Luqman
Maloto
Beki wa Klabu
ya Simba, Abdi Banda, aliye na uwezo mkubwa wa kusimama kama kiungo mkabaji,
yupo kwenye karantini! Kwamba hayupo kikosini kwa sasa akisubiri hukumu ya
kocha.
Beki fundi
wa Simba, Hassan Isihaka, yeye yupo kifungoni. Kosa lake ni utovu wa nidhamu.
Banda na Isihaka tatizo lao ni mgogoro na kocha.
Upo pia mgogoro
mkubwa kati ya uongozi wa Klabu ya Simba na beki wake wa kulia, Hassan Kessy.
Na unaendelea!
NINI KOKORO?
Sasa hivi
inawezekana kabisa kuutazama mgogoro wa Banda na Kocha wa Simba, Jackson
Mayanja kwa upande mmoja.
Hiyo ni kama
ilivyokuwa kwa Isihaka, alivyowekwa kando katika program ya kocha, baada ya
kutofautiana na mwalimu huyo raia wa Uganda.
Kwamba Kessy
ni mgogoro tu wa mkataba, kama ambavyo hata Haruna Niyonzima ‘Fabregas’,
alivyopata kutofautiana na menejimenti yake.
Utaona kuwa
angalau mgogoro wa Niyonzima na Yanga, ulimalizwa kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Yusuf Manji kutangaza kumwondoa klabuni, aliyekuwa katibu mkuu, Dk. Jonas
Tiboroha kwa kusababisha matatizo yaliyokuwepo.
Manji
alisema kuwa Niyonzima alihujumiwa na Tiboroha. Angalau hilo liliwekwa wazi
kisha aliyekutwa na hatia akawekwa kando, wakati huohuo mchezaji akarejeshwa
kundini.
Hivi sasa,
Kocha wa wa Stand United, Mfaransa Patrick Liewig, naye imeshaelezwa kuwa kuna
uwezekano mkubwa wa kutokuwepo na timu hiyo msimu ujao. Kisa haelewani na
wachezaji.
Wapo
viongozi wanahoji, ni kwa nini Leiwig anasababisha straika Elias Maguri asifunge
tena magoli kama ilivyokuwa zamani?
Nakumbuka
mwaka 2007, wakati Kelvin Yondan akicheza vizuri nafasi ya beki ya kati Simba
kwa kushirikiana na mkongwe, Victor Costa ‘Nyumba’, Makamu wa Rais wa klabu
hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ wakati huo akiwa mdau tu wa timu, alisema beki
huyo hafai.
Kaburu kama
mdau na memba wa kundi la Friends of Simba, ni mmoja kati ya wanene wa klabu
hiyo, waliokuwa na michango ya kusajili wachezaji kwa niaba ya klabu.
TUWEKE MZANI
SAWA
Mfano wa
Kaburu, ukupe jibu moja kuelekea kuondoka kwa Yondan Simba.
Kama Kaburu
alipokuwa mdau tu wa Simba alimkataa mchezaji huyo, inakuwaje baada ya kushika
umakamu wa rais? Yondan aliondoka, yakafuata maigizo na hayakusaidia kitu.
Tatizo ni
watu wanaoongoza soka. Wachezaji lazima wawe na utovu wa nidhamu kwa kocha kwa
sababu viongozi wa timu hutaka waonekane wao ndiyo kila kitu kuliko makocha.
Kocha
anaandaa kikosi, anaambiwa ampange mchezaji ambaye hayupo kwenye program ya
kocha. Kesho mchezaji hawezi kuwa na nidhamu kwa kocha wake. Anajua bila
kiongozi fulani, singecheza.
Ulaya kocha
ndiye mwalimu, vilevile meneja wa timu. Huku kwetu Bongo kocha ni mkufunzi tu
wa mazoezi.
Kwetu Bongo,
kocha ujanja wake unaishia kwenye mazoezi na kuwapika kwa mbinu za mchezo
lakini katika mechi, wanageuka maroboti, rimoti wanakaa nazo viongozi jukwaani.
Banda
anajitetea, eti: “Kocha aliniambia nipashe niingie kucheza nikamwambia amwachie
kwanza Tshabalala anaweza.”
Pamoja na
makosa, bado mchezaji anajiona alikuwa sahihi. Ukifuatilia, unakuja kugundua
kuwa yapo kiongozi anamjaza upepo, kichwa kinavimba.
Sir Alex
Ferguson, alipokuwa meneja wa Klabu ya Manchester United, alimuuza David
Beckham kwa Real Madrid, baada ya kuona mchezaji huyo anataka kumpanda
kichwani.
Na kwa
kawaida, uamuzi wa kocha lazima uheshimiwe. Kocha anapewa kila anachohitaji kisha
anabanwa katika matokeo. Ndiyo maana Beckham na ustaa wake, jumlisha mapenzi
makubwa kwa Man United aliyokuwa nayo, aliuzwa na timu iliendelea.
Hapa kwetu,
kocha anaingiliwa kisha timu ikifanya vibaya kocha anatimuliwa. Shida ipo kwa
wanaoongoza timu.
MAMLAKA YA
KOCHA YAHESHIMIWE
Viongozi
waache tabia ya kutengeneza matabaka kwa wachezaji. Wanawaharibu kuliko
kuwasaidia, vilevile kusaidia soka la nchi.
Wapo
wachezaji wengi walimaanishwa kutisha Ulaya lakini hawakufika popote kutokana
na malezi mabaya ya viongozi.
Ni kawaida
kabisa kwa mchezaji kuharibika anapotetewa katika nyakati anapoonesha vitendo
vya utovu wa nidhamu.
Msingi wa
malezi unakataa mtu kutetewa anapokosea. Hata kama atakuwa anaonewa, nguvu ya
juu kutetea husababisha mhusika avimbe kichwa.
Yanga kama
Toboroha angeonywa kisha Niyonzima akatetewa, kusingekuwa na maelewano wala
nidhamu kati yao. Ndiyo maana uamuzi uliochukuliwa umekuwa wa busara mno.
Viongozi
wanatakiwa kutanguliza weledi. Waache kuwavimbisha vichwa wachezaji mbele ya
makocha wao.
Lazima
kutambua menejimenti za klabu na kamati zao, zinahusika tu mikataba ya
wachezaji na utekelezwaji wa vijazilizi vya ajira, lakini benchi la ufundi,
bosi wake ni kocha, yeye ndiye mwalimu na anajua ni wakati gani mchezaji yupi
anamfaa kutokana na mazingira ya mchezo.
Maisha
lazima yabadilike, soka la Tanzania linapaswa kukua. Wachezaji wa Kitanzania
wanastahili kukua, waende kisasa. Nafasi ya kocha itambulike. Nidhamu kwa
wachezaji halipaswi kuwa suala la kuomba.
Malezi
yasiyofaa ya viongozi kwa wachezaji imekuwa sababu ya wachezaji wengi kushindwa
maisha ya soka nje ya Tanzania. Wanapenda kukumbatiwa na viongozi wao.
Kudekezwadekezwa. Shida sana!
0 comments :
Post a Comment