ads 728x90 B

Wanamchezea sharubu JK; Magufuli soma mchezo!



http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2935672/medRes/1161877/-/d7fn0tz/-/Magufuli+%2526+Kikwete+PHOTO.jpg
Luqman Maloto
NAPATA picha ni kwa nini viongozi wengi hutamani kukaa madarakani mpaka kifo kiwakute wakiwa wanatawala.
Kenneth Kaunda ‘KK’ alipokabidhi usukani wa nchi ya Zambia kwa Fredrick Chiluba (marehemu) mwaka 1991, ilikuwa kama ameruhusu kibao kimgeukie.
Askari waliokuwa watiifu kwake kipindi chote cha miaka 27 ya utawala wake, waligeuka chungu ya Kaunda kwa agizo la Chiluba. Zipo nyakati walielekeza bunduki kwa mwasisi huyo wa Taifa la Zambia.
Wapo viongozi waliokuwa watiifu kwa Kaunda lakini walijipendekeza kwa Chiluba, na kwa kujipendekeza kwao ikabidi wamsaliti Kaunda kwamba alikuwa kiongozi mbovu.
Ni kwa mwendo huohuo, waliomsifu Chiluba kwa uongozi uliotukuka, ndiyo baadaye walimlamba miguu mrithi wake, Levy Mwanawasa, kwamba yeye ndiye hasa mkombozi wa Zambia, huku wakimwita Chiluba mharibu nchi, dikteta, fisadi na mpoka haki za binadamu.
Chiluba angesoma mabadiliko ya waliokuwa watiifu wa Kaunda walivyogeuka wapambe wake kipindi ambacho yeye anamshughulikia rais huyo wa kwanza wa Zambia, labda angeshtuka.
Kilichotokea ni kuwa Chiluba alishtuka pale watiifu wake walipogeuka wapiga makofi wa Mwanawasa, kipindi hicho akimshughulikia yeye. Ni nyakati, ukishakabidhi madaraka lazima uisome namba, hata kama ni kimyakimya.
Hata Bakili Muluzi aliisoma namba Malawi alipokabidhi rungu la utawala kwa Bingu wa Mutharika.
Wapo waliopata kumgeuza Muluzi Mungu wao, kumpelekea umbea na kumpa sifa kemkemu za kipambe, wakinywa kahawa pamoja Ikulu ya Malawi, Lilongwe, baadhi yao walimuimbia mapambio Mutharika (Bingu), alipokuwa anamshughulikia Muluzi.
Na hawakusita kusema kuwa Muluzi ndiye aliibomoa nchi. Huu usiuite usaliti, bali ni fikra maslahi za binadamu. Kwamba ukiwa na ugali utanyenyekewa na kuimbiwa mapambio ya aina yote, ukiondoka, sifa zote zitamwelekea mwenye ugali kwa wakati wake.
Ni kama sasa, Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, yupo kwenye kipindi cha mgeuko. Waliokuwa watiifu wake ndiyo wanaosema kipindi chake kilikuwa hovyo kabisa.
Haiwezekani hii ikawa haimuumi! Ila bila shaka naye kwa wakati wake alipokea ‘visifa’ vingi vya kipambe, vilevile aliambiwa mengi kuhusu mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.
Unadhani Mkapa alifurahi kuitwa fisadi wakati wa utawala wa JK? Ilimuuma lakini alikosa namna ya kufanya kwa sababu ni kipindi ambacho alikuwa ameshakabidhi mamlaka. Hakuwa mtoa amri, mtengua uteuzi wala msitisha ajira.
Sura hiyo iende hata kwa Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, naye alipoitwa kiongozi goigoi na waliokuwa wasaidizi wake kwa sababu ya kutetea ugali wao kwa Rais Mkapa, aliumia, na vile Mungu alimuumba mpole, basi akavumilia na kuacha yapite.
Hivyo basi, huu ni wakati ambao JK anakumbuka mamlaka yake, anajikuta nyakati zimepita, na sasa waliokuwa wasaidizi wake wanathubutu kuingiza vidole machoni mwake.
Maneno ya hivi sasa kutoka kwa waliokuwa watiifu wake, ni sawa kabisa na kumchezea sharubu na kumpiga masingi, yaani ule mtindo wetu Uswahilini, wa kusukuma kichwa cha mtu kwa vidole.
Akiwa pale Msoga, Bagamoyo, Pwani, JK anaweza kukumbuka jinsi wanaomsema leo kuwa yeye ndiye alikuwa tatizo kuu katika awamu yake, walivyokuwa wakimnyenyekea na kumpongeza kwa uongozi uliotukuka.
Anaweza kukumbuka jinsi watu hao walipokuwa wakipokea simu yake kwa unyenyekevu wenye nakshi za woga huku wakijiuliza, “sijui mkuu anataka kuniambia nini?” na katikati ya mazungumzo jibu lao likuwa “ndiyo mkuu… ndiyo mkuu!”
Wazungu wanao msemo wao kuwa Things Will Never be the Same Again, kwamba mambo hayawezi kuwa na sura ileile tena. Kwa hiyo wanajua JK siyo rais tena, zama zake zimeshaondoka, kwa hiyo wanampigia zumari mkuu wa sasa.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, aliripotiwa akisema kuwa tatizo la serikali iliyopita ni mkuu wa nchini.
Kwa maana hiyo, anakosoa aina ya uongozi wa JK kwamba yeye ndiye alikuwa tatizo kuu.
Kauli ya Kitwanga inaweza kubeba tafsiri chanya au hasi kulingana na mapokeo, ila ukakasi ulio wazi ni kuwa yeye alikuwa sehemu ya uongozi uliopita, na alikuwepo kwenye Baraza la Mawaziri la JK mpaka mwisho.
Kwanza tumuelewe Kitwanga. Alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kati ya mwaka 2010-2012, akawa naibu pia katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, kati ya mwaka 2012-2014.
Na kuanzia mwaka 2014 mpaka JK alipokabidhi rungu la uongozi kwa Magufuli, Novemba 5, 2015 alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Kitwanga alidumu miaka yote mitano katika awamu ya pili ya JK kwa maono yapi? Ni dhambi kubwa kwenye uongozi kuhudumia wananchi chini ya mtawala ambaye anakufanya ushindwe kutimiza maono yako ya kutoa huduma.
Muongozo wa taaluma ya uongozi, unaelekeza kwa mtu kujiweka pembeni pale anapoona kuna hali ya kusigana kati ya dhamira yake na ile ya kiongozi wa juu.
Ni busara na uungwana kujiuzulu, unapoona maono yako au mtazamo ulionao siyo pacha na ule wa kiongozi wa juu.
Uongozi ni maono ambayo hujengwa na mtazamo. Ni usaliti wa hali ya juu kwa watu wenye kusigana mitazamo, kufanya kazi serikalini kama mtu na bosi wake.
Mtu kuwepo kwenye uongozi ambao hakubaliani nao, kisha akadumu mpaka mwisho, huyo anakuwa si mtumishi mwenye utashi, bali mtumikia maslahi.
Kwamba anafanyia kazi maslahi yake, wakati kile anachokifanya na maagizo ambayo anayatekeleza kama anavyotakiwa na bosi wake, ni kwa shingo upande.
Tafsiri ya kiongozi mwenye kufanya vitu kwa shingo upande pia ni usaliti. Ama anamsaliti kiongozi wake wa juu au wananchi wenye kuhitaji kuhudumiwa kwa nyoyo zenye ukunjufu usio na shaka.
Kitangwa hakupaswa kuibuka sasa na kusema JK ndiye alikuwa tatizo. Alitakiwa kujiondoa mapema. Zipo njia nyingi kwa waziri au mteule yeyote kujiuzulu  bila kutengeneza rabsha na mkuu wa nchi.
Kama angesimama leo akasema kuwa JK alikuwa tatizo ndiyo maana alijiuzulu uongozi au alikataa uteuzi, angekuwa na hoja yenye mantiki, ila anachokizungumza sasa hakina ladha nzuri masikioni.
Sanasana anajichonganisha na JK mwenyewe, vilevile anajitafutia uhusika wa ndumilakuwili ambao siyo mzuri kuwa nao kiongozi kama yeye.
Kiongozi anapaswa kuwa na msimamo thabiti, na hatakiwi kuwa na kauli zenye viashria vya kushindwa na visingizio. Alichokisema Kitwanga ni kutaka kujivua kasoro za utawala uliopita, kwa hiyo anataka JK ndiye atajwe kama tatizo sugu.
Ni dhambi kubwa kufanya jambo pamoja halafu yakionekana makosa, mtu aibuke aseme tatizo alikuwa mwenzake. Utendaji wa pamoja unakuwa na matokeo ya kuwajibika kwa pamoja. Ni utoto kunyoosheana vidole.
Kitwanga alipaswa kusema “utawala uliopita tulikosea sehemu kadha wa kadha”, siyo kumvalisha lawama zote JK. Kama aligundua mapema kuwa JK ndiye alikuwa shida, hakupaswa kukaa barazani mpaka mwisho wa utawala wake.
Kabla ya Kitwanga, alinukuliwa pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba akisema: “Serikali iliyopita watu walifanya kazi kwa mazoea.”
Kimsingi kumekuwa na hoja za hapa na pale kumsema Rais Kikwete na utawala wake kuwa ulileta au ulilea matatizo.
Hii kwa hakika inamuuma Rais Kikwete kwa namna ambavyo anasemwa. Anarushiwa maneno utadhani hajawahi kuihudumia nchi hii kwa mengi yenye kupaswa kupongezwa na kupigiwa mfano.
Yote hayo yanatokea kwa sababu Things Will Never be the Same Again! Ndiyo zama za JK haziwezi kujirudia tena, hivyo watu wanapata fursa ya kumsema kwa namna watakavyo.
Mwingine atasema ili ajioneshe kwa mkuu wa nchi aliyepo kuwa yeye ndiye mwarobaini wa matatizo ya nchi, kwa hiyo yaliyokwama sababu ni JK.
Bila shaka hata JK mwenyewe anaumia na kufikiria watu aliowaamini na kuwapa nafasi katika serikali yake, tena pengine walifanya makosa ya hapa na pale lakini aliwavumilia. Aliamini anawalea, ila sasa wanamsimanga. Shida ni kwamba hana jinsi, maana hizi ni zama za Magufuli.
Angekuwa na nafasi sasa au kama angefunuliwa kabla, bila shaka asingewapa nafasi kwenye serikali yake wale wote ambao wanamsema kuwa aliharibu.
Ni somo pia kwa Dk. Magufuli kutambua kuwa watu wanaomuimbia mapambio leo, si ajabu baada ya mwaka 2020 au 2025 akishakabidhi nchi kwa mrithi wake, atajikuta naye anasimangwa.
Ushauri wangu kwa Dk. Magufuli ni kuwa achunge sana msitu wa watu ambao leo hii wanampamba na kumsifu sana kuwa yeye ndiye kiongozi wa mfano, ikiwemo kumwahidi kuwa watakuwa naye pamoja daima, ipo siku atakapogeuka atajikuta peke yake. Kugeukageuka ndiyo zetu binadamu!


Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment