Na Luqman
Maloto
Wauza unga
wanafanana na wachawi wanaomiliki misukule. Kitabia na matendo, hawana tofauti.
Nitaeleza mbele ya safari na utanielewa, ila kwa sasa hebu ngoja kwanza niseme
hisia zangu.
Kwa mtu yeyote
mwenye ubinadamu aliyepata kumfahamu vizuri Rashid Abdallah Makwilo ‘Chidi
Beenz’, leo hii hawezi kushangilia mabadiliko ya msanii huyo.
Chidi Beenz,
mwite King Kong! Nyakati hizo alikuwa sahihi kujiita King Kong. Mwili mzuri, wa
mazoezi, shupavu kwelikweli. Na kama umeshaona muvi za King Kong, hapo tupo
sawa.
Sauti nzito,
jukwaani kifua wazi, mic mbili mkononi, anachezea sauti yake anavyotaka.
Jukwaani saa nne (dakika 240) alizimaliza. Leo hii alivyo, inauma sana!
Chidi Beenz
ndiye aliyejiita Busta Rhymes wa Bongo. Alistahili pia kujiita hivyo. Msikie
Chidi anavyochezea sauti yake, msikilize pia Busta, yule rapa wa Marekani,
mapafu manene, aliyewahi kutamba kuwa na uwezo wa kukabiliana na kifaru!
Ilikuwa
ukisema Chidi siye Busta, nani mwingine rapa wa Tanzania? Lazima kufika mahali
ukiri vipawa vya watu.
Chidi, rapa
mwenye pumzi hasa jukwaani. Siku moja aliwahi kuniambia: “Nikiwa jukwaani huwa
siyo binadamu wa kawaida.”
Siku
nyingine pia katika mazungumzo yetu, aliniambia: “Kuna madude huwa natumia, nikipanda
nakuwa mnyama jukwaani.” Vilevile alipata kunitambia: “Mimi ni animal.” Kwamba
yeye ni mnyama mkali!
Chidi,
aliitenda vema kazi yake. Alikuwa kiungo muhimu mithili ya chumvi kwenye mboga.
Kuna nyakati wanamuziki wengi waliona ili nyimbo zao ziwe na ladha sahihi, basi
vema kumshirikisha Chidi. Na kila aliposhirikishwa hakuharibu!
Kumbuka
Tundaman na Neilah yake, Mwasiti na Hao, Marlaw na Umenuna, Nonini wa Kenya
(wimbo Nifanye Muziki) na nyingine nyingi. Hapo sijataja za wana-Hip Hop ambazo
ni kibao.
Isisahaulike
kuwa kati ya mwaka 2007 mpaka 2010, Chidi Beenz aligeuza tuzo ya Hip Hop katika
Tuzo za Muziki Tanzania (Tuzo Kili), kama mali yake. Alizibeba mfululizo.
Mara ya
mwisho Chidi kubeba tuzo ya Kili, ilikuwa mwaka 2010, Tuzo ya Msanii Bora wa Hip
Hop, Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Baada ya hapo ndiyo ikawa mwisho
wa ufalme wa Chidi kwenye Hip Hop Tanzania.
Mwaka 2012,
Chidi alipanda jukwaani kukabidhi moja ya tuzo kwa Diamond Platnumz, Mlimani
City, Dar es Salaam. Siku hiyo, Diamond alishinda tuzo saba kwa mkupuo. Ona
heshima ya Chidi, tafakari huku alipofika. Kama ulimfahamu Chidi na huumii,
baki na ukosefu wako wa utu!
TULIE NA
WAUZA UNGA!
Usimcheke
Chidi Beenz kwa mabadiliko yake ya kimaisha, unachotakiwa kuelewa ni kuwa
safari ya Chidi kutoka Chidi Beenz Chuma, Animal, mpaka sasa ambaye anahitaji
huruma na upendo ili arejee kwenye ule Uchuma wake tunaoupenda, inamaanisha
safari ya muuza unga, kutoka hali fulani ya kimaisha mpaka utajiri.
Ndiyo
kusema, kuporomoka kwa Chidi kiafya, jinsi alivyokuwa anadhoofu ndivyo muuza
unga alivyokuwa anatengeneza fedha za kumfanya awe tajiri. Utajiri wa muuza
unga ndiyo kifo cha mtumia unga!
Ukivunjika
mbavu kwa madhila ya Ray C, dada yangu mpenzi Rehema Chalamila, hapohapo upate
picha kuwa safari ya kutoka Ray C yule Kiuno Bila Mfupa mpaka aliyeharibikiwa
na madawa, ndiyo safari ya muuza unga kutoka muuzaji mdogomdogo (pusha) mpaka
ulodi wa unga.
Hapo
namaanisha yule muuzaji wa unga mkubwa anayegawa kwa wauzaji wadogowadogo, kwa
hiyo anakuwa ameshatajirika. Amekuwa tajiri kwa kuua watu, kuharibu nguvu kazi
ya taifa. Utajiri wa kuyafanya maisha ya vijana kuwa mateso! Utajiri wa
kishenzi!
Kama
utayakumbuka maisha ya Ray C alivyokuwa anatengeneza pesa kwa muziki na
biashara ya maduka, mpaka kugeuka tegemezi, akiwa hana uwezo wa kuzalisha
kipato chake mwenyewe, zaidi akawa mgonjwa, unawezaje kumcheka na kumpigia
makofi muuza unga?
Ray C
alimiliki nyumba na gari akauza! Fedha zilikwenda wapi? Ziliishia kwenye unga.
Ndiyo kusema wakati Ray C anapoteza nyumba na gari kwa sababu ya unga, ndivyo
muuza unga alivyoweza kumiliki gari na nyumba kwa sababu ya unga.
Ni sawa tu
kusema kuwa gari, nyumba na mali zote za Ray C, zilihamia kwa muuza unga katika
mlango wa nyuma. Huwezi kuuita unyama?
IPO STORI
HII
Kuna msanii
mmoja maarufu kabisa. Ni teja! Simtaji jina leo kwa sababu ya tukio la aibu
ambalo lilimpata.
Alikwenda
kwenye ziara ya muziki nchi jirani akapata fedha nyingi. Aliporudi Dar es
Salaam, alikwenda kuripoti tu nyumbani kwao, akaacha begi la nguo kisha akatoweka.
Kumbe
mwanamuziki huyo alijiunga na wenzake, wakakaa hotelini, wanavuta unga. Pesa
zote zilikwisha na hoteli walifukuzwa.
Mwanamuziki
huyo alikwenda kwa wauza unga kukopa madawa, akapewa. Si wanamfahamu ni mteja
wao? Alipopewa alitumia palepale na kuzimika.
Ikawa
mchezo, akiamka wanampa tena madawa. Msanii akakonda kabisa. Ulevi wa madawa
makali bila kula.
Taarifa
zikafika nyumbani kwao, wakamfuata. Wale wauzaji wakakataa kumruhusu
mwanamuziki huyo kuondoka na ndugu yao kwa sababu wanamdai fedha za unga na
huduma za kila siku. Wakata wapewe shilingi milioni tatu.
Familia kwa
hofu kuwa wakienda polisi, watalifanya suala hilo kuwa zito na vyombo vya
habari kunasa, hivyo kumwaibisha ndugu yao ambaye ni maarufu, ikabidi
wajichange mpaka walipopata kiasi cha fedha kilichohitakiwa, wakaenda
kumkomboa.
Unaona
unyama wa wauza unga? Fedha zake walimmalizia, wakampa unga kwa deni na
kumfungia asiondoke mpaka ndugu walipe fedha walizosema wanamdai. Muuza unga
hawezi kuwa ndugu wala rafiki wa binadamu. Muuza unga siyo mtu! Muuza unga ni
mnyama!
TUELEWANE
Unga ni
janga. Usimcheke Chidi Beenz maana huijui kesho. Wapo wamegeuka mateja kwa
kulazimishwa, wapo waliohadaiwa.
Yupo
alitekwa akapewa mihadarati, damu yake ikaharibika. Naye akajikuta asipopata
madude anakuwa na alosto kama teja mwingine.
Wapo
waliodanganywa, wakapewa na kutumia bila kujua. Mwisho wakazoea, waliposhtuka wakawa
wameshachelewa. Na ukishaanza, kutoka ni ngumu. Wewe usicheke, omba Mungu
yasikukute.
Tunaendelea
kuishi, unaweza kumcheka teja wa leo, kesho mwanao akaingia kwenye mkondo
huohuo. Kama siyo mwanao, basi ndugu yako yeyote au rafiki unayempenda.
Ifike wakati
tuache kuwasimanga na kuwanyanyapaa waathirika wa madawa ya kulevya, bali
tuwaweke mbele ili tuwakabili wauza unga.
Twende mkono
kwa mkono na mateja wetu mpaka kwa matajiri wa unga. Tuwaambie: “Utajiri
mnaommiliki, ndiyo umesababisha ndugu zetu hawa wawe hivi.”
Lazima wauza
unga watambue hasira tulizonazo dhidi yao. Vema kuwanyooshea vidole na
kuwaambia wao wameharibu vipaji vizuri vya Chidi na Ray C. Tuwaambie kuwa
tunajua, kama siyo wao, Chidi angebaki kuwa King Kong, Ray C angeendelea kuitwa
Kiuno Bila Mfupa!
Wauza unga
ni sawa na wachawi wenye kumiliki misukule. Maana nao wanamfanya mtu mzima
anageuka ndondocha asiyejitambua.
Teja
barabarani ana tofauti gani na yule aliyetendwa vibaya na mchawi akafanywa
ndondocha? Athari wanazosababisha ni sawa kabisa.
Yule
msichana mrembo aliyekutwa shimoni Kimara, ikadaiwa aliwekwa msukule na tajiri
mmoja kwa sababu za kusaka utajiri, ana tofauti gani na kijana aliyekuwa
nadhifu, mchapakazi, mwenye maono ya kufanikiwa kimaisha lakini sasa hajiwezi
pale Manyanya, Kinondoni kwa sababu ya matumizi ya unga? Teja na ndondocha kuna
tofauti gani?
Wote mambo
yakishachachamaa wanakuwa hawajitambui. Hayupo kati yao mwenye uwezo wa
kuzalisha. Sanasana mateja wengi hugeuka kero mitaani wakipora watu ili wapate
fedha za kwenda kununua unga kisha waongeze utajiri wa wauza unga.
Sikiliza na
uache ubishi; Kama kuna siku uliibiwa na teja, hebu punguza hasira zako kwa
huyo teja, tazama utajiri wa muuza unga, halafu jiongeze kuwa vile vitu
ulivyoibiwa, vilikwenda kuongeza mali za haramia huyo wa madawa ya kulevya.
Teja ni
mtumwa wa uteja wake. Hana fedha na alishaharibikiwa. Sasa anafanyaje naye ni
mwathirika wa mihadarati? Inabidi akuvizie akuibie kisha aende akamtajirisha
muuza unga.
Ndiyo! Teja
alipokuibia alikwenda kuuza, fedha ambazo alizipata kwa mauzo ya vitu vyako,
alikwenda kuzitumia zote kwenye kununulia unga. Faida kuu kwa haramia muuza
unga!
Muuza unga
na mchawi anayebadili binadamu kuwa ndodocha hakuna mwenye nafuu! Wote ni
wanyama, tena washenzi hasa mbele ya Mungu. Ifike mahali tuwaambie wauza unga
wanaosema wanachukia uchawi, kuwa wao ni sawa na wachawi. Ni zao moja, ila
utendaji ni tofauti!
0 comments :
Post a Comment