ads 728x90 B

Mapenzi ni fursa, mheshimu, mlinde uliyenaye




Na Luqman Maloto
Awali kabisa wakati unasoma mada hii, nakuomba uitafakari glasi. Fanya tafakuri ya ndani ya kabisa. Utaweza kugundua kuwa thamani yake ni ikiwa nzima, ikishavunjika ndiyo basi tena. Hutaweza kuirejesha katika hali yake hata ufanye nini.
Vivyo hivyo katika mapenzi. Ni bora ukiwa nayo, ukishayachezea na kutoweka ni vigumu sana kuyarejesha. Wapo wanaojuta kwa kuwapoteza watu waliowapenda kwa moyo msafi kabisa lakini Shetani alipochezea vichwa vyao, kila kitu kikageuka historia.
Pengine hawajuti leo lakini walijuta huko nyuma. Wapo ambao walizeeka na kumbukumbu mbaya katika maisha yao. Wakijilaumu kwa ujinga au uzembe waliofanya na kusababisha wapenzi wao kuondoka. Hapo ndipo kwenye swali, kwa nini ujute baadaye?
Ni ukweli ulio wazi kuwa huna sababu ya kujuta, badala yake unachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wako leo. Siku zote ni lazima ukumbuke kuwa mapenzi uliyonayo au unayopata kutoka kwa mwenzi wako hivi sasa, yanaweza kuendelea au kukoma kutokana na uhusika wako.
Janga kuu ambalo limeendelea kusumbua ni kuwa mtu akiwa nacho anaweza kukifuja utadhani hakitaondoka. Ni kosa kubwa kushindwa kumtunza mwenzi wako kwa kiburi tu kuwa kwako ameshafika na hataondoka. Usicheze na moyo wa mwenzio. Usifanye majaribio ya kujuta baadaye.
Kufanya jambo lolote la maudhi kwa mwenzi wako kwa makusudi ni jaribio la wewe kujuta baadaye. Unayemuudhi ni binadamu, ana moyo kama ulionao wewe. Siku atakapofanya uamuzi ambao anaona unafaa, itakuwa ndiyo mwanzo wa majuto yako. Majuto ni mjukuu!
UCHAMBUZI KATIKA MAANA PANA
Unapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, lengo la juu kabisa la kwako wewe, linatakiwa liwe kumfanya mwenzi wako afurahi kuwa nawe, vilevile na yeye awe na msukumo unaofanana na huo wa kuhakikisha unafurahia mapenzi yenu siku zote.
Kama kila mmoja ataweka nia hiyo na kuitekeleza kwa vitendo, hapo ndipo unapoweza kuona kitu kinachoitwa ‘malavidavi’ au kwa swaga za mapenzi tunaita mahabati. Ikiwa ni kielelezo kuwa wahusika wa uhusiano wanakuwa kwenye kiwango kizuri sana cha kufurahia ‘kapo’ yao.
Tatizo kubwa hutokea pale ambapo wahusika kwenye uhusiano wanakuwa wanapishana mitazamo au uamuzi. Unajua kabisa hilo unalolifanya litamuudhi mwenzi wako lakini unakosa hofu, unatenda tu. Siku akisema “nakwenda” ndipo unashtuka na kudondosha machozi.
Ni kama unavyoelewa kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kufurahia mwenzi wake kusaliti. Unavaa ujasiri na kuanzisha uhusiano wa pembeni. Anapobaini hilo na kuondoka zake, unapiga magoti kumzuia asichukue uamuzi huo. Akiondoka unabaki kujutia ulichomfanyia.
Swali; Je, ulipokuwa unafanya mambo ambayo uliamini yatamuudhi, akili zako hazikuwa timamu? Ukishapata jibu, basi likupe muongozo kuwa mapenzi hayachezewi kwa sababu moyo wa binadamu siyo mwanasesere. Akishaakisi maumivu ya kutendwa hisia za kupenda hubadilika kuwa chuki.
Kuiweka hoja hii katika maana inayokubalika ni kuwa mtu anayekupenda leo, anayekuita majina mengi mazuri hivi sasa, anayetamani kukuona kila dakika, ni huyohuyo ambaye ukishamkera mpaka mwisho ataanza kukuchukia, asitamani kukuona na kukubatiza majina ya ovyo kabisa.
Kwa nini jana alikuita “sweetheart, mpenzi, asali wa moyo, darling” na mengineyo, iweje baadaye akuite “malaya, fuska, kahaba, kicheche, gumegume au gubegube?” Jibu ni kwa faida yako kuwa kizuri leo ni lazima kitunzwe, kikigeuka taswira yake ni mbaya kupita kiasi.
Yapo mengi ambayo husababisha mapenzi kufa! Unaonywa kuacha vitu vibaya ambavyo hata wewe mwenyewe unakiri kuwa havifai. Shetani anatuama kwenye kichwa chako, unashindwa kubadilika na kurejea mstarini. Hii ni wazi kwamba matokeo ya kuachana uliyatengeneza mwenyewe.
Hapendi ziara za usiku zisizo na faida wala tija. Mnazungumza leo, kesho unarejea yaleyale. Siku zinapita anakusamehe lakini hujirekebishi. Hii ni dunia, anapokutana na mtu ambaye anamuonesha kwamba hatakuwa na shughuli nyingi za usiku, lazima atamkimbilia.
Shika kile kinachomfaa mwenzi wako, nafasi ya kuhakikisha utamu wa mapenzi ambao mnauogelea sasa ni yako mwenyewe. Yakipaliliwa, kuwekewa mbolea na kumwagiliwa, lazima yatamea na kustawi. Yakitazamwa bila matunzo yoyote husinyaa.
Ikitokea unapanda mbegu wakati zinaanza kuchipua wewe lile shamba unaligeuza uwanja wa kuchezea mpira, unakanyagakanyaga, ile mimea itakufa, kwa hiyo na ile mbegu nzuri ambayo uliipanda nayo itapotea. Huo ndiyo mfano halisi wa mapenzi.
Ina maana kuwa pengine unaweza kuanza vizuri sana katika uhusiano wako, kile ambacho ulikiingiza kwa mwenzi wako ni mbegu nzuri sana. Ulipofika muda wa kuweka mbolea na kufanya umwagiliaji ili kile kilichopandwa kichipue na kustawi, mambo yanageuka kabisa.
Vitendo vyako vinakuwa sawa na yule anayekanyagakanyaga shamba lake aliyelilima na kupanda mbegu iliyo bora. Usifanye hivyo, maana kila kibaya unachomtendea mwenzi wako leo, tambua kinamuumiza sana. Kuna faida gani kwako kumfanya mwenzi wako ateseke?
Je, mateso yake wewe yanakupa ahueni ipi? Kwa walio kwenye mapenzi ya dhati ni kwamba mwenzi wako anapoteseka, na wewe pia unakuwa kwenye mateso makali. Maana furaha yake ni yako, maumivu yake yanakugusa pia. Vivyo hivyo kilichopo kwako naye kinamhusu kwa tafsiri pana.
Juu ya hapo ni kuwa hisia za maumivu katika mapenzi zina kawaida ya kuhama kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Unamtesa sana, siku akichukua uamuzi wa kusema “mwana kwenu kwa heri”, hapo ndipo unashtuka, eti huamini kinachotokea.
Maombi ya msamaha kutoka kwako kwenda kwake yanakuwa kwa unyenyekevu wa hali ya juu sana. Kwa nini mfike huko? Akili yako itumikishe kufanya uamuzi sahihi ambao ni kumtunza mwenzi wako ambaye anakutunza hivi sasa. Maudhi ya hapa na pale jiepushe nayo.
Mdharau mwiba guu huota tende! Usione anachokilalamikia mwenzi wako ni kidogo, mfanye afurahie uwepo wako kila siku. Usimruhusu akulilie, maana ipo siku utalia wewe. Hakikisha hatoi machozi ya maumivu, isipokuwa yawe ya furaha. Kinyume chake kuna siku yatakugeuka.
SOMA KWA MFANO
Kuna uhusiano wa Hawa na Matali, vilevile Gaudensia na Reina. Kila mmoja una soma lake. Hawa alimchezea sana Matali ambaye alipoona yamezidi aliondoka. Reina naye alijiona kidume, akamtenda sana Gaudensia aliyeona mazito, akatimka. Baadaye kila mtenda alilia kwa kusaga meno.
Kabla sijaenda zaidi kudadavua mifano hiyo, nieleze tu kwa kifupi kwamba tamaa na fedha ni sababu kuu ya majuto. Mwanamke au mwanaume, anaweza kudharau heshima na mapenzi anayopewa na mwenzi wake kwa sababu ya fedha au ‘upofu’ wa kudhani aliye mbele yake ana mvuto zaidi.
Ni shida! Mwenzi wako upo naye siku zote lakini macho yanakudanganya kwamba uliyekutana naye barabarani au katika mkusanyiko mwingine wowote ni mzuri kuliko mpenzi wako. Akili yako inaamini hivyo, matokeo yake unafanya uamuzi ambao baadaye unaujutia.
Mapenzi yana tabia ya kisasi, utakaposoma mifano ya Gaudensia na Reina, vilevile Hawa na Matali, utaelewa hili katika sura pana. Siku zote za maisha yako, jitahidi kubaki njia kuu. Uliyenaye ndiye mwenzi wako, umetoka naye mbali, kwa hiyo mpende na kumheshimu, achana tamaa zisizo na kichwa wala miguu.
Ni kweli ana mvuto lakini kabla ya hajakutana na wewe, ameshavutia wangapi? Je, unadhani aliyekuwa naye kwa nini aliinua mikono na kumwacha aende? Ikiwa yeye ndiye katendwa, ameshaumizwa mara ngapi? Kwa nini yeye? Unadhani nafasi yako inatosha kumfanya awe na furaha?
Utaingia kwake kwa kuona ana mvuto unaosuuza moyo wako, kumbe mwenzio ni mkali wa kuwapanga, hajui kukataa mtu! Siku za baadaye unakuja kugundua mpo kama sita lakini mwenyewe anajua jinsi ya kucheza karata zake, kwa hiyo hukuwahi kulijua hilo kabla.
Umeona pesa zake ni bora kuliko penzi safi na salama unalopata kutoka kwa mwenzi wako. Miezi miwili baadaye unajikuta upo kwenye kundi la wengine wengi ambao wanamtazama mtu mmoja kwa sababu ya fedha zake. Tayari unajigundua kwamba uliyenaye si wa uhakika, hana mapenzi, isipokuwa jeuri ya fedha inamuongoza kufanya uamuzi.
Labda ni fedha zako ndizo zinakufanya uwe na kiburi, unaamua kumtenda anayekupenda kwa dhati kwa hisia kuwa fedha ndiyo kila kitu. Hao wanaovutika na wewe, hawaji kwa upendo wenye mguso wa moyoni, wanavutiwa na noti zako. Unaweza usifilisike lakini kama hali ipo hivyo, siku ukiumwa itakuwaje?
Unahitaji mwenzi wako ambaye utamuona ndiye wako wa kufa na kuzikana. Anayekupenda kwa dhati, hatakukimbia ukiwa huna fedha au ukisumbuliwa na maradhi. Atahangaika na wewe mpaka mwisho. Nilishaandika uhusiano wa marehemu Sajuki na Wastara, waliishi vizuri nyakati ngumu za kusaka mafanikio, wakala matunda pamoja na katika majanga walishirikiana pamoja.
Hivyo ndivyo mapenzi yanataka, siyo kurukaruka kama kunguru. Na kila eneo ambalo nimeligusia hapo juu, huwa na matokeo ya kuumiza sana kwa aliyetenda. Karibu kila mmoja hapo hutamani kurejea kwa mwenzi wake aliyemfanyia ndivyo sivyo. Sasa hapo ndipo kwenye swali, kwa nini ujute baadaye?
WASOME REINA NA GAUDENSIA
Walianza uhusiano wao wakiwa chuo! Wote walikuwa wanasoma Chuo cha Uhasibu, Kurasini, Dar es Salaam ngazi ya diploma. Baada ya kuhitimu kiwango hicho cha elimu, waliamua kufunga ndoa kabla ya mambo mengine yoyote. Kwa bahati nzuri, wazazi wa Reina walikuwa na uwezo mkubwa kifedha.
Walimhakikishia mtoto wao kuwa watampa sapoti yote na maisha yao yasingeyumba! Ndoa ikafungwa, wazazi wa Reina waliwazawadia gari la kutembelea, nyumba na maduka mawili, moja la vifaa vya ujenzi la pili lilikuwa la kuuza vyakula kwa jumla. Maisha yanataka nini?
Miezi miwili baada ya ndoa yao, Reina akabadilika kwa kiwango kikubwa sana. Kuna maneno ambayo hapo kabla hakuwahi kumtamkia Gaudensia lakini kipindi hicho aliyatamka. Mwanzoni Gaudensia aliyaona kama majaribu ya ndani ya ndoa lakini siku zilivyozidi kwenda hali ikawa mbaya sana.
Siku za mwanzoni, walikubaliana Reina awe anasimamia mauzo ya duka la ujenzi na Gaudensia duka la vyakula lakini miezi miwili baadaye, ilibidi maduka yote awe na anasimamia Gaudensia kwa sababu Reina hakuwa na muda. Alitoka asubuhi pwee kwenda kujumuika na wanawake wa mjini na alirejea nyumbani alfajiri akiwa amelewa na siku nyingine hakurudi kabisa.
Gaudensia alivumilia, wakati mwingine alijitahidi kuzungumza na mume wake ili abadilike lakini haikuwezekana. Reina alimpiga marufuku Gaudensia kutumia gari walilopewa na wazazi wake. Zaidi ya hapo akawa anachukua fedha bila utaratibu kwenye maduka yote, Gaudensia akihoji anajibiwa: “Tulia hizi mali ni zangu, nimepewa na wazazi wangu, hukutoka nazo kwenu.”
Baada ya kuona manyanyaso yamezidi, huku mali walizopewa na wazazi wa Reina zikizidi kupukutika, Gaudensia akaona isiwe tabu, akaamua kwenda chuo angalau apate shahada ya kwanza. Alikwenda Udom, hali ambayo ikamfanya awe mbali na mumewe.
Huku nyuma akawa anapata taarifa za mume wake kuingiza wanawake mpaka kwenye chumba chao cha kulala. Alivumilia kwa kuhisi kwamba pengine angeweza kubadilika baadaye. Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti kabisa. Akiwa chuoni akasikia taarifa kuwa maduka yote yamefilika.
Aliumia sana ila hakujua afanye nini. Alipowalalamikia wazazi wa Reina, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kusikiliza na kukaa kimya. Maisha yalizidi kupiga hatua kwa kasi ya ajabu, kila likizo alirejea nyumbani lakini mapenzi kwa mumewe hakupata kabisa.
Reina alirejea nyumbani usiku wa manane akiwa amelewa. Kipindi hicho maduka yamefilisika na hana fedha kabisa, kwa hiyo akawa kazi yake kwenda kwa wazazi wake kupiga mizinga ndipo maisha yanakwenda. Hali ilikuwa mbaya sana.
Miezi kisha mwaka ulikatika, ukafuata wa pili baadaye wa tatu, mwisho akafanikiwa kumaliza shahada yake ya kwanza ya uhasibu. Ni kipindi ambacho Reina naye alifanikiwa kupata kazi kwenye kampuni ya Tanzanite One, Arusha kama mhasibu msaidizi, mambo yake yakawa supa upande wake.
Taarifa za Reina kupata kazi, Gaudensia alizipokea kwa furaha sana, akampigia simu kumpongeza lakini alipata majibu ya kukatisha tamaa lakini hakujali sana. Maana alipompigia simu kumpongeza, Reina alijibu: “Sasa pongezi za nini na inakuhusu nini, kazi nimepata kwa ujanja wangu,”
Gaudensia aliendelea na utaratibu wake wa kila siku, kila asubuhi ilikuwa lazima ampigie simu kumsalimia, mchana kumjulia hali na usiku kumtakia usiku mwema. Reina alipogoma kupokea, yeye alimtumia SMS na mambo yalikwenda.
Baada ya kumaliza chuo na kurejea Dar es Salaam, hakumaliza siku tatu, aliunganisha Arusha kwenda kuungana na mume wake. Kule palikuwa na hali mbaya sana. Gaudensia alipoingia ndani kitu cha kwanza cha kumuumiza kilikuwa ni kukuta boksi la kondomu, na alipotazama kapu la uchafu (dustbin) chumbani, alikuta kondomu zilizotumika.
Akamuuliza mumewe kuhusu uwepo wa kondomu hizo, akajibu: “Ulitaka nitembee nao bila kinga?”
Gaudensia: “Reina hebu onesha heshima kwangu, mimi ni mkeo wa ndoa, unanijibu unavyojisikia kweli, hiyo ni tabia gani?”
Reina: “Tatizo wewe mwanamke una gubu sana, badala ya kunipongeza kwa kuwa mwangalifu, wewe unanisema kukuta kondomu. Hizi nimeziacha makusudi ili uone jinsi ninavyojilinda.”
Gaudensia: “Kwa hiyo umeacha makusudi ili kunithibitishia kuwa ulikuwa ukitembea na wanawake ovyoovyo?”
 Reina: “Siyo kutembea ovyoovyo, kwani wewe ulitegemea muda huo wote ningekuwa bila mwanamke? Acha utani kabisa, hata wewe kule Dodoma mimi nitajuaje kama siku zote hukuwa na wanaume? Tena nyie wanafunzi wa Udom kwa wabunge ndiyo zenu.”
Huku akitokwa na machozi, Gaudensia alisema: “Basi baba, naona umeanza kunitukana, lakini angalia Reina mume wangu, hii ni ndoa, ilifungwa kwa tamko la jina la Mungu. Unavyoichezea, itakudhuru.”
Baada ya kuzungumza hivyo, Gaudensia alianza kufanya usafi kwa kuchukua kondomu zote, zile zilizotumika na ambazo hazikuwa zimetumika kisha akaenda kuzichoma moto. Hata hivyo, maisha hayakuwa na amani kabisa, vitimbi viliendelea kuchukua nafasi.
Kuna wakati Gaudensia alipigiwa simu na wanawake wa Reina kumtukana lakini hakuwajibu, alinyamaza na hata mume wake aliporejea nyumbani wala hakumuuliza. Alichojali yeye ni kujenga ndoa ya yake, aliamini upo wakati mume wake atabadilika na maisha yatakuwa mazuri.
Uvumilivu wake ulifika ukingoni siku moja baada ya kukuta karatasi kwenye suruali ya mume wake alipokuwa anafua nguo. Ile karatasi ilikuwa imeandikwa “WANAWAKE AMBAO NIMESHAWADUU”. Gaudensi akashtuka, akahesabu majina na kukuta yapo 71.
Gaudensia akagundua kuwa miongoni mwa wanawake hao, wapo marafiki zake wawili ambao alisoma nao nao Chuo cha Uhasibu, Kurasini, Dar es Salaam. Kwenye orodha hiyo kulikuwa na wahudumu wa baa na machangudoa. Ilimuuma sana.
Reina aliporudi nyumbani, ilikuwa usiku wa manane, kwa hiyo akamuacha alale, asubuhi alipoamka akamuonesha ile karatasi na kumuuliza sababu ya kuandika na kuihifadhi. Bila kutarajia, Reina aligeuka mbogo. Alimkaripia kwa kumchunguza kisha akaanza kumpiga.
Alimpiga na kumuumiza vibaya, baadaye alizimia. Reina bila kujali kama mkewe hana fahamu, aliita gari na kuchukua kila kitu, aliamua kuhama nyumba. Hata hivyo, mmoja wa vijana waliokuwa wanabeba vitu, aliingiwa na huruma, kwa hiyo baada ya kushusha vitu, alikwenda kituo cha polisi kutoa taarifa.
Polisi walifika pale chumbani na kumkuta Gaudensia bado hana fahamu, walimbeba mpaka Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mt. Meru ambako alihudumiwa na kurejewa na fahamu. Polisi walimtia nguvuni Reina lakini baada ya Gaudensia kupona, alikana kupigwa na Reina.
Hakutaka mume wake aingie kwenye matatizo. Pamoja na imani hiyo lakini Reina hakumjali na alimpiga marufuku kufika nyumbani kwake alipohamia na alikataa kabisa kumuelekeza. Ilimuuma sana Gaudensia, aliomba japo nauli ya kurudi Dar kwa wazazi wake lakini alinyimwa.
Ilibidi Gaudensia ampigie simu mama yake na alipomsimulia mateso aliyonayo, haraka sana alimkatia tiketi ya ndege na ile anafika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, mama yake alimwambia: “Mwanangu ni sawa kuvumilia lakini umetukosea sana, uvumilivu wako ni kama vile huna kwenu, kwa nini mwanaume akunyanyase kwa kiwango hicho na wewe uwe kimya?”
Dunia ina kawaida ya kurejesha majibu haraka, miezi sita baada ya Gaudensia kutimuliwa na Reina, tayari alikuwa ameshapata kazi nzuri katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), tayari alishajijenga sawasawa, akanunua kiwanja akiwa na ndoto za kujenga nyumba ndani ya miezi 10 inayofuata.
Reina alishafukuzwa kazi wakati huo, mambo yalishaharibika, wazazi wake hawakutaka kumuona. Mtaani alionekana kama kibaka kwa jinsi alivyochakaa. Maisha yalimdanganya, akarudi kwa Gaudensia kuomba msamaha. Kipindi hicho Gaudensia anaendesha gari lake aina ya Toyota Land Cruiser Prado milango mitatu.
Swali ni hili; Haya majuto ya Reina ya nini wakati alikuwa na nafasi ya kufanya uhusiano wake na Gaudensia uwe bora? Usimfanyie vitimbi mpenzi wako leo, maana hujui kesho yako ipo vipi. Majuto ya baadaye hayafai kabisa.
Niongeze hapo kwa kunukuu msemo wa Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela ambaye ni mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, aliye pia Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, John Samuel Malecela, aliyewahi kusema: “Ukimuacha mke unamuongezea PHD.”
Alimaanisha kuwa endapo utamfanyia vitimbi mwanamke wako kisha ukamtelekeza au kumwacha, usije ukadhani ndiyo utakuwa umemharibia maisha, badala yake ikae akili kwamba ukimfanyia hivyo unakuwa umemuongezea akili ya ziada. Usije ukashangaa baadaye ukikutana naye akiwa na maisha bora zaidi.
Hivyo ndivyo ilitokea kwa Gaudensia, akili yake ilifanya kazi zaidi baada ya kuachwa na Reina. Matokeo yakawa kinyume kabisa. Reina akawa anachunga muda wa Gaudensia kurudi nyumbani kwake kisha anakwenda kujibanza getini kuomba msamaha.
Kwa nini ujute baadaye? Tumia vizuri fursa iliyopo sasa. Ikiwa ipo wazi kuwa mpenzi wako anakuheshimu na anakupenda, linda heshima hiyo kwa kutomfanyia mambo ya ajabuajabu, kwani gharama yake ni kubwa sana pale mambo yanapogeuka kama ambavyo ilimgharimu Reina.
WASOME HAWA NA MATALI
Matali alikuwa mwenye upendo mkubwa sana na Hawa. Alijitahidi kumpa huduma zote muhimu. Hisia zake zilikuwa wazi mno. Hawa hakugundua hilo mapema, matokeo yake ule upendo wa Matali aliugeuza fimbo. Alimtenda sana kiasi ambacho kuna wakati Matali alipoteza kabisa furaha ya maisha.
Hawa kwa kiburi tu kwamba Matali anampenda sana, kwa hiyo hawezi kumwacha, alimfanyia vitimbi vingi. Kwa mfano; Matali alimpigia simu Hawa ambaye kwa kujisikia tu hakupokea. Alipomtumia SMS nazo hazikupata majibu. Hawa aliamua tu kumfanyia Matali vibweka.
Hakuishia hapo, Hawa akaanzisha uhusiano wa pembeni na wanaume wengine. Matali apoona mambo magumu, ikabidi aachie ngazi. Mwanzoni Hawa hakujutia, aliona sawa kwamba amepewa nafasi ya kutanua na aina ya wanaume anaowataka.
“Sitaki mwanaume mzembemzembe mimi, nataka mwanaume aliye ‘fiti’ kimazoezi, mwenye ‘six-pack’ ambaye tukiwa hata ufukweni, akikaa kifua wazi analipa,” yalikuwa ni maneno ya Hawa akisema mwanaume anayemtaka si aina ya Matali.
Hawa akawa anajiachia na wanaume wenye six-pack. Miaka miwili baadaye akashtuka kukuta Matali yupo mbali sana kiuchumi. Kampuni yake ilishapata mafanikio makubwa. Hawa aligundua hayo wakati ambao wanaume aliowataka walishampa maumuvi makali.
Baada ya kuhangaika na dunia kwa muda mrefu, mapenzi yakiwa sawa na msumari wa moto moyoni mwake, akili ilikaa sawa, akaona atafute kazi ambayo itampa kipato cha kusogeza maisha yake mbele. Hakuna mwanaume mwenye six-pack hata mmoja aliyemsaidia chochote katika maisha yake.
Dunia ilimwendea mrama, siku moja akasikia tangazo la nafasi za kazi redioni. Alichukua anwani, akaandika barua, alipoitwa kwenye usaili ndipo akagundua hiyo kampuni aliyokwenda kuomba kazi, mmiliki wake ni Matali, mwanaume ambaye alimpa mapenzi yote yeye akayapuuza.
“Ujinga wangu wa kudanganywa na dunia umenikosesha mengi, leo nakuja kuomba kazi niwe mtumishi wa kawaida, wakati kumbe ningemheshimu Matali na kuyatunza mapenzi yake, leo hii ningekuwa first lady wa hii kampuni yake,” aliwaza Hawa.
Baada ya kutoka kwenye chumba cha usaili, aliomba kumuona Matali. Katibu muhtasi alimjibu yupo ‘bize’ sana. Hata hivyo, wakati anageuka aondoke Matali alitoka ofisini kwake akiwa kwenye mwendo kasi, alipita anamuaga katibu muhtasi wake, akamwambia anakwenda kwenye mkutano ofisi ya uwekezaji, atarejea saa 9:30 alasiri.
 Hawa pamoja na kumuona Matali yupo mbiombio, hakutaka kumpa nafasi, akamzuia mlangoni, akamwambia: “Please Matali, naomba unisikilize japo kwa dakika moja.”
Matali akamjibu: “Ooh Hawa, sikujua kama ni wewe. Ila kwa muda huu siwezi kabisa, njoo kesho saa 3:00 asubuhi  tutatongea au ukiweza, urudi baadaye saa 11:00 jioni.” Baada ya kumjibu hivyo,  Matali alimuunganisha Hawa na katibu muhtasi wake.
Hawa hakutaka kwenda nyumbani, alizungukazunguka, saa 10:30 alasiri alirejea ofisini kwa Matali. Saa 11:00 alikuwa kwenye kiti anatazamana na Matali. Alipigwa na mshangao kukutana na ofisi nadhifu ambayo ilionesha wazi kuwa inatunzwa kwa gharama kubwa.
Bila aibu, Hawa alishindwa kuvumilia akaanza kuomba msamaha. Alikumbuka mengi kutoka kwa Matali, akakiri kuwa ni mwanaume wa kipekee kwake, aliyekuwa na mapenzi ya kiwango cha juu mno kuwahi kutokea katika maisha yake. Alitamani yote ya nyuma yajirudie.
Ni kipindi ambacho aligundua kumbe Matali ni mwanaume mzuri, ana sura nzuri, umbile la kiume, mrefu. Mwanzoni kwa tamaa za dunia hakuyaona yote. Ni hapo ndipo swali linafuata; Kwa nini Hawa anajuta baadaye wakati alikuwa na fursa pana akaichezea?
HITIMISHO
Mapenzi ni fursa, jaribu kumheshimu na kumlinda uliyenaye. Wengi hutambua uzuri wa wapenzi  wao muda mrefu baada ya kuharibu. Zingatia hisia za mwenzi wako, anapokwambia anakupenda, jaribu kuheshimu. Usithubutu kumtenda maana ukifanya hivyo ni lazima itajirudia kwako baadaye na kujuta.
 Tambua kwamba mpenzi mbaya ni kwa sababu upo naye, akishaondoka halafu ukakutana na wabaya wenyewe, akili itakurejesha kwa yule uliyemchezea kisha utaanza kujuta ila majuto ni mjukuu! Bahati mbaya ni kwamba unaweza kutaka kurudi kwake kipindi ambacho ameshawahiwa na anayemthamini kwelikweli.

Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment