ads 728x90 B

Zanzibar; Kuna kosa kubwa linakwenda kutokea





Luqman Maloto
MWAKA 1992, ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa Angola, hiyo ikiwa ni baada ya miaka 17 ya vita vya kiraia (Civil War).
Uchaguzi ulikutanisha vyama 11 lakini mchuano ulikuwa mkali kati ya Chama Tawala, MPLA na Unita.
Rais Jose Eduardo dos Santos alikuwa anatetea kiti chake akiwa na MPLA dhidi ya hayati Jonas Savimbi wa Unita.
Dos Santos ni Rais wa Angola mpaka sasa, alianza kuongoza taifa hilo mwaka 1979 baada ya kifo cha shujaa wa wakati wote wa nchi hiyo, marehemu Agostinho Neto, aliyetawala kati ya mwaka 1975 – 1979 alipofikwa na mauti.
Katika uchaguzi huo, pamoja na uwepo wa vyama 11 shiriki kwenye uchaguzi, mfumo mzima ulivibeba vyama viwili (two-party system), yaani MPLA na Unita.
Uchaguzi ulipofanyika Santos aliongoza kwa asilimia 49 na Savimbi alipata asilimia 40. Uchaguzi ukatakiwa kurudiwa. Maana katiba ilitaka mshindi atangazwe baada ya kuzidi asilimia 50.
Uchaguzi wa mara ya pili (runoff), uliitishwa kati ya Savimbi na Santos ili mmoja aweze kutangazwa mshindi kwa kupata kura zaidi ya asilimi 50.
Mvutano ukatokea, Savimbi alitaka mabadiliko kwenye tume kwa sababu alizodai kuwa Santos aliiba kura. Santos akasisitiza uchaguzi urudiwe hivyohivyo.
Ikawa vuta nikuvute, mwisho Santos akaamua kujitangaza kuwa rais halali na akatawala bila ya kuwepo kwa uhalali wa kidemokrasia (democratic legitimacy).
Uamuzi wa Santos ulikuwa wa kibabe na usiojali damu zisizo na hatia. Pamoja na ukorofi wa Savimbi, ilikuwa ni jambo jema kusikiliza madai yake na kuyafanyia kazi, kwamba tume irekebishwe ili uchaguzi uwe huru na haki.
Ikumbukwe kuwa nchi hiyo ilikuwa imefanya uchaguzi baada ya kusaini mkataba wa kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe (Bicesse Accords), ambao Santos na Savimbi walisaini Mei 31, 1991, chini msuluhishi ambaye ni Serikali ya Ureno.
Mkataba huo ulisainiwa baada ya vifo vya maelfu ya raia na wengine wengi kujeruhiwa. Zipo ripoti zinaitaja Angola kuwa taifa lenye watu wengi wenye ulemavu wa viungo kutokana na athari za vita.
Bila kujali maelfu ya watu kuendelea kupoteza maisha, wala kuhurumia maelfu wanaoendelea kupoteza viungo vyao kutokana na kujeruhiwa na mabomu, Santos aliziba masikio, akaendeleza utawala wake.
Angola ikarejea tena kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Waangola wengi wakazidi kupoteza maisha na kupata ulemavu. Vita iliendelea mpaka mwaka 2002 Savimbi alipouawa.
Unaweza kujiuliza; Ni kwa nini Santos na Savimbi hawakufikia mwafaka mwaka 1992 na kusababisha miaka mingine 10 ya vita? Ubishi wao ulileta matokeo ya vita vya kiraia Angola kufikisha umri wa miaka 27.
Savimbi aliuawa, sawa lakini kifo chake hakitoshi kufuta machozi ya damu iliyomwagika Angola. Wakati huohuo Santos yupo madarakani mpaka leo, kazi yake kuchezea katiba, anaula tu! Kamfanya mwanaye Isabel Dos Santos kuwa mwanamke tajiri zaidi Afrika.
Juzijuzi hapa, Santos na Isabel walitumia zaidi ya shilingi bilioni 4 kumwalika rapa wa Marekani, Nicki Minaj ili atumbuize kwenye sherehe binafsi ya kiongozi huyo. Fedha za Waangola zinaendelea kutumiwa vibaya. Santos hajawahi kulipia gharama za maisha ya Waangola na ulemavu wao, kuanzia mwaka 1992 alipong’ang’ania uongozi bila ridhaa ya kidemokrasia.
KAMA SEIF KAMA SHEIN
Ukiona wanasiasa hawataki kukubaliana maana yake hawajali athari ambazo zinaweza kutokea kwa kutokukubaliana kwao.
Na tafsiri ya kutokukubaliana huko ni kuingia kwenye chumba cha majadiliano kila mmoja akiwa na lake kuwa lazima litimie.
Katika muongozo wa kitaaluma, majadiliano (negotiations au bargaining) ndiyo huzaa maridhiano (reconciliation).
Zipo dhana mbili za majadiliano; Ipo ya mmoja apate mwingine akose (distributive negotiation), kwamba mnaingia kwenye chumba cha majaliano kuona kwa kutambua kuwa ni lazima mmoja akose mwingine apate. Katika dhana hii ni vigumu kupata maridhiano.
Dhana ya pili ni ile ya kuridhishana ili kila mmoja apate (integrative negotiation). Kwamba kunakuwa na mvutano wa maslahi kwa kila upande (win-win situation), hivyo maridhiano yanajengwa kwa mgawanyo sawa au unaokaribiana.
Suala la Zanzibar ilikuwa ngumu kujengwa na msingi wa majadiliano ya kimlinganyo (win-win negotiation) kwa sababu Dk. Ali Mohamed Shein anataka uchaguzi urudiwe, wakati Seif Sharif Hamad anashinikiza atangazwe kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Sasa hapo nani anapate na yupi akose ndiyo kwenye tatizo. Niliwahi kuandika katika makala yenye kichwa “Shein na Seif atakayekubali kukosa ndiye shujaa” kuwa afadhali ingekuwa kila mmoja nang’ang’ania alishinda, hapo suluhu kuu ilikuwa ni kurudia uchaguzi kuondoa ubishi.
Tatizo Seif akikubali uchaguzi urudiwe atajiona ameshindwa au Shein akikubali Seif atangazwe atakuwa amekubali kukosa. Ndiyo maana nilisema kuna utata na shujaa wa maisha na amani ya Wazanzibar ni yule atakayeelekea kwenye hitaji la mwenzake. Kuvutana hakuna jawabu.
MAMBO YA KUMULIKA
Suala la Zanzibar halitaki matamanio ya “lazima niwe rais”, vilevile kuweka misimamo ya vyama si jambo jema. Ni muda mwafaka kutambua kuwa hali ya sasa inaifedhehesha Tanzania yetu.
CCM na Cuf wasijitie upofu wala kujisahaulisha. Machafuko ya Januari 26 na 27, 2001 yalikuwa mabaya mno. Kama nchi hatupaswi kurejea makosa. Watu wafe, wengine wawe walemavu kwa sababu za ubishi wa wanasiasa.
Kuna idadi kubwa ya Wazanzibar waligeuka wakimbizi kwa sababu ya machafuko ya Januari 2001. Asiye na aibu wala huruma, anaweza kuona sawa kuendeleza chokochoko zinazoweza kuleta machafuko kwa mara nyingine.
Hakuna matakwa na tamaa za wanasiasa, zenye kulingana na thamani ya damu hata ya mtu mmoja. Seif na Shein waelewe kuwa Zanzibar ni muhimu kuliko wao.
Watambue kuwa Cuf na CCM siyo vyama vya siasa kama amani na mfumo wa kisiasa haupo. Palipo na machafuko hakuna siasa, kuna vikundi vya mapigano na uasi. Vyama vinafuata baada ya amani, usalama na utulivu.
Hali ya Zanzibar ilipofikia, muhimu kwa sasa siyo nani ni rais, bali maridhiano yenye tija, yatakayoviacha visiwa hivyo vikiwa na amani na upendo.
Muhimu kuonya hili; Kama inavyofahamika kuwa Zanzibar hakuna siasa bali kuna chuki. Uamuzi ambao hautakuwa na maridhiano, utaongeza uhasama na uadui.
Pemba kwa sehemu kubwa hawaitaki CCM. Na kwa miaka 20 sasa tangu Uchaguzi Mkuu 1995, hali imekuwa hivyo.
 Madai ya Zec kama yalivyosemwa na Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, dosari nyingi zilitokea Pemba. Ipo shaka kubwa hapo!
Kama bila shaka yoyote kuwa Wazanzibar kwa kura nyingi wamemchagua Seif, CCM wakubali tu hata kama wanaona chaguo ni baya. Waachwe Wazanzibar wenyewe watajutia uchaguzi wao kama wamekosea. Ni kosa kuwalazimisha. Ni uamuazi wao!
Uchaguzi unapofanyika mshindi hupatikana kwa njia ya hesabu ya kura. Uamuzi umeshafanywa na wananchi kwenye masanduku ya kupigia kura.
Kwa kuzingatia ukweli huo kuwa uamuzi ni ule ambao ulifanyika kwenye masanduku ya kura, ndiyo tunakuwa na majibu kuwa vikao vinavyoendelea kwa sasa vinafanyika baada ya makosa.
Kwamba Zec kama wakosaji wakuu, Cuf na CCM wanafuata kwa upande wa pili katika kila kosa.
Kama kweli uchaguzi ulikuwa na dosari, maana yake Cuf wanahusika kwa kushirikiana na maofisa wa Zec.
Ikiwa hakukuwa na dosari, maana yake CCM watakuwa walikataa kushindwa, hivyo kumpa shinikizo Jecha afute matokeo na kuitisha marudio ya uchaguzi.
Jinsi hali ilivyo sasa na misimamo ya vyama, inataka mtu mkweli na mwenye hofu hasa ya Mungu, kusimama na kukiri makosa ya upande wake ili amani ichukue mkondo wake.
Mwandishi na Mwanahistoria mashuhuri nchini Marekani, Timothy B. Tyson, alisema: “If there is to be reconciliation, first there must be truth.”
Kiswahili: Kama yatafanyika maridhiano, ukweli lazima utangulie.
Mkazo hapo ni kuwa kama pande mbili zinazosigana kuhusu mgogoro wa Zanzibar hazitatanguliza ukweli, hayo maridhiano hayatakuwa na maana yoyote.
Hapohapo vema kuwakumbusha kwamba hali imefika kwa kiwango cha sasa kwa sababu ya kukosekana kwa ukweli. Wanasiasa wanajiwekea ulazima kinyume na matakwa ya wananchi.
Isingekuwa “lazima mimi” au “lazima sisi”, Zanzibar isingefika ilipo leo. Makubaliano ya kweli yatapatikana kama wataweka utaifa mbele, siyo vyama.
Waziri Mkuu wa zamani wa Australia, John Malcolm Fraser, aliwahi kusema kuwa maridhiano hayapatikani pasipo kuwepo kwa mabadiliko ya kimsingi ndani ya pande zenye kusuguana.
Fraser aliyefariki dunia Machi 20, mwaka huu, alisema: “Reconciliation requires changes of heart and spirit, as well as social and economic change. It requires symbolic as well as practical action.”
Kiswahili: Maridhiano yanahitaji mabadiliko ya moyo na roho , vilevile mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Yanahitaji ishara vilevile utekelezaji wa kivitendo.”
Mazungumzo kuhusu maridhiano yanapasa kuhusisha pande mbili ambazo wahusika wake wanakuwa na nyoyo rahisi kwa mabadiliko (flexibility).
Maridhiano ya Zanzibar ni ndoto kama wahusika wa mazungumzo wanakuwa na nyoyo ngumu zisizo na hali ya utayari kwa ajili ya mabadiliko (stiffness).
Mazungumzo yatakuwa mepesi na maridhiano itakuwa rahisi kupatikana kama Seif na Shein pamoja na pande zao (vyama vyao), wataweka maslahi ya Zanzibar na Tanzania mbele. Wao kama walivyo binadamu wengine katika zama hizi, wataondoka, Zanzibar itaendelea kuwepo.
Maridhiano hayatachukua njia ndefu kufikiwa kama Shein na Seif pamoja na vyama vyao, wataanza kwa kujiuliza nini Wazanzibar wanataka.
Matakwa ya Wazanzibar yatazamwe kuanzia katika kuchagua, uamuzi wao ulikuwaje? Na je, wanataka uchaguzi urudiwe au matokeo ya mchakato wa Oktoba 25 yatangazwe? Ni busara na uungwana wa hali ya juu kuheshimu hisia na mahitaji ya Wazanzibar.
Mkondo wa maridhiano utakuwa wenye thawabu nyingi kutoka kwa Mungu kama mazungumzo ya mwafaka yataweka mbele hatma ya Wazanzibar kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Kinyume chake ni dhambi kubwa.
Kama Seif alishinda, asifanywe kuwa mfalme wa huzuni (king of sorrow) katika kila uchaguzi, mnyonge anyongwe lakini haki yake apewe. Na Shein kama ameshindwa, ni uungwana kukubali matokeo, asijigeuze mfalme wa uonevu (king of intimidation).
Seif pia awe mkweli, kama uchaguzi ulitawaliwa na dosari nyingi, hakuna sababu ya kung’ang’ania ushindi wenye kasoro. Labda kama anapenda urais hata bila uhalali (legitimacy).
Ni kuhusu ukweli na haki, Shein na Seif kila mmoja anayo nafasi nzuri ya kujenga heshima yake kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Atajwe kuwa shujaa hasa wa siasa za Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Uungwana na uvumilivu wa Seif nautambua. Ni mwanasiasa wa mfano. Shein amekuwa na rekodi ya upole na ustaarabu bila makuu. Kila mmoja atambue sifa yake njema inayombeba. Asikubali kuipoteza sasa, kwani ni sawa saumu kuifungulia alasiri inayoishia.
KOSA KUBWA AMBALO LINATAKA KUFANYIKA
Majadiliano ni wazi yamekufa, na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alianza kwa kumweleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Zanzibar kuna amani na wananchi wanasubiri tarehe ya uchaguzi.
Kisha Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha alitangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Marudio Zanzibar ni Machi 20, mwaka huu.
Kauli hizo ni kosa kubwa la kiufundi. Kinachotaka kufanywa ni ubabe ambao hautakuwa na matokeo mazuri siku za usoni.
Unaweza kulazimisha kama ambavyo Balozi Iddi na Jecha walisema katika mazingira ya mfumo wa ukiritimba wa chama kimoja (one-party dominant system), Zanzibar kwa sasa ni mlinganyo wa vyama viwili (two-party system) kati ya CCM na Cuf.
Hata kama machafuko yatadhibitiwa kwa nguvu kubwa ya dola, lakini uchaguzi utasusiwa kwa asilimia kubwa kama tu Seif na Cuf watashikilia msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi.
Bila shaka yoyote uchaguzi utafanyika (CCM wakiamua), na kwa vile Seif atasusa, ni uhakika kuwa Shein atashinda kiurahisi. Itaitwa ushindi wa kishindo lakini haitakuwa awamu nzuri ya uongozi kwa maana Wazanzibar wengi watasusa.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alisema juzi kuwa tume haipaswi kuingiliwa, kwamba hatma ya Zanzibar iachwe kwa Zec.
Lubuva anapaswa kutambua kuwa suala la Zanzibar linahitaji maridhiano kuliko uamuzi.
KOSA LA SEIF
Msingi wa majadiliano, kitaaluma na kimkakati, huundwa na pande tatu kisha kushika mambo mawili.
Mosi; Usuluhishi (mediation), hapo huwa ni mazungumzo ya kawaida na kupeana maneno matamu na kuridhishana ili kila upande utoke umeridhika.
Pili; Uamuzi (arbitration), huambatanisha vielelezo, ushahidi, haki na sheria kisha uamuzi hufanyika kutokana na ushahidi, vilevile tafsiri za kisheria.
Mazungumzo ya mgogoro Zanzibar yaliyokwama, sababu yake ni kukosekana kwa upande wa tatu, vilevile usawa haukuwepo.
Seif alikuwa mjumbe pekee katikati ya msitu wa wajumbe wa CCM. Usawa upo wapi?
Seif anachuana na Shein lakini Shein ndiye akawa mwenyekiti wa majadiliano. Nilitegemea kukwama kwa mazungumzo mapema mno.
Kama dhamira ya kweli ilikuwepo, ilitakiwa Seif awe na timu yake, vilevile Shein na wenzake kisha uwepo upande wa tatu ambao ungekuwa unasikiliza na kushauri. Hilo halikufanyika. Seif alikubali kushiriki mazungumzo ya aina hiyo.
NINI KIFANYIKE?
Kama kweli Seif na Shein wanaipenda Zanzibar, basi warudi upya kwenye majadiliano ambayo yatajengwa kwa usawa na yashirikishe pande tatu. Yaani kuwepo na upande mmoja ambao siyo sehemu ya mgogoro na hauna maslahi yoyote kwenye mgogoro.
Vilevile Zec, kama wahusika wa kuharibu uchaguzi nao wahusike. Mazungumzo yafanyike kwa mjadala huru bila kuweka mbele hisia ili kupata suluhu.
Wafahamu kuwa majadiliano siyo mchezo kuambulia sifuri (zero-sum game), lazima maslahi ya kila upande yavutwe katikati kisha maridhiano yatokee.
Kikubwa zaidi wote wawe wa ukweli. Na lazima tuombe ukweli ushinde matakwa. Katika sintofahamu ya Zanzibar, ukweli hasa ni upi? Je, Seif alishinda au uchaguzi ulivurugwa? Kisha ukweli ushinde matakwa na kuleta maridhiano.
Mungu Inusuru Zanzibar.
Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment