ads 728x90 B

Ukawa, ACT wanahitaji santuri bora zaidi




Na Luqman Maloto
Serikali ya Rais John Magufuli dhidi ya upinzani, kwa hali ilivyo hivi sasa, hasa Tanzania Bara, ni sawa na msanii maarufu (supastaa) dhidi ya yule ambaye bado anahangaika kupata mafanikio (underground artist).
Hali hiyo ni upinzani na vyama vyao kwa jumla, yaani ACT-Wazalendo, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na vingine vyote.
Kipindi cha utawala wa Rais wa Nne, Dk. Jakaya Kikwete, serikali na upinzani, hususan Ukawa, walikuwa na mvutano mkubwa na walipimwa kwa nani zaidi kama vile klabu za soka za Simba na Yanga.
Kipimo cha upinzani na serikali katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 na 2015, zaidi 2010 kuelekea 2015, ilikuwa sawa na mchuano wa wanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na hasimu wake Ali Kiba. Wafuatiliaji wa muziki wa kizazi kipya wanaelewa minyukano ya wasanii hao.
Kwa kawaida Serikali lazima iwe juu lakini pia upinzani ulikuwa juu mno kipindi cha awamu iliyopita. Na wakati mwingine upinzani ulitengeneza vichwa vya habari katika zile habari kiongozi (lead stories) kwenye magazeti kuliko serikali na Chama Tawala (Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’).
Zipo nyakati wahariri wa magazeti waliambizana: “Habari za upinzani zinauza kuliko za CCM na serikali.” Na kwa sababu ya shabaha ya kulenga soko, ikabidi wapinzani wamulikwe na wapewe nafasi.
Ilikuwa wapinzani wakifanya tukio, na Serikali wakifanya tukio lao, wahariri wanachekecha na kufanya mchezo wa kuchagua kwa kubahatisha, ‘ana anado’, ipi habari kubwa.
Haikuwa na tofauti yoyote na ambavyo Diamond na Ali Kiba wakitoa nyimbo kwa kufuatana, jinsi ambavyo ma-DJ wa redio na televisheni pamoja na watangazaji wanavyochekecha na kuzipima upi bora kuliko mwingine.
Kwa kawaida wimbo wa Diamond, Ali Kiba na nyota yoyote yule anayetambulika, ni rahisi kuchezwa redioni na kwenye televisheni hata kama siyo mzuri kutokana na jina ambalo amekuwa amejitengenezea.
Redio zinaachaje kuucheza wimbo mpya wa mwanamuziki Vanessa Mdee au Barnaba wa THT hata kama siyo mzuri? Wataucheza tu! Baadaye utakaposhindwa kutamba, hayo ni matokeo ya baadaye lakini unakuwa umeshachezwa kutokana na nguvu ya jina la msanii.
Msanii asiyefahamika (underground artist), akitoa wimbo ili uchezwe inabidi afanye kazi hasa. Na wimbo wenyewe uwe na ubora usiotia shaka ili kuwashawishi watangazaji na ma-DJ ambao hawamfahamu kabisa.
Watangazaji na ma-DJ wenyewe wanaangalia wimbo umeimbwa na nani. Hivyo, ili wimbo wa underground uchezwe ni lazima uwe na viwango vya kumshawishi DJ na mtangazaji kuucheza.
Kama siyo kumshawishi DJ au mtangazaji, basi wimbo uwe umepenya kwenye nyoyo za watu ambao wataomba uchezwe. Na kwa sababu redio ni kwa ajili ya msikilizaji, runinga kwa mtazamaji, basi wimbo ukiombwa utachezwa.
Waandishi wa magazeti nao wanajua msanii gani akiandikwa ndipo gazeti linakuwa na heshima. Ili msanii chipukizi apate nafasi ya kuandikwa hapo ni lazima awe anafanya kazi yenye nguvu ya kumshawishi mwandishi husika.
Hali hiyo ya masupastaa wa muziki, imekuwa sawa na siasa za Tanzania kwa wakati huu, hususan Tanzania Bara. Hapa sigusii Zanzibar kabisa!
Ghafla Serikali ya Rais Magufuli imekuwa supastaa (msanii maarufu). Upinzani kwa sasa umekuwa underground (msanii asiyefahamika).
Kila kazi au tukio linalofanywa na serikali yake, linakuwa kivutio cha vyombo vya habari hata kama ni la kawaida tu. Ni sawa na msanii supastaa kutoa wimbo wa kawaida, utapewa kipaumble cha kuchezwa.
Upinzani kwa sasa ili upate nafasi ya kusikika vizuri na kupata kipaumbele kwenye vyombo vya habari, inatakiwa wawe na matukio yenye nguvu kubwa. Ni sawa na msanii underground kutoa wimbo wenye mvuto usiotia shaka.
Kitendo cha upinzani kufanya matukio yenye nguvu ndogo, ni kusababisha Magufuli na serikali yake kuendelea kung’ara katika vyombo vya habari kwa matukio ya kawaida tu.
Hiyo ni sawa na wimbo wa msanii mdogo kutochezwa redioni au runingani kwa sababu ubora wake ni wa kawaida lakini wa supastaa ambao ni wa kawaida unachezwa vizuri kabisa. Umaarufu unalipa!
Alama za nyakati zinafaa kuwasha taa kuwa Serikali ya Magufuli imeweza kupata umaarufu mkubwa tangu kuanza kwake kazi, hivyo ni jicho la kwanza la vyombo vya habari kabla ya upinzani.
Nyakati za sasa zinataka wapinzani wawe wabunifu. Kutazama ni matukio yapi ambayo wakiyafanya yatachukua nafasi pana kwenye vyombo vya habari ili kushindana na matukio ya kawaida ya Serikali ya Dk Magufuli.
Kama uteuzi wa Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Vincent Mashinji ulizidiwa na uteuzi wa wakuu wa mikoa, hapo lazima kutambua ipo kazi inatakiwa kufanyika kwa upinzani, kukabili mvuto wa Serikali ya Magufuli.
Vilevile itakumbukwa kuwa tukio la muundo wa safu mpya ya sekretarieti ya ACT, halikupata nguvu kubwa. Ni vizuri kutambua mapema mahali ambako vitu haviendi kwa unyoofu wake ili marekebisho yafanyike.
Hapa niweke wazi kuwa sina maana kuwa wapinzani hawana jipya ila huu siyo muda wake. Magufuli amekuwa na mtindo mpya ambao umewafanya Watanzania wakumbatie ‘kipya kinyemi’.
Hiki ni kipindi ambacho neno la Dk Magufuli lina nguvu kuliko matukio ya Ukawa na ACT. Ni wakati ambao ukitaka usemwe vibaya au hata kuzomewa umkosoe Magufuli na matendo yake ya kutumbua majibu.
Kwa nini umaarufu wa upinzani umeshuka?
Jibu ni kwamba hawajaonesha jipya katika utendaji wao wa kila siku. Mtindo wa miaka 10 ya kipindi cha Dk Kikwete, unatakiwa ufanyiwe mabadiliko makubwa ili kuendana na kasi.
Upinzani wa kipindi cha JK, hauwezi kushabihiana na wa Magufuli. Ni marais wawili kutoka Chama Cha Mapinduzi lakini mtindo wao wa uongozi ni tofauti kabisa. Ikulu ya JK na ile ya Magufuli, ni tofauti mithili ya jua la asubuhi na mchana.
Hivyo, ni vizuri kuangalia namna mpya ya kufanya siasa za upinzani kulingana na kasi ya Magufuli. Ni dhambi kubwa kwa upinzani kubaki kimya na kuiacha serikali iliyo madarakani ikichanja mbuga yenyewe kwa kujidai.
Upinzani kunywea dhidi ya serikali ni ukosefu wa ubunifu. Kinachotakiwa sasa hivi ni kuwa kadiri inavyopaswa kuwa ni lazima wapinzani wazame ndani na kuibua kasoro za kimsingi ambazo zinatendeka serikalini.
Hali ilipofikia kwa sasa ni kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kauli zake zimekuwa na nguvu kuliko matamshi ya viongozi wakubwa wa upinzani kitaifa? Umuhimu wa wapinzani kujinoa upya unaonekana waziwazi.
Ikumbukwe kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwezi uliopita alifanya mkutano na waandishi wa habari kukosoa mtindo wa Magufuli wa kutumbua majipu.
Maneno yake yalipata nguvu kiasi gani? Mapokeo hayakuwa yale ambayo ilitokea miezi kadhaa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu 2015. Wala hiyo isiitwe hali ya hatari, ni tahadhari au fundisho kuwa hizi ni zama tofauti kabisa.
Bunge la Januari mwaka huu, tulishuhudia jinsi hoja chache za wapinzani zilivyoweza kutia ladha ya mijadala bungeni. Wabunge, Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na Tundu Lissu wa Singida Mashariki (Chadema), waling’ara vilivyo.
Taswira ya bunge la Januari, ilitosha kuonesha kuwa bado wapinzani wanayo nafasi kubwa ya kutamba kwenye siasa za nchi. Kinachotakiwa ni wakati gani na hoja zipi za kusimamia.
Hapa ndipo hoja ya msingi ya wapinzani kuhitaji santuri bora zaidi inapoibuka. Mwanamuziki anapoona mzunguko wa nyimbo umebanwa na nyimbo nzuri au za wasanii maarufu zaidi, anachotakiwa kufanya ni kufyatua tungo bora yenye uzani kuliko nyingine zilizopo kwenye mzunguko.
Kipindi hiki ambacho mzunguko wa habari ni msisimko wa Rais Magufuli mpaka katika mitandao ya kijamii, kinachotakiwa ni wapinzani kuibuka na matukio au hoja zenye afya kuzimisha mvuto wa Dk Magufuli.
Hapo inahitaji kufikiri kwa makini, vilevile ubunifu unahitajika. Siasa za mazoea hazitawasaidia wapinzani kwa wakati huu.
Huu siyo wakati wa JK. Hata nyimbo za msibani na harusini haziwezi kuwa sawa. DJ mzuri wa nyimbo za mapambio kilioni, hata mara moja hawezi kuwa hodari klabu. Nasubiri kuona mwamko wenye nguvu wa upinzani lakini gia lazima ibadilike.

  


Share on Google Plus

About LUQMAN MALOTO

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment