KUNA siku niliombwa na waandishi wenzangu wa habari,
tukutane tuweze kubadilishana mawazo kuhusu ujenzi wa maandishi yenye mvuto na
yasiyochosha katika uandishi wetu wa kila siku.
Tulipokutana, jambo la kwanza ambalo niliwapa ni kuwa
inahitaji mtu binafsi kwa utashi wake, awe mzuri ndipo atamjua mzuri.
Kwamba mwandishi mzuri ni lazima awe mpenda kusoma, tena
usomi wa kidadisi. Ni katika kusoma ndipo itakuwa rahisi kuyajua maandishi
mazuri pamoja na mwandishi mzuri.
Na ukishayajua maandishi mazuri na mwandishi mzuri, ndipo
utaweza kuandika vizuri, maana taratibu utajifunza njia mbalimbali za uandishi
wenye ladha tamu kwa kuiba maarifa ya uliowasoma na kuongezea ubunifu wako
kisha kuunda njia zako.
Nimeshakutana na baadhi ya waandishi wa habari, wananiambia:
“Najitahidi sana lakini sifikii kiwango cha kuitwa mwandishi mzuri.”
Jawabu langu huendana na maswali mawili: “Je, unayajua
maandishi mazuri? Je, unawajua waandishi wazuri?” Siku majibu hayo yakiwa
“ndiyo”, basi na wewe ni mwandishi mzuri na utafikia daraja la kuitwa bora.
Na huo ndiyo hasa mfumo wa maisha ya kila siku. Unahitaji
kuwa muungwana ili uwajue waungwana wapoje.
Haiwezekani wewe uwe muongo halafu umtambue mkweli. Zipo
njia ambazo mnapishana, kwa hiyo hamtaweza kwenda sambamba hata siku moja.
Ni kwa sababu wewe umezoea kuongopa, ndivyo utaona na maneno
ya ukweli kutoka kwa mkweli ni uongo mtupu. Lazima uyatie kasoro, maana umezoea
kusema uongo, wewe unaendana na waongo wenzio.
Ndoa nyingi zipo kwenye misukosuko, mume na mke
wanaparurana. Wananyoosheana vidole, kila mmoja anamuona mwenzake ni tatizo.
Niliwahi kukutana na mke na mume wenye migogoro.
Tulipozungumza pamoja kila mmoja alikuwa anatetea upande wake.
Nikaomba kuzungumza na mmoja-mmoja, na kila mmoja
nilimwambia: “Hutafikia pointi ya kutambua uzuri wa mwenzako mpaka wewe
mwenyewe uwe mzuri. Utatambua kwamba mwenzi wako ni bora kama wewe mwenyewe
utabadilika na kuwa bora. Badilika na uwe bora halafu ufanyie kazi malalamiko
ya mwenzio ili asiendelee kulalamika.”
Nilipompa maneno hayo
kila mmoja, baadaye niliwaita wote nikawaambia wakafuate yale ambayo
niliwaambia. Baada ya mwezi mmoja, walinipigia simu, mke akaniambia: “Mwalimu
asante sana, nilichelewa kufahamu kuwa nina mume bora kuliko wanaume wote chini
ya jua.”
Kisha mume naye akaniambia: “Nilikuwa nimeshajidanganya kuwa
nilikosea kuchagua na kuoa, nikadhani wapo wanawake wazuri zaidi. Tangu
tumetoka kwako mwezi uliopita, na kufanyia kazi ushauri ulionipa, nimeweza
kuona mabadiliko makubwa ya kimaisha kutoka kwangu binafsi na mke wangu.
“Na sasa nathubutu kusema nimekuwa mwanaume mwenye bahati
kubwa kumpata na kummiliki mke wangu. Upendo wangu kwake umeongezeka, amekuwa
mwanamke bora kupata kumshuhudia. Sidhani yupo mwingine wa kumfikia.
Nakushukuru, hakika huyu ndiye mke wangu chaguo nililoelekezwa na Mungu.”
Pokea ukweli huo
kwamba ndoa bora na yenye furaha hujengwa na watu wawili wazuri. Usikimbilie
kusema mwenzangu hafai, jiulize wewe mwenyewe kwanza, je, unafaa?
Upo kazini na unagombana na wenzako kila leo, unasema
hawakuheshimu, wanakubagua. Jiulize, je, wewe unayo heshima kwa wenzako na
huwabagui?
Ni rahisi mno kwa mtu asiye na heshima kwa wenzake kuona
haheshimiwi. Kama ilivyo kwa mbaguzi, ni mwepesi kunyoosha kidole kuwa
anabaguliwa.
Ndoa nyingi zinapata misukosuko kwa sababu roho wa kukosa
uaminifu ndiye ametawala. Kila mmoja anakuwa anamhisi mwenzake anachepuka.
Sikiliza ndugu yangu; Unahitaji kuwa mwaminifu ndipo
utabaini kuwa mwenzako ni mtu mwaminifu kuliko wote duniani.
Ukosefu wa uaminifu ni roho mchafu. Akishakutawala, nawe
utapoteza imani kwa mwenzako. Hata awe mtulivu vipi, bado utamtilia shaka
kwenye mawasiliano yake. Utanyata upekenyue simu yake, hata usipopata
unachohitaji, utajiambia: “Amefuta, ipo siku nitamkamata.”
Na siku zote utamuona mwenzako ni tatizo. Lakini siku
ukiamua kumfukuza roho wa kukosa uaminifu kwenye mzunguko wa maisha yako. Ukawa
mwaminifu na mwenye kujiamini, utajikuta unakuwa na imani kubwa kwa mwenzako.
Ukimpigia simu asipopokea, hutasema yupo maeneo mabaya,
utaona ni bahati mbaya, kwamba labda simu ipo mbali au amebanwa na kazi.
Uaminifu lazima uanze na wewe.
Wapo watu wengi waliwapa akili ya usaliti wenzi wao kutokana
na kuwatuhumu. Kila siku anatuhumiwa, anajiuliza hapa na uaminifu wangu siaminiwi
sasa uaminifu wa nini? Anaamua kuchepuka, mwisho anakuwa mtaalamu wa kucheza
nje cup.
Aliyekwambia nani kama inaweza kutokea mwizi akamwamini mtu?
Uwe mwaminifu kiasi gani lakini atakuona tu unamwibia.
Bosi kila siku anafukuza wafanyakazi kwa sababu anaamini
wanamuibia. Sababu ni kuwa yeye mwenyewe ni mwizi, sasa atawezaje kumwamini
mtu?
Wanasiasa wengi wana hulka za kilaghai pamoja na
udanganyifu, ndiyo maana nyakati za uchaguzi duniani kote lazima kutokee
malalamiko ya kuchezeana rafu au hata kuibiana kura. Huo ndiyo mwendo.
Unatakiwa kuwa jirani mzuri ili uwaone majirani zako ni watu
bora kuishi nao. Wewe ukiwa mbinafsi, uungwana wa majirani zako unaweza
kuutafsiri kama kujipendekeza kwao kwako.
Utauona ubora wa marafiki zako kama wewe mwenyewe utakuwa
rafiki bora. Ukijitengeneza kirafiki daima kila mmoja atapenda kukusogelea na
utaitwa mtu wa watu.
Watu wanapokuwa mbali na wewe usiseme umetengwa, jaribu
kujiuliza, je, tabia yako inavuta watu au inawakimbiza? Nidhamu ya kuishi
inakutaka uanze kujinyooshea kidole wewe kabla hujafanya hivyo kwa wenzako.
Nidhamu ya maisha ilimtaka Winnie Mandela kuwa mwanamke bora
ndipo angeutambua utukufu wa Nelson Mandela. Ni kwa sababu hakuwa bora, hivyo
hakumwelewa mwanaume bora, na matokeo yake heshima ambayo alistahili kuipata,
ilikwenda kwa Graça Machel.
Ni watu wengi tu kwa kushindwa kwao kuwa watu wema, hupatwa
na upofu wa kutowatambua watu wazuri na matokeo yake kupoteza fursa kubwa
baadaye kama ilivyotokea kwa Winnie alivyompoteza Mandela.
James Sirleaf hakujua safari njema ya Ellen Johnson Sirleaf,
matokeo yake alipomuoa hakutaka asome, alilazimisha kumfanya mama wa nyumbani
na tegemezi kwake.
Sirleaf hakuwa na macho mazuri ya kuitazama kesho, kwa hiyo
hakugundua kuwa Ellen ni mwanamke mkubwa mno. Wenyewe humwita tembo.
Ndiyo maana juhudi za Ellen kuitafuta kesho yake, Sirleaf
aliichukulia kama kupoteza muda na kutozingatia majukumu yake ya nyumbani kama
mama wa familia. Sirleaf aliamini Ellen ni golikipa tu, yaani mke mwenye
kutegemea tu mfuko wa mume wake.
Ellen alipokuwa analazimisha kusoma ili kubadili maisha yake
na kuyafikia malengo ya kuwa kiongozi katika Taifa la Liberia, Sirleaf aliinua
mikono, akampa talaka. Alitaka Ellen awe mke mpika chakula, muosha vyombo,
mpiga deki sakafu, mfua nguo na mbembeleza watoto tu.
Nini kimetokea leo, Ellen ndiye Rais wa Liberia. Na ameweka
rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza mwafrika kuwa kiongozi mkuu wa taifa. Sirleaf
hakuyaona, Ellen aliyaona.
Sirleaf alimuona Ellen msumbufu na mwanamke asiyefaa kuwa
mke na mama bora. Ellen alijiona anaweza kupanda milima na kufika alipo sasa.
Inahitaji macho yenye kuona vizuri ndipo mtakuwa na ushuhuda unaofanana. Siyo
mmoja aone, mwingine haoni, kisha wote muwe mashahidi. Haiwezekani!
Inahitaji watu wawili wenye ndoto za kufanana ndipo
itawezekana kusafiri pamoja. Kama mnapishana hamtaelewana. Ni rahisi mwenzako
kukuelewa kama wewe mwenyewe ndiye utaanza kumwelewa.
Binadamu ni kama kioo, jinsi unavyotabasamu ndivyo na
taswira yako kwenye kioo itakavyokuwa hivyohivyo. Na ukinuna, kioo chako
kitakununia.
Ukitabasamu mbele
mbele ya mwenzako naye atatabasamu. Mtu mwenye kabila moja na Shetani ndiye
pekee anaweza kumkasirikia mwenzake mwenye kumuonesha tabasamu.
Cheka na mwenzako ili akuchekee. Kuwa na furaha wakati wote ndipo
utaona na wenzako wanaonesha furaha wanapokuwa na wewe.
Siku zote uzuri wa mwenzako unaanza na wewe. Uungwana
ukiuanzisha utakufuata. Ukikunjua tabasamu utakunjuliwa. Ukijishirikisha kwa
wenzako nao watashiriki kwako. Siku zote ushirikiano humuelekea mpenda
ushirika.
Asante.
Ndimi Luqman Maloto
0 comments :
Post a Comment