Baba na Mama Rosemina, walikuwa na mawazo sana. Wakiwa
njiani walitamani kufika nyumbani haraka ili wamvae hausiboi wao anayeitwa
Chaka. Alifanya kitu ambacho wao walikitafsiri kuwa ameingiza kirusi kwenye
nyumba yao.
Walikuwa wanatokea hospitali ambako walimpeleka binti yao
Rosemina kupimwa, huko aligundulika ana ujauzito wa miezi minne. Walipomhoji
kwa kituo, akafichua ukweli kwamba mhusika wa mimba ni Chaka.
“Naombeni sana msimdhuru Chaka, nampenda sana,” Rosemina
alijaribu kumtetea Chaka.
“Kelele wewe, tena funga kabisa bakuli lako. Tunakusomesha
kwa pesa nyingi, leo unapewa mimba na hausiboi, aibu gani hii?” Baba Rosemina
aliwaka kwa hasira. Chupuchupu amchape kibao Rosemina.
Mama Rosemina alikuwa amefura kwa hasira, machozi yakimtoka.
Aliona mwanaye ameharibiwa maisha. Naye alitamani afike nyumbani haraka kisha
amkamate Chaka, amlambe japo vibao vitano vya kikekike.
Jinsi Baba Rosemina alivyopaki gari, ilikuwa ishara tosha
kuwa siku haikuwa ya kawaida. Alishuka na kumshusha Rosemina himahima, akamvuta
kuingia ndani. Mama Rosemina naye akawafuata kwa nyuma akiwa na sura ya
kisharishari.
Ungebahatika kuwaona, basi moja kwa moja ungeamini siku hiyo
pangechimbika, mtu angekong’otwa na kuzikwa akiwa hai. Baba Rosemina alipofika
ndani kwenye korido, hakutaka kupoteza muda, alipaza sauti kuita jina la Chaka.
“Naam,” Chaka aliitika.
“Leo utanieleza kwa nini umempa mimba Rosemina,” Baba
Rosemina alizungumza kwa hasira. Upande wa pili Chaka alibaki kimya, hakujibu
chochote.
“Wewe Chaka,” Baba Rosemina aliita kwa mara nyingine.
“Naam baba,” Chaka aliitika kwa unyenyekevu.
“Usiniite baba, mimi siyo baba yako. Nataka unieleze ni kwa
nini umempa mimba Rosemina?” Baba Rosemina alimuuliza Chaka ambaye alikaa
kimya.
“Unaniletea dharau siyo, sasa leo utaniambia,” Baba Rosemina
alimwambia Chaka, wakati huo Chaka alikuwa ameshajitokeza.
Akajibu: “Sina dharau baba, tatizo kule chumbani nilipokuwa
nilikuwa nasikia jina tu, maneno mengine sikuwa nasikia.”
“Acha utoto wewe, haya niambie hapahapa, ni kwa nini umempa
mimba Rosemina,” Baba Rosemina alihoji.
“Sawa baba, mimi nitakujibu, ila naomba kwanza uende kule
chumbani, ujionee mwenyewe, utakuwa unasikia jina tu, hilo hakuhakikishia,”
Chaka alimwomba Baba Rosemina ambaye alikataa: “Usilete utoto wako, hebu nijibu
haraka.”
“Nimekwambia nitakujibu, nenda kwanza kule chumbani wewe
utaona. Utakuwa unasikia jina tu, Mimi sina dharau baba,” Chaka aliendelea
kumsisitiza Baba Rosemina.
Baba Rosemina akaona isiwe tabu. Alikwenda kule chumbani ili
kumaliza ubishi, akijua kwamba atakaporudi, Chaka hatakuwa na kisingizio
kingine zaidi ya kujibu swali alilomuuliza kuhusiana na kumpa mimba Rosemina.
“Baba,” Chaka aliita. Wakati huo Baba Rosemina alikuwa
ameshaingia kule chumbani ambako mwanzoni alikuwepo Chaka.
“Nakusikia,” Baba Rosemina alijibu.
“Kwa nini umewapa mimba mahausigeli wawili hapa nyumbani,
alianza Monica, akaja Zuleha, wote sasa hivi ni nyumba ndogo zako, ukiwapa
mimba unawahamisha, kwa nini unafanya hivyo baba?” Chaka aliuliza.
Baba Rosemina akawa kimya, Chaka akaita: “Baba.”
“Nimesema nakusikia,” Baba Rosemina alijibu.
“Kwa nini uliwapa mimba Monica na Zuleha halafu
ukawalazimisha waache kazi hapa nyumbani kisha ukaenda kuwapangishia nyumba huko
nje?” Chaka aliuliza tena.
Kwa swali hilo, Baba Rosemina aliendelea kuwa kimya. Baada
ya muda, alitokeza pale kwenye korido, akasema: “Dah, kweli nimeamini, ukiwa
kule chumbani unasikia jina tu.”
Mama Rosemina akawa mkali: “Hakuna lolote, leo nyie wote mtanieleza,
hakuna chochote kwamba ukiwa kule chumbani hamsikii maneno mengine, mnasikia
sana ila mnataka kuleta masihara.”
“Mama usiwe mbishi,
hebu na wewe nenda kule utaona, utakuwa unasikia jina tu,” Chaka alimwomba Mama
Rosemina ambaye awali alikataa lakini baadaye alikubali. Akaenda kule chumbani
ili naye ajionee.
“Nakwenda, ila nikirudi mtanikoma nyie wote. Iwe mlikuwa mnasikia
jina tu au uongo, mtanitambua nikirudi,” Mama Rosemina alisema akiwa anaelekea
kule chumbani.
“Mama eeh,” Chaka aliita.
“Haya ongea, nakusikia,” Mama Rosemina alijibu.
“Kwa nini kila baba
akisafiri hapa nyumbani anakuja kulala yule mangi muuza duka la mtaa wa pili?
Huyu mdogo wetu wa mwisho, Jorum, umezaa na yuleyule mangi na wanafanana kweli
lakini unamdanganya baba ni mwanaye, kwa nini unafaya hivyo?” Chaka aliuliza.
Mama Rosemina hakujibu kitu, alikaa kimya tena kwa utulivu
wa hali ya juu kama maji mtungini. Chaka akaita: “Mama unanisikia?”
“Nakusikia Chaka,” Mama Rosemina alijibu.
“Naomba ujibu ni kwa nini unatembea na yule mangi muuza
duka, unamkosea heshima baba kiasi kwamba kila akisafiri, unamwita anakuja
kulala hapa nyumbani tena chumbani kwake, mnalala kitandani kwake. Haitoshi,
umezaa naye lakini unamdanganya baba kwamba Jorum ni mwanaye wakati unaujua
ukweli kuwa yule ni mtoto wa mangi,” Chaka alizidi kusasambua.
“Jamani, ni kweli kabisa, ukiwa kule chumbani huwezi kusikia
neno ligine lolote zaidi ya jina tu,” Mama Rosemina alisema akiwa amerejea
kwenye korido. Alikuwa akitazama chini kwa aibu.
“Wote hamna lolote, kila kitu kinasikika, uchafu wenu wote leo
upo hadharani, sasa nimuone mtu wa kunisema na hii mimba yangu. Wewe mama ni
mchafu, baba umeshindikana, sasa mniache na Chaka wangu tupendane,” Rosemina
aliongea.
Baba na Mama Rosemina aibu iliwashuka, hakuna aliyethubutu
kumjibu Rosemina, maana kama ni fedheha ilikuwa ya mwaka. Waliumbuka kuliko
mfano wa kawaida.
0 comments :
Post a Comment