Luqman
Maloto
MTENDWA wa
usaliti hupata maumivu makali, wakati huohuo mwanzoni msaliti hukenua kwa
kudhani ameshinda. Maisha hayapo hivyo!
Anayesalitiwa
humwaga machozi kwa kilio cha mahangaiko ya moyo. Husahau kumshukuru Mungu.
Hutamani kulipa kisasi. Hushindwa kutambua kuwa mzunguko wa maisha ya binadamu
kama Maulana alivyoumba, tendo baya humrudia mtendaji mwenyewe wasaa unapotimu.
Laiti kila
mmoja angejua mataabiko ambayo wasaliti hukutana nayo, kungekuwa na nafuu kubwa
ya kimaisha. Idadi ya vitendo vya usaliti ingepungua.
Msaliti
anapaswa kujua; Unapomsaliti mwenzio maana yake unakuwa sawa na kuyageuza
maisha yake juu chini. Hilo siyo jambo dogo, kwani unaharibu mfumo wa maisha
yake. Maumivu unayompa ni makubwa mno.
Katika
uhusiano wa kimapenzi au ndoa, unapomsaliti mwenzio unakuwa umeingiza kaa la
moto ndani ya moyo wa mwenzako. Aliwekeza upendo wake na imani kubwa, usaliti
wako unamsababishia aende kuanza upya!
Wachumba
wanaachana, ndoa zinavunjika. Yupo ambaye amewahi kutafsiri usaliti kama mfano
wa mtu aliyetumia muda mrefu kujenga ghorofa lakini wewe unakuja kubomoa kwa
siku moja.
Imani
inajengwa na huchukua muda mtu kumwamini mwenzi wake kwa kiwango cha kutokuwa
na shaka juu yake. Inapotokea anabaini kufanyiwa kitu tofauti na imani
aliyokuwa nayo, kila kitu hubadilika. Imani yote huondoka na ni vigumu mno
kumwamini tena.
UNAYAJUA
MATAABIKO YA DAUD?
Daud ni mtu
wa Mungu lakini alipofanya dhambi ya usaliti, alikutana na majanga makubwa.
Jaribu kufikiria kama Daud pamoja na ukuu wake aliotakaswa na Mungu yalimfika,
wewe mwenzangu na mimi je?
Ukweli ni
kuwa matokeo ya kujirudia kwa vitendo viovu vya nyuma, hudhihirika kwa namna
mbalimbali. Tatizo ni kuwa wahusika huwa hawajitokezi na kutoa ushuhuda.
Nitaeleza!
Kabla ya
kufika kwenye pointi ya kuchambua mateso kama siyo mataabiko ya wasaliti, tubaki
kwenye kuyamulika mataabiko ya Daud.
Kwa
kujivunia ufalme wake, Daud alimchukua mwanamke anayeitwa Bathsheba ambaye ni
mke wa Uriah, aliyekuwa askari katika moja ya vikosi vyake.
Daud
aliwatuma walinzi wake wakampeleka Bathsheba chumbani kwake, pamoja na kuambiwa
kuwa huyo ni mke wa Uriah, bado hakurudi nyuma, akalala naye!
Baada ya
kulala na Bathsheba, Daud akanogewa, akaamuru Uriah auawe akiwa kwenye uwanja
wa mapambano. Maskini ya Mungu, Uriah aliponzwa na mkewe. Eti kosa lake ni kuwa
na mke mzuri.
MUNGU
ALIPOMKASIRIKIA DAUD
Katika
Biblia Takatifu, Soma 2 Samuel 12, utaona mtiririko huu;
1. Ndipo
Bwana akamtuma Nathan aende kwa Daud. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na
watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
2. Yule
tajiri alikuwa na kondoo na ng'ombe wengi sana.
3. Maskini
hakuwa na chochote, isipokuwa kondoo mmoja ambaye alimtunza sana.
4. Siku moja
yule tajiri alipata ugeni. Akataka kumtengenezea kitoweo, badala ya kuchinja
moja kati ya mifugo mingi aliyonayo, akaenda kumtwaa yule kondoo wa maskini.
5. Ndipo Daud
akashikwa na hasira, akamwambia Nathan, huyo tajiri aliyemdhulumu mwenzake
kondoo anastahili kuuawa kwa unyama aliofanya.
6. Daud akasema
pia tajiri anapaswa kulipa fidia ya kondoo mara nne, kwa sababu alikosa huruma
kwa maskini.
7. Basi Nathan akamwambia Daud, wewe ndiwe mtu
huyo. Bwana, Mungu wa Israel, asema hivi: “Nalikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israel,
nikakuokoa na mkono wa Sauli.”
8. Nathan
anaendelea kumkariria Daud maneno ya Mungu: “Nami nikakupa nyumba ya bwana
wako, na wake za bwana wako kifuani mwako; nikakupa nyumba ya Israel na ya
Yuda; na kama hayo yangalikuwa machache, ningalikuongezea mambo kadha wa kadha.”
9. Nathan
sasa anazungumza kumsema Daud; “Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya
yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uriah, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa
mkewe awe mke wako, nawe umemuua huyo kwa upanga wa wana wa Amon.”
10. Ona sasa
ahadi kali ya Mungu kama ilivyosemwa na Nathan: “Basi, sasa upanga hautaondoka
nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uriah, Mhiti, kuwa mke
wako.”
11. Nathan
anaendelea kuisema adhabu kali kwenda kwa Daud kwa kitendo alichofanya: “Bwana
asema hivi, angalia, nitakuondoshea kinga uovu katika nyumba yako, nami
nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na
wake zako mbele ya jua hili.”
12. Muogope
Mungu, ona Daud mtu wa Mungu alivyoambiwa: “Maana wewe ulifanya jambo lile kwa
siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israel wote na mbele ya jua.”
13. Si una
kiburi kuwa Mungu husamehe haraka? Hata Daud aliomba msamaha, alimwambia
Nathan: “Nimemfanyia Bwana dhambi.” Nathani akamwambia Daud: “Bwana naye
ameiondoa dhambi yako; hutakufa.”
14. Nathan
akaendelea: “Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa
ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.”
15. Naye
Nathan akaondoka kwenda nyumbani kwake. Basi Bwana akampiga yule mtoto ambaye
mkewe Uriah alimzalia Daud naye akawa hawezi sana.
16. Basi
Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto; Daud akafunga, akaingia, akalala
usiku kucha chini.
17. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka,
wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi, lakini hakukubali, wala
hakula chakula pamoja nao.
18. Ikawa siku ya saba, yule mtoto akafa. Nao
watumishi wa Daud wakaogopa kumwambia ya kuwa mtoto amekufa, maana, walisema, angalieni,
yule mtoto alipokuwa angali hai, tulisema naye, asitusikilize sauti zetu, basi
hatazidi kujisumbua, tukimwambia ya kuwa mtoto amekufa?
19. Lakini alipoona ya kuwa watumishi wake
wananong'onezana, Daud alitambua ya kuwa mtoto amekufa, basi Daud akawauliza
watumishi wake, Je, mtoto amekufa? Nao wakasema, amekufa.
Nakatisha
mistari ya Biblia ili uone namna ambavyo Daud alipata mataabiko. Dhambi ile
ilileta madhara makubwa kupita kiasi.
Ukichimba
zaidi, utagundua kuwa licha ya kusababisha uzinzi, pia yapo madhara mengine
yaliyojitokeza. Kulitokea mauaji ya mtu asiyekuwa na hatia (Uriah). Jina la
Bwana lilitukanwa kutokana na mpakwa mafuta wa Bwana (Daud) kuanguka katika
dhambi.
Baada ya
uzinzi ule, mtoto batili alizaliwa na vilevile akafa. Uasi ulitokea nyumbani
mwa Daud na kusababisha aibu kubwa ya Absalom (mwana wa mfalme) kulala na wake
za babaye, tena mbele ya kadamnasi ya Waisrael.
Kulitokea
laana ya upanga kutoondoka katika nyumba ya Daud, ubakaji, mauaji na kadhalika.
Yaani amani ilitoweka kabisa nyumbani mwa mfalme Daud. Rejea ahadi ya Nathan
kama alivyotumwa Mungu amwambie Daud.
Kwamba yeye
akiwa na wake wengi si alimtamani Bathsheba, mke pekee wa Uriah, na akaamuru
auawe? Sasa naye wake zake walitembea na mwanaye Absalom. Tena mbele ya
kadamnasi. Ni ile ahadi ya kuwa aibu hiyo itadhihirika mbele ya Israel yote.
Huyu aliyetendwa hivi ni mpaka mafuta wa Bwana. Hasira za Mungu kwa mkimbilia
mali za watu ni za kiwango gani?
Ni ukweli
kuwa Mungu alikuwa na uwezo wa kumdhibiti Daud asifanye ushenzi kwa Bathsheba
lakini bila shaka aliacha yatokee ili kudhihirisha mambo mawili makuu.
Mosi; Ni
kuthibitisha kuwa binadam anabaki kuwa kiumbe dhaifu pamoja na kupakwa mafuta
ya utakatifu.
Pili;
Ionekane kuwa Mungu habagui, yeyote anayekosea atakutana na adhabu kali bila
kujali nafasi yake.
MALIPO NI
DUNIANI
Chickens
come home to roost; Hii ni methali ya Kiingereza yenye maana kuwa ubaya wowote
ambao utaufanya, baadaye utakuja kukurudia.
Methali hiyo
ina zaidi ya karne saba. Katika nahau hiyo, ubaya ambao mtu huufanya,
unafananishwa na kuku, kwamba ni kawaida kuku hutoka kuzunguka akitafuta
chakula lakini mwisho hurejea bandani.
Kwamba mtu
anapofanya ubaya, huzunguka huku na huko lakini ipo siku ubaya wake utamrejea
kwenye banda lake.
Msemo huo
ulipata umaarufu mkubwa pale mwanaharakati Malcolm X, alipoulizwa maoni yake
kuhusiana na kuuawa kwa Rais wa 35 wa Marekani, John Kennedy, aliyepigwa
risasi. X alijibu: “Chickens come home to roost.”
Kwamba
watawala walikuwa hawachukui hatua pale Waafrika walipouawa, kwa hiyo kifo cha
Kennedy ni matokeo ya kufuga jipu la ukatili, kwa hiyo limewatumbukia wenyewe.
Ipo dhana ya
Karma, ikianza kwenye imani ya Buddha, kuwa jambo lolote ambalo unalifanya leo,
lina malipo yake. Ukitenda mema, wema wako utaukuta mbele ya safari. Ukifanya
mabaya, hutajua siku lakini lazima utaukabili zamu inapofika.
DHAMBI
HAIKIMBIWI
Harrison ni
jaji, usiku mmoja akiendesha gari, taa ilimulika gizani na kuwaona watu
wakimuua mwenzao. Bahati nzuri aliwatambua wote. Aliyeuawa ni James, wauaji
walikuwa watatu, Larry, Jaden na Chris.
Baada ya
wiki moja Harrison akiwa kazini alipangiwa kusikiliza kesi ya mauji ya James.
Mtuhumiwa aliyeletwa mbele yake ni Jorum. Kumbuka kuwa Harrison kama jaji
aliwaona wauaji. Lakini maadili ya kazi yake hayamtaki kusema alichokiona,
isipokuwa kutoa hukumu kutokana na matokeo ya mwenendo wa kesi.
Kesi
ilipofika wakati wa ushahidi, vilitolewa vizibiti vya nguvu kabisa kuonesha
wazi Jorum ndiye aliyehusika na mauji. Mpaka ushahidi unakamilika hakukuwa na
namna yoyote ya kumuokoa Jorum na hukumu ya kifo kutokana na mauaji ya James.
Harrison
akawa anaumia mno, maana yeye aliwaona wauaji na anawajua. Anafahamu fika kuwa
James hakuhusika na mauaji yale. Kilichomuumiza Harrison ni kuona kuwa
anakwenda kumpa mtu adhabu ambayo hakuwa na hatia nayo. Ushahidi ulitengenezwa
na umethibitisha kuwa Jorum ndiye alimuua James.
Siku moja kabla
ya hukumu, Harrison alikuwa mwenye mawazo mno. Hukumu ya Jorum ilimtesa hasa.
Mwisho aliamua kwenda gerezani ambako Jorum alikuwa amewekwa mahabusu.
Harrison
akamwambia Jorum: “Najua kabisa wewe siye uliyemuua James.”
Jorum
akajibu: “Ni kweli mheshimiwa, mimi naonewa. Hii kesi imetengenezwa.”
Harrison
aliwaza kisha akamuuliza Jorum: “Bila kunificha kabisa, kabla ya tukio hili,
wewe huko nyuma umewahi kuua?”
Jorum: “Ni
kweli niliwahi kuua zamani lakini hakuna aliyejua.”
Harrison
akasema: “Basi hukumu ya kesho nitaitoa kwa ajili ya yale mauaji ambayo uliua
na hukujulikana. Nilikuwa napata shida kumhukumu mtu asiye na hatia, kumbe
hatia unayo.”
Chukua hii;
Unapokuwa kwenye kipindi cha maumivu, usilalamike sana kuwa unaonewa, nawe
kumbuka uliyoyafanya nyuma. Kama uliwahi kuumiza wenzako pokea kuwa nawe muda
wako umefika wa kuumia. Ndiyo maisha, ndivyo safari ya kiroho inavyokwenda.
Unapoingilia
uhusiano wa watu kwa mabavu, ukijidaia fedha zako, tambua kuwa zipo adhabu za
aina nyingi. Dunia siyo uwanja wa fujo kama wengine wanavyojidanganya, ipo
nguvu isiyoonekana, ambayo huwalipia visasi waja wanyonge kwa namna ya kuumiza
kabisa.
Bure alikuwa
mume wa Justa. Bosi wa Bure anaitwa Kamau, naye akampenda Justa. Ili aweze
kumfaidi vizuri Justa, Kamau alimhamisha Bure kituo cha kazi, alimtoa Dar es
Salaam akampeleka Mwanza.
Kamau ana
mke wake, kwa hiyo burudani zake na Justa zilikuwa mchana tu. Justa mumewe
hayupo, usiku akaona siyo vibaya kumuingiza Francis chumbani kwake. Kamau akawa
wa mchana na kuvuna pesa, usiku anakuwa na Francis, anamhonga na wanalala wote.
Bure akiwa
Mwanza akajua kila kilichokuwa kinaendelea, akafanya taratibu za talaka,
akaachana na Justa. Kumbe Francis ni mwathirika wa homa ya ini (Hepatitis B),
alimwambukiza Justa ambaye naye alimpa Kamau. Na hivi mzunguko wao ulikuwa kwa
mara kwa mara, maambukizi yalikuwa makali.
Wote watatu,
yaani Francis, Justa na Kamau, walifariki dunia baada ya mateso makali ya
kuugua kansa ya ini (liver cancer) na ini kuharibika (cirrhosis of the liver).
Bure mpaka leo yupo, anadunda. Ana familia yake aliyoianzisha baada ya kuachana
na Justa. Alipata kazi bora zaidi baada ya kuachana na kampuni ya Kamau.
Helen ana
umri wa miaka 37 sasa, alishaapa kuwa hataolewa tena. Anadai wanaume hawaaminiki
na hawatosheki. Pale alipo ana watoto wanne, kila mmoja ana baba yake.
Alishaolewa ndoa tatu, zote zilivunjika kwa sababu ya kufanana.
Mtoto wa
kwanza Helen alimpata alipokuwa na uhusiano na mume wa mtu anayitwa Kibuda. Mke
wa Kibuda aliujua uhusiano kati ya Helen na mumewe na aliumia sana.
Walishawindana mitaani mpaka kupigana.
Mke wa
Kibuda alimuonya mno Helen kuachana na mume wake lakini haikuwezekana, matokeo
yake Helen akazaa mtoto na Kibuda. Mwenyewe alisema alifanya vile kumkomoa mke
wa Kibuda.
Siku
zikapita Helen akampata Modest, wakafunga ndoa. Kipindi akiwa mjamzito, Helen
alishtuka kugundua kuwa mume wake anatembea na housegirl. Ule mshtuko alioupta,
alijifungua mtoto kabla ya siku zake, yaani njiti.
Ulipita
muda, Helen akawa anaumia, mume wake kutembea na housegirl aliona
kadhalilishwa.Pamoja na mtoto mchanga, alilazimisha apewe talaka. Ndoa
ikavunjika, Helen aliondoka kwenye nyumba, housegirl akabaki anatawala.
Maisha ya
kulea watoto wawili bila mume yalimtesa sana Helen. Mtoto alipokua, alipata
mwanaume mwingine, Vincent, walikwenda bomani wakafunga ndoa. Walipata mtoto
mmoja, akawa wa tatu kwa Helen.
Helen
akagundua kuwa Vincent ana nyumba ndogo na kazaa naye, moto ndani ya nyumba
uliwaka, wakaachana. Helen akawa mama pekee (single mother) akiwa na watoto
watatu.
Umri
unaenda, naye ana kiburi cha urembo, Helen baadaye akatua kwa mwanaume
anayeitwa Bob. Huyu hata hawakufunga ndoa, waliamua kuishi tu.
Tatizo la
Bob likawa ni kukosa uvumilivu anapoona mwanamke. Kila rafiki wa Helen alimtongoza,
wengine alitembea nao, wapo waligombana na Helen. Walipata mtoto mmoja, akawa
wa nne kwa Helen. Mwisho waliachana.
Siku zote
Helen wimbo wake ni kuwalaumu wanaume kuwa baba yao ni mmoja, kuwa hakuna
mwenye afadhali, kila aliyekutana naye amekuwa na vioja vya kipeke yake.
Ambacho
Helen huwa hakumbuki ni makosa aliyoyafanya kwa Kibuda. Hakumbuki kama
alimuumiza mke wa Kibuda. Hajui kuwa anavyotangatanga ndivyo ambavyo kuku
wanarudi bandani (chickens come home to roost). Vilevile anatimiza ukweli
kuhusu dhana ya Karma.
Lyndon ni
mkurugenzi wa kampuni kubwa, anajulika na watu wanamheshimu kutokana na uwezo
mkubwa kifedha. Kitu ambacho wengi hawakijui ni kuwa maisha yake ya kimapenzi
yamejaa mateso makubwa.
Kutokana na
jeuri ya fedha na ubosi wake, Lyndon amekuwa hachagui aina ya mwanamke wa
kutembea naye. Wafanyakazi wa kampuni yake ambao ni wake za watu hutembea nao.
Ana mke
pamoja na nyumba ndogo za kudumu tatu. Kote huko ni mateso kwake, kwani kila
akipindua anagundua watu wanamlia vyake, yeye anahudumia watu wanakula bure.
Kwa mkewe pia wasio na woga hupita.
Yeye ni
kidume mpaka kwa wake za watu, lakini anateswa na jinsi vidume wenzake
wanapoingia kwenye himaya zake na kumlia viota vyake, mbaya zaidi mpaka kwa
mkewe. Anaishi kwa kuteseka, mara akodi wahuni kwa ajili ya kuwadhuru wale
ambao anakuwa amewahisi wanaingia kwenye nyumba zake. Chickens come home to
roost!
Umeoa?
Heshimu ndoa yako, maana ukicheza faulo yoyote lazima malipo utayapata.
Umeolewa? Hakikisha unakuwa mke bora. Ukijisahau, maisha yatakufundisha umuhimu
wa kuwa mkweli kwenye ndoa.
Unaye
mchumba? Hakikisha unakuwa mkweli kwake? Je, boyfriend au girlfriend? Husika
kama ambavyo unatakiwa. Kila hatua ambayo unapiga ina malipo yake. Ukienenda
vizuri, utalipwa mazuri, ukienda vibaya utapata unachostahili.
Kama
wasemavyo kuwa ujana ni maji ya moto, wengi hudanganyika wakiwa vijana.
Wanapoteza muda wao kutembea na wake za watu au waume za watu. Hujisahau pale
ambapo wao wakiingia kwenye ndoa na kujikuta wanalipa gharama za matumizi
mabaya ya ujana.
Chukua hii;
Ukiwa kijana mzuri, unajiheshimu na unaziheshimu ndoa za wengine, Mungu atakupa
mwenzi bora ambaye hatakuumiza, hatakusaliti na mtashirikiana kuifanya ndoa
yenu kuwa mfano bora. Ndoa yenye upendo na maelewano!
Pokea na hii;
Ukiwa kijana wa hovyo, hujiheshimu na unaingilia ndoa za watu bila woga. Elewa
tu kuwa Mungu atakupa mwenzi msumbufu ambaye daima mtasumbuana, mtafumaniana,
mtaumizana. Lazima kuku warejee bandani!
Bwire na
Martha ni wanandoa na kila mmoja ana historia yake ya nyuma. Bwire alivunja
ndoa ya watu, alipotembea na mke wa jirani yake. Martha amekuwa hodari wa
kutoka na waume za watu mpaka alipotua kwa Bwire.
Martha na
Bwire walipooana, walijidanganya kuwa wamekua na waliyoyafanya nyuma
hayatawarudi. Martha akawa anapokea taarifa za wanawake wa nje wa Bwire. Martha
akaona ujinga, akamlipizia, naye akawa anatoka nje hovyo. Alitembea mpaka na
watu wa karibu na mumewe, tena mpaka kitandani kwake.
Bwire
alipokuja kugundua ushenzi wa mkewe, moto uliwaka kisha wakaachana. Hawakujua
kuwa Mungu aliwakutanisha ili waumizane kwa sababu ya malipo ya uhuni
waliofanya kwenye ndoa za wenzao. Ukivunja ndoa ya mwenzako na yako itavunjwa
tu! Kuku lazima arudi bandani.
Malcolm X
kwa chuki yake dhidi ya usaliti, alisema: “To me, the thing that is worse than
death is betrayal. You see, I could conceive death, but I could not conceive
betrayal.”
Kiswahili:
Kwangu, kitu kibaya kuliko kifo ni usaliti. Unaona, naweza kujenga fikra kuhusu
kifo lakini siwezi kuupatia picha usaliti.
Mwandishi wa
Kijapan, Mineko Iwasaki, naye alisema: “Stab the body and it heals, but injure
the heart and the wound lasts a lifetime.”
Kiswahili:
Uchome mwili kisu utapona, lakini jeruhi moyo na jeraha lake litaishi maisha
yote.
Wote
tunapaswa kuuogopa usaliti maana malipo ni duniani. Wote tuuchukie usaliti,
maana unatuumiza sisi wenyewe.
0 comments :
Post a Comment