ads 728x90 B

WAFALME NDANI YA NYUMBA ZA MASKINI!




UMEWAHI kujiuliza ni kwa nini Mbwana Samatta siyo mtoto wa Said Salim Bakhressa?
Vipi kuhusu Diamond Platnumz, ni kwa vipi siyo mwana wa Rostam Aziz?
Je, Hasheem Thabeet, si angekuwa mtoto wa Ally Mufuruki?
Mbona Lionel Messi hajawa mtoto wa Bill Gates? Cristiano Ronaldo kuwa mwana wa Warren Buffet, Floyd Mayweather Jr kuwa mtoto pendwa wa Carlos Slim Helu. Ni kwa nini haikuwa?
 Ili maji yafuate mkondo Ronaldo de Lima si angekuwa mtoto wa Mfalme Pele? Galacha wa kikapu, Bill Russell ni kwa nini siyo baba wa Michael Jordan? Au Magic Johnson si ingependeza akawa baba yake LeBron James?
Ukiwa na jawabu ni kwa nini bondia mkali kuwahi kutokea duniani, Joe Louis siyo baba wa Mike Tyson, haitakusumbua leo kuona kuwa Muhammad Ali siyo kizazi cha mbavu nene ulingoni, Jack Johnson.
Mayweather Sr, hakuwa bondia tishio kwa wakati wake lakini ndiye baba wa Mayweather Jr. Vipi Sugar Ray Robinson mbona hakuna aliyemfuata katika masumbwi? Sanasana mwanaye, Ronnie Robinson alijikita zake kwenye mchezo wa roller derby.
Chukua siri hii; Mungu hufanya uteuzi katika mazingira ambayo wengi hawayatarajii. Hata manabii wake, nazungumzia wale wa ukweli, wengi walitoka katika mazingira duni kabisa.
Bikira Maria (Mariam) alikuwa nani mpaka abebe mimba ya Yesu (Isa bin Mariam)? Au Aminah bint Wahb mbona alikuwa wa kawaida tu lakini ndiye mama wa Mtume Muhammad (S.A.W). Mungu huteua anavyotaka!
Mungu amekuwa na utaratibu usiokoma, wa kupandikiza uzao wa matajiri na wafalme katikati ya familia zinazoishi kwenye lindi la umaskini.
Ni kawaida kabisa Mungu kuingiza kipaji kikubwa kwenye familia ya watu wasio na vipaji. Mwanamke anaweza kunasa mimba ya mwanaume mlevi au jambazi lakini mtoto akatoka mchamungu wa mfano. Mungu hupanga!
Angalia familia ya Manara, watu waliokuwa na vipaji pamoja na uwezo mkubwa wa soka, Kassim, Kitwana na Sunday ‘Computer’, mbona hatuoni nyayo za watoto wao?
Justin Bieber ni mwanamuziki tajiri duniani, ila mama yake, Pattie Mallete alikuwa mtumia unga, akawa pia kibaka, baba yake, Jeremy Bieber, alikuwa mlevi kupindukia. Ila walipokutana, ilipatikana mimba, akazaliwa Justin ambaye leo hii ameishika dunia kwa muziki wa Pop.
Kama Pattie Mallette angebeba mimba ya Michael Jackson kwa vile ni Mfalme wa Pop, hakika asingepatikana Justin Bieber. Nina uhakika hili huwezi kubisha hata kidogo, maana Justin ni muunganiko wa kibaiolojia kati ya Jeremy na Pattie.
Watu wengi hutamani kuzaa na watu wenye hadhi ya juu kwa kudhani ndiyo watapata watoto wazuri. Huko ni kujidanganya! Mambumbumbu, makuli, wapigadebe, wasukuma maguta, wamachinga, mama ntiliye na wengine wengi ndiyo huzaa watu wakubwa. Matokeo yameonesha hivyo!
Ni nadra sana kumpata George Bush, Rais wa Marekani kisha na mwanaye (George Bush Jr) kuwa rais wa nchi hiyo baadaye, au Uhuru Kenyatta kuongoza taifa la Kenya ambalo lilikombolewa na baba yake Jomo Kenyatta kutoka kwa Muingereza.
Tawala za kifalme inawezekana kwa sababu ni kurithishana, ila katika nchi zenye uchaguzi wa kidemokrasia ni vigumu.
Na hapo ndipo unajionea mwenyewe kuwa Barack Obama, maskini wa Kijaluo mwenye asili ya Kenya, leo hii ni Rais wa Marekani, tena kwa vipindi viwili. Dk. John Pombe Magufuli, mtu duni kutoka Chato, Geita, kwa sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Usijindangaje kuwa ukizaa na Edibily Lunyamila atapatikana Lunyamila Jr. Au mtoto wa Ali Kiba naye aje aitwe King Kiba Jr. Mr. Nice kumleta mfalme mwingine wa Takeu kutoka kwenye maungo yake, vivyo hivyo kwa akina Muumini Mwinjuma, Ally Choki, Banza Stone, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Joseph Haule ‘Prof. Jay’. Ni mpaka Mungu apange!
Haikuhitajika muunganiko wa damu ya Mwalimu Julius Nyerere kumpata Zitto Kabwe au Oscar Kambona ili azaliwe Edward Lowassa, Kwamba Halima Mdee atokee kwenye kizazi cha Bibi Titi Mohamed au Mashavu bint Kabonge ndiye amzae Anne Kilango Malecela, vivyo hivyo Ester Bulaya awe mjukuu wa Tatu Mzee. Vipi Ummy Mwalimu kuwa damu ya Binti Kipara? Mungu hateui hivyo!
Hii ndiyo sababu Sir Isaac Newton, yatima ambaye hata hakumuona baba, akakosa malezi ya mama ambaye alichukuliwa na mwanaume, yeye akiwa bado mchanga, akabaki kulelewa na bibi, lakini ndiye mwanahisabati na sayansi ambaye atakumbukwa nyakati zote kutokana na uvumbuzi wake.
Mtazame Aristotle, mtu aliyekuwa na kichwa cha ajabu mno ambaye atakumbukwa na vizazi vyote! Lakini ni mtoto wa mtumishi wa mfalme. Bila shaka mfalme angetamani kupata mtoto kama Aristotle lakini Mungu hakumpa.   
Hakuna aliyewahi kujichagulia wazazi, unajikuta tu ndani ya familia ya kimaskini kama ambavyo mtoto wa Bill Gates alishtukia yupo ndani ya familia yenye baba na mama wote matajiri. Ndivyo ilivyo kwa watoto wa marais, viongozi wakubwa, maskini wa kutupwa na kadhalika.
Kuzaliwa maskini siyo laana wala kituko. Mjinga pekee ndiye anaweza kumcheka mtoto aliyezaliwa kwenye familia ya kimaskini. Tangu enzi, Mungu amekuwa na utaratibu wa kupandikiza watu wakubwa, matajiri, viongozi wenye heshima na hata wafalme ndani ya nyumba za maskini.
Abraham Lincoln alizaliwa maskini, aliishi kimaskini akizingirwa na hali duni mno, mwisho akawa Rais wa Marekani baada ya kutokata tamaa. Mtoto wa Lincoln akaitwa mwana wa rais, lakini hakuweza kuyakamata masafa ambayo baba yake alisafiri.
Musa alizaliwa kwenye familia hohehahe lakini ndiye aliyemaliza jeuri ya Firauni. Watu wengi mashuhuri ulimwenguni, walitoka kwenye familia duni lakini wakapambana na kupenya katikati ya ‘wakubwa’, wakaketi meza moja kabla ya kuanza kuongoza msafara. Ni mara nyingi tu watwana wamegeuka mabwana!
Tafakari kidogo kuhusu namna Nelson Mandela alivyoilazimisha dunia kumnyenyekea na kumtukuza wakati mwanzoni walimwita gaidi. Ni Mandela mmoja tu duniani, hakuna mwanaye wala mjukuu wake kama yeye.
Ndivyo ilivyo kwa Oprah Winfrey! Nani wa kumcheka leo? Ana kila kitu ambacho kila mwanamke anapenda awe nacho. Amefikia mafanikio ambayo binadamu wote wangependa kuyafikia. Waliomcheka siku za nyuma, wanatamani siku zirudi nyuma waanze kumheshimu na kumnyenyekea tangu akiwa amevaa magunia yake.
‘Akili-kushindwa’ wanaishia tu kusema: “Usimuone vile Oprah, alikuwa anavaa magunia ya kubebea viazi, tulikuwa tunamcheka!” Shombo ya jana ni historia kama aliyekuwa ananuka, alipata sabuni na kuoga. Ni kituko kama siyo kichekesho kusema fulani alikuwa ananuka, wakati ni nadhifu na ananukia leo.
Iwe kuongea kwa kujifariji, kuponda au kumpongeza, ukweli unabaki palepale kuwa Oprah wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumnunulia nguo, wakawa wanaungaunga magunia ya kubebea viazi, wakayatengeneza kama nguo za kumvisha binti yao.
Leo hii anabadili nguo anavyotaka. Yale maduka wanayoingia viongozi wakubwa wa Marekani na dunia pamoja na matajiri wanaoheshimika ulimwenguni, ndiyo na yeye anaingia kufanya manunuzi humohumo.
Ishi kwa tabasamu kila siku. Hata uwe ndani ya nyakati ngumu kiasi gani, elewa tu kuwa utavuka. Mungu aliyekuumba anakuona, analo fungu lako bora kabisa.
Jambo la kutambua na kuheshimu ni kuwa Mungu anajua namna ya kukupa mafanikio. Anaweza kukufanikishia ukiwa kijana, wakati wa makamo au hata uzeeni.
Mafanikio yanaweza kuja kwako moja kwa moja (direct) au kupitia mlango wa nyuma (indirect). Ila yote ni mafanikio yako.
Mafanikio mlango wa nyuma; Yale ya kuja moja kwa moja hayahitaji ufafanuzi, kwa upande wa yenye kuja kupitia mlango wa nyuma ni kama vile mzazi kuvuna kupitia kwa mwanaye aliyemzaa na kumlea kwa tabu au hata mtoto aliyemuasili na kumlea.
Hii ikupe muongozo wa kutambua kuwa mtoto ni zawadi. Omba Mungu akuongoze na usibague, maana hujui kuwa pengine huyo unayembagua ndiye mama au baba wa daktari bingwa atakayegundua dawa za Ukimwi, Homa ya Ini (Hepatitis B na C), Kisukari na kadhalika. Mheshimu kila mtu!
Mtoto wako mtunze, mpe malezi bora kadiri Mungu anavyokujalia. Huwezi kujua kuwa pengine huyo ndiye mkombozi wako.
Wewe mtoto, ukizaliwa kwenye familia ya kimaskini, ikuongoze kuchangamsha ubongo. Wewe ndiye shujaa wa familia yako, jitume ubadili hali ya maisha ya wazazi wako na ndugu zako.
Kuzaliwa kwenye familia maskini ni ishara kuwa wewe ni mfalme. Ukipambana na kufanikiwa, unaitwa mfalme. Watoto wa Bakhressa wana fedha lakini siyo wafalme. Wamekuta mteremko wa maisha!
Unabisha? Daud alikuwa na uwezo gani wa kuwa Mfalme wa Israel mbele ya Saul? Daud alikuwa mtu duni kabisa lakini ndiye alimpiga Goliath. Usicheze na Mungu na uteuzi wake!
Zingatio kwa mama; Usitoe mimba, usinyonge kichanga wala usitelekeze mtoto. Huyo anaweza kuwa ndiye ameletwa na Mwenyezi Mungu kuwa mafanikio yako ila wewe unayakataa.
Baba; Usikatae mimba, usiwe chanzo cha mimba kutolewa, usikimbie damu yako, hakikisha unakuwa mlezi bora wa mwanao kwa hali na mali. Huwezi kujua ni zawadi gani ambayo mtoto huyo ametumwa na Mungu akuletee.
Wazazi; Hakikisha mnatoa malezi bora kwa watoto. Kile ambacho mnakifanya, kiwe ndiyo uwezo wa juu kulingana na nafasi. Wapeni watoto mapenzi makubwa na muwafanye wawe na furaha. Hao ni hazina yenu ya baadaye.
Mtoto; Wewe siyo chochote bila wazazi wako. Wangeamua, ungetolewa ukiwa mimba changa. Unapopata mafanikio, elewa kuwa wazazi wako wana thumni yao kwenye kila jasho lako. Wafanye wazazi wako wafurahie kipato chako, usiwaache wakipata shida na wewe upo ilhali uwezo wa kuwasaidia unao.
Mafanikio yako yatapaa zaidi, vilevile utakuwa ni mwenye kubarikiwa mno kama wazazi wako utawalinda kadiri kipato chako kinavyoruhusu.
Nakutakia Ijumaa Kareem.
Ndimi Luqman Maloto
Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment