ads 728x90 B

Shein anastaajabisha, Seif anashangaza, Jecha anaduwaza




Na Luqman Maloto
MASIKITIKO yapo, mshangao unakuwepo na kuvunjika mbavu nako kupo. Zanzibar ya tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015 kisha kuahirishwa kabla ya kuitishwa wa marudio ni mazingaombwe tupu.
Kwanza vuta subira kidogo nikwambie Zanzibar ni pacha na nchi gani. Kwa kinachotokea sasa kuelekea uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu na yale yaliyojiri kabla, utadhani Zanzibar ina unasaba na Haiti. Ni kama mapacha!
Ingekuwa na mataifa yanapimwa undugu kwa kutumia teknolojia ya ugunduzi wa vinasaba (DNA), basi tungeziingiza Zanzibar na Haiti maabara tupate majibu. Tatizo nchi hazipimwi kama mwanamuziki Diamond Platnumz na mwanaye Tiffah. Nimechomekea!
Undugu wa Zanzibar na Haiti; Kwanza zote zilifanya Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015 lakini hazikuweza kupata rais.
Tofauti yao; Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, alifuta matokeo kwa maelezo kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi.
Haiti, uchaguzi ulifanyika lakini matokeo ya jumla hayakufanikisha kumpata rais kwa sababu hakuna aliyepata kura zaidi ya asilimia 50. Hivyo basi, wagombea wawili wa juu, Jovenel Moise aliyepata asilimia 32 na Jude Celestin asilimia 25 walipaswa kurudia uchaguzi (runoff election).
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) alikuwa anatetea kiti chake, lakini Haiti, rais wake, Michel Martelly hakuwa mgombea, baada ya kuongoza taifa hilo tangu mwaka 2011, hivyo kuwa na kikomo cha kikatiba lakini anampigania Moise kushinda kiti hicho.
Zanzibar na Haiti, kote wapinzani wamegoma kurejea kwenye uchaguzi wa marudio, japo sababu ni tofauti. Zanzibar, mgombea wa Cuf, Seif Sharif Hamad alitaka atangazwe kwa kuwa alishinda. Haiti, Celestin alilalamika kuwa atachezewa rafu.
Haiti uchaguzi wa marudio ulipangwa Desemba 27, 2015 ukaahirishwa, ukatangazwa kufanyika Januari 17, mwaka huu, ukapigwa tena kalenda mpaka Januari 24, mwaka huu, Celestin akasisitiza kutoshiriki.
Wachambuzi walitoa uelekeo wa uchaguzi kwenda kufanyika kwa ushiriki wa mgombea mmoja yaani Moise. Hata hivyo, kelele zilipokuwa nyingi, Februari 7, mwaka huu, seneti (bunge) ilimuweka kando Martelly na kumteua rais wa mpito, Jocelerme Privert ambaye ni Rais wa Seneti, Jamhuri ya Haiti.
Sasa uchaguzi wa marudio (runoff) wa Hait umepangwa kufanyika Aprili 24, mwaka huu. Itakuwa ni ama Moise na chama chake cha PHTK na Celestin wa LAPEH.
Zanzibar, baada ya matokeo kufutwa, ilifuatwa ile hali ya “nitangazeni… turudie.” Mara tukashuhudia tukio la kiungwana mno, Seif na Shein kwa kushirikisha pande zao, walikutana kufanya mashauriano.
Mara safari za Ikulu kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli zikachukua nafasi. Alianza Seif, akafuata Shein, lugha ikawa: “Tunaendelea vizuri na mazungumzo.”
Upepo ulibadilika siku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi, alipokwenda Ikulu, Magogoni kumwambia Dk. Magufuli: “Wazanzibar wanangoja uchaguzi kwa hamu. Amani imetamalaki.”
Seif na Cuf wakasisitiza kutoshiriki. Baada ya kauli ya Iddi, Jecha akatangaza uchaguzi Machi 20, mwaka huu na akasisitiza hakuna mgombea kujitoa.
Dk. Magufuli akaambiwa simamisha uchaguzi, maridhiano yachukue nafasi. Siku ikawa nzuri na jua lake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva, akamtembelea Magufuli, walizungumza pembeni.
Kisha Lubuva mbele ya waandishi wa habari akasema: “Nilikwenda kumwabia Rais Magufuli sisi ni tume huru na hatupendelei. Hata Zanzibar watu wanasema Magufuli aingilie kati, Zec ni tume huru, Rais hawezi kuiingilia.”
Bila shaka Dk. Magufuli alipumua, maana baada maneno hayo ya Lubuva, naye aliitisha mkutano na wazee wa Dar es Salaam, akasema: “Zec ni tume huru, siwezi kuiingilia.”
Hebu jiulize kama mimi; Ikiwa ni kweli Zec ni huru na haiingiliwi, iweje Jecha hakutangaza uchaguzi wa marudio mpaka mazungumzo ya Seif na Shein yalipokwama?
Ni kwa nini Jecha alitangaza uchaguzi wa marudio muda mfupi tu baada ya Iddi kuzungumza na Dk. Magufuli kuwa Wazanzibar wanajiandaa kwa uchaguzi na kwamba amani ni tele visiwani?
Ni sababu gani uchaguzi wa marudio ulichelewa kutoka Oktoba 25, 2015 mpaka Machi 20, mwaka huu? Yaani miezi mitano kasoro siku siku tano (siku 147).
NGOJA SASA NIMSHANGAE SEIF
Awali kabisa nimpe pole kwa kuumwa. Namuombea kwa Mungu amponye ili arejee kwenye afya yake imara.
Mshangao wangu ni kuwa kitendo chake cha kususa kushiriki, hakina faida kwake binafsi wala chama, ni sawa tu na kumsusia fisi bucha au nguruwe shamba la mihogo.
Uamuzi wa kusuia uchaguzi una faida tu ya kutaka kuhurumiwa na mataifa ya kigeni lakini hayamjengi katika ushindani wa kisiasa.
Ni kwamba kwa uamuzi wake, maana yake wafuasi wake wengi hawatapiga kura, hivyo Shein atapata urahisi wa kushinda.
Itatokea kama ya Angola mwaka 1992. Uchaguzi wa awali Eduardo dos Santos wa MPLA alipata asilimia 49 na Jonas Savimbi wa Unita alipata asilimia 40. Hakuna aliyezidi asilimia 50.
Uchaguzi wa marudio ulipoistishwa Savimbi alisusa kwa madai ya kuibiwa kura. Haikumsaidia, Santos aliendelea kuongoza, Savimbi akarudi msituni. Mwisho aliuawa.
Seif angeweza kusimama imara kutetea ushindi wake kwa kukubali kushiriki, ila tume ifanyiwe mabadiliko. Ahamasishe watu wake kumpigia kura, hakika kama ipo ipo tu!
Kususa kwake ni chereko kwa Shein ambaye akili yake yote ni kuhakikisha amani inakuwepo. Mengine atavumilia tu. Kumsusia uchaguzi kiongozi aliye madarakani kwa nchi zetu za Kiafrika ni sawa na kumpa urahisi wa kushinda.
JECHA ANADUWAZA
Hafanani na Sam Kivuitu (marehemu), yule alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya, aliyetangaza matokeo kinyumenyume na kusababisha damu imwagike mwaka 2008, ila kuna hatua wanaendana.
Kivuitu alibadili matokeo, ila Jecha alifuta matokeo. Jecha alisema uchaguzi uliharibika, ila hakusema nani aliharibu. Kasoro hazikufafanuliwa. Mambo yamekwenda kibubu-bubu.
Jecha anaduwaza maana kama watu waliharibu uchaguzi ni kwa nini hawakuchukuliwa hatua? Nani anaweza kuelewa uchaguzi uliharibika bila walioharibu kutambuliwa na kubainishwa waziwazi?
SHEIN ANASTAAJABISHA
Uchaguzi utafanyika na bila shaka atashinda, maana Seif kamsusia. Swali kwake, ataongoza kwa raha ipi akiwa na watu wengi ambao hawana furaha wala radhi na uongozi wake?
Tunajua wanasiasa wanapenda sana kupendwa, matokeo yaliyofutwa yameshatoa uelekeo jinsi asivyokubalika Pemba. Hali ikiwa hivyo, halafu serikali yake inakosa uungwaji mkono. Bila shaka atakuwa rais mwenye wakati mgumu.
Yeye ndiye Rais wa Zanzibar, anapaswa kuwa mkali kwa rasilimali za Wazanzibar na Tanzania kwa jumla. Kama ndivyo, ni kwa nini hajachukua hatua za kushughulikia waliovuruga uchaguzi, maana wameharibu rasilimali za umma?
Ni kwa nini hajamfukuza kazi Jecha kwa uzembe, baada ya tume yake kushindwa kufanya kazi yake inavyotakiwa hadi kukaribisha uchaguzi wa marudio? Utaona kuwa uchaguzi unakwenda kufanyika ila kwa hakika, Shein anastaajabisha.
Unaweza kulazimisha uchaguzi na ukatawala kwa chereko zote katika mazingira ya mfumo wa ukiritimba wa chama kimoja (one-party dominant system), Zanzibar kwa sasa ni mlinganyo wa vyama viwili (two-party system) kati ya CCM na Cuf, na wananchi wamegawanywa hivyo.
Hata kama machafuko hayatatokea, lakini kundi kubwa litakuwa na kinyongo na uongozi wa Shein. Kama hili halifikirii, kweli anastaajabisha!

Mungu Ibariki Zanzibar, Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia.

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mwandishi wa vitabu, vilevile mchambuzi w masuala ya siasa, utawala, jamii na sanaa.
  

Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment