosi mpenda sifa kushushwa cheo, kiongozi mwenye makeke kunyimwa kura na mengineyo.
Naomba tuzungumze biashara rahisi lakini yenye mtaji mkubwa, inayoweza kukufanya ufurahie maisha yako yote. Biashara isiyo na majuto. Hata siku moja haitakufanya ujilaumu kuifanya. Biashara yenyewe ni uwekezaji kwa mtoto. Wekeza kwa mwanao kisha utaona jinsi maisha yanavyoweza kubadilika kwa kasi.
Ni suala la kuvumilia mwanzoni tu, jikaze na umlee kwa imani.  Ukipata nafasi ya kuzungumza na Gloria Marie James, atakwambia raha za kuwekeza kwa mtoto. Yeye ameweza kuyafanya maisha yake kubadilika kutoka sifuri hadi kuchezea mamilioni ya fedha kwa siku. Anatumia, mwanaye anazo!
Gloria ni mama wa staa wa kikapu katika Ligi ya NBA, LeBron James. Maisha ya kumkuza mkali huyo wa kuteleza kwenye marumaru za uwanja wa kikapu (basketball court) hayakuwa rahisi hata kidogo. Msisitizo; hayakuwa rahisi kabisa.
Hata hivyo, Gloria aliamini mwanaye ndiye mkombozi wake, akapambana kumtengenezea barabara ya kupita. Hakika amefanikiwa, kutoka dhiki za kuwaza japo mlo wa siku, leo anakoga mapato kutokana na ingizo kubwa la mamilioni ya mwanaye katika kikapu.
Akaunti benki inafoka dola za Federal Reserve System (FRS), yaani Benki Kuu ya Marekani. Umri unasogea lakini ndiyo kwanza vijana wanamuona mrembo mbichi. Analipa kutokana na matunzo. Hana dhiki, mahitaji yote yapo ndani ya uwezo.
ALIKUWA MTOTO AKAZAA MTOTO
Anayefikisha umri wa miaka 18 ndiye anatambulika ametoka hatua ya utoto na kuhamia utu uzima. Gloria alinasa ujauzito akiwa na umri wa miaka 16 tu. Pamoja na hali hiyo, alijisimamia ipasavyo kumlea mwanaye.
Hakuwa na mpenzi wa kueleweka, ila sanaa tu za ujana na mapenzi ya kujifurahisha ndiyo yaliyomfanya anase. Alimjua mwanaume aliyempa ujauzito lakini hakuweza kushirikiana naye kwenye malezi.
Pamoja na umri mdogo aliokuwa nao, Gloria hakutaka kumuwazia mwanaume aliyempa ujauzito. Alijiaminisha tu kuwa mwanaume huyo ni baba wa bahati mbaya, kwa hiyo aliamua kujihesabu yeye kama baba na mama wa LeBron.
Hata LeBron mwenyewe amekuwa akikiri mara nyingi kwa kuandika kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram: “Mama yangu ndiye kila kitu kwangu. Yeye ndiye baba na ndiye mama yangu.”
Gloria anamtaja baba wa LeBron kuwa ni Anthony McClelland na katika mara chache ambazo amemzungumzia, alisema tu kwa kifupi: “Alipogundua tu nina ujauzito alikimbia, hakutaka kuniona tena.”
SHURUBA ZA MALEZI
Kwanza Gloria anastahili pongezi kwa sababu sheria ya nchi yake (Marekani), ilikuwa inampa ruhusa ya kutoa mimba kutokana na umri mdogo.
Kwa wakati huo, watoto waliopata ujauzito, walihesabiwa ndani ya kapu moja na wale wenye matatizo ya kujifungua, hivyo kupewa ruhusa ya kutoa mimba. Hata hivyo, Gloria aliamua kuitunza na kuzaa. Na Mungu alimsimamia hatua kwa hatua.
Mama wa Gloria, yaani bibi yake LeBron, Freda James alikuwa karibu kusaidia mjukuu wake anapata kilicho bora. Na kwa vile umri wa Gloria ulikuwa mdogo, mara nyingi alikaa pembeni akitazama mwanaye akihudumiwa na Freda.
Gloria akiwa na umri wa miaka 19, wakati huo LeBron akifikisha miaka mitatu ya kuzaliwa, Freda alifariki dunia ghafl kwa shambulio la moyo. Ni hapo ndipo hali ilikuwa mbaya kupita kiasi.
Miezi michache baada ya kifo cha Freda, Gloria alinyang’anywa nyumba aliyoachiwa na mama yake, hivyo kuanza kutangatanga kutafuta hifadhi yake na mtoto wake.
Kupata chakula chake na cha mtoto wake ilikuwa shida, malazi ikawa kituo cha manyanyaso. Mavazi kwa kuombaomba.
Pamoja na shida zote hizo, kuishi bila uhakika wa kupata chakula, sehemu ya kulala wala kuvaa, hakuwahi kumuona LeBron ni mzigo. Na kwa msimamo huo, Mungu amemuangazia nuru ya aina yake.
AMUOMBEA HIFADHI LEBRON
Kwa kupigana huku na huko, mama yake LeBron alijitahidi akapata chumba kimoja cha kupanga. Miaka ikawa haisogei kutokana na ujazo mkubwa wa dhiki uliokuwa unawaandama.
Pamoja na hivyo, ilifika kipindi LeBron alifikisha umri ambao haikuwa heshima kuendelea kuchangia chumba na mama yake. Ni hapo Gloria aliamua kumuombea hifadhi mwanaye.
Gloria alikuwa na ndoto za kumfanya LeBron kuwa mwanamichezo mkubwa. Na katika umri wa miaka tisa, alikuwa anafundishwa soka na kocha malum. Gloria alimuomba kocha huyo msaada wa kuishi na LeBron katika kipindi akihangaika kutafuta fedha za kumuwezesha kupanga nyumba yenye vyumba viwili.
Mbali na suala la kupata nyumba yenye vyumba viwili, sababu kubwa ambayo Gloria aliitoa ni kuwa LeBron kwa hatua aliyofikia, alihitaji kujengwa zaidi kimchezo na kihuduma, mambo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wake.
Alisema, kwa kuwa mbali na LeBron kipindi anaishi na kocha wake, alilenga kujipanga ili apate uwezo wa kumhudumia mtoto wake yeye mwenyewe.
Katika kufafanua sababu ya kumpeleka LeBron kwa kocha, Gloria alimwambia mwanaye: “Ulikuwa uamuzi mgumu. Tambua ilikuwa ngumu lakini najua haikuwa kwa ajili yangu. Ilikuwa kwa ajili yako. Nililazimika kukuweka wa kwanza.”
Kocha wa LeBron, Frank Walker ‘Big Frankie’ hakumuangusha Gloria, alimlea LeBron vizuri na kupata kila sapoti ambayo aliona anastahili katika kumkuza ipasavyo kimichezo.
LeBron anazungumzia hali hiyo ya kuhamishiwa kwa kocha Big Frankie kama sadaka kubwa iliyofanywa na mama yake. Anasema: “Alihitaji nipate utulivu, na kweli kwa mwaka mmoja ndani ya nyumba ya Big Frankie kwa mwaka mzima niliishi nyumba moja, nililala kwenye kitanda kilekile, nikasoma shule ileile, tofauti na mwanzo nilipokuwa nahamahama kwa kukosa msimamo wa kimaisha.
“Mama alitaka niwe mwanaume bora, kwa hiyo alitaka nipate maisha yenye utulivu, yale tuliyokuwa tunaishi naye kwa kutangatanga hayakuwa na nafuu. Na kweli Big Frank alinisaidia sana, kwani ni yeye aliyenikutanisha na timu yangu ya kwanza ya kikapu. Kipindi hicho, nilimuona mama yangu wikiendi tu.
“Mama alipopata uwezo wa kupanga nyumba ya vyumba viwili kwa msaada wa serikali, nilirudi kuishi naye tena. Tuliishi pamoja mpaka nilipomaliza elimu yangu juu ya sekondari, mengine yaliyosalia yanabaki tu kuwa historia.”
LEBRON ANAUJUA USHUJAA WA MAMA YAKE
LeBron anasema: “Mama yangu ndiye shujaa wangu. Tulihama nyumba nyingi kila mara kwa sababu hatukuwa na uwezo. Tulizunguka huku na huko bila mafanikio na matumaini hayakuonekana.
“Mama yangu alijitupa huku na huko kufanya kazi, na hakuchagua kazi ya kufanya ilimradi tupate cha kutukutanisha kwenye meza ya chakula. Pamoja na dhiki zote, nilikuwa na uhakika wa jambo moja, ni upendo. Mama yangu alikuwepo karibu yangu kunifunika blanketi na kunipa ulinzi niliohitaji. Hakuna aliyekuwa na umuhimu kwake zaidi yangu.”
Anaongeza: “Watu siku zote wanasema nimekuwa mwaminifu sana kwa mama yangu, hiyo ni kweli kabisa kwa sababu naye amekuwa mwaminifu kwangu. Mama alinifundisha ladha ya upendo wa kweli, nami nampa. Kwa mfano wake, nimekuwa nikiwasaidia watoto wanaolelewa na mama zao bila baba. Ni kwa sababu nina uwezo na ni kwa sababu mama yangu amenifanya niwe hivi nilivyo.”
MCHEZO ULIGEUKA KITAMBO
LeBron anasema kuwa tangu alipoanza masomo ya sekondari ya juu (high level), kodi ya nyumba ilibaki historia kwa sababu kipaji chake kilimuwezesha kuingiza fedha ambazo zilisaidia kulipia bili zote za nyumbani.
Mwaka 2003, alifuzu chaguo la kwanza katika chujio la vyuo kuingia Ligi ya NBA. Alijiunga na Timu Cleveland Cavaliers, aliyoitumikia mpaka mwaka 2010 kabla ya kujiunga na Miami Heat alikocheza kati ya mwaka 2010 na 2014 kisha kurejea tena Cavaliers.
LeBron ni staa mkubwa sana duniani kwa sasa, uwezo wake anapokuwa uwanjani umempa heshima ya kipekee. Na wengine humwita King James, yaani Mfalme James, kwamba viwango vyake ni vya kifalme. Zaidi ni mshindi mara nne wa tuzo ya NBA Mchezaji mwenye Thamani kuliko wote (MVP).
Kwa miaka miwili mfululizo amekuwa akiingiza kwa mwaka dola milioni 72 (shilingi bilioni 152), mshahara ukiwa dola milioni 19 (shilingi bilioni 40) na mikataba ya matangazo ikiinenepesha akaunti yake kwa dola milioni 53 (shilingi bilioni 112).
Utajiri wa jumla ambao LeBron anatajwa kuumiliki ni dola za Marekani milioni 425 (shilingi bilioni 896.15). Huwezi kuyazungumzia mafanikio bila mama nyuma yake. Gloria ameweza kumfikisha mwanaye hapo alipo.
Leo hii, Gloria anajulikana ulimwenguni kote hususan kwa wapenda kikapu na wengine wanamwita Mama Kikapu, kwa maana tumbo lake limemleta duniani staa mkubwa wa kikapu.
 Gloria hajui tena shida, anakula matunda ya mwanaye. Anaendesha gari ghali kabisa aina ya Porsche Panamera toleo la mwaka 2014 lenye thamani ya dola 200,000 (shilingi milioni 422). Anaishi kwenye jumba la mtoto wake, lililopo Akron, Ohio, lililo na kila aina ya burudani, likiwa na ukubwa wa futi za mraba 30,000 na thamani ya dola milioni 9.2 (karibu shilingi bilioni 20).
Wakati anatangatanga na mwanaye, wanaume walimkwepa kwa kuogopa kubeba mzigo wa malezi, zaidi walimuona hana mvuto kwa sababu ya uchakavu wa sura na mwili, vilivyotokana na ukosefu wa matunzo.
Gloria ana umri wa miaka 47 lakini kutokana na maisha kumuendea sawa, vijana wanajigonga kwake, kwani ananawiri, na mpenzi wake wa sasa ni mwa Hip Hip Da Real Lambo, 33. Na wengi tu wanammezea mate.
Utamu huo wa maisha anaupata baada ya kuamini kuwa mtoto siyo mzigo bali zawadi. Ni vizuri kuchukua somo kwamba mimba haitolewi wala mtoto hatelekezwi. Ipende mimba kwani ndiyo inaleta neema yako. Mlee mwanao kwa upendo, si ajabu ndiye nuru yako.
ONDOKA NA HILI
Hii ikupe muongozo wa kutambua kuwa mtoto ni zawadi. Omba Mungu akuongoze na usibague, maana hujui kuwa pengine huyo unayembagua ndiye mama au baba wa daktari bingwa atakayegundua dawa za Ukimwi, Homa ya Ini (Hepatitis B na C), Kisukari na kadhalika. Mheshimu kila mtu!
Mtoto wako mtunze, mpe malezi bora kadiri Mungu anavyokujalia. Huwezi kujua kuwa pengine huyo ndiye mkombozi wako.
Wewe mtoto, ukizaliwa kwenye familia ya kimaskini, ikuongoze kuchangamsha ubongo. Wewe ndiye shujaa wa familia yako, jitume ubadili hali ya maisha ya wazazi wako na ndugu zako.
Kuzaliwa kwenye familia maskini ni ishara kuwa wewe ni mfalme. Ukipambana na kufanikiwa, unaitwa mfalme. Watoto wa Bakhressa wana fedha lakini siyo wafalme. Wamekuta mteremko wa maisha!
Unabisha? Daud alikuwa na uwezo gani wa kuwa Mfalme wa Israel mbele ya Saul? Daud alikuwa mtu duni kabisa lakini ndiye alimpiga Goliath. Usicheze na Mungu na uteuzi wake!
Zingatio kwa mama; Usitoe mimba, usinyonge kichanga wala usitelekeze mtoto. Huyo anaweza kuwa ndiye ameletwa na Mwenyezi Mungu kuwa mafanikio yako ila wewe unayakataa.
Baba; Usikatae mimba, usiwe chanzo cha mimba kutolewa, usikimbie damu yako, hakikisha unakuwa mlezi bora wa mwanao kwa hali na mali. Huwezi kujua ni zawadi gani ambayo mtoto huyo ametumwa na Mungu akuletee.
Wazazi; Hakikisha mnatoa malezi bora kwa watoto. Kile ambacho mnakifanya, kiwe ndiyo uwezo wa juu kulingana na nafasi. Wapeni watoto mapenzi makubwa na muwafanye wawe na furaha. Hao ni hazina yenu ya baadaye.
Mtoto; Wewe siyo chochote bila wazazi wako. Wangeamua, ungetolewa ukiwa mimba changa. Unapopata mafanikio, elewa kuwa wazazi wako wana thumni yao kwenye kila jasho lako. Wafanye wazazi wako wafurahie kipato chako, usiwaache wakipata shida na wewe upo ilhali uwezo wa kuwasaidia unao.
Mafanikio yako yatapaa zaidi, vilevile utakuwa ni mwenye kubarikiwa mno kama wazazi wako utawalinda kadiri kipato chako kinavyoruhusu.


Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment