ads 728x90 B

Mariah Carey kutoka uhudumu migahawani mpaka ubilionea




Luqman Maloto
ISHI kwa tabasamu kila siku. Hata uwe ndani ya nyakati ngumu kiasi gani, elewa tu kuwa utavuka. Mungu aliyekuumba anakuona, analo fungu lako bora kabisa.
Jambo la kutambua na kuheshimu ni kuwa Mungu anajua namna ya kukupa mafanikio. Anaweza kukufanikishia ukiwa kijana, wakati wa makamo au hata uzeeni.
Mafanikio yanaweza kuja kwako moja kwa moja (direct) au kupitia mlango wa nyuma (indirect). Ila yote ni mafanikio yako.
Mafanikio mlango wa nyuma; Yale ya kuja moja kwa moja hayahitaji ufafanuzi, kwa upande wa yenye kuja kupitia mlango wa nyuma ni kama vile mzazi kuvuna kupitia kwa mwanaye aliyemzaa na kumlea kwa tabu au hata mtoto aliyemuasili na kumlea.
Mungu amekuwa na utaratibu usiokoma, wa kupandikiza uzao wa matajiri na wafalme katikati ya familia zinazoishi kwenye lindi la umaskini.
Zingatio kwa mama; Usitoe mimba, usinyonge kichanga wala usitelekeze mtoto. Huyo anaweza kuwa ndiye ameletwa na Mwenyezi Mungu kuwa mafanikio yako ila wewe unayakataa.
Baba; Usikatae mimba, usiwe chanzo cha mimba kutolewa, usikimbie damu yako, hakikisha unakuwa mlezi bora wa mwanao kwa hali na mali. Huwezi kujua ni zawadi gani ambayo mtoto huyo ametumwa na Mungu akuletee.
Wazazi; Hakikisha mnatoa malezi bora kwa watoto. Kile ambacho mnakifanya, kiwe ndiyo uwezo wa juu kulingana na nafasi. Wapeni watoto mapenzi makubwa na muwafanye wawe na furaha. Hao ni hazina yenu ya baadaye.
Mtoto; Wewe siyo nchochote bila wazazi wako. Wangeamua, ungetolewa ukiwa mimba changa. Unapopata mafanikio, elewa kuwa wazazi wako wana thumni yao kwenye kila jasho lako. Wafanye wazazi wako wafurahie kipato chako, usiwaache wakipata shida na wewe upo ilhali uwezo wa kuwasaidia unao.
Mafanikio yako yatapaa zaidi, vilevile utakuwa ni mwenye kubarikiwa mno kama wazazi wako utawalinda kadiri kipato chako kinavyoruhusu.
PATRICIA HICKEY ANAVUNA ALICHOPANDA
Patricia Hickey ni mama wa mwanamuziki mkubwa duniani, Mariah Carey. Anavuna alichopanda, alichostawisha na alichokitunza. Anaishi kwa uhakika mkubwa. Maisha yamekuwa bora mno.
Maisha ya Pattie wakati anamzaa Mariah yalijaa dhiki mno. Kwanza alitengwa, yeye ni Mzungu mwenye asili ya Ireland, akaenda kuzaa na mtu mweusi, Alfred Roy, Mmarekani –Mwafrika mwenye asili ya Venezuela.
Babu yake Mariah, Francisco Nunez, alipohamia Marekani kutokea Venezuela, alijiongeza jina la Carey na ndiyo maana staa huyo anaitwa Mariah Carey.
Pattie alifanya kazi kama mkufunzi wa sauti (vocal coach), vilevile alijishughulisha na kuimba muziki wa Opera ambao asili yake ni jamii ya Latini, ukiimbwa zaidi makanisani, hasa Roman Catholic.
Pattie na Alfred walikutana wakati mama akiimba Opera, baba akifanya kazi ya uinjinia wa vyombo vya muziki. Na hapo ndipo mapenzi yao yalipoanza.
Walipofunga ndoa, familia ya Pattie iliwatenga kwa sababu hawakuona sawa mtoto wao Mzungu kuolewa na mwanaume mwenye asili ya Afrika.
Tabu ya kwanza ya Pattie ilianzia hapo. Alimpenda Alfred wake, wakati huohuo wazazi wake ndiyo hawakutaka kabisha kumsikia. Uamuzi wake ukawa kuziba masikio, akasikiliza moyo unavyoongea kisha akasonga mbele.
Wakiwa ndani ya Jiji la New York, kila kona waliishi Wazungu, na katika miaka ya 1960, Mwafrika alionekana kama kituko vile.
Familia ya Carey ilipata wakati mgumu sana. Jamii iliwasimanga na kuwatenga. Mama yake Mariah (Pattie), alibezwa kwa kufanya uamuzi ambao Wazungu waliuita wa kipumbavu, kuolewa na Mwafrika.
Mwaka 1969 wakati Mariah anazaliwa, alikuta maisha ni magumu mno kwa sababu ya jinsi familia yao ilivyokuwa inachukuliwa kama kituko.
Mariah aliwahi kusema: “Yalikuwa maisha magumu sana. Kila kona nilikutana na wasichana wa Kizungu, mimi nilionekana kituko. Niliishi kwenye familia isiyokubalika kabisa.”
Pattie naye alizungumza: “Nilitengwa na kuitwa kila jina baya lakini sikuweza kuiacha familia yangu. Watoto wangu ni muhimu sana kwangu, sikujali wana rangi gani. Kwao walionekana wabaya ila kwangu ni malaika bora kabisa.”
 Mateso hayakuwa hayo tu, msoto mwingine ulifuata baada ya Alfred na Pattie kuachana. Malezi ya mama tu bila uwepo wa baba, na kukosa kipato cha uhakika, vilisababisha changamoto kubwa.
Dada mkubwa wa Mariah, Allison aliambatana na baba yake, huku na Mariah mwenyewe na kaka yake Morgan wakibaki na mama yao.
Wakati wazazi wake wakitengana, Mariah alikuwa na umri wa miaka mitatu. Alianza kushuhudia maisha ya kuhamahama kwa sababu mama yake hakuwa na uwezo mzuri wa kumudu kulipia makazi ya kudumu.
Pattie aliendelea na kazi yake ya kuimba Opera, vilevile kufundisha sauti, kiasi alichopata alikielekeza kwa wanaye ambao aliota kuwapa maisha bora na ya uhakika.
Mariah alipokuwa na umri wa miaka minne, alianza kupenda muziki na mara nyingi akiwa nyumbani alipenda kuwa karibu na redio ili kusikiliza nyimbo na kukariri.
Alipoanza shule ya msingi, mapema sana alifanya vizuri masomo ya muziki, fasihi na sanaa kwa jumla.
Wakati Mariah anamaliza shule ya msingi, mama yake (Pattie), alikuwa ndiyo anafanikiwa kupata kipato cha uhakika, angalau akaweza kupata nyumba (apartment) ya kuishi na familia yake.
Mariah alipojiunga Shule ya Sekondari ya Juu (High School) ya Harborfields, iliyopo Greenlawnd, New York, tayari alikuwa na uwezo wa kuandika mashairi na kuyatungia sauti. Hivyo uwezo wa kutunga nyimbo aliupata kipindi hicho.
Kuhusu muziki, Maria anasema kuwa tamaa ya kufanikiwa kupitia muziki aliipata tangu akiwa mtoto kwa sababu ya namna ambavyo aliona maisha ya shida kwenye familia yao.
“Ilikuwa ngumu sana kwangu, kuhamahama kila mara, nikaona bora nijikuze mimi mwenyewe. Fikiria mwenyewe wazazi wangu wameachana, na kila siku nilijiona wa tofauti ukilinganisha na wengine waliokuwa majirani zetu.
“Nilikuwa mtu wa jamii tofauti, Mwafrika. Na hiyo wakati mwingine ni tatizo kabisa. Kama unaangalia njia fulani, kila anayepita ni msichana wa Kizungu, inabidi na mimi nipite, baadaye unagundua upo peke yako. Najikuta sifanani nao,” anasema Mariah.
Akiwa high school, Mariah alianza kujitahidi kuonesha kipaji chake katika matukio mbalimbali na kila aliyepata kumsikiliza, alimuelewa kwa haraka na kukubali kwamba hakika ana kipaji kikubwa.
Mariah alimtafuta mwanamuziki mkongwe wa R&B, Gavin Christopher, akawa anatunga naye nyimbo na kufanya mazoezi pamoja, hivyo kuendelea kukuza kipaji chake.
MARIAH NA MAISHA YA KUTANGATANGA
Pamoja na hali ya mama yake kuimarika, Mariah alipomaliza high school hakutaka tena kuendelea kukaa nyumbani, aliamua kujitupa kutafuta mafanikio ya kimaisha kupitia muziki.
Mariah anasema kuwa msukumo mkubwa kutafuta mafanikio ya muziki wake ulitokana na dhiki ndani ya familia yake lakini zaidi ya ubaguzi wa rangi aliokuwa anakabiliana nao.
Kazi kubwa alianza kuifanya baada ya kuondoka nyumbani kwao ni uhudumu katika migahawa. Alipata vibarua vya hapa na pale kwenye migahawa mbalimbali ili kupata fedha za kulipia pango na mahitaji mengine.
Rekodi zinaonesha kuwa Mariah alikuwa akitimuliwa kazi mara kwa mara. Inaelezwa kuwa hakuna mahali ambako aliwahi kufanya kazi na kudumu kwa wiki mbili.
Sababu ya kutimuliwa mara kwa mara ni kwa kuwa hakuwa akitoa muda mzuri kwenye kazi, badala yake aliwaza zaidi muziki wake na jinsi ya kutoka mpaka kufikia kuwa staa.
Alihangaika usiku na mchana kutengeneza kanda, kama demo iliyokuwa na nyimbo nne kisha kuanza kutafuta makampuni ya kuingia nayo mkataba kwa ajili ya kuundeleza muziki wake.
Baada ya kukamilisha demo yake, haikuwa rahisi kupata mkataba, kwani kila alipokwenda kwenye makampuni ya muziki, alifeli, zaidi aliambiwa hajui kuimba.
Katika kuhangaika huku na huko, ndipo Mariah alipokutanishwa na mwanamuziki wa Pop aliyekuwa akiinukia kwa wakati huo, Brenda K. Starr ‘The Freestyle Queen’.
Mariah alipokutana na Starr, waliunganisha urafiki ambao umuwezesha kuwafikia wadau wakubwa wa muziki. Hii ni kwa sababu kwa kipindi hicho Starr alikuwa ameshatengeneza jina kwenye muziki.
Hata hivyo, mambo bado hayakufunguka, mwaka 1988, Starr alimshirikisha Mariah kwenye demo yake yenye nyimbo kadhaa. Demo hiyo Starr aliipeleka kwa Tommy Mottola ambaye ni Bosi Mkuu wa kampuni kubwa ya muziki Marekani na duniani kote, Columbia Records.
Mottola alipopata demo hiyo, aliichukua na kuisikiliza akiwa kwenye gari, baada ya nyimbo tatu alijikuta anavutiwa na sauti ya Mariah.
Baada ya hapo Mariah ndiye aligeuka dhahabu, maana Mottola alimtafuta usiku na mchana ili amsainishe mkataba waanze kazi.
Zilipita wiki mbili Mottola akimtafuta Mariah, ndipo alifanikiwa kukutana naye, kufanya mazungumzo kisha kumsainisha mkataba ambao ulimuwezesha kuingia kwenye ramani ya biashara kubwa ya muziki.
Albamu yake ya kwanza yenye jina Mariah Carey, ilitikisa mauzo Marekani, Ulaya na duniani kote, vilevile ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye chati za Billboard 200, huku nyimbo nne zikikamata namba moja katika chati za Billboard Hot 100.
Hiyo ilikuwa rekodi ya peke yake, kwani kabla ya hapo ni Kundi la The Jackson 5, lililowahi kufanikiwa kuingiza nyimbo nne kwenye Billboard Hot 100 kutoka kwenye albamu moja.
UNADHANI NINI KILIFUATA?
Hakuna kingine zaidi ya kuogelea kwenye mafanikio na utajiri. Kuonana na Mottola kulibadili kila kitu, maana bosi huyo alihitaji fedha ambazo aliziona zipo kwa wingi kupitia kipaji kikubwa cha muziki alichonacho Mariah.
Ghafla Mariah akageuka bosi, kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990, magari ya kifahari na kuishi kwenye majumba mazuri yenye umiliki wake, siyo kitu cha ajabu tena.
Chini ya Columbia Records, Mariah aliendelea kufyatua kazi zenye mafanikio kwa miaka 10 mfululizo mpaka mwaka 2000 walipovunja mkataba.
Bosi Mottola alivutiwa na Mariah, wakavutiana, penzi jipya lilizaliwa, ikafuata ndoa lakini mwaka 1998 walitengana. Na hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya mkataba na Columbia kufikia ukingoni.
Mwaka 2000, alisaini mkataba wenye thamani ya dola milioni 100, na Kampuni ya Virgin Records America lakini ilibidi Mariah alipe dola milioni 50 kuununua mkataba huo ili apumzike.
Kipindi hicho Mariah alikuwa na msongo wa mawazo ya kutengana na Mottola. Mwaka 2002, Mariah alisaini mkataba wa fedha nyingi na Island Records ambao ulimrudisha kwenye soko, vivyohivyo kuendelea kutengeneza pesa nyingi.
Mpaka sasa, Mariah anakadiriwa kuwa ameshauza zaidi ya nakala milioni 200 katika kazi zake, hivyo kumfanya kuwa mmoja wa wanamuziki ambao wameuza zaidi katika historia ya muziki duniani.
UTAJIRI WA MARIAH
Mariah anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola milioni 550 ambazo kwa chenji ya shilingi ya Kitanzania, unapata takriban trilioni 1.1.
Kwa utajiri huo, Mariah amekuwa na wakati mzuri wa kumpa mama yake (Pattie), mahitaji yote muhimu na kuongezea starehe.
Pattie wa sasa, siyo yule wa kuungaunga maisha, anaendeshwa kwenye magari ya kifahari na madereva walioajiriwa na mwanaye (Mariah).
Umri unakwenda lakini afya bado ipo, maana anapata matunzo ya kutosha. Sasa anakula matunda matamu ya kuzaa na kulea mtoto katikati ya chuki na manyanyaso.
Pattie ana umri wa miaka 78 kwa sasa lakini hakuna usumbufu wa umri anaoupata, maana mahitaji yote muhimu anayapata kwa ukaribu, mwanaye amemuwekea watumishi wanaomuangalia kwa ukaribu sana.
Mariah yupo naye kwa ukaribu mno, anamtoa out na vizuri ni kuwa anajua kwamba mama yake anapenda maonesho ya muziki wa Opera, kwa hiyo humpeleka kuburudika.
USHUJAA WA PATTIE
Kama angefuata masharti ya wazazi wake na ndugu wengine kwamba hatakiwi kuwa na mwanaume mwenye asili ya Afrika, maana yake Mariah asingezaliwa.
Maana ukamilifu wa Mariah ni mchanganyiko wa Kibaiolojia kati ya Pattie na Alfred. Hakuna namna nyingine ya kumpaka Mariah nje ya hapo.
Hii inakuja na maana kuwa uamuzi wa kukubali kutengwa ndiyo ushujaa uliosababisha ujio wa Morgan,  Allison na Mariah.
Pointi ya pili ni jinsi alivyopambana kuwalea watoto wake. Alikuwa maskini lakini hakuchoka kutafuta mpaka kuhakikisha wanaye wanasoma japo kufikia kumaliza high school.
Pattie alifanya kazi usiku na mchana kwa kuungaunga mpaka kufanikisha kipato kizuri chenye kuwahakikishia mahitaji watoto wake, hasa Mariah na Morga, maana Allison alikwenda kuishi na baba yake.
Pattie aliigundua sauti nzuri ya Mariah na ndiye ambaye alianza kumtafutia njia za kukuza kipaji chake. Alimpeleka mpaka kwenye muziki wa Opera lakini Mariah hakuvutiwa nao. Alitaka kuimba Pop na R&B ili atengeneze fedha.
USHUJAA WA MARIAH
Kutambua kipaji ni jambo moja lakini kukifuatilia ni jambo la pili na lenye umuhimu mkubwa. Huwezi kukaa nyumbani kusubiri kwamba ndoto zako zitatimia.
Tafakari jinsi alivyokuwa binti mrembo lakini kwa sababu alikataa umaskini na dharau ya ubaguzi wa rangi, aliamua kutomsumbua mama yake, akakubali kufanya vibarua vya uhudumu wa migahawa ili apate fedha za kujisukuma kulipia pango, vilevile za kumuwezesha kutengeneza demo.
Ni mihangaiko hiyo ndiyo iliyomuwezesha kukutana na Starr kisha Mottola. Na zaidi ni uchapakazi wake ndiyo umewezesha kuwa mwanamuziki tajiri.
Ana umri wa miaka 46 kwa sasa, ni mama wa watoto wawili, wa kiume anaitwa Moroccan Scott Cannon, wa kike ni Monroe Cannon.
Baada ya kuachana na Mottola, mwaka 2008 alifunga ndoa na rapa, Nicholas Scott Cannon ‘Nick Cannon’ ambaye pia ni muigizaji, vilevile comedian.
 Cannon ndiye baba wa watoto hao wawili wa Mariah, kwani katika ndoa yake ya kwanza na Mottola, hawakubahatika kupata mtoto.
SOMO LA KUJIFUNZA
Vumilia manyanyaso na ukatize katikati ukijiamini kwa sababu hakuna gumu lenye kudumu. Mungu aliamua kumtengeneza Mariah kuwa malkia katikati ya familia dhalili kabisa.
Watu waliokuwa wakimcheka Mariah na ndugu zake kwa sababu ya Uafrika wao, leo hakuna mwenye ubavu wa kuinua sauti kufanya hivyo.
Mariah amewaacha mbali kabisa. Ni vizuri kujifunza kuwa unaweza kumdharau mtu kwa mtazamo wa juu lakini kumbe ndiye mwenye mbegu ziletazo matajiri, wafalme na malkia wa fani mbalimbali.
Mheshimu kila mtu na usibague, maana huijui kesho yako na yake. Amini tu kwamba kila mja na bahati yake.
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment