ads 728x90 B

Ursula Burns - Shule imemtoa kwenye ufukara mpaka ubilionea






Luqman Maloto

ELIMU huleta heshima, hupandisha daraja la msomi. Ni nyezo inayosababisha chakula kifike mezani bila usumbufu. Ni silaha inayorahisisha maisha kwa upana kabisa.
Elimu ndiyo silaha rahisi inayoweza kumfanya mtoto wa maskini kunyenyekewa na kuogopwa hata na matajiri! Mtoto wa mtumwa msomi, aliweza kuwafanya Wazungu wakae mezani na kujadili uhuru wa mtu mweusi.
Pamoja na mambo mengine yote yanayoweza kutamkwa lakini ukweli ulionyooka ni kuwa ni elimu ndiyo iliwafanya Wamarekani kunyoosha mikono kwa Jaluo wa Kenya, Barack Obama kisha kumkabidhi nchi awaongoze.
Obama asingesoma, hata angekuwa na karama ya aina gani Wamarekani wasingemchagua. Hata chama chake, Democrats, kisingempitisha kuwa mgombea urais. Waliompendekeza wasingeshawishika kumuona anafaa. Hata yeye mwenyewe binafsi, asingekuwa na jeuri ya kujitokeza.  
Elimu humjengea mtu hali ya kujiamini. Wapo watu wengi wenye uwezo mkubwa lakini hushindwa kunyoosha maneno mbele ya wasomi. Na hatua muhimu ya mtu kuyaelekea mafanikio yake binafsi ni kujiamini. Mpe mwanao elimu ili ayaone haya maisha ni mepesi!
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela, aliwahi kusema: “Education is the most powerful weapon which you can use to change the world.”
Kiswahili: Elimu ni silaha yenye nguvu kuu ambayo unaweza kuitumia kuibadili dunia.
Mwanasaikolia, msomi wa Botania na mvumbuzi mashuhuri wa Marekani, George Washington Carver, aliwahi kusema: “Education is the key to unlock the golden door of freedom.”
Kiswahili: Elimu ni ufunguo wa kufungulia mlango wa dhahabu wa uhuru.
Wito na msisitizo wa muda mrefu umeshatolewa kuhusu umuhimu wa kumuelimisha mtoto wa kike. Ipo kaulimbiu maarufu kuwa ukimuelimisha mtoto wa kike, umeelimisha jamii nzima.
Ursula Burns ni mmoja wa wanawake wa kuigwa mno katika ulimwengu wa sasa. Yeye bila shaka yoyote, ameweza kuyafanya yasiyowezekana kuwezekana.
Mtoto wa mkimbizi, aliyelelewa na mama maskini, tena Mwafrika katika jamii iliyojaa ubaguzi wa rangi. Sasa ni mwanamke wa mfano, tajiri na mwenye kunyenyekewa mno.
Anaingiza fedha nyingi kutokana na mshahara anaolipwa. Siyo maskini tena, kwani mamilioni ya dola lakini mabilioni ya fedha kwa kulinganisha na sarafu ya Tanzania (shilingi), yanaingia kwenye akaunti yake kila mwaka.
Ni kweli anastahili pongezi lakini upande wa pili hakuna maajabu yoyote hapo, ni elimu ndiyo imefanikisha kila kitu. Kama upo shuleni soma, ikiwa upo mitaani lakini unayo fursa, nenda kasome. Elimu ni fedha, ni heshima, vilevile ni mamlaka.
Ursula anazungumziaje hatua aliyofikia? Anasema: “Dreams do come true.” Akimaanisha: “Ndoto hutimia kuwa kweli.”
Anasema: “Ndoto huwa kweli, lakini siyo bila ya msaada wa wengine, elimu nzuri, kuwa na maadili imara ya kazi na ujasiri wa kufikia makusudio yako.”
Hapo utaona kuwa Ursula anaeleza umuhimu wa elimu nzuri kama nyenzo muhimu ya kufikia mafanikio kama yake. Mengine yote yanawezekana, kwa maana ya msaada kutoka kwa watu wengine, kuwa na maadili na ujasiri lakini elimu je? Lazima usome kwanza.
URSULA NI NANI?
Ursula ndiye Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) , vilevile Mwenyekiti wa Shirika la Xerox, Marekani. Kutokana na ukuu huo, Kampuni ya Fortune 500 ambayo huchapisha jarida maarufu Marekani la The Fortne 500, limekuwa likimtambulisha kama mwanamke mwenye nguvu zaidi.
The Fortune 500 ni jarida ambalo hutoka mara moja kwa mwaka, likiwa na orodha ya mashirika 500 makubwa.
Katika orodha hiyo, huangaliwa mapato kwa mtindo wa ile ambayo imefanya vizuri zaidi hadi nafasi ya 500 katika mwaka husika wa fedha.
Ursula akiwa bosi bosi wa Xerox, alitokea kuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika, kuongoza orodha ya mashirika 500 katika jarida la The Fortune 500, kutokana na mafanikio anayopata.
Vilevile akawa mwanamke wa kwanza kuongoza katika The Fortune 500 akimrithi mwanamke mwenzake, Anne Mulcahy.
Mulcahy ndiye alikuwa CEO wa Xerox, nafasi ambayo alimwachia Ursula ambaye anaendelea kuishikilia kwa mafanikio makubwa.
Xerox  ni shirika ambalo linajikita kwenye mauzo ya huduma za kibiashara na nyaraka za kiteknolojia kwa ajili ya bidhaa za kibiashara na kwa serikali katika ukubwa na viwango vya aina mbalimbali.
Makao makuu ya Xerox yapo Norwalk, Connecticut, kabla ya hapo, yalikuwa Stamford, Connecticut, Marekani. Makao hayo yalihamishwa Octoba 2007 kwa sababu za kibiashara na kihuduma.
Ni shirika linalotengeneza faida kubwa na ndiyo maana kwa miaka mfululizo, limekuwa likishika namba moja. Hii ni kwa sababu limekuwa likitengeneza faida kubwa kila mwaka.
Kutokana na mafanikio hayo, ukiachana na jarida la Fortune 500, upande mwingine jarida la The Fortune, limekuwa likimtaja kama mwanamke mfanyabiashara bora kwa miaka sita mfululizo, tangu mwaka 2009.
Mwaka juzi (2014), jarida maarufu kwa takwimu mbalimbali ulimwenguni, Forbes, lilimtaja Ursula kuwa mwanamke wa 22 kati ya 100 wenye nguvu zaidi ulimwnguni.
Ni bilionea, mwaka 2014, mshahara wake ulitajwa kuwa dola milioni 18.7 ambazo kwa ubadilishaji wa fedha kwa Shilingi ya Tanzania ni sawa na bilioni bilioni 40.9.
Fahamu ya kwamba hizo siyo mali zake, huo ni mshahara tu kwa mwaka husika, yaani 2014.
Mafanikio yote hayo, yamefuata baada ya msoto wa hali ya juu. Mwenyewe anakumbuka kila kitu na shukurani zake za kipekee huzielekeza kwa mama yake mzazi kwamba alikuwa bora sana katika kumsimamia na kumjenga hadi kufikia mahali alipo hivi sasa.
Ursula anasema: “Nimelelewa na mama bora sana, mama mzuri mno. Hakuwa na fedha lakini mapenzi yake kwa mimi mtoto wake yalikuwa ni zaidi ya kitu chochote kile. Hakuwa na maisha ya uhakika, lakini alihakikisha naishi na kupata elimu bora.
“Mimi na mama yangu tuliishi katika makazi duni yaliyo kwenye mpango wa msaada wa serikali, katika bonde la Mashariki ya Mji wa Manhattan katika Jiji la New York.
“Wakati wa ukuaji wangu, watu wengi walianiambia nilikuwa na majanga ya aina tatu yaliyokuwa yakinikabili. Kwanza nilikuwa mtoto mweusi, pili nilikuwa msichana, tatu nilikuwa maskini.
“Kwa kujumlisha mambo hayo matatu, watu walisema nilikuwa na bahati mbaya na kwa hivyo, nisingeweza kufanikiwa. Leo hii ninapojitazama na kugundua nimethibitisha tofauti kwa wale walioamini sitaweza kufanikiwa kutokana na kasoro tatu nilizokuwa nazo, hakika namshukuru Mungu.”
Ursula anasema kuwa siyo uongo kwamba kulikuwa na changamoto pevu. Anaeleza kuwa maisha yalikuwa magumu, yenye kujaa ubaguzi na manyanyaso ambayo ilitaka moyo kuvumilia.
Anabainisha kuwa kama siyo mama yake kumtia moyo na kumjaza maadili ya namna bora ya kuenenda katika maisha, pengine angeharibikiwa akiwa binti mdogo au hata kukata tamaa.
Ursula anasema: “Watu walisema nina upungufu kwa umaskini wangu, weusi wangu na vilevile ni mtoto wa kike, lakini mama hakunitazama kwa macho ya aina hiyo. Aliamini ningeweza kutoka nilipokuwa na kufika mahali bora zaidi.”
Chukua hii; Kama mzazi, mtoto wako anahitaji neno kutoka kwako. Huwezi kuamini lakini ni ukweli kuwa neno la kumtia moyo na kumfariji linaweza kumjenga mpaka kuona anaweza kuubeba Mlima Kilimanjaro begani.
Mwambie mwanao anaweza kushinda. Anafanya vibaya darasani lakini hilo lisikuvunje moyo, mweleze kuwa yeye ni bora na ana akili nyingi. Huwezi kutambua lakini ndiyo ukweli kuwa utakuja kugundua baada muda anatengeneza A badala F ulizozizoea.
Ni hivyo ndivyo Ursula alivyojengwa na mama yake. Katika jamii iliyokuwa inamdharau na kumuona siyo kitu, mama wa Ursula alimwambia mwanaye: “Elimu ndiyo njia pekee ya kukupandisha na kukutoa kimaisha. Wewe ni bora kuliko wao.”
Ursula anasema: “Kwa kipato duni ambacho mama yangu alipata, alijinyima na kudunduliza kisha kunipeleka kwenye shule nzuri. Nilisoma kwenye shule nzuri za Kanisa Katoliki. Haikuwa rahisi lakini mama yangu alijituma kufanya kazi na kupata fedha za kutosha kunilipia ada na michango mingine.
“Nyakati hizo, nilitamani kusoma ili nipate kazi ya haraka angalau niweze kumsaidia mama yangu. Nilitamani kuwa mhubiri, mwalimu au nesi. Hizo ndizo zilikuwa ndoto zangu kwa kipindi ambacho nilikuwa binti mdogo wa shule. Sikujua kama ningemudu kufika kwenye daraja nililopo kwa sasa.”
Ursula anaendelea kusema: “Katika vipaumbele vyangu hivyo vitatu, uhubiri, ualimu na unesi, hakuna hata kimoja kiliweza kudumu kwenye mapenzi yangu. Nilipokuwa napanda madarasa ya juu, nilitamani kuwa mhandisi. Na hii ni kwa sababu nilikuwa namudumu vizuri masomo ya Sayansi na Hisabati. Kila muda niliwaza uhandisi. Nilitamani kuwa mhandisi mashuhuri.
“Baada ya kufuatilia ndoto zangu na maendeleo yangu shuleni, chuo cha Brooklyn Polytechnic Institute kilinipa ofa kujiunga nao kwa ajili ya masomo ya uhandisi. Wakati ilitarajiwa kuwa kwa ofa hiyo ningeshangilia na kuona ndoto zangu zinakwenda kuwa kweli, mimi nilichanganyikiwa.”
Ursula anasema kuwa kilichomfanya achanganyikiwe ni kwamba hakuwa mwangalifu tangu mapema juu ya kipi hasa ambacho alikuwa anahitaji kusomea, maana uinjinia ulikuja tu kama wimbo kutokana na jinsi alivyokuwa anazungumza na wanafunzi wenzake na matokeo ya masomo yake.
“Ni ofa sawa lakini niliona natakiwa kuwa mwangalifu kuhusu kipi hasa napenda kukifanya. Nilikuwa sijajifanyia maandalizi ya kutosha. Kingine niliona chuo kilikuwa na mazingira tofauti, maana Brooklyn niliona ipo tofauti na maeneo mengine ya New York.
“Nilihofia pia umbali, kwa hiyo niliona nitakuwa kama mgeni na mazingira yote yangekuwa mageni kwangu. Kingine kilichonipa hofu ni wanafunzi wengine, niliamini wangekuwa na akili sana kuliko mimi,” anasema Ursula.
Hatma yake ilikuwaje? Ursula anasema: “Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nilikuwa nipo njiapanda. Upande mmoja akili yangu iliniambia niende chuo, upande wa pili inanirudisha nyuma kwa kuamini mazingira yangenipa shida.
“Ilikuwa rahisi zaidi kuacha ndoto zangu ziende kisha kupanga upya safari ya maisha yangu kwa namna ambavyo ningeona ni rahisi. Asije kukwambia mtu, ukiwa na mama mzuri ni mtaji mkubwa sana katika maisha yako. Mama yangu ni mtaji mkuu.
“Mama alinipa ujasiri, aliniambia Brooklyn isingenishinda na wanafunzi wasingekuwa na akili kuliko mimi. Alinijenga kiakili na nikakomaa kisaikolojia. Ukijumlisha na mafunzo ya kiroho niliyoyapata katika shule ya Kikatoliki ya Cathedral High School, nilijikuta napata moyo na kuamua kujiunga na chuo hicho.
“Nilipofika shule mambo hayakuwa mepesi. Ilibidi nisome kwa bidii ili niweze kwenda sawa na wenzangu. Nilikuwa kiumbe wa ajabu baharini. Chuo kilikuwa na wanafunzi wengi wanaume Wazungu. Mimi nilikuwa mwanamke, Mwafrika.”
Anaeleza kuwa alijitahidi kuzoea mazingira na kutokatishwa tamaa, ingawa kwa muda mrefu alikuwa akijihofia kila alipokuwa akiwatazama wanafunzi wenzake waliokuwa wamemzunguka.
“Nilianza kusoma chemical engineering, ambayo nilijikuta naichukia, na baada ya muda nilibadilisha na kusoma mechanical engineering, ambayo niliipenda. Na taratibu nilijikuta naweza, napenda mazingira ya shule, kuwaelewa na kuwakubali wanafunzi wenzangu, na hapo ndipo nilianza kufanya vizuri zaidi katika masomo.
“Kuanzia wakati huo, maisha yangu yalibadilika na kuwa na mtiririko mzuri. Nikiwa bado nasoma, nilijiunga na Xerox, ofisi zao za New York, kwa ajili ya mafunzo ya mafunzo ya vitendo kisha nikaenda Ivy League school ambako nilifanikiwa kumaliza shahada yangu ya kwanza ya uhandisi.
“Baada ya kuhitimu shahada yangu, niliajiriwa na Xerox, nilifanya kazi lakini baadaye nilirudi tena chuo ambako nilisoma shahada yangu ya pili, na hapo ndipo nilipoanza kupanda ngazi mpaka juu kabisa katika kampuni.
“Nikiwa CEO wa Xerox, nimelifanya shirika kutoka katika mkondo wa nakala na uchapishaji, kisha kuliingiza kwenye ulimwengu wa kiteknolojia pamoja na upana wa huduma zake.”
Ursula anasisitiza: “Ndoto hutimia lakini ni rahisi zaidi ukiwa na elimu nzuri pamoja na watu. Ndiyo maana nimetumia muda mwingi na shirika ambalo linajihusisha na utoaji wa msaada kwa mtu mmojammoja.
“Wito wangu kwa wanawake ni kuwa kutafuta elimu na kuipata, vilevile kuheshimika inatakiwa juhudi, kuota ndoto kubwa na natumaini ipo siku kila kitu kitalipa kwa yeyote mwenye kuweka bidii na kudhamiria kweli kufanikiwa.”
NI BOSI WA MUME WAKE
Ursula ni mke wa Lloyd Bean, ambaye alikuwa mfanyakazi wa Xerox. Na kipindi akiwa mfanyakazi kwenye shirika hilo, mume huyo alikuwa chini kicheo kwa Ursula.
Wanaishi Manhattan, New York. Ursula na Bean wana mtoto mmoja wa kike anaitwa Melissa lakini mume wake, ana mtoto mwingine wa kiume Malcolm ambaye alimpata kabla hajafunga ndoa na Ursula.
Alizaliwa September 20, 1958, hivi sasa ana umri wa miaka 57. Hujishughulisha na siasa na chama chake ni Democrats.
Asili ya Ursula ni Panama ambako ndiko asili asili ya wazazi wake wote wawili. Mama yake alihamia Marekani na kuchukua uraia wa nchi hiyo na ndiyo ikawa sababu kwa Ursula kuwa Mmarekani.
MWANAMKE SOMA
Michelle ambaye ni mke wa Rais wa Marekani, Barack Obama, aliwahi kuwaambia watoto wa kike:  “Unapokuwa shule ni eneo la kujenga msingi wako wa maisha. Unaweza kuwa unamaanishwa kuwa na nafasi kubwa lakini macho ya karibu yakikupotosha utapoteza fursa kubwa ya baadaye.
“Mimi sikuruhusu mvulana achezee maisha yangu, nilipokuwa high school nilisoma kwelikweli na kila siku nilizingatia masomo yangu, leo hii najivunia kuwa mke wa Rais wa Marekani. Usiwe na haraka, soma!”
Michelle aliongeza: “Hakuna mvulana katika umri wenu ambaye ni mzuri (handsome) sana au ana mvuto sana kiasi cha kukufanya wewe usisome, hakuna.
“Kama ningeingia wasiwasi kuhusu nani alinipenda na yupi alifikiri kwamba mimi ni mzuri. Ningefikiria vijana wazuri (ma-handsome), leo hii nisingekuwa mke wa Rais wa Marekani.”
Michelle aliwaambia wanafunzi wasichana kuwa wavumilivu na kujipa msukumo katika miaka minne wanapokuwa ‘high school’ na kuachana na vitu vidogo ambavyo vinaweza kuwachanganya.
“Hutakiwi ukiwa na umri wa miaka 60 uwe unakumbuka na kujuta kwa miaka minne ambayo hukujituma inavyotakiwa. Utakuwa na fursa, na utakuwa na udhibiti wa maisha yako kufanya uchaguzi wa mambo yako mwenyewe. Na hutakuwa na ulazima wa kusikiliza wazazi kwa sababu utakuwa na kazi yako na bili zako utazilipa mwenyewe. Unataka uhuru. Uhuru utakuja baadaye, kwa sasa soma kwanza.
“Sasa unawekeza. Sasa unajenga uwekezaji wako. Sasa unatakiwa kuwa mvumilivu. Hii ni kwa sababu kama hutakuwa hivyo sasa, utakwenda kuishi maisha ya hovyo katika uhai wako wote uliosalia,” alisema Michelle.

Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment