Na Luqman
Maloto
Mfalme wa
Temeke, Juma Kassim Kiroboto ‘Sir Nature’, ameomba mpambano na janki pedeshee
wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’.
Nilipoona
habari hizi nilicheka, nikakumbuka mbali. Kweli muziki ni katili na soko lake
halina huruma hata kidogo.
Diamond
amekuwa mkubwa mno kimuziki, siyo tu Bongo, bali Afrika yote. Wakati dogo huyo
kibopa wa Bongo wa Fleva akinawiri kimuziki, ndiyo kipindi ambacho Mfalme
Nature ‘Kibla’ alikuwa anamalizia enzi yake.
Kwa kifupi
Nature alipishana na Diamond. Wakati Baba Zari, samahani, namaanisha Baba
Tiffah Dangote, alipokuwa bize akiwasha taa zake za kumng’arisha kimuziki, ndipo
Nature alipozima taa zake za mng’aro wake.
Nature yule
ambaye alipendwa na mashabiki wa Bongo Fleva kuliko chakula, leo hayupo kwenye
mzunguko wake wa soko. Wakati huohuo, Diamond ndiye mbabe wa soko lenyewe. Huu
muziki hauna mfalme wa kudumu!
Akumbukwe
Nature wa Ugali. Ukumbi wa Diamond Jubilee, pale Upanga, haukutosha mwaka 2003.
Nature wa
Hili Game na Sitaki Demu. Nature wa Kighetto Ghetto na Inaniuma Sana. Nature wa
Hakuna Kulala na Sonia. Huyu mtu alifanya ‘mabalaa’ ya uhakika kwenye muziki wa
Tanzania.
Alitikisa
kwenye rap, alipoimba Kwaito watu walimwelewa. Nature alikuwa juu kabisa ya
kilele cha muziki.
Kipindi
ambacho Bongo Fleva uliitwa muziki wenye utamu wa Big G, Nature alivuka mwaka
mmoja mpaka mwingine akiwa juu kabisa. Nature apewe heshima yake.
Nature na
ubabe wake ule wa kimuziki, leo hii anatamani kufanya mchuano wa jukwaani na
Diamond. Tena amesema: “Hakuna mwanamuziki mwingine anamuweza Diamond jukwaani
kasoro mimi.”
Soko la
muziki halina huruma! Ni Nature mwaka 2006 alivuka mipaka na kushiriki Tuzo za MTV
Ulaya (MTV Europe Music Awards), akishindania Tuzo ya Mwanamuziki Bora Afrika (Best
African Act).
Katika tuzo
hizo, Nature alishindana na kundi la Freshlyground (Afrika Kusini), Nameless
(Kenya), P-Square (Nigeria) na Anselmo Ralph (Angola). Kundi la Freshlyground
ndilo lililonyakua tuzo hiyo.
Kituko cha
tuzo hiyo ni kuwa Nature hakwenda kuhudhuria tuzo hizo, zilizofanyika kwenye
Ukumbi wa Bella Center, Copenhagen, Denmark. Nature kwa kutokuhudhuria kwake,
alimlaumu aliyekuwa meneja wake, Said Fella ‘Mkubwa’ kwa kutomfanikishia safari!
Soko halina
huruma! Godfrey Tumaini ‘Dudubaya’ na Nice Lucas Mkenda ‘Mr. Nice’, walitikisa
vilivyo na bifu lao. Walipogombana ikawa gumzo nchi nzima.
Mwaka jana,
Dudubaya na Nice walikutana na kutangaza kumaliza bifu kisha wakafanya maonesho
kadhaa ya muziki pamoja na hakuna mtu aliyeshtuka. Ni kipindi ambacho soko lao
lilikuwa limeshahama.
Hakuwa
Dudubaya wa Mwanangu Huna Nidhamu, Dege la Jeshi, Tupa Mawe, Nakupenda Tu,
Mpenzi na nyinginezo.
Mr. Nice
huyo hakuwa yule wa Kidali Po, King’asti na nyingine zilizotamba. Maisha
yameshabadilika kwa kasi kubwa.
Bado huamini
kuwa soko la muziki halina huruma? Hapo jiulize yupo wapi Joslin na MB Dog?
Amekwenda wapi Z Anto?
Maisha ya
kimuziki mbona yamekuwa siyo rafiki tena kwa Matonya? Wakati wake ilikuwa ni
vigumu kumpata kwa shoo, maana alijaza kila tarehe kwa mwaka.
SIYO BONGO
TU
Ngoja
nikukumbushe; DMX aliposhika usukukani wa soko la rap Marekani, aliuza platinum
nyingi mno.
Ghafla
akaibuka Ja Rule, hapo ndipo ufalme wa DMX ukapotea. Soko la rap duniani likawa
halifunui kinywa upande wake. Sauti zege, tungo tamu za kimalovee. Ja Rule
bwana!
Soko halina
huruma! Alipoibuka 50 Cent ndiyo ikawa mwanzo wa kupotea Ja Rule. Hata hivyo,
50 Cent wa leo, siyo yule! Naye biashara siyo asali upande wake.
SHULE NDANI
YAKE
Hakuna jambo
zuri kama mwanamuziki kutambua soko la muziki linapomuelekea.
Kinachotakiwa
kwa mwanamuziki ni kuhakikisha anakuwa na wakati mzuri wa kupanua soko lake.
Vema
kutambua kuwa itafika wakati mwanamuziki mwenye soko leo, kesho hatakuwa na
soko hilo.
Haiwezekani
wewe ukawa mwanamuziki mwenye kuuza kila siku. Upo wakati utafanya kazi
unayoiona nzuri na hutauza.
Kumbuka
Michael Jackson ‘The Jacko’ ambaye unaweza kumwita Mfalme MJ, aliuza nakala
milioni 100 kwa albamu moja. Itambue albamu ya Thriller na maajabu yake.
Mwaka 2001,
Jacko alitoa albamu yenye maandalizi makubwa inayoitwa Invincible. Akatanguliza
singo babkubwa You Rock My World. Kilichotokea ni kuwa aliuza nakala milioni 10
tu.
Ni ukweli
kuwa nakala milioni 10 ni nyingi kwa biashara lakini siyo kwa hadhi ya Jacko.
Ni kwamba alidhani zilikuwa zama zake lakini hazikuwa zile.
Tupac Shakur
tangu alipotoa albamu yake ya kwanza 2pacalyps mwaka 1991, aliweka rekodi ya
kuuza platinum tu.
Aliweka
rekodi ya kuuza platinum mpaka mara 10 (diamond), na kuweka rekodi ya kuwa
mwanamuziki wa Hip Hop wa kwanza kufikia mauzo hayo.
Alipokufa,
mauzo yake yalipaa zaidi na zaidi. Kila albamu yake aliyotoka ilipiga platinum.
Mwaka 2006, ilipotoka albamu ya Pac’s Life, ilidorora kabisa na mauzo yake
hayakufika hadhi ya dhahabu (nakala 500,000). Soko lilishahama!
Ifahamike
kuwa utafika muda Diamond hatakuwa anauza kama sasa, kama ambavyo juhudi za Q
Chiller kurejea sokoni zinavyogonga ukuta.
Mwanamuziki
heshimu wakati wako. Ukiwa kwenye wakati mzuri wa kuuza, jitahidi kuwekeza, upo
wakati utafika hutaweza kuuza. Kitakachokufaa ni uwekezaji wako.
0 comments :
Post a Comment