ads 728x90 B

Usaliti, maumivu, rangi zake na aibu ya matokeo




Na Luqman Maloto
Umewahi kusalitiwa? Ulipogundua ilikuuma bila shaka. Maumivu ni makali mno pale unaposalitiwa na mtu unayempenda na zaidi unayemwamini. Hangaiko la moyo wako halitafanana kwa kila usaliti utakaofanyiwa.
Umewahi kusaliti? Ulipogundulika ilikuingiza kwenye fedheha ya kiwango cha juu. Unapoitwa msaliti maana yake unakuwa umewekwa kwenye kundi la hovyo. Mtu mwenye tamaa na usiyefaa kuaminika hata kidogo.
Hakuna aliyeanza kusaliti akawa hajui madhara ya anachokifanya. Zaidi, usaliti siyo tendo la bahati mbaya, ni kuchagua. Yaani unajifikiria kisha unaamua kufanya tendo lenye matokeo ya kumuumiza mwenzio, kujiaibisha na kusababisha usiaminike tena, zaidi kujidhalilisha.
Baada ya muda mwenzio anakuja kugundua kuwa wewe siyo mwenye kutosheka, una hila, unatamani vingi kwa wakati mmoja. Unamuumiza kwa sababu umemfanya ajione siyo mwenye kukutosha. Unampa mataabiko ya moyo ambayo tiba yake siyo rahisi.
Katika maisha yangu ya kila siku na tafiti ambazo nimekuwa nikizifanya, jibu la moja kwa moja ni kuwa hata vijana ambao hawajaanza kubeba majukumu wapo kwenye kiwango kizuri cha kuhisi maumivu ya usaliti pale yatakapowatokea.
“Mke anauma sana, yaani mke wangu atoke nje ya ndoa kweli!” kijana mmoja aliwahi kujibu baada ya kumuuliza kama anajua maumivu ya usaliti pale atakapokuwa ameoa au atakapokuwa na mwenzi wake, ama mpenzi au mchumba.
“Mwanamke atakayetembea na mume wangu sijui nitamfanya nini, ila sitamuacha salama!” Maneno haya alinitamkia binti mwenye umri mdogo kabisa. Anajua matokeo ya baadaye. Maumivu ya usaliti yapo kiasili zaidi. Binadamu hayajui baada ya kufundishwa. Yanakuja yenyewe!
USALITI NI UZEZETA WA AKILI
Inabidi kutumia neno upumbavu lakini pia halitoshi, usaliti ni uzezeta wa akili! Usaliti siyo ujinga kwa sababu mjinga ni yule ambaye anakuwa hajui kitu, akielimishwa anaelimika kisha anafuata njia inayofaa.
Msaliti ni zezeta wa akili kwa sababu anafanya kitu ambacho anakijua lakini anafanya tu! Matokeo yakishajiri anabaki kujilaumu kwa aibu. Ni upumbavu kusubiri kujilaumu wakati ulikuwa na nafasi ya kuepukana na janga.
Usaliti hutokea kwa sababu ya kutawaliwa na fikra mfu. Kukosa mawazo sahihi. Kudanganywa na leo kisha kusahau kwamba ipo kesho. Kushindwa kumkataa Shetani wa usaliti na kumtii hatua kwa hatua mpaka kitendo.
Msaliti huwa hafikirii athari baada ya usaliti wake kugundulika, hujikita kwenye tamaa za machoni tu. Kama mtu anaweza kuwa na macho yenye kukosa udhibiti wa akili, basi huyo ni kipofu kuliko mlemavu wa macho.
Mume wa mtu damu inamchemka, hisia zipo wima, anawaza kutenda dhambi na mwanamke mwingine. Tena anaweza kuwa mke wa mtu. Anachoshindwa kufikiri vizuri ni kuwa mkewe au mume mwenye mali akibaini mgogoro utakuwa mkubwa.
Mke wa mtu amepumbazwa na macho, akili inashindwa kufanya kazi tena. Anafikiria tu kutoka nje ya ndoa. Haifikirii mara mbili kuhusu aibu atakayoipata baada ya matokeo ya usaliti kugundulika. Hawazi kuhusu maumivu anayoweza kumsababishia mume wake.
Kichekesho cha akili; Mtu una mwenzi wako, upo huru naye kabisa. Mnaweza kujadiliana kila siku nini cha kufanya, mpeane nini kwa uhuru na utashi wenu. Hakuna wa kumhofia. Ni ninyi wenyewe kwa raha zenu.
Nani anapenda kuitwa mwizi? Kumiliki mali yako na kuitumia bila kuhofia macho ya wengine ni jambo lenye afya na heshima kubwa. Popote kule unakuwa huru kwenda na mali yako. Ukikutana na watu, kwa kiburi cha umiliki, unasema “huyu ndiye.” Naye atatamka “mwenyewe ndiye huyu.”
Fumba macho kwa sekunde kadhaa kisha uwaze raha za kuwa mmiliki. Ile hali ya kujiamini ambayo unakuwa nayo popote pale. Unaweza kumshika mkono barabarani, kuketi na kukutana naye kokote. Hakuna asiyependa uhuru huu!
Kituko kinakuja, mtu huyohuyo mwenye uhuru wake anajiingiza kwenye uhusiano wa siri, yaani mapenzi ya wizi. Mapenzi yenye presha za kujitakia. Kukutana mpaka mazingira ya kutafuta. Unapokwenda sehemu unahofia watu wanaokujua wasiwepo. Unatembea ukiwa umejaa wasiwasi.
Kabla ya kwenda lazima umsikilizie mwenzi wako, ratiba zake zipoje? Unaamua kudanganya safari ili kufanikisha malengo yako. Unakosa uhuru kwenye simu yako. Hutaki mwenzio ajue maneno au namba za siri za akaunti zako za kijamii. Simu yako huna uhuru nayo. Unaweza kwenda nayo mpaka chooni.
Ikiita mbele ya mwenzio unagopa kupokea. Ikiita ukiwa mbali kidogo unaweza kukaribia kuvunja mguu ili uwahi mwenzio asipokee au kusoma sms. Ukijitutumua na kupokea huongei kwa uhuru, unajibu kwa kutojiamini na unataka mazungumzo yaishe haraka na unajitahidi kumzuga mwenzio pembeni yako asielewe.
Akikuuliza nani huyo unajibu: “Nanii… naniii… rafiki yangu, nanii dada.” Unatengeneza jina litakalomridhisha. Kosa lako ni kujidanganya kuwa mwenzio hana akili. Atakushtukia.
Jaribu kuwaza; Wakati kwa mwezi wako una uhuru wa kwenda naye popote. Kutoka naye out bila kubughudhiwa na mtu. Unajiingiza kwenye uhusiano wenye mapenzi ya pande mbili tu.
Upande wa kwanza ni mawasiliano ya mtandao, iwe kuchati kwenye simu, sms za kawaida, facebook, wahatsapp, viber, skype, instachat, BBM na kadhalika. Upande wa pili chumbani. Mapenzi sawa na biashara ya ngono mitandaoni.
Wanaofanya biashara za ngono mitandaoni ndiyo hukutana kwa staili hiyo. Unaangalia mtandaoni, unaridhishwa na mwanamke au mwanaume anayejiuza, unafuata maelekezo, unalipa kisha unatoa anuani ya mahali ulipo, uliyemnunua akifika hakuna kingine zaidi ya kukamilisha biashara.
Mke au mume wa mtu naye anajiingiza kwenye mapenzi ya mtindo huu. Mepenzi mengi kwenye simu, facebook, whatsapp na kadhalika. Siku ya kukutana ni chumbani tu! Mtu mwenye kufikiri vizuri atajisikia vibaya na kuacha mapenzi haya yenye kukosa uhuru na heshima.
AINA ZA USALITI
Usaliti kwa maana pana ni ukosefu wa uaminifu, ustaarabu na uungwana. Ni kumtenda mwenzio kinyume na inavyostahili. Juu zaidi ni tendo la kikatili. Unaweza kusema huwezi kuua mtu lakini watu walishamwaga damu kwa usaliti.
Unaweza kusalitiwa na mzazi wako au wewe mtoto kumsaliti mzazi wako. Wafanyabiashara kudhulumiana. Mfanyakazi mwenzio anaweza kukusaliti. Marafiki kugeukana. Kwa kifupi ni kuwa usaliti una pande nyingi. Siyo katika uhusiano tu wa kimapenzi.
Angalizo kwako ni kuishi kwa kuwatendea wema wenzako. Kile ambacho ni maumivu na mateso ukitendewa basi usimfanyie mwenzako, kwani naye ana moyo, nyama na damu kama ulivyo wewe.
Zaidi, unaposaliti, jihesabu tu kuwa umekosa ustaarabu, uungwana na siyo mwaminifu. Kama sifa hizo siyo zako kwa nini utende yale ambayo yatakufanya ubebeshwe wasifu mbaya? Juu ya yote usaliti ni kutokujiheshimu! Je, wewe hujiheshimu? Kama hujiheshimu, maana yake hufai kuheshimiwa.
ATHARI ZA USALITI
Ni rahisi sana kuvunja uaminifu lakini kuaminiwa kwa mara nyingine ni vigumu mno. Wapo mke na mume walizeeka pamoja lakini manung’uniko hayakuisha. Kumbukumbu za usaliti waliofanyiana nyakati za ujana wao ziliwatesa mpaka walipotengana kila mmoja akiingia kwenye kaburi lake.
Athari namba moja unapokwenda kusaliti, kaa ukijua kuwa unatengeneza kitu ambacho mwenzio akikibaini, atapoteza kabisa imani juu yako. Hata akikusamehe, utamfanya asiamini tena kama unaweza kujitunza ukiwa mbali na macho yake.
Elewa kuwa usaliti wako unakwenda kupiga mstari wenye kufuta neno ‘mwamunifu’ kwenye mzunguko wa maisha yako yote na kuandikwa ‘msaliti’. Siku zinaweza kupita ukadhani yaliyotokea yamepita na watu wamesahau. Hutasahaulika.
Maisara alifunga ndoa na Baraka. Maisha yao ya kimapenzi yalikuwa mazuri mno. Ungewaona nyakati za mwanzo wa uhusiano wao, usingepata tabu kujua kweli kwamba wanapendana na kwa hakika walichaguana.
Walijenga familia bora, wakawa na watoto watatu, walijenga nyumba Kigamboni, Dar es Salaam. Baraka alikuwa mhangaikaji sana. Alijituma mno kufanya kazi zake za kila siku ili kuongeza pato la familia. Maisara kazi zake zilikuwa za kawaida, kutoka asubuhi kurejea nyumbani majira ya alasiri.
Baraka hakuwahi kumtilia shaka mkewe, alimwamini sana. Si kwamba hakuwahi kusikia chochote kuhusu mkewe, la hasha! Imani yake kwa mkewe ilikuwa ya kiwango cha juu mno. Yote aliyapuuza.
Kumbe Maisara alikuwa anasaliti ndoa kadiri alivyojisikia. Baraka akiamini mkewe ni mwaminifu, majirani na hata ndugu walidhani hajielewi ndiyo maana anamwacha mkewe anasaliti. Maisara akadhani Baraka ni mjinga. Aliichezea imani kubwa aliyopewa na mumewe.
Huwezi kudanganya siku zote! Nyakati zilifika, Baraka akabaini kuwa mkewe siyo mwaminifu, ugomvi ulitokea mkubwa sana. Mpaka watoto wao watatu wakabaini mgogoro uliokuwepo kwa wazazi wao.
Ghafla Baraka akawa hawezi kufanya kazi zake inavyotakiwa. Alibaki anagombana nyumbani na mkewe ambaye naye alishindwa kwenda kazini kwake. Mara kupigana, mara vikao, ikawa mateso juu ya mateso.
Maisara alipoteza uzito na alikonda sana. Baraka kiasili ni mweupe, alikonda na kuwa mweusi tii! Watoto shuleni wakawa hawasomi, mawazo yote yakawa kwenye migogoro ya wazazi wao.
Ni nyakati ambazo watoto walishuhudia baba yao waliyemuona mpole siku zote na aliye na upendo kwao na kwa mama yao, akitamka maneno makali mno kwa mama yao. Maneno yenye kudhalilisha. Maneno ambayo hakuna mtoto ambaye angependa kusikiliza mama yake akiambiwa.
Shuleni watoto walifeli mpaka walimu walishangaa. Waliwaita wazazi wajadiliane lakini hakuna hata mmoja aliyekuwa tayari kwenda kusikiliza mashauri ya watoto shuleni. Kila mmoja alivurugwa. Maisara hakutaka tena mapenzi ya nje na ndani yaligeuka kaa la moto.
Baraka alijitahidi kumsamehe Maisara alishindwa. Miezi ilikatika misuguano iliendelea, mwisho aliamua kumtimua Maisara. Ndani ya muda mfupi katika ndoa yao walipiga hatua kubwa kimaendeleo. Walijenga nyumba, wakawa na mashamba, Maisara akawa na biashara zake, waliweza kuwa na magari matatu. Sasa hivi wanarudi nyuma.
Kumbuka kuhusu vifo vya watu, wengine kusababishiana ulemavu. Kwa pamoja hayo yote ni matokeo ya usaliti. Uadui mkubwa kati yako na mwenye mali uliyoiba (mume au mke).
Namkumbuka Mama Jayden, alipobaini mume wake ni msaliti na ameweza kutembea mpaka na rafiki yake, aliona hawezi tena kuishi. Alimpenda sana mume wake Baba Jayden. Maskini Mama Jayden, akamnywesha kwanza mwanaye Jayden sumu, alipokufa. Akanywa na yeye! Hakutaka kumwacha mwanaye kwenye ulimwengu huu uliojaa matatizo.
Haukuwa uamuzi wa busara ambao Mama Jayden aliuchukua lakini huwezi kuingia ndani yake na kujua ni kiasi gani aliumia. Ukiona mtu anaumia sana baada ya kusalitiwa, maana yake alimwamini sana aliyemsaliti. Kusalitiwa na usiyemwamini haiumi sana. Si unajua haaminiki? Hana mwanama!
Maureen ni kati ya wateja wangu wa siku nyingi. Nimewahi kufanya naye mashauriano katika masuala kadhaa yaliyomtatiza. Aliwahi kunisimulia kisa cha yeye mimba yake kutoka baada ya kuona sms ya kimapenzi kwenye simu ya mchumba wake.
“Afadhali ningekuta inbox, ningewaza watu wanatuma tu! Sms niliikuta outbox kuonesha mchumba wangu ndiye ametuma. Sikumgombeza mchumba wangu wala mwanamke aliyetumiwa sms lakini mshtuko nilioupata ulisababisha mimba yangu itoke,” alisema Maureen.
Mfano mwingine ni James ‘Jimmy’ ambaye sasa hivi yupo jela, alikohukumiwa kifungo cha miaka 15 baada ya kukutwa na hatia ya kumchoma kisu Modest. Alimchoma kisu tumboni na kwenye jicho. Modest yupo hai lakini ana chongo hivi sasa. Jimmy alichukua uamuzi huo baada ya kugundua Modest anatembea na mkewe.
Helen sasa hivi sasa ni mlemavu wa ngozi. Watu wakimuona hudhani ni albino au Mzungu. Mwenyewe alikuwa na rangi ya chocolate. Weusi wa kung’ara (black beauty). Alipoteza ngozi yake ya asili baada ya kumwagiwa maji ya moto yaliyochanganywa na mafuta ya moto.
Sababu ni wivu wa mapenzi. Helen ni mfanyakazi mwenzake Sufian ambaye ni mume wa Rehema. Walikuwa wafanyakazi wanaoelewana sana. Rehema kukuta sms ya Helen kwenye simu ya Sufian halikuwa jambo la kushangaza.
Sufian alimtambusha Helen kwa Rehema kama mfanyakazi mwenzake. Sufian alimwita Helen dada, naye akamwita Rehema wifi. Siku ya siku Rehema akagundua Helen anatoka kimapenzi na Sufian. Aliumia sana, “kumbe wananifanya mjinga!” aliwaza.
Rehema alijiridhisha kila kitu baada ya kufuatilia nyendo zao. Akajipa uvumilivu, akajifanya hajabaini chochote. Akaendelea kumchangamkia Helen. Siku moja alimwalika nyumbani kwake, Helen akaenda. Hakujua ndiyo anaifuata adhabu yake.
Helen akiwa amekaa sofani, alimwagiwa maji ya moto yaliyochanganywa na mafuta ya moto kisha Rehema akakimbia. Mpaka leo Rehema hajulikani alipo. Helen kawa mlemavu, Sufian hajui mkewe (Rehema) alipo. Ndugu wa Helen walimlazimisha Sufian amuoe kwa sababu kawa mlemavu kwa sababu yake.  
Mifano hiyo ikupe picha kuwa katika usaliti lolote linaweza kutokea. Inategemea na hasira za mtendwa. Matukio ya mifano ni mingi. Usimsahau aliyepigwa risasi tumboni na mama yake akauawa na mchumba wake ambaye naye alijiua.
Zakia ni mteja wangu wa ushauri, aliniambia: “Mume wangu alikuwa mtu mwema sana, alikuwa ananiita majina mazuri kila siku. Alipenda kuzungumza yale ninayopenda, na alinipamba mbele ya ndugu zangu, zake, marafiki zangu na wake.
“Siku alipogundua nimemsaliti alibadilika kabisa. Nilizowea kumsikia akiniita mke wangu, sweetheart, darling, honey na mengine ya kupendeza, ghafla akawa ananiita malaya, changudoa, kicheche na mengine mabaya. Hili huwa linaniumiza sana. Natamani nikutane na kila mwanamke nimwambie athari ya usaliti. Ni mbaya sana.”
KIWANGO CHA USALITI
Kuna usaliti katika mapenzi ni rahisi kusameheka na yakaisha, mwingine athari yake hudumu na kudumu. Upo ambao unaweza kubabisha kesi ndogo, mwingine ni vita kubwa na uadui usioisha.
Fikiria mwanaume unatoka kimapenzi na dada, mdogo au ndugu wa mkeo. Vivyo hivyo, mke kutembea na kaka, dada au ndugu yeyote wa mume. Hapo unakwenda kutengeneza doa lisilokwisha. Una akili timamu, unajua athari hii.
Mwanamke unatembea na mfanyakazi mwenzie mume wako au bosi wa mumeo. Mume kutembea na mfanyakazi mwenzie mkeo au bosi wa mkeo . Mke kutoka na rafiki wa mume, kadhalika mume kutoka na rafiki wa mkewe.
Athari zinatofautiana, yote ni maumivu na kukosa uaminifu. Mke kutembea na houseboy na mume kutoka na housegirl. Kila eneo lina athari yake. Muhimu ni kuepuka usaliti na kutunza uaminifu. Muhimu zaidi ni kukwepa kufarakanisha ndugu. Usiwafanye ndugu wa damu wawe maadui kwa sababu ya tamaa zako.
Hafidh na Amiru ni ndugu tumbo moja, ila viapo vyao ni kuwa hawatazikana. Hafidh ni kaka wa Amiru na ndiye alimsomesha. Uadui ulikuja baada ya Amiru kutembea na mke wa Hafidh. Stella hataki tena kumsikia mdogo wake Roseheart, kisa ni Stella kubaini Roseheart anamzunguka kwa mumewe.  
UMESALITIWA? HUJADHALILISHWA
Ni kweli inauma kwa kiwango cha juu mno. Lakini katika mambo ambayo hutakiwi kuumiza kichwa juu yake ni hisia kuwa mumeo au mkeo anapokusaliti anakuwa amekudhalilisha. Hapana! Anakuwa amejidhalilisha yeye mwenyewe.
Hupotezi heshima kwa kusalitiwa, ila anapoteza thamani na utu wake anapobainika siyo mwaminifu. Mzee Nelson Mandela, alifariki dunia kisha akazikwa kwa heshima kubwa. Hakuwahi kupoteza thamani yake kwa usaliti aliotendewa na aliyekuwa mkewe, Winnie Mandela.
Tambua pia kuwa thamani na utu wa Winnie, vilipungua mara tu alipobainika kuwa amesaliti ndoa. Mtu anayejiheshimu ni yule ambaye analinda heshima ya ndoa yake. Usipoilinda utaonekana mtu wa hovyo mbele ya jamii!
Fununu tu zilisababisha Mfalme Kaisari aache mke. Baraza la Wazee lilifanya uchunguzi na kurejesha ripoti kwa Kaisari kuwa mkewe hajasaliti ndoa na kijana aliyesemwa, ni uvumi tu, Kaisari akasema: “Mpaka asingiziwe maana yake anaishi vibaya.” Kaisari akampa talaka mkewe. Aibu kwa mke kuwa na nyendo mbaya.
Unaposalitiwa usisage meno kuwa mkeo au mumeo humridhishi ndiyo maana anakusaliti. Zingatia, kuna tamaa na kuridhika. Wapo wengi baada ya kufumaniwa ndipo walijuta kwamba walichokuwa wanakifukuzia nje hakikuwa bora kuliko kile wanachokipata ndani.
Mwasiti alirudi kwa mchumba wake na kupiga magoti: “Nisamehe mpenzi wangu, wewe ni mwanaume bora sana, sijui hata kilichokuwa kinanipeleka nje. Ni tamaa, ni Shetani.” Kama Mwasiti, ndivyo na wanaume wengine hujuta, wake zao ni bora, wazuri, warembo lakini wakishasaliti na kugundulika, husaga magoti kuomba msamaha.
Wengi wakishafumaniwa huomba msamaha, hata wakitia kiburi baadaye hurudi na machozi mengi. Ni kipimo kuwa mwizi wako siyo bora kuliko wewe, ila tamaa tu! Kuna aliyetoka na hougirl au houseboy! Yupo anayetembea ni muuza genge au bucha! Unadhani hao ni bora zaidi? Ni tamaa za msaliti na kukosa kujiheshimu.

Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment