WANAKUCHEKA
kisa huna chochote? Hutakiwi kuchachamaa na kulazimisha usichekwe. Pokea
vicheko vyao kwako, piga moyo konde!
Vicheko vya
dharau dhidi yako dawa yake siyo kukasirika au kupambana na wachekaji. Elewa tu
unachekwa lakini ni vicheko vya muda mfupi. Kamwe haviwezi kudumu!
Ukikaa peke
yako usijikunyate, maneno ya dharau yasikufanye ujione mnyonge. Katu usivunjike
moyo. Badala yake tabasamu kwa dharau zao pamoja na vicheko vyao.
Wala usiende
mbele yao kwa tambo na majigambo kisha upayuke: “Ipo siku yenu mtaniheshimu.”
Acha mwisho uje udhihirishe mantiki (let the end to justify the means).
Upo kwenye
jamii ambayo unabanwa, mchango wako wa mawazo hausikilizwi. Hata hupewi nafasi
ya kuzungumza. Unabaguliwa na kuonekana mtu duni wa daraja la mwisho. Najua
inauma sana!
Kifua
kinakujaa kwa hasira, unatamani kulia kwa sauti kubwa. Nakuomba uamke,
usiruhusu machozi yako yaonekane kwa watu wengine. Tafadhali sana simama imara,
hebu kuwa kama askari mateka mwenye busara!
Unajua
askari mateka wa kivita mwenye busara huwa anakuwaje? Akishakamatwa na maadui
hujifanya mjinga. Huvumilia kila mateso na manyanyaso ya maadui, wakati huohuo
akipiga hesabu kali za namna ya kuwakabili maadui pamoja na kutoroka.
Ule uzoba
kama siyo uzezeta wa askari mateka, pamoja na utiifu wake, huwapumbaza askari
maadui, hivyo kupunguza umakini dhidi yake. Na hapo ndipo hufanya kosa. Na
pindi askari mateka anapopata mwanya, wale maadui hubaki kusimulia kwa majuto!
Hebu tafuta mwanya, ili wanaokudharau wajute!
Haya sasa,
hebu tuanze; Wanakusema vibaya, wewe tabasamu. Wanakufanyia dharau waziwazi,
jifanye huoni hayo, wewe cheka. Wanakubagua, igiza kwamba hilo siyo tatizo,
cheka nao. Chanua tabasamu lako mbele yao.
Acha waseme
kuwa wewe ni kabwela kwa maisha yako yote. Siyo kosa lao, ni kwa vile hawajui
maisha. Nikupe siri; Yeyote mwenye hulka ya kumcheka asiye nacho, mlemavu wa
viungo na kadhalika, mhurumie kwa kuwa hajui maisha na nidhamu yake!
Chukua hii;
Wengi waliofanikiwa katika maisha, ni wale waliovumilia manyanyaso ya
walimwengu, wakajionesha wajinga. Ni kweli walipata hasira ila walizificha
hasira zao. Ukionesha hasira unakuwa mtu wa chuki.
Mungu
hapendi mtu wa chuki, maana huwa yupo karibu sana na kisasi. Binadamu wazuri
huwaogopa wenzao wenye chuki, hushindwa kushirikiana nao. Chuki zako
zitakufanya uogopwe na hata usioneshwe njia za kufanikiwa. Jifunze kutabasamu
hata unapoumia.
Ngoja
nikwambie; Nelson Mandela ‘Madiba’ alifungwa na Makaburu miaka 27 jela.
Walimnyanyasa na kumchukulia uhuru wake. Waliifanya afya yake kuwa dhaifu.
Mandela
alikuwa na msimamo lakini alitabasamu mbele yao. Hata walipomtoa jela,
aliendelea kukaa nao meza moja, mwisho ikawa sababu ya kufanyika uchaguzi wa
kwanza wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini na Mandela alishinda na akawa rais
wa kwanza mzalendo kuongoza taifa hilo.
Baada ya
Mandela kushinda, dunia nzima ikasema: “Tuone sasa, si walimfunga, ngoja
awalipizie kisasi!” Mandela wala hakujishughulisha na ulipaji kisasi,
alijielekeza kwenye kujenga demokrasia na uchumi shirikishi kwa kila raia wa
Afrika Kusini.
Wakati
Mandela anafariki duniani, aliweka rekodi ya kuwa mtu anayeheshimika zaidi
ulimwenguni, maana kifo chake kiligusa mataifa yote. Mandela angejielekeza
kwenye ulipaji kisasi, wala asingevuna heshima aliyoondoka nayo, iliyoifanya
dunia nzima ijielekeze Afrika Kusini wakati wa mazishi yake.
Nikupe stori
nyingine; Mahathir bin Mohamad akiwa mzalendo hasa kwa nchi yake ya Malaysia,
vilevile mwanachama hai wa chama tawala cha United Malays National Organization
(UMNO), alionekana kiherehere kwa misimamo yake ya kutetea maslahi ya nchi.
Chini ya
utawala wa Waziri Mkuu, Abdul Rahman, Mahathir alifukuzwa kwenye chama cha
UMNO, alitimuliwa ubunge kwa kudhalilishwa na kusemwa vibaya sana. Hiyo ilikuwa
mwaka 1964.
Mahathir
alivumilia miaka sita tu, kwani mwaka 1970, Abdul Rahman alilazimishwa
kujiuzulu uwaziri mkuu, vilevile urais wa UMNO. Ni hapo ndipo Mahathir
aliporejeshwa kwenye chama, akarejeshewa ubunge wake kisha akateuliwa uwaziri.
Mwaka 1976
Mahathir akawa naibu waziri mkuu na mwaka 1981, alichaguliwa na chama chake
kuwa Waziri Mkuu wa Malaysia, ikiwa ni miaka 17 tangu alipodhalilishwa kwa
kuitwa msaliti, mchochezi na mwenye kiherehere.
Uwaziri Mkuu
kwa Malaysia ndiyo ukuu wa serikali kama ilivyo Urais kwa Tanzania. Wakati
Mahathir anakuwa waziri mkuu, Abdul Rahman alishuhudia. Yalikuwa mateso makubwa
kwake.
Nakwambia
usiwaze kulipa kisasi, jielekeze kwenye ukweli na mihangaiko halali ya
kimaisha. Wanaokucheka leo, kesho wanaweza kutamani kuketi meza moja na wewe na
wala muda huo usipatikane.
Amka usilie,
dunia ina visa vingi hii; Ni kweli inauma kusimangwa lakini mbona wengi
waliosimangwa siku hizi ndiyo wanayenyekewa?
Mwanamitindo
raia wa Urusi, Natalia Vodianova, mbona alinyanyaswa sana akiwa anauza ndizi
barabarani? Alichekwa na beseni lake lenye matunda kichwani, lakini leo hii
anaingiza shilingi bilioni 20 kwa mwaka.
Ukisimangwa
leo ni njia ya kunyenyekewa kesho; Muone Roman Abramovich. Mtoto wa kimaskini, mama
yake alipata mimba nyingine wakati Abramovich akiwa mtoto mchanga.
Kutokana
hali duni, na ugumu wa kumlea Abramovich, aliona mzigo utakuwa mzito, akafanya
jaribio la kuitoa mimba hiyo. Maskini ya Mungu, hiyo ikawa sababu ya mama yake
Abramovich kufariki dunia.
Abramovich
alilelewa na bibi yake. Alinyanyaswa kwa umaskini wao, akasemwa kwa kifo cha
mama yake wakati wa kutoa mimba, akasimangwa na wenye vyao.
Baadaye alikuwa
mmachinga, akijihusisha na uuzaji wa midoli ya kuchezea watoto. Ila sasa ni
bilionea wa kuogopwa ulimwenguni. Ndiye mmiliki wa Klabu ya Chelsea, akiajiri
makocha, anawalipa fedha nyingi na kuwafukuza. Anasajili wachezaji nyota kwa
malipo makubwa. Ameigeuza Chelsea kutoka klabu hohehahe mpaka kuwa tishio Ulaya
na duniani kote.
Kisasi ni
roho mchafu na ni kifo; Yupo rafiki yetu alibahatika kupata mabilioni ya
shilingi kwa ujanjaujanja katika machimbo ya Tanzanite, Mirerani. Alipata awamu
ya kwanza akatumia zikaisha, akapata awamu ya pili, nazo siyo tu kwamba hazipo
tena, bali na yeye mwenyewe yupo kaburini.
Ndugu yetu
huyo alisema analipa kisasi kwa sababu alinyanyasika mno wakati wake wa
umaskini. Eti, wanawake walikuwa hawamtaki kwa ubaya wa sura yake pamoja na
umaskini aliokuwa nao.
Kwa hiyo alitembea
na wake za watu, alivunja ndoa nyingi, aliharibu uchumba wa wengi, maana
aliishi na wapambe kwa ajili ya kumtafutia wanawake. Kila mwanamke alimtaka
yeye. Wanawake wote waliowahi kumkataa wakati wake wa umaskini, alihakikisha
anawapata kwa jeuri ya fedha.
Ndugu yetu
aliishi hotelini. Hakukumbuka hata kubadili hali ya maisha ya nyumbani kwao. Na
kwa hakika alifanya vurugu. Fedha zilipoisha na afya yake ilidhoofu. Alijaribu
kwenda Ulaya ili afiche aibu lakini alirudishwa akiwa taabani. Mauti yalimkuta
akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Unakata
tamaa kwa maneno ya walimwengu? Unaona maisha magumu kama vile dunia umeibeba
begani? Nikupe siri; Almasi ni madini yenye thamani mno, lakini hukandamizwa na
uzito mkubwa zinapokuwa chini ya milima.
Almasi
ikishatolewa chini ya mlima, hutamaniwa na kila mmoja. Wewe pia ni almasi.
Dunia ni nzito lakini jitahidi, ukishaitua, dunia itakubeba kisha utatamaniwa
na kila mtu mithili ya almasi yenyewe.
Mandela,
Mahathir, Natalia na Abramovich ni almasi, wao pia walikuwa chini
wakikandamizwa na milima lakini baadaye walichomoka kisha dunia ikawabeba.
Wakawa tamanio kila mmoja kwa daraja lake, kiutawala, kifedha na kiurembo.
Nakusihi tena acha kulia.
Mwanariadha
bingwa, Usain Bolt alipata kuandika kwenye akaunti yake ya Twitter: “One day,
the people that didn’t believe in you, will tell everyone how they met you.”
Kiswahili;
Siku moja wale ambao hawakukuamini, watamwambia kila mtu jinsi ulivyokutana
nao.
Tafsiri pana
ni kuwa waache wenye kukudharau na hata kukuwekea kauzibe kwenye maisha yako ya
kazi. Wala usishindane nao, maana utafika wakati wao ndiyo watakuwa mstari wa
mbele kusimulia wanavyokujua na mahali ulipotoka.
Chukua hii;
Matumizi mabaya ya muda ni kuusotesha ubongo wako kufikiria magumu ya maisha na
kejeli za walimwengu, badala ya kupiga hesabu makini za namna bora ya kubadili
kibao cha maisha, kutoka dhiki za kila siku mpaka faraja na neema.
Tambua kuwa
maisha ya binadamu yana mengi katikati yake. Zipo kumbukumbu nyingi za kuumiza,
zipo pia za kufurahisha. Ni kosa kubwa kwa kesho yako, endapo utaruhusu
kumbukumbu za maumivu ziteke hatma yako.
Umetendewa
jambo baya, umeumia, sema “asante Mungu”, unachotakiwa kufanya ni kuelewa kuwa
kwa vile bado upo hai basi unalo jukumu la kufanya. Maumivu yote weka pembeni.
Ni ukweli
kuwa huwa vigumu kusahau unapotendwa mambo mabaya lakini hiyo isikutawale.
Amini kuwa ni mapito kisha mwenyewe jisemee moyoni: “Nyakati zijazo zina neema
kubwa!”
Asante.
Ndimi Luqman
Maloto
0 comments :
Post a Comment