ads 728x90 B

Naiona Zanzibar ngumu, ile ya Salmin na Karume




Na Luqman Maloto
Uchaguzi umepita ila sasa kije kipindi cha maridhiano. Mgogoro wa Cuf na CCM sababu ni uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, basi baada ya marudio kukamilika, upande wenye mnofu ufungue ukurasa mpya.
Vema kukumbusha kuwa tangu ruhusa ya mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, kipindi kizuri cha utawala Zanzibar kilikuwa kati ya mwaka 2010 na 2015, Dk. Ali Mohamed Shein alipoongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hapa ni kumaanisha kuwa Awamu Pili ya Dk. Salmin Amour mwaka 1995 mpaka 2000 na vipindi viwili vya Dk. Amani Abeid Karume kati ya mwaka 2000 mpaka 2000 kulikuwa na ghasia nyingi.
Afadhali awamu ya pili ya Dk. Karume, miaka yake miwili ya mwisho, aliongoza bila kokoro baada ya kukamilisha mazungumzo yaliyofanikisha kuandikwa kwa Katiba Mpya yenye kuruhusu muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uchaguzi wa mwaka 2010, ndiyo pekee kokoro haikuwa kubwa baada ya nguli wa siasa za Zanzibar, Seif Sharif Hamad wa Cuf, kukubali mapema matokeo ya kushindwa, hivyo Shein kuongoza kwa baraka zote.
Kuna mambo mawili vema kuyaweka wazi. La kwanza ni kwamba pamoja na Seif kukubali matokeo kisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuundwa mwaka 2010, bado minong’ono ilikuwa mingi kwamba Shein hakushinda, isipokuwa Cuf iliridhia ushindi wake kwa uungwana pamoja na dhamira ya kuijenga Zanzibar moja baada tofauti za muda mrefu.
Jambo la pili ni kukumbusha ni kuwa watu wengi walijenga kijiwe Hoteli ya Bwawani na kupiga kelele matokeo yatangazwe. Kelele nyingi zilikuwa Seif alishinda lakini mwenyewe alipokubali kushindwa, zogo likaondoka.
KUMBUKUMBU NI MWALIMU
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2000, Cuf walikataa matokeo na kwa hivyo, walifanya uamuzi wenye sura mbili.
Kwanza walitangaza kuwa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Cuf waliotangazwa kuwa wameshinda, wasingehudhuria wala kushiriki vikao vya bunge na baraza kwa sababu ya kutokukubaliana na matokeo kwa jumla.
Pili, waliandaa maandamano ya kupinga matokeo ambayo yalipangwa kufanyika Januari 26, 2001. Ni maandamano hayo yaliyosababisha maafa ya watu, raia wa kawaida na askari wa Jeshi la Polisi, Januari 26 na 27, 2001.
Ni kipindi ambacho Tanzania iliingia doa la kuzalisha wakimbizi. Ipo sehemu ya Wazanzibar ilikimbilia Kenya na Somalia kutokana na machafuko hayo.
Hata baada ya machafuko hayo, Cuf waliendelea na msimamo wao kwa wabunge na wajumbe wao wa Baraza la Wawakilishi kutohudhuria vikao vya bunge na baraza.
Msimamo huo ulisababisha nguvu ya upinzani ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupwaya, huku kwenye Baraza la Wawakilishi kukosekana kabisa.
Bungeni, wapinzani wa vyama tofauti walijiunga na kumchagua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini (Chadema), Dk. Aman Walid Kabourou kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani.
Mgomo wa Cuf ulifikia kikomo baada ya mwafaka kati ya chama hicho na CCM, uliosaniwa Oktoba 2001 mbele ya waliokuwa wenyeviti wa vyama hivyo, Benjamin Mkapa (CCM) na Profesa Ibrahim Lipumba (Cuf).
Ni kwamba mgomo wa Cuf uliisha kwa wabunge na wajumbe wao wa Baraza la Wawakilishi kuanza kuhudhuria vikao kuanzia Januari 2002. Hata hivyo, utekelezaji wa jumla wa mwafaka ulikwama hadi Uchaguzi Mkuu wa 2005 ambao pia matokeo ya urais yalipingwa na Cuf.
Hali ilikuwa tete Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu 2005, na vilevile tuwe na kumbukumbu kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu 1995, hali haikuwa shwari, na mwaka 1997, baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mkunazini kuwania ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, mwanasiasa mkongwe Juma Duni Haji na wenzake walikamatwa kwa kosa la uhaini na kuwekwa mahabusu mpaka mwaka 2000.
Katika uchaguzi huo, Duni alishinda lakini hakufanya kazi yake kama mjumbe kutokana na kesi hiyo ya uhaini.
Nimeweka muhtasari huo wa kumbukumbu, kama mwalimu wa kukumbusha nyakati ngumu za maelewano mabovu ya kisiasa, kupitia hapo itoshe kuonesha umuhimu wa maridhiano.
MARIDHIANO NI LAZIMA
Msimamo wa Cuf ulikuwa na taswira nyoofu ni kuwa hata kama kuna kiongozi wa chama hicho atashinda, bado hawatakubali.
Taswira hiyohiyo na unyoofu wake ilionesha hali ya kususia uchaguzi huo hasa kwa upande wa Cuf, hivyo CCM si maajabu kushinda kwa kishindo.
Na kwa vile Zanzibar inatawaliwa na siasa za vyama viwili, CCM na Cuf, muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambao hautashirikisha moja kati ya vyama hivyo, utakosa vionjo stahiki. Bila uzandiki ni kuwa serikali ‘itaboa’.
Katiba ya Zanzibar inaelekeza mtu atakayeshika nafasi ya pili awe Makamu wa Kwanza wa Rais na chama chake kishirikiane na Chama Tawala kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hamad Rashid Mohamed wa Chama cha ADC ameshika nafasi ya pili. Japo kura hazimpi uteuzi kikatiba, Shein anaweza kumteua kiungwana.
Na kama atafanya hivyo, basi ifahamike kuwa CCM na ADC kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, haitakuwa serikali yenye hadhi yake, bora tu CCM ijitegemee yenyewe katika kutawala visiwa hivyo.
CCM na Cuf ni vyama vyenye nguvu karibu sawa Zanzibar. Na Visiwani humo, siasa za vyama hivyo ni kama dini.
Nguvu ya viongozi wa kisiasa Zanzibar na maneno yao ambavyo hugusa nyoyo za wafuasi wao, ni karibu sawa na mashehe, wachungaji na mapadri wanaponena maneno ya Mungu kwa waumini wao. Mazingatio huwa ni makubwa mno.
Siasa hizo za Zanzibar, ndizo ambazo zinatoa picha ya ugumu wa serikali kuongoza na kutimiza malengo yake, kwa kususiwa na upande mmoja kati ya vyama hivyo.
Hivyo basi, CCM ambao ndiyo washindi wa uchaguzi, baada ya kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, hawapaswi kushangilia sana, watatakiwa kurudi mezani na Cuf.
Maridhiano ni deni la Wazanzibar kwa CCM na Cuf. Wazanzibar wanatakiwa kutengenezewa daraja la ushirikiano. Vyama hivyo vinaweza kujenga au kubomoa daraja.
Ikiwa CCM na Cuf watakaa mezani, watakuwa wamejenga daraja la ushirikiano kwa wananchi, mgomo ukiendelea chuki itakuwa kubwa na hakutakuwa na ushirikiano.
Machafuko ambayo yamekuwa yakiendelea kuripotiwa. Wapo watu wanaoitwa mazombi wamekuwa wakifanya matukio ya kihalifu ambayo yanahusishwa na siasa za chuki visiwani humo.
Hali na matukio hayo, ni kuonesha kuwa suala la maridhiano Zanzibar halina hiari. CCM na Cuf wanapaswa kutambua kuwa Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko vyama vyao. Wazanzibar watangulizwe mbele kabla ya matakwa ya kisiasa.
NINI KIFANYIKE?
Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015 kufutwa Zanzibar, Seif na Shein walifanya mkutano wa kutafuta mwafaka. Suluhu ilikuwa ngumu kupatikana kwa sababu kila mmoja alishika lake.
Seif alisisitiza kuwa alishinda uchaguzi, hivyo atangazwe, wakati Shein alishikilia msimamo wa Zec kuwa uchaguzi urudiwe. Ilitakiwa mmoja akubali kushindwa, jambo ambalo halikuwa rahisi.
Ni afadhali kila mmoja angekuwa anasema ameshinda, hivyo suluhu ilikuwa kuwafanya wote wakose kwa kufuta matokeo na kuitisha uchaguzi wa marudio. Tatizo mvutano wao ulikuwa mtego mkali, na wa kukubali kushindwa hakuonekana.
CCM kama washindi, wanatakiwa kutambua hali halisi, hivyo kuwaangukia Cuf ili washirikiane kuiongoza Zanzibar.
Cuf wanaihitaji Zanzibar yao ikiwa moja. Msimamo wao wa sasa ni kinyongo cha kuona hawatendewi haki na wenye mpini.
Baada ya uchaguzi, na kama wataitwa mezani ili washirikiane kuijenga Zanzibar yao, hapo watakuwa ni ama wakubali au wakatae.
Ipo wazi kuwa tatizo la Zanzibar lipo kwenye nafasi mbili za juu, ile ya Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais, nani awe mkuu na yupi bosi namba mbili.
Na kwa vile Shein alishatangazwa na kula kiapo, hapo bila shaka nafasi itakuwa imejaa. Hata hivyo, deni lake ni kuhakikisha Seif anashirikiana naye.
Shein akifanikiwa kumshawishi Seif akubali kuwa bosi namba mbili, yaani Makamu wa Kwanza wa Rais, maana yake kila kitu kitakuwa kimemalizika. Nafasi za chini zitajitengeneza zenyewe.
Natambua ugumu wa Seif na Cuf kukubali kushawishika, lakini naiona zaidi Zanzibar ikiwa ngumu kuliko nyakati zote kama Shein atashinda na kula kiapo kisha kuongoza serikali bila baraka za Cuf na Seif.
Ugumu huo wa Zanzibar ni deni kubwa kwa Shein. Hivyo basi, baada ya uzuri wa kutangazwa mshindi, sasa atambue umuhimu wa Zanzibar kubaki moja, hivyo ajishushe na kumshawishi Seif mpaka akubali ili salama ya kweli ipatikane.
Ikumbukwe; Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa kwa msuli mkubwa, haipendezi ikabezwa na kuvunjwa kirahisirahisi.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilifanikishwa kwa fedha nyingi. Mabadiliko ya Katiba, Kura ya Maoni, vikao vya maridhiano bila kusahau safari za nje na mialiko ya wataalamu, kupata ushauri wa namna bora ya kumaliza misuguano na kuibakiza Zanzibar kuwa moja.
Tumesahau? Haiwezekani kukawa na usahaulifu wa kiwango hicho. Hatupaswi kusahau.
Nisisitize; Bila maridhiano, naiona Zanzibar ngumu kama ile ya Dk. Salmin, yenye uhasama wa wazi. Naiona Zanzibar tata kama ile ya muhula wa kwanza wa utawala Dk. Karume.
Mungu Ibariki Zanzibar, Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment