ALIPATA
kutokea kijana mzuri lakini maskini kwenye utawala wa Kifalme. Wazazi wa kijana
huyo walikuwa kwenye daraja la huruma kutokana na ufukara waliokuwa nao. Kijana
huyo aliitwa Jamal.
Kwa uzuri
wake Jamal alipendwa mno na wanawake. Hata hivyo, Mungu alimjalia unyenyekevu,
kadiri alivyopendwa ndivyo alivyozidisha nidhamu.
Sifa ya kuwa
kijana mwenye nidhamu, iliongeza mvuto wa Jamal. Wanawake kwenye makutano yao
ya ususi, visimani, mitoni, sokoni na kwingineko walimzungumzia Jamal kwa
kumpamba.
Jinsi
wanawake walivyokuwa wakimzungumzia, ndivyo na wengi wao walivyopata hamu ya
kuwa na Jamal kimapenzi. Miongoni mwa wanawake hao, walikuwepo pia wake za
watu.
Jamal
alimpenda Daniya, msichana mrembo aliyezaliwa na wazazi wenye uwezo wa wastani.
Jamal alifanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo yake ya kuwa na maisha
bora, vilevile kutimiza ndoto zake za kumuoa Daniya.
Ikaja
kutokea, kati ya wanawake waliompenda Jamal, alikuwepo pia mke wa mfalme.
Alitamani mno kuyapata mapenzi ya kijana mwenye kuimbwa kwa nyimbo nzuri za
kupendeza na kila mwanamke.
Mzozo ukawa
mkubwa zaidi baada ya mfalme naye kudhamiria kumtwaa Daniya ili awe mkewe.
Yaani akawe mke wa pili wa mfalme.
VITA YA
MAPENZI
Wazazi wa
Daniya walikubali binti yao aolewe na mfalme. Si unajua tena, mzazi anawezaje
kukataa mtoto wake kuolewa na mfalme?
Hata hivyo,
haikuwa rahisi kwa mfalme kumpata Daniya. Vivyo hivyo, haikuwezekana kwa mke wa
mfalme kulipata penzi la Jamal.
Mfalme baada
ya kuona dhamira yake ya kumuoa Daniya inashindikana, alimuona Jamal adui,
kwamba Daniya hisia zake zote zipo kwa Jamal. Hivyo, mfalme akapanga kumuua
Jamal.
Mke wa
mfalme naye kutokana na wakati mgumu ambao aliupata katika mpango wake wa
kulinasa penzi la Jamal, akili yake ikamtuma kumuua Daniya.
Mipango
ikasukwa! Kuna kipindi Jamal alifungwa gerezani na kuandaliwa kuuawa lakini mke
wa mfalme alimtorosha.
Mke wa
mfalme pia akaagiza Daniya akamatwe na kuwekwa jela, mfalme alipopata taarifa
alitoa amri aachiwe huru.
Kuna wakati
mke wa mfalme alimnyatia usiku na mchana Jamal. Alitengeneza mpaka funguo za
mlango wa Jamal. Mke wa mfalme aliingia chumbani kwa Jamal. Jamal alipoingia
chumbani kwake, alimkuta mke wa mfalme akiwa mtupu kisha kumlazimisha washiriki
mapenzi.
Siku moja
kulitokea mtifuano mzito chumbani kwa Jamal baada ya kuingia na kumkuta mke wa
mfalme amejilaza akiwa mtupu. Mke wa mfalme alilazimisha mapenzi, Jamal
alikataa katakata kuwa hawezi kumsaliti Daniya wake.
Baada ya
mvutano wa muda mrefu, mke wa mfalme alisema: “Nilijitahidi kukulinda mfalme
asikuue, ila kwa hivi ulivyonidhalilisha, sasa huna budi kufa.”
Mke wa
mfalme alitoka chumbani na kuwapitia walinzi wake nje kisha wakarejea kwenye
kasri la mfalme akiwa na hasira kali.
Njia nzima
hakuzungumza na mtu yeyote. Alichotaka ni kufika kwa mumewe (mfalme) na
kumshawishi atume vikosi vyake vikamuue Jamal.
Mke wa
mfalme aliingia ndani himahima, moja kwa moja mpaka chumbani kwa mfalme.
Alimkuta mfalme katikati ya jaribio la kumbaka Daniya.
Hasira za
mke wa mfalme ziliongezeka, alimsukuma mfalme na kwenda kumkaba shingo Daniya,
ugomvi ukawa mkubwa mno.
Mfalme baada
ya kuona hali ni mbaya, aliita askari wake, wakawatenganisha mke wa mfalme na
Daniya ambaye alibaki analia. Muonekano wake ulithibitisha unyonge wake na
maumivu makali juu ya uonevu aliokuwa anafanyiwa.
Mke wa
mfalme na Daniya baada kushatenganishwa, kila mmoja alifungiwa kwenye chumba
chake. Upande wa pili mfalme alipokea taarifa kutoka intelijensia yake kuwa
mkewe alionekana mara kadhaa akiingia na kutoka chumbani kwa Jamal.
Taarifa hizo
ziliamsha hasira kali kwa mfalme. Yeye aliamini kuwa Jamal ana uhusiano na
mkewe. Akajiongeza pia kwamba Daniya hamtaki kwa sababu ya kiburi anachopewa na
Jamal.
Mfalme
akaagiza askari wake wakamteke na kumuua Jamal. Askari 20 wa mfalme wakiwa na
silaha zao, walivamia nyumbani kwa Jamal na kumteka kisha kwenda kumuua porini.
Jamal
alipigwa mno, alipata mateso makali kupita kiasi. Agizo la mfalme ni kuwa Jamal
atenganishwe kichwa na kiwiliwili kisha kichwa apelekewe ushahidi.
Pale
walipokuwa wanamtesa Jamal ni chini ya mwembe. Hivyo kabla Jamal hajafa na
wakiwa wanajiandaa kumchinja kama walivyoagizwa na mfalme, tawi kubwa la mwembe
lilikatika na kuwaangukia walinzi watatu kisha kundi kubwa la nyuki
liliwashambulia.
Walinzi 17
walikimbia na nyuki waliwakimbiza na kuwang’ata kadiri walivyokimbia. Walinzi
watatu walikuwa hoi kwa maumivu ya kuangukiwa na tawi kubwa la mwembe na
walishindwa kulisukuma pembeni ili watoke. Lilibaki limewakandamiza huku
wakipiga kelele, mwisho fisi walitokea na kuwala.
Nyuki wote
waliwakimbiza wale askari wa mfalme waliokuwa wanakimbia. Jamal akiwa na
maumivu makali alinyanyuka na kukimbia kwa kujikokota kuelekea usawa wenye
usalama.
Mfalme
alishangaa giza linaingia askari wake hawarudi. Akiwa anasubiri kwa hamu kubwa,
aliona askari sita wakiwa wanaingia kichovu, wamevimba. Wakasimulia madhila ya
tawi la mwembe na nyuki, vilevile kutokewa na chatu ambaye alimmeza mwenzao
mmoja. Na kwamba wengine walipoteza maisha kwa shambulio la nyuki pamoja na
kuangukiwa kisha kubanwa na tawi la mwembe.
Upande wa
pili Daniya alipofunguliwa kwenye jumba la mfalme, aliona akirejea nyumbani
kwao, angetafutwa na kuuawa, hivyo akaamua kwenda porini ili apotelee mbali.
Safari ya
usiku na mchana, akila matunda, akinywa maji kwenye madimbwi na chemchemi za
porini, hatimaye aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu.
Jamal baada
ya kunusurika kifo, aliamua kufanya maisha yake porini. Alitengeneza kibanda na
kuishi kwa kuwinda wanyama pori. Akiwa kwenye mawindo yake, siku moja alimuona
mwanamke amelala, akamsogelea.
Hakuamini
macho yake alipogundua ni Daniya. Mwanamke anayempenda kuliko uhai wake.
Alimbeba mpaka kwenye kibanda chake. Alipomfikisha, alichukua maji na
kumkandakanda. Daniya alizinduka na kupigwa na mshangao kuona anayemhudumia ni
Jamal wake. Mwanaume anayemiliki kila kitu ndani ya moyo wake.
Jamal alimpa
chakula Daniya, alimpa maji akanywa. Walizungumza mengi. Wakapeana ahadi kuwa
kifo pekee kitawatenganisha. Wakakumbatiana na kusemezana kuwa jinsi
walivyokutana na changamoto, ndivyo mioyo yao inavyoshibana. Kwamba misukosuko
imekuza mapenzi yao.
Siku moja
Jamal akiwa kwenye mawindo yake, alisikia nyasi zinatikisika akajua ni myama,
akalenga mshale lakini ajabu ikatoka sauti ya binadamu. Ghafla Jamal akawa
amezungukwa na askari wa mfalme.
Kumbe,
mfalme baada ya kumtafuta sana Daniya, aliamua kuchukua askari wake na kuingia
nao porini kumsaka. Wakiwa katikati ya pori, aliwaaga askari wake na kwenda
pembeni kujisaidia. Ni hapo ndipo Jamal alihisi ni mnyama, pale nyasi
zilipokuwa zinatikisika.
Mshale
uliingilia mkono wa kushoto na kuzama moja kwa moja kwenye moyo. Mfalme
alifikwa na mauti palepale. Askari kuona mfalme wao amekufa, wakaanza kumsulubu
Jamal.
Wakiwa
wanataka kumuua, walitokea simba watano, wale askari kila mmoja akakimbia
upande wake, simba wakawafukuza.
Jamal
alipona kwa mara nyingine, alirejea kwenye kibanda chake na kumsimulia Daniya.
Wote walishikwa na woga juu ya kile ambacho kingetokea.
Askari wengi
waliuawa na simba, huku wengine ikishindwa kujulikana walipopotelea. Askari nane
walirejea salama na kutoa taarifa za kuuawa kwa mfalme, aliyepigwa mshale na
Jamal.
Kati ya
askari hao nane, watatu walikuwepo kwenye jaribio la kwanza la kung’atwa na
chuki, hivyo waliwasimulia maajabu wazee kuwa Jamal anaweza kuwa siyo binadamu
wa kawaida.
Baada ya
tafakuri ya wazee kwa wiki nzima, lilipatikana jawabu la kumtafuta Jamal ili
asimikwe ufalme kutokana na historia ya nidhamu yake, jinsi ambavyo amekuwa
akipona katika mkono wa kifo, hujuma alizofanyiwa za kutaka kuuawa, vilevile
anavyopendwa na watu.
Ujumbe wa
wazee wanne kwa kuongozana na askari sita, uliingia porini kumtafuta Jamal.
Baada ya majuma mawili, waliweza kukizingira kibanda cha Jamal kisha kumpata
mwenyewe na kuzungumza naye.
Wazee
walirejea kishujaa. Ilifanyika sherehe kubwa ya kumsimika Jamal ufalme. Baada
ya hapo ndoa ilifungwa kisha Daniya naye alisimikwa umalkia. Jamal akawa
mtawala mkuu, Daniya akatambulika kama first lady.
NINI
TAFSIRI?
Mungu
analinda wakati wote. Akiamua usipate baya lolote na halitakutokea.
Hapo ulipo,
hujui ni mipango mingapi miovu imewahi kupangwa ili kuondoa uhai wako na Mungu
akaidhibiti.
Jamal na
Daniya, walikula raha, heshima na madaraka makubwa baada ya kulindwa na Mungu.
Jiulize tawi
la mwembe lilikatwa na nani? Nyuki walitokea wapi? Simba walinusa nini? Na kwa
nini Simba hawakujishughulisha na Jamal, badala yake waliwafuata askari
waliokuwa wanakimbia?
Ni kwa nini
Jamal na Daniya hawakuwahi kushambuliwa na wanyama hata mara moja? Shika jibu;
Ulinzi wa Mungu upo karibu mno na waja wake wema. Waja wake wenye kuonewa.
Mungu hapendi mja wake aonewe.
Dk. Steven
Ulimboka alipona vipi Msitu wa Pande? Unadhani waliomfanyia unyama ule walitaka
leo awe hai? Nani aliyempeleka Msitu wa Pande mtu yule aliyemuona kwa mara ya
kwanza? Polisi nao walimkuta akipumua. Acheni Mungu apewe utukufu wake!
Ukidhani Absalom
Kibanda yupo hai kwa sababu waliomvamia na kumfanyia unyama uliogharimu afya na
macho yake hawakutaka kumuua, utakuwa unajidanganya.
Hata wewe
hapo ulipo, inawezekana kabisa imeshakuwepo mipango kadhaa ya kuukatisha uhai
wako lakini ulinzi imara zaidi wa Mungu, unateketeza silaha za adui bila wewe
kutaarifiwa.
Wengi
hudhani bunduki ni silaha bora zaidi ya kujilinda. Mbona tunao viongozi wengi
waliouawa na kupinduliwa wakati walikuwa wanalindwa na bunduki?
ISHI KWA
IMANI
Huna fedha,
tena wewe ni maskini, lakini unayo sababu moja tu muhimu ya kuringa. Kwamba
wewe ni mteule wa Mungu ambaye ndiye mlinzi mkuu wa maisha yake.
Ni nani
mwenye kuweza kufanikisha dhamira ovu juu yako kama Mungu Mfalme hataki? Ukielewa
hivyo, hutakuwa na hofu ya kitu. Mungu anakulinda mno.
Acha maadui
waje, Mungu atakuongoza kuwashinda. Bunduki silaha dhaifu mno, makombora na
vifaru ambavyo Mungu ameviweka kukulinda vina uwezo mkubwa kuliko Jeshi la
Marekani. Kaa na Mungu kila siku, kisha jiamini!
Ndimi Luqman
Maloto
0 comments :
Post a Comment