ads 728x90 B

UKWELI UNA KAWAIDA YA KUCHELEWA!




BINADAMU tunaongozwa na hisia ambazo hutengeneza pupa. Kila mja huumba mambo yake na kutaka kuyatimiza kwa wakati anaotaka.
Ni vizuri kujiwekea malengo na matarajio lakini subira ni muhimu zaidi. Amini kuwa hayatimii mambo kwa matakwa ya binadamu, bali kwa ridhaa ya Mungu Mfalme.
Umesingiziwa, imekuuma sana. Lakini kosa ambalo unafanya ni kuwaza ulivyosingiziwa kupita kiasi. Unataka ukweli udhihirike mapema ili waliokusingizia waumbuke.
Kadiri muda unavyosogea ndivyo unazidi kuumia. Unataka matokeo ya haraka. Unasononeka na hata usingizi hupati. Mara unashindwa kula, presha inashuka, vidonda vya tumbo navyo vinabisha hodi.
Niruhusu nikwambie kitu ndugu yangu; Sononeko lako ni kwa sababu hutambui kuwa ukweli una kawaida ya kuchelewa na hungonja wakati mwafaka ndipo ujidhihirishe.
Unaweza kutamani ukweli udhihirike leo lakini kumbe siyo wakati mwafaka. Kwa fikra zako unaweza kudhani ndiyo muda hasa, lakini kumbe sivyo. Ni kwa sababu Mungu ndiye huamua kipindi gani mwafaka cha ukweli kufanya kazi yake.
Umedhalilishwa? Vuta subira, usilazimishe heshima ya haraka. Amini kuwa wakati ukifika utaheshimiwa. Na si ajabu waliokudhalilisha ndiyo wakadhalilika wao. Ukweli una tabia ya kulipa kisasi, muda wake unapowadia.
Kosa la kiufundi ambalo wengi wetu hulifanya ni kutaka kulazimisha kuheshimiwa pale wanapokuwa wamefanyiwa kitendo au vitendo vya udhalilishaji. Amini katika kusubiri, heshima yako utaipata tu.
Ndugu yangu ambaye nilipata kufanya naye kazi, marehemu Adolph Balingilaki, alikuwa na msemo wake aliopenda kuurudia mara kwa mara: “Mtaka heshima kwa nguvu, utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Hekima za Balingilaki, Mungu amuweke mahali pema, ni msisitizo uleule kuwa ukifanyiwa jambo lenye kudhalilisha , ukitaka ulazimishe kuheshimiwa, unaweza kujikuta unadhalilika zaidi.
George Stinney Jr, angekuwa na umri wa miaka 87 sasa kama Mungu angemuweka hai. Aliuawa akiwa mtoto mwenye umri wa miaka 14.
Maskini George, aliponzwa na Uafrika wake ndani ya Marekani ambako nyakati hizo ubaguzi wa rangi ulikuwa umekithiri.
Akasingiziwa ameua mabinti wawili wa Kizungu ambao walikutwa wamekufa. George akakamatwa, eti kwa sababu ndiye alionekana nao kwa mara mwisho. Akalazimishwa kukiri kosa.
Majaji Wazungu (all-white jury), walijifungia na kumhukumu George, bila hata utetezi. Hakuwekewa wakili wa kumtetea. Akahukumiwa kuuawa kwa shoti ya kiti cha umeme.
George alikuwa mtoto, na aliweka rekodi ya kuwa mtoto mdogo zaidi kuuawa kwa adhabu hiyo ya kiti cha umeme. Taarifa zinasema kuwa mateso yalikuwa makali mno, alipasuka mpaka kichwa, maana kiti kile cha umeme hakikutengenezwa kwa ajili ya watoto. Kililazimishwa kutumika kumuua George.
Jaribu kujiuliza George aliumia kiasi gani kuuawa kwa kosa ambalo hakulifanya? Wazazi na ndugu zake waliumia kiasi gani? Unadhani George hakupenda ukweli ujulikane kabla hajauawa?
Mungu alitaka kuwaumbua Wazungu! George aliuawa Juni 16, 1944. Mwaka 2014, yaani miaka 70 baada ya kifo chake, ndipo Mahakama Kuu Marekani, ilitoa hukumu ya kukosoa hukumu ya mwaka 1944 (Conviction vacated), kwamba George alionewa. Ikaamriwa familia yake ilipwe fidia.
Mwaka 2004, mwandishi Mmarekani ambaye ni mbobezi wa historia, George Frierson, ndiye aliyeibua kila kitu. Baada ya kufanya marejeo na rekodi mbalimbali, kesi ilirudishwa mahakamani na hukumu tofauti ilitolewa   
Mbona Yusuf alitumbukizwa kisamani na ndugu zake kisha wakamwambia baba yake kuwa ameliwa na wananyama wakali? Mbona Yusuf huyohuyo alisingiziwa amembaka Zulaikha ambaye ni mke wa aliyekuwa Mfalme wa Misri, Potiphar.
Matokeo yake Yusuf alifungwa jela. Siku ukweli ulipodhihirika, Yusuf alitoka jela kama shujaa, na mwokozi wa taifa la Misri. Ndugu zake pia walifedheheka kwa kumtenda ubaya na kusingizia kuwa ameliwa na wanyama.
Nini kilimpata Zulaikha? Zipo taarifa kuwa Potipher alimuua Zulaikha kimyakimya baada ya kubaini ukweli kuwa alimsingizia Yusuf, na kwamba ni yeye ndiye aliyemtaka kimapenzi.
Jiulize, hapo ulipo una wasiwasi gani? Mbona unakuwa na haraka? Vuta subira, muda utafika na wewe utakuwa huru. Usijiumize kwa kutaka matokeo ya papo kwa papo.
Karne 12 kabla ya Yesu (BC), walikuwepo ndugu wawili, Anubis ambaye alijulikana pia kama Anpu na mdogo wake, Bata. Waliishi vizuri sana na walisaidiana kwenye shughuli za shamba.
Siku moja wakiwa shamba Anubis alimtuma Bata nyumbani kwenda kuchuchukua mbegu ili wapande shambani.
Bata alipofika nyumbani, alikuta mbegu ni nyingi, kwa hiyo ili isiwe mizunguko ya nenda rudi, aliamua kubeba mzigo wote kwa wakati mmoja.
Uwezo huo wa kubeba wa Bata, ulimuonesha ni kijana mwenye nguvu. Mke wa Anubis (kaka yake Bata) aliyekuwa nyumbani, alivutiwa na msuli wa Bata, akamtongoza.
Bata alishangazwa na namna ambavyo mke wa kaka yake alivyomtamkia maneno ya kimapenzi. Kwa hasiri Bata alimwambia shemeji yake: “Usirudie siku nyingine kuniambia maneno ya kishenzi kama hayo.”
Baada ya kumjibu hivyo, Bata alibeba mbegu zote mpaka shambani kisha wakaendelea na shughuli za shamba pasipo kumsimulia chochote kaka yake kwa kutambua, angemweleza bila shaka ndoa ingeweza kuvunjika.
Hata hivyo, yule mwanamke, yaani mke wa Anubis, aliona kitendo alichofanyiwa na Bata ni cha dharau, na kumkosea heshima, kwa hiyo aliamua kumkomoa kwa kumchonganisha na Anubis.
Anubis na Bata waliporudi nyumbani, mke wa Anubis alimwita mumewe chumbani watete, wakati huohuo Bata aliingia zizini kulisha mifugo.
Kule ndani, mke wa Anubis alimuonesha mumewe nguo iliyochanika, alama za mwili kama vile alipata kashkashi nzito, akasema akiangua kilio: “Bata, huyuhuyu mdogo wako unayempenda, alinitaka kimapenzi, nilipomkatalia, alinilazimisha mpaka kutaka kunibaka. Ndiyo hii hali unaiona hapa.”
Bata akiwa kwenye mifugo, anapewa taarifa kupitia wale wanyama kuwa Anubis anataka kumuua baada ya kupewa maneno ya uchonganishi na mkewe. Anaelekezwa akimbie haraka kabla hajauawa, kwani Anubis ana hasira sana.
Kweli, Anubis akiwa na hasira kali, anakwenda zizini akiwa na panga ili amtenganishe Bata kichwa na kiwiliwili kama adhabu ya jaribio lake la kumbaka shemeji yake. Anubis aliumia sana mdogo wake kipenzi ambaye wameishi kwa mapenzi yote miaka nenda rudi, kuthubutu kumtaka kimapenzi mkewe na hata kujaribu kumbaka.
Anubis alipofika zizini hakumkuta Bata. Alimtafuta huku na huko bila mafanikio. Bata alikimbilia mbali mno.
Bata aliumia mno kusingiziwa, alitamani ukweli ujulikane haraka ili yeye na ndugu yake waelewane. Haikuwa hivyo. Ukweli una kawaida ya kuchelewa lakini ukiwadia hutoa adhabu kali kwa mlengwa na walengwa.
Anubis aliishi kwa hasira, akimuwinda mdogo wake. Alitamani kumuua. Nyakati hizo nchini Misri, ukimtongoza mwanamke wa mtu, adhabu yako ni kifo. Anubis alitaka Bata afe kufidia makosa ya kujaribu kuingilia ndoa yake.
Ngoja sasa nikwambie. Vuta pumzi kwanza japo kidogo. Haya sasa, uongo uliopikwa na mke wa Anubis, ulizunguka siku zote kwenye kichwa cha Anubis, na kujenga hasira kali kwa Bata.
Sasa tambua kuwa ilifika wakati Anubis aliuelewa ukweli, na siku hiyohiyo hakumkwawiza mkewe, alimuua kikatili, kwa hasira zenye ujazo wa aina mbili. Kwanza kumsaliti, hadi kumtaka mdogo wake, pili kumfitinisha na mdogo wake kipenzi.
Hiyo ndiyo inaitwa hasira za ukweli. Tambua kwamba uongo unaweza kutawala hata miaka 10, lakini siku ukiamua kujidhihirisha huwa na matokeo makubwa.
Ona hata sasa, zimefika nyakati ambazo wafu wanakumbukwa. Wanahitajika mno kuliko wakati wowote.
Waliitwa magaidi na majina mengine chungu nzima. Walisemwa ni wao wanaoifanya dunia kuwa mahali hatari. Waliandamwa na kuuawa kinyama.
Chuki ya Marekani dhidi ya aliyekuwa Rais wa Iraq, Saddam Hussein, ilikuwa kubwa mno. Kizazi kwa kizazi. Mwisho wakafanikiwa kumuondoa na kumuua.
Wamarekani walidhamiria hasa kuhakikisha aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi anang’oka. Hawakufanikisha hilo tu, bali pia na mauti yake.
Na Gaddafi alionya: “Marekani na wenzake wa Magharibi wanataka niondoke lakini wanatakiwa kufahamu kwamba uwepo wangu ni salama mno kwao.” Maneno hayo hawakuamini, wakamuua.
Leo hii Wamarekani wanawalilia Saddam na Gaddafi! Ted Cruz ni mgombea urais, anayetafuta tiketi ya uteuzi kupitia Chama cha Republican, moja ya mambo ambayo amekuwa akiyasimamia ni kuwa nchi yake ilifanya makosa kuwavamia Saddam na Gaddafi.
Anasema: “Mashariki ya kati ingekuwa salama zaidi kama Saddam na Gaddafi wangeendelea kuwepo. Kuuawa kwa watu hao wawili kumesababisha machafuko kuwa mabaya. Mashariki ya Kati imekuwa sehemu hatari zaidi ya kuishi.”
Mgombea mwingine wa urais wa Marekani, anayewania tiketi ya Republican, Donald Trump, anasema: “Siyo Mashariki ya Kati tu, dunia nzima ingekuwa salama kama Gaddafi na Saddam wangekuwepo.”
Trump anasema kuwa Marekani imefanya kosa kubwa kuivamia Syria na kutaka kumng’oa Bashar al-Assad, kwani machafuko yamekuwa makubwa zaidi.’
Wana haki ya kulia; Kwa mujibu wa ripoti za Serikali ya Marekani, vitendo vya ugaidi Mashariki ya Kati kuanzia mwaka 2002 na 2014, vimeongezeka kwa asilimia 4,500. (Msisitizo asilimia 4,500).
Ripoti zinaonesha pia kuwa kabla ya mwaka 2003 wakati Marekani ilipoivamia Iraq, taifa hilo halikuwahi kuwa vitendo vyote vya ugaidi na kujitoa mhanga chini ya Saddam. Ilala sasa kuna mashambulizi 1,892.
Taarifa za Serikali ya Marekani zinaonesha kuwa nchi hiyo imetumia dola trilioni 6, ambazo kwa fedha za Kitanzania ni karibu shilingi trilioni 13,000 (quadrillion 13).
Idadi hiyo ya fedha, inakadiriwa kuwa sawa na kila makazi nchini Marekani kupewa gawio la dola 75,000 (shilingi milioni 161). Na inashtumiwa kuwa fedha nyingi kati ya hizo ni za kukopa.
Ongezea kuwa zaidi ya wanajeshi 7,000 wa Marekani wamesharipotiwa kufariki dunia kutokana na vita hizo. Makumi elfu ya wanajeshi wamekuwa hawatambuliki walipo.
Hakika, ukweli unapotokeza huwa na nguvu sana. Hutoa kishindo kizito. Una kelele nyingi.
Ndimi Luqman Maloto
        
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment