YUPO mtu
alikuwa nakabiliwa na umskini wa kiwango cha juu. Kutokana na dhiki kumwandama,
ilifikia wakati alitamani kufa kuliko kuendelea kuishi.
Pale
alipokuwa anaishi, kulikuwa na eneo lenye msitu mkubwa ambao ndani yake
linaishi zimwi lenye kula watu. Na katika historia ya msitu huo, hajawahi
kupita binadamu salama, wote walioingia msituni waliliwa.
Yule mtu
alikata shauri la kujiua na aliona njia rahisi ya kifo ni kuingia msituni ili
akaliwe na zimwi. Basi akaingia katikati ya msitu!
Haikuwa
uongo, alipokatiza katikati ya msitu, alijikuta amesimama mbele ya zimwi kubwa lenye
hasira kali. Lile zimwi kabla halijamtafuna yule mtu, lilimuuliza: “Wewe
binadamu, hujaambiwa kuwa huku naishi mimi zimwi nakula watu? Huogopi kuliwa?”
Yule mtu
akajibu: “Taarifa zote ninazo, nami nimekuja huku niliwe nife, maana sina raha
ya maisha.”
Zimwi
akamuuliza: “Una tatizo gani mpaka useme huna raha ya maisha?”
Akajibu:
“Umaskini, dhiki zangu zimenizidi kimo. Nimekata tamaa kwa ufukara nilionao.”
Zimwi liliposikia
hivyo, lilimwangalia yule mtu kwa dakika kadhaa, halafu likamwambia: “Nisubiri
hapohapo nakuja, usijaribu kunyanyua mguu wako hata mara moja.”
Zimwi likatoweka,
baada ya muda mfupi, lilirejea likiwa limeshika vipande viwili vya miche ya
dhahabu. Likamkabidhi na kumwambia yule mtu: “Umesema shida yako ni umaskini,
sasa chukua hizo za dhahabu zikawe utajiri wako, ila siku ukirudi tena
nakutafuna bila kukuuliza.”
Yule mtu
akaondoka msituni akiwa haamini macho yake. “Bahati iliyoje, unaenda msituni na
kukutana na zimwi ili likutafune ufe, lenyewe linakupa dhahabu za kubadilisha
maisha yako,” alijisemea yule mtu akitembea kwa hatua za haraka kuelekea
nyumbani kwake.
Alipofika
nyumbani kwake, ile anafungua mlango, akamkuta malaika mtoa roho yupo ndani
anamsubiri. Akamuuliza: “Umefuata nini nyumbani kwangu?”
Malaika mtoa
roho akamjibu: “Mimi mgeni wako, nimefuata roho yako. Siku zako za kuishi hapa
duniani zimekwisha.”
Yule mtu
akalalamika: “Mbona mimi sina bahati? Yaani nimehangaika siku zote na umaskini
wangu, leo nimepata dhahabu za kunifaa ili niondokane na dhiki, ndiyo siku
zangu za kuishi zinafika ukingoni.”
Hata hivyo,
yule mtu akamuomba malaika mtoa roho: “Naomba japo siku mbili, niuze hizi
dhahabu, nipate pesa ili niwagawie maskini wenzangu angalau wabaki na nafuu ya
maisha, umaskini unatesa sana. Nitajiskia vibaya nikifa na kuacha hizi dhahabu
humu ndani, halafu zije ziokotwe na tajiri, wakati maskini wanateseka.”
Aliposema
maneno hayo, malaika mtoa roho alimwambia: “Umeongea jambo jema lenye kumpendeza
Mungu. Sadaka ni kitu kizuri sana. Basi nakupa hizo siku mbili.”
Malaika mtoa
roho akaondoka zake. Yule mtu akafanya kama alivyoahidi, aliuza zile dhahabu na
kupata mamilioni ya pesa. Akawazungukia maskini wale wenye dhiki na uhitaji
mkubwa, aliwagawia fedha zote.
Baada ya
siku mbili, yule mtu alibaki nyumbani kumsubiri malaika mtoa roho atokee.
Kweli, muda ulipofika malaika alitokea. Yule mtu akatabasamu, akamuuliza:
“Kabla hujanitoa roho, ningependa kujua, je, Mungu amependa sadaka niliyotoa?”
Malaika mtoa
roho akamjibu: “Mungu amefurahi sana, umewasaidia watu maskini sana kubadili
maisha yao. Na kwa furaha hiyo, Mungu amekuongezea siku za kuishi. Amekupa
miaka mingine 80, utakuwepo duniani na utapata mafanikio makubwa.”
Yule mtu
akalalamika: “Hapana, usiniache, naomba uchukue roho yangu. Mimi sikubali
kabisa, nitaishi vipi na umaskini huu? Umeniacha nimegawa mali zote ndipo
unasema nitaendelea kuishi. Sasa nawezaje kuishi na ufukara huu ambao
nilishaukatia tamaa?”
Malaika mtoa
roho wala hakujishughulisha kumjibu, alipaa zake. Yule mtu aliwaza, akasema
hawezi kuishi, akaamua kurudi msituni ili aliwe na zimwi ambalo alipoliona tu,
alijigalagaza miguuni mwake huku akilia:
“Nitafune nife, mimi sitaki kuishi.”
Zimwi
likamuuliza: “Niambie kwanza kilichokufanya uje hapa kwa mara nyingine,
nilikupa dhahabu na nikakwambia usirudi tena.”
Yule mtu
alimsimulia zimwi kila kitu. Zimwi likaondoka tena, likampa miche miwili
mingine ya dhahabu. Likasema: “Hii ni mara ya mwisho, usirudi tena. Ukirudi
sikuulizi kitu, nakutafuna moja kwa moja.”
Alipokea
miche ile ya dhahabu kwa wasiwasi, alipokuwa anatoka msituni, aliamini akifika
nyumbani angekutana na malaika mtoa roho. Alifungua mlango kwa tahadhari,
hakumkuta.
Alikaa kuona
kama angetokea lakini haikuwa hivyo. Asubuhi ya siku iliyofuata alikwenda kuuza
zile dhahabu, akapata fedha nyingi. Alifungua miradi mbalimbali ambayo ilimpa
faida kubwa. Akawa tajiri mkubwa
Siku zote
aliishi vizuri na watu. Aliukumbuka umaskini wake wa zamani, akawa mtoa sadaka
mzuri kwa maskini. Alifanya ibada akikumbuka ahadi ya miaka 80.
Miaka 80
ilipowadia, malaika mtoa roho alimtokea na kutimiza ahadi. Roho ya mtu mwema
ilitoka taratibu, huku malaika mtoa roho akimbembeleza na kumliwaza.
KISA KINGINE
Yupo mtu
alikuwa maskini lakini mchamungu mno. Akawa pia mlemavu wa mguu, alitembelea
gogo.
Alifanya
ibada kwa uaminifu lakini shida zilimwandama, akaona bora ajiue. Alikwenda
kwenye mlima mrefu wenye miamba. Akapanda mpaka kileleni, akakusudia kujitupa
aangukie kwenye miamba ya chini afe.
Alipoanza
kuhesabu ili ajirushe, akaona kiumbe mwenye umbo la binadamu, aliyekuwa na
mavazi meupe halafu ana mbawa. Akamtolea macho yule kiumbe alipokuwa
anamkaribia.
Kiumbe huyo
alipomfikia yule mtu, alimwambia: “Kujiua ni dhambi mbaya mno, ukifa hapa
unakwenda moja kwa moja motoni. Mwenye jukumu la kutoa roho ni mimi hapa
malaika mtoa roho,”
Malaika mtoa
roho alimbeba yule mtu mpaka chini, akamwambia: “Mungu amenituma nije nikuokoe
kwa sababu wewe ni mtu mwema. Unafanya sana ibada ndiyo maana hakutaka ufe kifo
haramu cha kujiua.”
Akaendelea
kumwabia: “Najua shida yako ni umaskini, nitakupa njia nzuri. Kuna mfalme
tajiri sana anauguza mwanaye kwa miaka mingi, waganga wote wameshindwa kumtibu.
Na ameshatangaza kuwa siku akipatikana mtu wa kumtibu atampa nusu ya utajiri
wake wote.”
Baada ya
kusema hivyo, malaika mtoa roho alimchukua yule mtu mpaka kwenye mti,
akamwambia achume jani. Akambeba tena na kumtua nje ya jumba la mfalme,
akamwelekeza aingie ndani, aseme anayo dawa ya kumtibu mtoto wa mfalme.
Kabla ya
kuondoka, malaika mtoa roho alimwambia yule maskini mlemavu: “Utapata utajiri,
utaishi miaka 40 tu. Kumbuka njia zitakazompendeza Mungu na faida yako ya
kesho.”
Maskini
aliingia ndani, akajitambulisha. Aliporuhusiwa kumtibu mtoto wa mfalme,
alilitoa jani lake, akalifikicha kisha ule unyevunyevu aliutumia kumpaka
kichwani. Ghafla mgonjwa akapiga chafya, akanyanyuka. Furaha isiyo na kifani
ikachukua nafasi kwenye nyumba ya mfalme.
Ahadi
ilitimizwa, yule maskini alipewa nusu ya utajiri wa mfalme, akawa siyo tena maskini,
akageuka tajiri mkubwa.
Kilichofuata
baada ya hapo ikawa starehe, dharau, dhuluma na visa vingi. Aliutumia utajiri
wake kunyanyasa wengine, kuchukua wake za watu na vurugu nyingine za
kiulimwengu. Alisahau kuwa alipewa miaka 40.
Siku moja
alikuwa kwenye msafara mkubwa na wapambe wake, akiwa na fedha nyingi akipeleka
benki. Kuna sehemu walifika wakamkuta
babu mchovu amejilaza barabarani.
Tajiri
aliyekuwa maskini akapaza sauti: “Wewe maskini unalala njiani unazuia msafara
wa mtu mkubwa na tajiri kama mimi, unatafuta nini? Hebu pisha njia haraka.”
Yule babu
mchovu akaomba kuzungumza na tajiri, alisema analo neno muhimu kwa ajili yake.
Tajiri alimfuata akiwa na hasira kali: “Wewe nani mpaka utake kuzungumza na
mimi?”
Babu mchovu
akamwambia: “Usiwe mkali, tuliza munkari. Unakumbuka kuna siku ulitaka kujiua
na ukaokolewa na kiumbe fulani? Unakumbuka alikupa njia za kupata utajiri na
alikueleza utaishi miaka 40 duniani?”
Tajiri
akapigwa butwaa, akashangaa babu yule amezipataje zile habari? Babu akamuuliza
tena: “Unakumbuka?”
Ikabidi
tajiri ajibu kuwa anakumbuka. Alipokiri tu kuwa anakumbuka, hapohapo babu
alibadilika na kugeuka yuleyule kiumbe mwenye mbawa! Malaika mtoa roho,
akawambia: “Miaka 40 niliyokupa, mwisho ni leo.”
Tajiri
aliyekuwa maskini akaishiwa nguvu, kwa kuchanganyikiwa akasema: “Basi naomba
nafasi kidogo nipeleke hizi pesa benki.”
Malaika mtoa
roho akajibu: “Kweli mali zinapendwa ila ni fitina kubwa kati ya Mungu na
binadamu. Yaani badala hata kuomba nafasi usali utubu, wewe unataka kwenda benki
kwanza. Nafasi hiyo huna.”
Aliposema
hivyo, hapohapo malaika mtoa roho alichukua nafsi ya maskini aliyegeuka tajiri,
mchezo wa duniani ukafika tamati palepale barabarani.
FITINA YA
MAMLAKA NA FEDHA
Kila
binadamu anapenda fedha, awe na mali nyingi. Watu wengi wanataka madaraka.
Wengi ambao wamejikuta matajiri walikuwa mafukara. Idadi kubwa ya wenye mamlaka
hivi sasa walikuwa watu duni nyakati zilizopita.
Fedha na
mamlaka ni vitu ambavyo huwafitinisha sana binadamu na Mungu wao. Lakini ni vitu
pendwa mno kwa binadamu.
Yupo mwenye
fedha hutaka kufanya chochote kisa anazo fedha. Anaweza kuwaonea wengine kwa
kiburi cha kwamba yeye ni tajiri.
Kuna mwenye
mamlaka anaweza kufanya dhuluma na uchafuzi, hata kuua watu kwa kiburi tu cha
mamlaka. Wenye fedha na mamlaka, hutenda maovu na kusahau kuwa juu yupo Mungu.
Wapo ambao
hutaka wanyenyekewe hata na wazazi wao, kisa ni matajiri au wana vyeo. Wengine
hutamani walambwe miguu.
USHAURI:
Ukiwa tajiri au kupata madaraka, omba sana Mungu akuongoze vizuri. Hiyo ni
fitina kubwa.
Ikiwa ndugu
yako ni tajiri au ana madaraka makubwa, muombee sana kwa Mungu. Huo ni uadui
kati yake na Mungu.
Ishi vizuri
na uwe mtu mzuri kila siku, Mungu atakusimamia. Najua unapenda fedha na
ungependa uwe na mamlaka, ila tambua hilo ni tego la imani. Ukipata kimojawapo
au vyote kwa pamoja, jitahidi kukaa kwenye njia ya Mungu ili ulishinde tego.
Ndimi Luqman
Maloto
0 comments :
Post a Comment