Luqman Maloto
POLISI Tanzania hugeuka watumwa wanapowakamata watumiaji wa
madawa ya kulevya, kwani hulazimika kuwatafutia mihadarati hiyo na kuwapa
watumie ili kuwapa ahueni wakiwa mahabusu.
Watumiaji wa madawa ya kulevya, maarufu kama mateja, hupatwa
na maumivu makali, kukosa nguvu, mwili kulendemka na kuwashwa mwili mzima pindi
wanapopitisha muda bila kutumia mihadarati hiyo, hivyo kuwa usumbufu mkubwa kwa
polisi waliowakamata.
www.luqmanmaloto.com
inazo taarifa mpya na za muda mrefu kuhusu madhila ambayo polisi huyapata
kutokana na kuwakamata mateja na kuwahifadhi mahabusu, hivyo kuwafanya wakae
muda mrefu pasipo kupata madawa yao.
Mkuu wa kituo kimoja cha polisi, ndani ya Mkoa wa Kinondoni,
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, amemweleza mwandishi wetu kuwa kumfungia teja
mahabusu ni mateso, kwani zipo nyakati hulazimika kutafuta unga ili kuwapa
watumie.
Mkuu huyo wa kituo aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa sababu za
kikazi, alisema: “Kukaa na mateja mahabusu ni utumwa, ukiwa nao lazima ujiandae
kuwatafutia madawa yao wavute. Na huwa inatubidi tufanye hivyo ili kuwasaidia
wawe sawa.”
Aliongeza, mateja huwaelekeza mahali ambako huwa wanauziwa
unga, hivyo kwenda kuwakamata wauzaji na madawa yao ambayo badala ya kutumika
kama kizibiti cha wauzaji mahakamani, huwapa watumiaji waliothirika kwa kukosa
madawa.
Alisema, ugonjwa wa mateja unaosababishwa na kukosa madawa
ya kulevya, unaojulikana kama alosto, ni mbaya mno na husababisha kero kubwa
kwa watuhumiwa wengine waliopo mahabusu ambao siyo watumiaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Wilibroad
Mtafungwa, alisema kuwa nyakati alipokuwa Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD), Kinondoni,
alishuhudia kadhia ya mateja kuchafua mahabusu kutokana na kuzidiwa na alosto.
“Wakishazidiwa na ugonjwa wao unaweza kukuta mahabusu imejaa
kinyesi, maana wanatokwa na haja bila ya wao kujitambua. Hapo utaona ni
usumbufu kiasi gani kwa watu ambao siyo watumiaji, wanaokuwa mahabusu pamoja na
mateja,” alisema Mtafungwa.
Alichokisema Mtafungwa, kipo sawa na kilichoelezwa na wakuu
wa vituo kadhaa jijini Dar es Salaam ambao walizungumza na Jambo Leo kwa ombi
la kutotajwa gazetini kwa sababu wao kwa nafasi zao hawaruhusiwi kuwa wasemaji
wa jeshi.
“Ukiwafungia mahabusu mateja, jiandae kusafisha kinyesi,
wale watu wakishaharibika, kuwaweka muda mrefu bila kutumia ulevi wao ni kuzidi
kuwaumiza,” alisema mkuu wa kituo kimoja cha Mkoa wa Kipolisi, Ilala, Kanda
Maalum ya Dar es Salaam.
Mwenzake wa Mkoa wa Kipolisi, Temeke, Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, alisema kuwa suala la kuwasaidia kupata madawa ya kulevya mateja,
halina maana ya kuwaunga mkono kwa uteja wao, ispokuwa ni kuwanusuru na kifo
cha haraka.
“Wewe mwenyewe ukiwaona wanapokuwa kwenye alosto utaogopa,
utaona wanakufa, sasa kama binadamu unafanyaje? Kuweka msimamo wa kukataa
kuwapa madawa yao ni kuharakisha kifo chao,” alisema mkuu huyo wa kituo.
Akaongeza: “Afadhali siku hizi tuna utaratibu mzuri wa kuwapeleka
mateja kwenye rehab (kliniki za kuwaponya mateja), huko angalau kuna wataalam
ambao huwasaidia kupona taratibu.”
DAKTARI WA POLISI AELEZA MSAADA WAO
Ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania, vipo vituo kadhaa vina
hospitali za polisi na kwa mujibu wa uchunguzi wetu, wapo mateja kutokana na
hali zao kuwa mbaya hupelekwa kwenye vituo hivyo kwa matibabu.
Mmoja wa madaktari katika hospitali za polisi, naye kwa
sharti la kutotajwa jina gazetini, alisema kuwa wakati mwingine inakuwa vigumu
kutambua kama mtu anayepelekwa kwa ajili ya matibabu anakuwa anasumbuliwa na
alosto au maradhi ya kawaida.
“Anaweza kuletwa mtu ambaye anakuwa na homa kali sana,
vilevile analalamika anasikia maumivu makali. Ukimwangalia ni kama ana malaria,
typhoid au amiba. Unaweza kudhani labda anayo matatizo pia kwenye njia ya
mkojo,” alisema daktari huyo.
Aliendelea kusema: “Tukishampima, matokeo ya vipimo yanakuwa
hayana uwiano na hali yake. Ukikaa vizuri na mgonjwa anakwambia ukweli kuwa
anasumbuliwa na alosto. Hali ikishakuwa hivyo, tunakuwa hatuna namna zaidi ya
kumsaidia.
“Sisi kwa upande wetu humpa dawa ya usingizi, mara nyingi ni
valium (dawa ya usingizi). Akishalala na kuamka anakuwa na nafuu kiasi. Hawezi
kulalamika yale maumivu kama mwanzoni, ingawa nguvu ya valium ikiisha
malalamiko yake hurejea palepale.”
Alizidi kufafanua kuwa pale inapotokea mgonjwa anaonesha
dalili zote kuwa tayari ni mwathirika wa madawa ya kulevya, madaktari huwa
hawajisumbui, kwani humpa valium kwa haraka ili apate usingizi na kumpa nafuu
ya maumivu yake.
“Alishawahi kuletwa kijana kimoja kwa macho ya kawaida
huwezi kudhani kama ni mwathirika. Alikuwa bado anaonesha ana afya, kwa kifupi
alikuwa hajaariwa sana na madawa ya kulevya.
“Yule kijana alikamatwa kwenye oparesheni za kipolisi za
kukamata vibaka. Alipofikishwa kituoni baada ya kama saa 12 alianza kulalamika
maumivu. Alitolewa mahabusu kuletwa hospitalini kwetu akipiga kelele,” alisema
dokta huyo. “Tulidhani mgonjwa wa kawaida maana hakuonesha kama ni teja.
“Nilipozungumza naye pembeni alikiri anasumbuliwa na alosto,
ikabidi palepale nimpe valium. Na kwa kawaida nikishampa valium, namweleza
mpelelezi wa kesi yake kuhusu hali ya mgonjwa wake ili kuangalia namna bora ya
kuendelea.”
Kuhusu askari kuwapa mateja unga ili kuwasaidia, alisema:
“Nasikia kitu kama hicho lakini siwezi kukitolea ushahidi kwa sababu sijawahi
kushuhudia moja kwa moja. Ila sisi wote ni askari, sema tu nipo upande wa afya,
tunazungumza na kupeana michapo ya hapa na pale, mambo kama hayo yanasemwa kuwa
yapo.”
MAKAMANDA WA DAR ES SALAAM WAZUNGUMZA
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Temeke, Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
ACP Andrew Satta alisema kuwa ni ukweli kuwa watumiaji wa madawa ya kulevya
huchafua mahabusu wanapopatwa na hali ya ukosefu wa madawa ya kulevya kwa
sababu ya kushikiliwa na polisi.
Alisema: “Wanapochafua tunasafisha. Unajua haya mambo ni
vigumu kuyaelezea sisi kwa sababu yapo kitaalamu zaidi. Madaktari wanaweza
kusema ni kwa nini wanakuwa hivyo, ila upande wetu sisi wanapochafua
tunasafisha.
“Polisi tunakamata watu wa aina mbalimbali. Mfano vichaa,
unakuta mtu amejitapakaza kinyesi mwili mzima au amejisaidia na kutapakaza
kinyesi mahabusu yote. Sisi hapo tunachofanya ni kusafisha tu mahabusu.”
Kuhusu kuwasaidia watumiaji wa madawa ya kulevya kupata
madawa yao ili wapate nafuu, alisema: “Sisi kwanza kama polisi huwa hatujui
hayo madawa yanauzwa wapi, kwa hiyo inakuwa vigumu kuwatafutia. Kitu kama hicho
hakipo.”
Majibu ya ACP Satta, yalishabihiana na yale ya Kamanda wa
Mkoa wa Kipolisi, Ilala, Dar es Salaam, SACP Lucas Mkondya, aliyesema kuwa
mahabusu husafishwa ila kuwasaidia mateja kupata madawa ya kulevya ni jambo
lisilowezekana.
“Sisi ndiyo tunakamata wauzaji na watumiaji wa madawa ya
kulevya, sasa inawezekana vipi tena sisi wenyewe ndiyo twende tukawasaidie
watumiaji kutumia?
“Ni kweli kwamba wale watu wanapokosa madawa yao hupatwa na
hali fulani hivi mbaya, tena wakati mwingine unaweza kudhani anakaribia kufa,
lakini ile hali ni sumu na baada ya muda huwa inaondoka. Kitu ambacho huwa
tunafanya, wanapozidiwa huwa tunawapeleka hospitali,” alisema SACP Mkondya.
Upande wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, ACP Christopher Fume alisema kuwa kuwatafutia madawa
ya kulevya mateja ni jambo ambalo halina ukweli.
“Yapo masuala umesema kuhusu hali zao jinsi zinavyokuwa
mbaya, unajua kwa nafasi yangu nakuwa sishughuliki moja kwa moja na hao mateja,
kuweza kuona wanapokuwa na alosto inakuwaje. Hayo mambo ya kuhusu mahabusu
nitakuunganisha na mkuu wa kituo aseme inavyokuwa,” alisema ACP Fume.
Fume, alimwahidi mwandishi wetu kumpa namba ya Mkuu wa Kituo
cha Oysterbay, yalipo makao makuu ya Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, lakini
hakuweza kutimiza ahadi hiyo.
MATEJA WATOA USHUHUDA
Hemedi Jacha, maarufu kama Ngololo, mkazi wa Kinondoni, Dar
es Salaam, aliliambia Jambo Leo kuwa yeye binafsi amewahi kusaidiwa kupata unga
pale alipokuwa amezidiwa. Jina la kituo limehidhiwa kiusalama.
Alisema, aliwekwa siku mbili mahabusu ndipo hali yake
ilipokuwa mbaya kupita kiasi na kupoteza fahamu.
“Kumbe wakati sina fahamu polisi walinisaidia kubembea
(kutumia madawa ya kulevya). Kiukweli wale masoja (askari) niliwaona waungwana sana
kwa sababu pengine ningekufa,” alisema.
Alieleza kuwa hata baadhi ya mateja wenzake waliwahi
kukamatwa na kusaidiwa kupata unga baada ya kuzidiwa na alosto.
“Unajua ukiwa na alosto, mtu ambaye anaweza kuacha
kukusaidia unga ni katili sana, ni kama kunusa kifo,” alisema Ngololo. “Mimi
nimewahi kupewa ngada (unga), na nilipopata nafuu nilipelekwa mahakamani lakini
baadaye niliachiwa kwa dhamana, na sasa hivi napeta mitaani.”
Mtumiaji mwingine James Nubi, alisema kuwa wamewahi kusomwa
na polisi pamoja na mateja wenzake kwenye maskani yao ya Detroit, Kijitonyama,
Dar es Salaam.
“Tulipokamatwa tulizidiwa sana, baadaye ilibidi tutafutiwe
madude (unga) ndiyo tukaweza kurejea kwenye usawa wetu. Ni ukweli kuwa mahabusu
ilichafuka, si unajua tena mambo ya alosto?” alisema Nundu kwa mtindo wa
kuhoji. Jina la kituo walichowekwa limehifadhiwa.
Kwa upande wa hali wanayojisikia wanapopatwa na alosto,
Nundu alisema kuwa hupatwa na maumivu makali mwili mzima na wakati mwingine
huchemka mwili mithili ya mtu mwenye homa kali.
Alisema: “Mimi natumia, nashindwa tu kuacha. Nasikia kuna
kliniki, nitajitahidi kwenda ili nione nawezaje kupona. Ushauri wangu kwa wale
ambao hawajawahi kutumia wasithubutu
kabisa, maana ni hatari.
“Kuna wakati mtu unajisikia kama vile upo kuzimu, unajiona
kabisa upo karibu na kifo. Ukishakuwa mteja unajiona haupo sawa na binadamu
wengine wa kawaida. Unakuwa katikati ya binadamu na mnyama.”
VITUO VINGI WAOGOPA KUKAMATA MATEJA
Uchunguzi wa Jambo Leo umepata majibu kuwa vituo vingi vya
polisi hukwepa kukamata mateja kwa sababu ya kuhofia usumbufu wa kuchafua
mahabusu na kuwatafutia tiba wanapokuwa na alosto.
Mkuu wa mmoja wa kituo kidogo (post), ndani ya Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni, alisema: “Hakuna mtu ambaye anataka usumbufu wa mateja,
wale watu ni hatari sana. Mimi nimejionea mwenyewe.
“Tukiwakamata basi ujue kuna kosa la moja kwa moja kumhusu
teja husika lakini misako ya kuwalundika mahabusu hapana. Usumbufu ni mkubwa
mno wanapokuwa na alosto. Siyo kwetu tu hapa, vituo vingi pia wanawakwepa.”
Katika kueleza uzoefu wake kuhusu mateja, mkuu huyo wa kituo
(jina limehifadhiwa), alisema kuwa ni watu wenye vitendo vingi vya ajabu.
Mkuu huyo wa kituo alitoa simulizi ya jinsi ambavyo
walikutana na tena msumbufu aliyefanya uhalifu nyumbani kwa mtoto wa aliyekuwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Said Mwema.
“Yule teja alipoiba nyumbani kwa mtoto wa IGP Mwema,
alipoona anakaribiwa kukamatwa, alijisaidia kisha akajipaka kinyesi mwili mzima
ili asikamatwe. Tulipomkamata na kumuweka kwenye gari, alijisaidia tena na
kuchafua gari lote,” alisema mkuu huyo wa kituo.
Akaongeza: “Hayo mambo kwa kweli ni usumbufu mkubwa. Na
ndiyo sababu vituo vingi tunakwepa kuwakamata mateja, labda inapotokea
tunawachukua na kuwapeleka moja kwa moja kwenye kliniki zao, vinginevyo unaweza
kujikuta ni mtumwa, awachafulie chumba cha mahabusu, na ulazimike kumtafutia
dawa ili kumsaidia apone.”
0 comments :
Post a Comment