ads 728x90 B

Kama siyo hulka, Boban, Chuji wangemtangulia Samatta




Na Luqman Maloto
NYOTA wa soka  jicho la Watanzania, Mbwana Ally Samatta, ameendelea kuiweka hai furaha ya Watanzania.
Kuanzia tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani, kusajiliwa barani Ulaya kwenye timu ya Koninklijke Racing Club Genk (KRC Genk) ya Ubelgiji na baadaye kuanza vizuri kwa kutikisa nyavu ni mambo yaliyawapa burudani Watanzania.
Februari 28, mwaka huu, Samatta alifunga goli muhimu, lililoiwezesha KRC Genk kupata ushindi wa mabao 3-2 nyumbani dhidi ya vinara Ligi Kuu ya Ubelgiji, Club Brugge KV.
Mambo mswano kabisa! Kila jema ambalo Samatta analifanya ndivyo anavyowatoa kimasomaso Watanzania.
Watanzania waliomba na kutarajia na hakika imekuwa kweli. Hongera sana Mbwana kwa kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Bara la Afrika kisha kupata matunda mema Ulaya.
Tuzo ya Samatta na mafanikio yake kwa jumla, yana maana kubwa kwa mtu yeyote anayehitaji mafanikio. Neno moja tu lina uzito wa kutosha kutoa tafsiri pana ya hatua anazopita mchezaji huyo aliyetokezea Mbagala, Dar es Salaam.
Na neno lenyewe ni nyakati. Naam! Samatta alizitafuta na sasa amefikia wakati wake, ilikuwa lazima ashinde tuzo kisha kupata mafanikio Ulaya ambayo ameanza nayo kwa sababu huu ni wakati wake.
Samatta ilikuwa vigumu mno kwake kushinda tuzo mwaka jana, na kutikisa Ulaya hapo kabla kwa sababu haukuwa wakati wake.
Mwaka jana na mingine michache iliyopita ilikuwa awamu yake ya kutikisa kwenye Klabu ya TP Mazembe ya DRC.
Mwakani anaweza kushinda tuzo nyingine kubwa zaidi, yaani ile ya Mchezaji Bora wa Afrika (tuzo ya jumla) kama itakuwa ni wakati wake. Na anaweza kushinda tena na tena!
Mafanikio ya Samatta yanamaanisha nini? Jawabu moja, attitude! Hicho ni Kiingereza, Kiswahili tunaita hulka.
Wapo wachezaji wengi wamepita nchini, walikuwa na vipaji pamoja na viwango vikubwa kuliko Mbwana lakini hawakuweza kufika popote kwa sababu ya hulka (attitude).
Hulka bora ndiyo nidhamu. Wapo wachezaji wa soka walimaanishwa kutikisa nchini na duniani kwa jumla wakitokea Tanzania, lakini hulka zao ziliwaponza. Madini yao ya ndani ya uwanja, yameishia mchangani! Maskini yao!
Lazima kuheshimu hulka ili kutumia wakati wako vizuri. Na hii ni kwa kila fani, siyo katika soka peke yake.
Mwanamuziki Diamond Platnumz au Nasibu Abdul Juma, anatikisa Afrika kwa sasa akitokea Tanzania, ni kwa sababu hulka yake ilimfanya aufanye wakati wa sasa kuwa mwafaka kwake.
Yeyote anayejituma, na akiwa na hulka njema, anaweza kufanya maajabu yenye kugeuza chupa kuwa almasi.
Na mafanikio ya Samatta na Diamond, yawe fundisho kwa kila mmoja kutambua wakati wake na kuutumia vizuri kufika mbali na kupata mafanikio stahiki.
Wapo wengi hawakutumia vizuri nyakati zao. Alikuwepo fundi Haruna Moshi ‘Boban’, akasajiliwa Gefle IF ya Sweden mwaka 2010. Akatarajiwa kufika mbali. Haikuwa hivyo, alirejea nchini kwa kususa na alipofika Bongo, hakuwa Boban yule tena!
Ameishia wapi Athuman Idd ‘Chuji’? Alikuwa kiungo aliyekamilika kiukweliukweli. Alihitaji nidhamu tu, yaani kuwa na hulka kama za Samatta, hakika dunia nzima ingemwelewa.
Jaribu kuwaza kipaji cha Boban, halafu angeongezewa na nidhamu ya Samatta. Jibu unaweza ukawa unalo ni wapi ambapo leo hii angekuwa.
Mlete Chuji kwenye mawazo yako, kifikirie kile kiwango chake, hapohapo itoshe kukupa jawabu kuwa wacheza soka wa Tanzania walitakiwa kuwa wenyeji wa Ulaya miaka mingi nyuma ila wamekuwa wakiponzwa na hulka zao.
Shika muongozo kuwa juhudi na nidhamu huvuta bahati, kisha bahati ndiyo itakufanya ufike kwenye kipindi chako cha mafanikio. Kwa hiyo hulka inapaswa kuanza kabla ya vyote.
Muongozo ni wewe kujituma na utakapofika kwenye wakati wako, hakikisha unautumia vizuri ili utakapopita, watu waseme “alikuwepo fulani bwana!”
Pambana kwenye eneo lako ili utengeneze wakati wako mzuri. Utakuwa mwenye kupendwa na kuheshimika sana kama utafikia wakati wako na kufanya kile kinachohitajika.
Kila mwanasoka, hususan wale chipukizi, wanalo la kujifunza kupitia kwa Samatta, vilevile wajiongeze kutoka walipokwama akina Boban, Chuji na wengine ambao walikwama njiani kutokana na hulka zao.


Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment