ads 728x90 B

Hilary Devey Abakwa, azalishwa akiwa mtoto, sasa hakamatiki kwa utajiri






Luqman Maloto
PUMZI unayovuta ina maana kubwa mno. Kila unapoingiza oksijeni na kupokelewa na mapafu yako, hilo ni deni kwa Mungu. Jiulize unaitumiaje?
Tundu zako za pua zinapotoa nje hewa ya kabon (carbon dioxide), kinachomaanishwa ni kuwa uhai unao, kwa hiyo unalo jukumu la kufanya.
Kila nukta inayokwenda kwa Mungu, humaanishwa kukatishwa kwa uhai wa binadam kwa makundi. Ukiona umemaliza sekunde 60 ukiwa hai, tambua kuwa Muumba bado anao mpango mahsusi na wewe.
Hebu itikia mpango wa Mungu juu yako. Acha kuwazia ugumu wa maisha unaokukabili, anza kupiga hesabu za kufanikiwa.
Watu wengi huumiza kichwa kwa unyonge wao, wakifikiria shida na changamoto za maisha, badala ya kuupa ubongo nafasi ya kupumua kisha uutumie kuwaza njia za mafanikio.
Chukua hii; Matumizi mabaya ya muda ni kuusotesha ubongo wako kufikiria magumu ya maisha, katika kipindi ambacho unatakiwa kupiga hesabu makini za namna bora ya kubadili kibao cha maisha, kutoka dhiki za kila siku mpaka faraja na neema.
Ni kwamba kama unavyoishi hutambui kuwa umeachwa kwa sababu maalum, hutafanya chochote cha maana. Ni kwa sababu hujui hata sababu za wewe kuishi.
Ukiwa mnyonge maana yake hujiamini. Hutambui kuwa wewe ni mteule wa Mungu, kwa hivyo kama ambavyo anaendelea kukupa pumzi, ndivyo na ulinzi wake unavyoandamana na wewe. Kama Mungu ndiye mlinzi wako, sasa unyonge wa nini?
Tambua kuwa maisha ya binadamu yana mengi katikati yake. Zipo kumbukumbu nyingi za kuumiza, zipo pia za kufurahisha. Ni kosa kubwa kwa kesho yako, endapo utaruhusu kumbukumbu za maumivu ziteke hatma yako.
Umetendewa jambo baya, umeumia, sema “asante Mungu”, unachotakiwa kufanya ni kuelewa kuwa kwa vile bado upo hai basi unalo jukumu la kufanya. Maumivu yote weka pembeni.
Ni ukweli kuwa huwa vigumu kusahau unapotendwa mambo mabaya lakini hiyo isikutawale. Amini kuwa ni mapito kisha mwenyewe jisemee moyoni: “Nyakati zijazo zina neema kubwa!”
Wapo wanaume wenye hulka za kinyama, wao bila kubaka wala hawaoni fahari. Je, imekutokea hivyo, ni kweli inauma kupita kiasi, lakini unayo nafasi ya kumshikisha adabu mbakaji wako hata kama hukumfikisha kwenye mkono wa sheria.
Ni adabu gani? Tafuta fedha mama! Nakuhakikisha ukishafanikiwa, huyo mbakaji wako hatakuwa na amani, maana atahisi wakati wowote unaweza kumrudi kwa kitendo kibaya alichokufanyia.
Chukua hii; Watu waovu, huombea kila siku wale waliowatendea mambo mabaya wasifanikiwe katika maisha yao. Akili zao za dhambi huwatuma kuwaza kwamba watalipiziwa kisasi.
Unadhani una haja ya kulipa kisasi? La hasha! Utapoteza muda, endelea kutengeneza fedha na utaona jinsi ambavyo mbaya wako anavyosulubika.
Alikuwa na akili sana yule aliyeanzisha ombi kwa Mungu, kuwapa umri mrefu maadui zake ili washuhudie mafanikio yake.
Chukua hii; Huhitaji bunduki wala upanga kumsulubu adui yako, tafuta fedha mpaka uzikamate. Hatua zako za mafanikio ni sawa na silaha ya maangamizi kwa adui yako. Kadiri unavyojitanua kwa mafanikio, ndivyo anavyotaabika na maisha.
Ni kama Hilary Devey, alibakwa, akapewa mimba akiwa binti mdogo mwenye umri wa miaka 12.
Devey baada ya kufanyiwa kitendo hicho, hakuona kama maisha yamemuelemea, alichukulia kuwa ni ajali kama ambavyo huwakuta wengine, kwa hiyo alijikita kuitazama kesho yake.
Ona matunda ya kuyawazia mafanikio ya maisha, leo hii Devey ni mwanamke tajiri. Yupo kwenye namba za juu katika matajiri wanawake nchini Uingereza.
Akiwa na mtoto mgongoni huku na yeye akiwa mtoto, alikumbana na misukosuko mingi ya kimaisha, malezi bila fedha, kula ya shida, mahitaji ya mwanaye kwa ngama, lakini yote hayo ni historia.
Devey bila elimu, amethibitisha kuwa mafanikio katika maisha hayana tafsiri ya kukaa darasani peke yake, bali inawezekana kabisa kuitwa tajiri pasipo kuwa na shule kichwani, muhimu ni kujitambua na kujituma.
Kwa nini kujitambua? Ni kwamba kwa mtu anayetambua kuwa anao upungufu wa kielimu, atajua namna ya kuenenda ili kuziba mwanya ambayo unaweza kuonekana. Devey aliweza.
Nchini Uingereza ni nani ambaye hampi heshima yake Devey leo. Hata yeyote anayepata nafasi ya kumsoma, alivyohangaikia maisha mpaka kufika alipo akilimiliki mamilioni ya pauni (mabilioni ya shilingi), ni lazima atie adabu kwa mwanamke huyo shujaa.
Devey ni mwanamke wa shoka, amethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba mafanikio yanatafutwa na yanapatikana. Kwamba hayajaumbiwa wengine, bali yanamhusu kila mwenye kujituma.
ILIKUWAJE AKABAKWA?
Machi 10, mwaka huu, Devey atatimiza umri wa miaka 59, anasema kumbukumbu ya tukio la kubakwa ilimuumiza kupita kiasi na ilikaribia kumfanya akate tamaa ya maisha.
Anasema: “Moyoni mwangu kila siku nilijisemea mwenyewe kuwa lazima nitafanikiwa. Hiyo ndiyo sababu pekee ambayo ilinifanya nisikate tamaa. Niliamini kuwa nitakuwa mtu fulani mwenye hadhi.”
Kwa mara ya kwanza, Devey alifichua siri yake ya kubakwa na kupewa mimba mwaka 2013, alipofanya mahojiano na gazeti la The Sun la Uingereza.
Alieleza siri hiyo ikiwa ni baada ya kuificha kwa zaidi ya miaka 43, alisema: “Niliponzwa na dada mmoja jirani yetu ambaye alikuwa mkubwa kwangu, nakumbuka jina lake ni Sandra. Nilikuwa ndiyo nafika nyumbani, hata sare za shule nilikuwa sijabadilisha. Sandra aliniita, name kwa kumheshimu niliitikia wito.”
 “Nilikuwa na umri wa miaka 12. Tukio lenyewe lilitendeka jirani na pub ya wazazi wangu. Kipindi hicho wazazi wangu walikuwa wakimiliki pub hiyo kama biashara pekee ya kuendeshea familia.
“Sandra alinichukua mpaka kwenye nyumba hiyo jirani na pub ya wazazi wangu. Akanikutanisha na mwanaume. Ghafla nikashangaa Sandra anaondoka, yule mwanaume akanivamia. Alikuwa ananuka harufu mbaya.”
Devey anaendelea: “Nilikuwa msichana mdogo, yeye alikuwa mkubwa. Kwa nguvu sikuweza kushindana naye kabisa. Alinizidi kwa kila kitu. Mwisho alinibaka na ikawa mara yangu ya kwanza kuingiliwa na mwanaume.
“Baada ya kumaliza hakuniacha nirudi nyumbani, aliendelea tena na tena mpaka asubuhi. Nilipata maumivu makali sana. Na kwa tukio hilo ndiyo ikawa sababu ya kunasa ujauzito.”
Je, ujauzito huo uliharibu ndoto za maisha yake? Devey anapinga hilo, anasema: “Ndiyo maana nipo hapa. Hatua ambayo nimefikia haifanani na mtu aliyewahi kupoteza matumaini ya kutimia kwa ndoto zake.
“Tena kwa sasa naweza kukujibu kwa kujiamini kuwa ndoto zangu zimetimia. Pamoja na mengi magumu niliyokutana nayo lakini nilibaki kwenye mstari wangu. Hii ndiyo sababu leo najivunia kufanikiwa kwa ndoto zangu.”
Akikumbuka tukio la kubakwa, Devey anasema: “Sandra aliniwinda kwa muda mrefu. Nikimfikiria ni kama alikuwa na lengo baya na mimi tangu muda mrefu. Alianza kwa kujipendekeza kwangu, akijifanya anataka kuwa rafiki yangu. Alinisumbua sana kutafuta urafiki na mimi.
“Mwanaume aliyenibaka ni raia wa Italia na alinichania mpaka nguo zangu za shule.
“Nililia na kupiga kelele lakini hakuna msaada wowote ambao nilipata. Nilimuomba yule mwanaume aniruhusu niende nyumbani lakini hakunijibu chochote. Msisitizo wake ulikuwa kwenye kitendo alichokuwa anafanya. Ni mwanaume katili mno.”
Pamoja na kufanyiwa unyama huo, Devey hakufunua kinywa, anasema: “Yule mwanaume alinionya kuwa kama ningethubutu kusema chochote angenifanyia kitu kibaya sana.
“Kwa kumbukumbu ya unyama alionifanyia na kile kitisho alichonipa, niliamini kuwa usalama wangu ni kunyamaza kimya. Niliogopa kusema kitu wala kufanya chochote chenye kuashiria kutoa siri. Nilijua angejua na kunibaka tena, vilevile kunifanyia unyama mkubwa zaidi.
“Kikubwa zaidi niliogopa kuuawa, maana katika vitisho vyake alisema pia anaweza kuniua. Ndiyo maana tukio hili limebaki kuwa siri yangu. Nimekaa nalo mpaka leo nikiwa mtu mzima ndiyo nathubutu kutamka.”
Aliporudi nyumbani ilikuwaje? Devey: “Baba na mama walikasirika sana, waliamini kilichonilaza nje ya nyumba ni kupenda kwangu, kwamba nilikuwa na mvulana, kumbe haikuwa hivyo.
“Baba hakusema sana, alisema tu nilikuwa na mvulana usiku mzima. Alikasirika na hasira zake niliziona waziwazi. Mama alikwenda mbali zaidi, maana zilipita siku kadhaa akawa hanisemeshi kwa chochote. Hili pia liliniumiza sana.”
Devey anasema kuwa kitendo cha mama yake kutozungumza naye, kilikuwa adhabu kubwa kwake, ambayo ilimfanya awe anakaa peke yake lakini hakuwahi kulia wala kutokwa machozi.
“Nilijikuta nimepatwa na roho ngumu ajabu. Nilihimili presha yote. Sikuwahi hata kufikiria kuomba msamaha. Nilijua ulimwengu wangu umebadilika lakini sikujilaumu kwa sababu sikuwa na kosa. Niliumizwa lakini nilihofia maisha yangu kuwaambia wazazi wangu.”
UMASKINI WA WAZAZI WAKE ULISABABISHA ABAKWE
Hili huwezi kupingana nalo, kwamba uwezo wa mzazi ni ulinzi madhubuti kwa mtoto wake.
Ni vigumu mno kusikia mtoto wa tajiri amebakwa, labda huyo mwana wa tajiri awe ndiye ametengeneza mazingira ya ‘kujibakisha’.
Inawezekana vipi mtoto wa kiongozi mkubwa serikalini abakwe? Huyo mwenye jeuri ya kutenda ubakaji huyo ni nani? Hajipendi?
Na hivyo ndivyo ilikuwa sababu ya Devey kubakwa. Wazazi wake walikuwa hohehae, kwa hiyo Sandra na Muitaliano wake, waliamini wasingefanywa chochote.
Chukua hii; Unawajibika kuushinda nguvu umaskini wako kisha uukaribishe utajiri. Ukifanikiwa hilo, utakuwa umefanikiwa kujitengenezea ulinzi binafsi na wa familia yako. Hakuna atakayethubutu kuleta dharau wakati anajua una uwezo mkubwa wa kumshughulikia.
Devey alizaliwa na kukuta familia yake ni bora kabisa. Wazazi wake walikuwa na uwezo mzuri wa fedha na mali, maana baba yake alikuwa mfanyabiashara mkubwa.
Tangu akiwa mdogo, Devey alijionea utamu wa maisha yenye kutosheleza. Hata hivyo, alikutana na matokeo tofauti alipofikisha umri wa miaka sita, baada ya baba yake kufilisika.
“Baba alipofilisika, maisha yalihama kutoka kuwa na maisha ya kuheshimiwa hadi kuonekana watu tusiokuwa na thamani. Tulichekwa na majirani. Baba yangu alibadilika na kuwa mnyonge.
“Hakuna wakati mgumu katika maisha kama kuwa na mali kisha ziondoke. Baba alihangaika na baadaye ilibidi afungue pub angalau kufanikisha mahitaji ya familia.”
Anaongeza: “Sandra na mwanaume wa Kiitaliano, waliona nguvu ya baba yangu haipo tena, waliniona ni mtu wa familia maskini, ndiyo maana waliandaa na kufanikisha mtego wao wa kunibaka kwa imani kwamba sitaweza kufanya chochote.”
UTAJIRI BILA ELIMU
Baada ya kupata mimba Devey alijitahidi lakini ilishindikana, ilibidi akubali matokeo ya kuachana na shule.
Anasema: “Katika familia yetu ninao kaka wawili, wote wamefika mpaka chuo kikuu. Mimi pekee sijafika hatua nzuri kielimu. Lakini Mungu ni mkubwa kuwa mafanikio yangu yameweza kuziba kasoro ya kutofika chuo.”
Devey anaeleza kuwa baada ya kujifungua mtoto wake wa kiume ambaye ndiye wa pekee mpaka sasa, aliamua kujishughulisha na kazi mbalimbali kwa lengo la kujitafutia riziki pamoja na huduma kwa mtoto wake.
“Kazi yangu ya kwanza ilikuwa kumsaidia baba katika pub, nilifanya kwa muda. Baadaye nilipata kazi Jeshi la Anga la Uingereza kitengo cha wanawake, nilifanya kazi pale kama mhudumu.”
Tukipitia maisha ya Devey mpaka kuwa tajiri, hili liweke kwenye ubongo wako kuwa wakati mwingine unapokuwa unafanya kazi huku na huko, bila kujali taaluma, eneo ambalo utaliona jepesi kwako, pengine ni hapohapo pa kutilia mkazo.
Kwa kawaida upo mvutano wa asili kati ya utashi binafsi na kazi ya maisha yako. Kazi ya maisha yako utaiona nyepesi hata kama ina changamoto nyingi kiasi gani. Kazi ambayo haikumaanishwa yako, haiwezi kukuvutia kuifanya hata kama ni rahisi, japo ujitume kiasi gani.
Uthibitisho wa hilo ni kuwa baada ya Devey kuondoka kwenye utumishi wa Jeshi la Anga la Uingereza, alifanya kazi mbalimbali lakini akajikuta anapendelea kazi ya usambazaji wa vifurushi.
Na kwa taarifa yako, kazi hiyo ndiyo ilimpa mawazo ya utajiri mkubwa ambao anang’ara nao leo hii.
“Nilikuwa na umri wa miaka 20 nilipoanza kufanya kazi kwenye kampuni za upokeaji na usambazaji wa vifurushi. Nilifanya kazi kama karani wa mauzo. Nilijikuta navutiwa sana na kazi hiyo,” anasema Devey.
Wakati huo, mtoto wake Mevlit alikuwa anazidi kukua. Na alikuwa anamlea peke yake bila uwepo wa baba, yaani akisimama mama pekee (single mother).
Hii ilimfanya aachane na kazi za kuajiriwa kwa muda wote wa kazi, hivyo kuwa ofisa masoko huru, akijishughulisha na makampuni tofautitofauti kisha alipata malipo kulingana na jinsi alivyofanikisha upatikanaji wa kazi.
Sababu ya kuwa ofisa masoko huru na mshauri ni ni ili apate muda mzuri wa kuwa karibu na mtoto wake.
Mwaka 1996, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 39, Devey alisikia redioni maelezo ya mteja kuwa ilikuwa inachukua siku 12 kupata kifurushi chake kwa sababu mtoa huduma alitaka mpaka apate mizigo ya kutosha kujaza lori, ndipo isafirishwe.
“Ilizungumziwa miji ya Cardiff na Carlisle, nilijiuliza inakuwaje kufikisha siku 12 kati ya miji hiyo. Na hiyo ndiyo ilinipa wazo la kuanzisha kampuni yangu ya Pall-Ex ambayo sera yake ni kufikisha kifurushi mahali husika siku inayofuata. Yaani tukipokea leo, kesho tunafikisha kifurushi mahali kinapotakiwa kufika,” anasema Devey.
Msingi wa mawazo ya Devey ilikuwa kumaliza kero kwa watu, kwamba kifurushi kikitumwa kifike mahali panapokusudiwa haraka. Aliona suala la uchelewaji wa vifurushi ni tatizo, na kwake tatizo hilo aliliona ni fursa, hivyo alijikita kutaka kulitatua.
UKIJIAMINI WAZO LAKO NI ZAIDI YA BENKI
Haikuwa rahisi, ingawa mwanzoni alijiamini. Alizunguka kwenye mabenki na taasisi za mikopo kuomba kukopeshwa mtaji bila mafanikio.
Siku zilikuwa zinakwenda, na alijiamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee. Nyakati hizo alihitaji pauni 125,000, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 400.
Baada ya kuona mambo magumu, aliamua kuuza nyumba yake, aliyorithi kutoka kwa wazazi wake, gari lake pia alilipiga bei, ndipo alipata mtaji wa kuanzisha kampuni yake hiyo ya vifurushi.
Tambua kuwa uamuzi huo wa Devey ulimfanya akose mahali pa kuishi, bila usafiri, fedha zote alizielekeza kwenye uanzilishi wa kampuni.
Maisha yalikuwa magumu zaidi. Alikosa mpaka pesa ya kula, aliishi kama mwanamke wa mtaani.
Hata kampuni ilipoanza kazi, alijikuta akiwa mfanyakazi peke yake. Yeye mwenyewe atafute wateja, kisha apokee oda na kusimamia kusafirisha vifurushi kwa haraka na kwa namna ilivyotakiwa.
“Ni kampuni iliyoanza kama ya mwanamke pekee lakini leo hii ina wafanyakazi wengi,” anasema Devey, anaongeza: “Tumetoka mbali. Baada ya muda niliweza kuajiri wafanyakazi 35 na leo hii tunatengeneza faida ya pauni milioni 75 kila mwaka.”
Kiasi hicho cha fedha ambacho Devey anakisema ni karibu sawa na shilingi bilioni 250 kwa mwaka. Je, mpaka hapo maisha yanataka nini?
Na kwa sasa, kampuni hiyo ya Devey, Pall-Ex, inafanya kazi zake bara zima la Ulaya, hivyo kumfanya mwanamke huyo kuwa mwenye nguvu mno.
Katika kitabu chake kinachoitwa How I Made My First Million, Devey anaandika kuwa mafanikio yake ni matokeo ya kutokata tamaa na kutofikiria ya nyuma, zaidi kujikita kwenye yajayo ambayo ndiyo yanakuwa na umuhimu mkubwa katika maisha ya kila mtu.
Hivi sasa, Devey anamiliki utajiri unaokadiriwa kuzidi pauni milioni 100 ambazo ni takriban shilingi bilioni 350.
UTAJIRI TU?
Hapana, Devey alinenepa na kupoteza muonekano wake. Hali hiyo ilimnyima raha, maana alitamani kuwa na tumbo bapa kama wanawake wengine.
Hiyo ilimlazimisha mwaka 2009 kufanyiwa oparesheni ya kutengeneza tumbo ambayo ilimsababishia madhara ya kupooza sehemu ya mwili wake.
Alilala kitandani, maana hakuweza kunyanyuka na theluthi moja ya ubongo wake iliharibika. Hiyo ilimchukua muda mpaka kupona.
Vilevile mwanaye, Mevlit aligeuka mtumia madawa ya kulevya wa kutupa. Kila kilichokuwa ndani alibeba na kuuza ili apate fedha za kununua heroin. Alipambana kwa miaka saba kumsaidia mwanaye ambaye alipona kabisa mwaka 2011.
HITIMISHO
Jiongeze mwenyewe sasa, kwani Devey amefanikiwa kibiashara akiwa mwanamke tu ambaye hata shule alikimbia kutokana na hali duni ya kwao, hasa baada ya baba yake kufilisika.
Ukiachana na biashara, Devey amekuwa mtangazaji mwenye mafanikio makubwa, akitikisa televisheni ya BBC kupitia program ya Dragons’ Den. Mpaka sasa anaendelea kuwa staa wa televisheni mwenye mafanikio.
Amekuwa akiandaa vipindi vyenye kuhamasisha watu kuajiamini kuwa wanaweza kufanikiwa, kwa kuwapa historia za matajiri mbalimbali, changamoto walizopitia kabla ya kufanikiwa. Kazi hiyo pia inamuongezea fedha kila siku.
Mwenyewe umejionea ushujaa wa Devey. Ni kwa nini asiitwe Mama Mhujaa? Nawe amka upambane.
  
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment