Luqman
Maloto
KUHARIBU ni
rahisi kuliko kuunda, kutambua hili haihitaji kurejea nukuu ya mwandishi mkubwa
wa vitabu raia wa Czech, Ivan Klima. Ila unachopaswa kuzingatia ni kuwa
kuharibu ni kuunda, kuunda ni kuharibu (To create is to destroy, to destroy is
to create).
Mantiki;
Huwezi kuunda kitu pasipo kuharibu kingine. Tofali haliwi mpaka mchanga, saruji
na maji viharibiwe. Na unapoamua kuharibu, vilevile unaunda kingine, ulikuwa na
nyumba imevunjwa, kimebaki kiwanja. Hiyo ni kanuni!
Unapomshughulikia
mtu kumchafua, huishii kumharibu. Badala yake unajikuta unampa wasifu mwingine.
Alionekana mtu mzuri, wewe unavumisha kuwa ni mwizi, ile heshima aliyokuwa nayo
inaondoka, sifa yake mpya ni mwizi.
Edward
Ngoyai Lowassa ana mengi ya kuumiza. Ndoto za Ikulu hazipo, zimepotea, sizioni
zikiwa hai (sizungumzii ubishi wa sasa). Msisitizo wangu upo palepale,
inahitaji majaliwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa uhai na afya, ipo siku inawezekana
Muumba akitaka.
Maisha bila
unafiki yanawezekana, yapo mambo inabidi kuyasemea waziwazi. Lazima kumkumbusha
Lowassa watu ambao wamesababisha afike alipo. Anawajua ila haonekani kama vile
anawakumbuka.
Ni dhambi
kuilaumu Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ilimuonea kumkata.
Ni utovu wa fikra sahihi, kumtazama Rais Jakaya Kikwete kwa macho mabaya kwamba
ndiye aliyempa paja (kumuwekea kizingiti) Lowassa asiingie Ikulu.
Vema kurejea
kule ambako Lowassa alichafuka baada ya kuchafuliwa. Ambako kulisababisha
apoteze sifa za kuongoza (legitimacy). Kamati Kuu ya CCM ilitenda kazi yake kwa
hofu kubwa. Ni wazi Lowassa alihitajika lakini ilihofia heshima ya chama na
mashambulizi ya wapinzani baada ya kupitishwa.
CCM
kilihofia kufanya kampeni zake kwa mtindo wa kujibu hoja na kumtetea mgombea.
Maana zipo kashfa nyingi kumhusu. Ni uzandiki kukwepa kusema kuwa Lowassa
amekuwa alama ya ufisadi nchini kama vyombo vya habari vilivyoripoti na
wapinzani kupaza sauti.
Tukumbuke;
Lowassa akiwa kwenye kiwango chake bora kabisa, akitetemekewa nchi nzima, akionekana
mtendaji bora, waziri mkuu mithili ya hayati Edward Moringe Sokoine, mtu wa
kufanya uamuzi mgumu kwa wakati, alidhalilishwa na kudhalilika mno!
Akaporomoka
kutoka mtu wa kutetemekewa na watendaji serikalini, mpaka wa kulia-lia: “Nimefadhaika
sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana.” Hakufika hapo mwenyewe, kuna watu
walimfikisha.
Kama ilivyo
somo la mwendo wa kitu (Classical mechanics), Lowassa alikuwa anasubiri muda tu
kuingia Ikulu, Magogoni. Hakuna mwingine angeweza kushindana naye katika mbio
za kumrithi Rais Kikwete.
Hakuna wa
kupinga; Lowassa alikuwa katika mwendo kasi mnyoofu (linear momentum) kwenda
Ikulu. Kwa maana uzani wake (mass) kiuongozi na kisiasa, ulishabihiana barabara
na kasi (velocity au speed) aliyokuwa nayo.
Wanafizikia
wanajua ili kukizuia kitu kilichoshika mwendo wake mzuri ni lazima kigongane na
kingine. Mwandishi Saed Kubenea anahusika moja kwa moja kuzipeleka makumbusho,
ndoto za Lowassa kwenda Ikulu.
Hakuna namna
ya kumzungumzia Kubenea na safari ya Lowassa kwenda Ikulu iliyokwama pasipo
kutaja neno “unafiki”. Ni sikitiko langu kuwa wananchi wa Jimbo la Ubungo
wamemchagua mnafiki awe mbunge wao kwa miaka mitano. Ndivyo walivyoamua!
Rejea ripoti
ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba kati ya Kampuni ya Kufua Umeme
(Richmond) na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya serikali na Shirika la
Ugavi wa Umeme (Tanesco).
Kati ya
ushahidi uliotumiwa na kamati hiyo ya bunge, iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe,
lilitajwa Gazeti la Mwanahalisi ambalo bosi wake ni Kubenea.
Na wakati
anajitetea, Lowassa aliliita Mwanahalisi ni gazeti la udaku, ingawa hakutaja
hivyo moja kwa moja. Mjumbe wa Kamati ya Mwakyembe, Injinia Stella Manyanya,
alisema hawakuchukua ushahidi katika magazeti ya udaku, isipokuwa walilitumia
Mwanahalisi.
Unafiki wa
Kubenea; Rejea matoleo ya nyuma jinsi Mwanahalisi walivyomshughulikia Lowassa
kila toleo na kila makala. Kisha kumbuka jinsi Mwanahalisi walivyogeuka
watetezi wa Lowassa kila toleo na kila makala baada ya kuhamia Chadema, kisha
kuwa mgombea urais kupitia mwavuli wa Ukawa.
Katika hili
la unafiki wa Kubenea, kuna mambo mawili lazima kuyaweka wazi. Mosi; Kama
habari na makala alizokuwa anaandika kuhusu Lowassa zilikuwa ni uzushi na
alimsingizia, huo ni unafiki wa kiwango cha juu.
Pili; Ikiwa
alichokuwa anakifanya kilikuwa sahihi, kwamba Lowassa alifanya uchafu mwingi,
kama alivyoandika na kuchapishwa na Mwanahalisi, maana yake aligeuka na
kumsifia baada ya kuhamia upande wenye maslahi naye. Hakika huo ni usaliti wa
miiko, maadili na taaluma ya uandishi wa
habari kwa jumla.
Turejee
kwenye mosi; Kama alimsingizia, tuusimamishe ukweli kuwa Kubenea hana ubavu wa
kuwa na uhasama na Lowassa. Maana yake alitumiwa na maadui wa Lowassa.
Mwandishi anayetumika kuchafua wengine ni mnafiki, ni msaliti wa taaluma, ni
kanjanja!
Twende
kwenye pili; Tunaposimamia kipengele hicho, maana yake ni mtu maslahi. Kwa
namna alivyomgeuza Lowassa kutoka ubaya wa Shetani mpaka kumpamba na kumpa uzuri
wa Malaika, maana yake anaweza kuandika chochote kusherehesha kilicho na maslahi
yake binafsi.
Tukumbuke;
Wakati magazeti mengine yaking’ata na kupuliza kuhusu Lowassa, Mwanahalisi
lilijipambanua kuwa gazeti bora la uchunguzi kwa kumchunguza Lowassa na kuanika
kile ambacho walikitambulisha kwa wasomaji kuwa ni “habari za ndani” au “habari
za kiuchunguzi”.
Kubenea na
Mwanahalisi yake waligeuka marafiki wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, enzi hizo Nape akiutaka uenyekiti wa UVCCM.
Nape
alimshambulia Lowassa kwa msaada wa Mwanahalisi. Iliibuliwa mpaka kashfa eti,
Lowassa aliingia mkataba haramu, wa kifisadi wa jengo la UVCCM, Upanga, Dar es
Salaam. Ikaelezwa kuwa mkataba wenyewe ulisainiwa usiku.
Mwanahalisi
ndilo pekee liliandika habari hiyo. Kipindi hicho kukawa na uswahiba mkubwa tu
kati ya Kubenea, Mwakyembe na Nape. Zikawa zinapigwa habari za kumtandika
Lowassa bandika-bandua.
Mwanahalisi
ndilo lililoandika bila woga kuwa Lowassa ni fisadi. Likamshambulia Rais
Kikwete kwa kumlinda. Ni gazeti hilo lililowaonesha Watanzania kuwa hapa nchini
hakuna fisadi kama Lowassa.
Baada ya
Mwakyembe kusoma Ripoti ya Richmond, kisha Lowassa akajiuzulu, wakati wa
majumuisho ya hoja (windup) baada ya michango mbalimbali ya wabunge, Mwakyembe
alisema: “Lowassa aliwajibika kutokana na makosa ya watu wa chini yake.”
Nikiri kuwa
Mwakyembe alikosea, maana sehemu ya kwanza alieleza mambo mengi kuonesha jinsi
Lowassa alivyokosa maadili ya kiungozi mpaka kutoa maelekezo kwa ‘vimemo’ kuwa
Richmond ipewe zabuni ya kufua umeme wa dharura megawati 100.
Baada ya
hapo, Mwakyembe alikaa kimya. Na zipo taarifa kuwa ukimya wake haukuwa na maana
ya kujiweka kando, badala yake alifanya kazi ya kumlisha ‘nondo’ Kubenea ambaye
aliendelea kumfanya vibaya Lowassa kupitia Mwanahalisi.
Nyakati hizo
ndipo Mwanahalisi lilikuwa kwenye ubora wake. Walimgeuza Lowassa kupitia vichwa
vya habari kadiri walivyotaka. Walimpaka masizi, shombo na kila aina ya uchafu
mpaka kumsababishia anuke na kuogopwa!
Kubenea
kupitia Mwanahalisi lake akaandika kuhusu mpango wa Lowassa, kuwekeza shilingi
bilioni 8, kwa ajili ya kujisafisha na kashfa mbalimbali zilizomuandama ili
kujitengenezea njia ya Ikulu. Kubenea, Kubenea, Kubenea!
Hebu cheka
kidogo; Mwaka 2015, Kubenea akageuka adui wa Nape na Mwakyembe. Alikwenda mpaka
Kyela kufanya kampeni za kumwangusha Mwakyembe. Hawakuishia hapo, walimtandika
kisawasawa Nape. Mara Mwanahalisi, mara Mawio.
Mwandishi
maarufu wa vitabu, mlokole Israel Ayivor, aliwahi kuzungumza: “Save your skin
from the corrosive acids from the mouths of toxic people. Someone who just
helped you to speak evil about another person can later help another person to
speak evil about you.”
Kiswahili
chake: “Linda ngozi yako dhidi ya tindikali hatari kutoka kwenye vinywa vya
watu sumu. Yule aliyekusaidia kuzungumza mambo mabaya kuhusu mwenzako, ndiye atakayemsaidia
mtu mwingine kuzungumza uovu juu yako.”
Hapo ni
rahisi mno kuelewana, kwani Nape na Mwakyembe walimtumia Kubenea kuzungumza
uovu dhidi ya Lowassa, ila baadaye waligeukwa. Wakasemwa vibaya sana, maana
mwenzao alishageuka na kuwa upande wa Lowassa.
Wakati
nikiendelea kusherehesha mada hii, inatosha kupiga mstari kuwa ama kwa kutumika
au kuipigania nchi yake, Kubenea amehusika kuziharibu ndoto za Lowassa.
Maandishi yake makali, yaliingia kwa watu ambao walimuona hafai.
Kubenea
alimfanya Lowassa aimbwe ni fisadi. Lowassa akawa na sifa mbaya kwenye jamii.
CCM nao walitaka mpaka kumvua uanachama (kujivua gamba), wakasita na kuendelea
naye. Ikaja kwenye urais, wakaogopa kumsimamisha agombee.
Binafsi
naamini kuwa kama baada ya Richmond, ukimya ungefuata, Lowassa asingeandamwa na
kashfa za ufisadi, leo hii ndiye angekuwa anasubiri kuapishwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maana CCM ingempitisha kugombea na angeshinda
kirahisi kutokana na nguvu kubwa binafsi aliyonayo pamoja na ya chama.
Lowassa siye
mjinga, naamini anapotuliza kichwa kukumbuka mahali ambako safari yake
iliharibika, moja kwa moja Kubenea lazima atokeze haraka na gazeti lake,
Mwanahalisi.
Ni kituko
wengine kupiga kelele, kumlalamikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Jaji Damian Lubuva, kumshambulia Rais Kikwete, au kumtazama kwa kijicho, Rais
Mteule, Dk John Magufuli, wakati kwa takriban miaka 10 mfululizo, Kubenea
alipandikiza mbegu ya kuharibu ndoto za Lowassa kwenda Ikulu.
Rais wa 16
wa Marekani, Abraham Lincoln ‘The Great Emancipator’, alikuwa na maadui wengi
ambao waliamini kwa umaskini wake, kamwe asingeweza kuwa Rais wa Marekani.
Walimwekea vikwazo vingi kwa kumdharau tu kwamba hawezi. Na kweli alishindwa
mara nyingi kabla ya kuzifikia ndoto zake.
Baada ya
kuwa rais, wakati akitarajiwa angepambana vilivyo na maadui zake waliomdidimiza
huko nyuma, Lincoln alihoji: “Do I not destroy my enemies when I make them my
friends?” Kiswahili: Je, siwaangamiza maadui zangu pale nitakapowageuza kuwa
marafiki zangu?
Lowassa kwa
kutumia falsafa hiyo ya Lincoln, aliamua kuwageuza wale waliokuwa na
viherehere, kumsema vibaya, akawafanya kuwa marafiki zake. Kubenea huyo,
akasema hata Richmond alionewa!
Mwandishi wa
habari, uliandika habari ya uchunguzi kuwa Lowassa ni fisadi, miaka michache
baadaye unasema Lowassa alisingiziwa kuitwa fisadi. Sasa hapo aliyemsingizia ni
nani? Kama siyo wewe na kalamu yako!
Pengine
Kubenea alikuwa na ndoto ya kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, baada ya Lowassa kushinda urais. Au labda aliota kuwa Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu. Hayo mambo yameshindikana, hiyo ni kwa sababu ya shamba la
chuki dhidi ya Lowassa alilolilima kwa Watanzania.
Kubenea
asifikiri Lowassa amesahau, mwanamashairi, hayati Maya Angelou aliwahi
kuandika: “I've learned that people will forget what you said, people will
forget what you did, but people will never forget how you made them feel.”
Kiswahili: Watu
watasahau kile ulichosema, watasahau kile ulichofanya, ila hawatasahau ulivyowafanya
wajisikie.” Lowassa hatamsahau Kubenea. Na hivi urais umekwama, hasira zake
lazima zipae juu zaidi.
Chuki ya
Lowassa kwa Kubenea na Mwanahalisi; Mwaka 2010, Lowassa akiwa vizuri hasa,
imara kama chuma cha pua, nilikutana naye bungeni, nikampiga picha, alikuwa
amezungukwa na watu, akanishika mkono (siyo kwa shari), akaniambia: “Kuna
magazeti hayaruhusiwi kunipiga picha.”
Nikamuuliza
ni yapi hayo, hakutaka kujibu, akaniambia tu “yapo na yenyewe yanajijua”,
katika wale watu waliokuwa na Lowassa, mmoja wao aliamua kutoa sentensi nyoofu:
“Mojawapo ni Mwanahalisi!”
Unaweza
kuwaza mbona Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mwanasheria wa chama hicho,
Tundu Lissu na wengine nao waliwahi kumshambulia Lowassa na sijawaandika.
Itakuja makala kuhusu majina ya watu waliomnyima urais Lowassa mwaka 2015.
Ripoti ya Chopa la Jambo wiki hii
haipo kwa sababu ya utaratibu maalum wa kiofisi. Wiki ijayo ni ahadi kwamba
itakuwepo kama ilivyo utaratibu.
0 comments :
Post a Comment