Luqman
Maloto
ULITOKEA
mgawanyiko mkubwa wa kimawazo pale Anne Semamba Makinda, alipobarikiwa na
Kamati Kuu ya CCM, kuwa mmoja wa wanawake watatu waliopigiwa kura na wabunge wa
CCM baada ya Uchaguzi Mkuu 2010.
Yalizungumzwa
maneno mengine zaidi baada ya Makinda kuchaguliwa na wabunge wa CCM kama
mwanamke chaguo la kwanza kati ya wanawake watatu waliopitishwa kuwania Kiti
cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hoja tu kuwa “ni
zamu ya mwanamke”.
Kwamba
ulikuwa muda wa mwanamke kwa sababu tangu uhuru, haikuwa imewahi kutokea kwa
mhimili wowote wa dola, Serikali (Executive), Bunge (Parliament) na Mahakama
(Judiciary) kuongozwa na mwanamke.
Kamati Kuu
ya CCM (CC), ilifanya uamuzi kwamba ni zamu ya mwanamke, hivyo wanaume watatu
waliokuwemo kwenye mchakato waliondolewa.
Walioondolewa
ni Spika wa Bunge la Tisa, Samuel John Sitta, aliyekuwa anatetea kiti chake, wa
pili ni mwanasiasa mtata, aliyetajwa kwenye kashfa nyingi za ufisadi Tanzania,
Andrew John Chenge na Mbunge wa Kongwa, Job Yustino Ndugai ambaye yeye alipozwa
kwa kuteuliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge na sasa ndiye Spika wa Bunge.
Bungeni,
Makinda alishinda kwa kura nying, aligombea na mwanasiasa mkongwe nchini,
Mabere Nyaucho Marando (Chadema). Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kushika majukumu
makubwa zaidi nchini, lakini zaidi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka rekodi kubwa
ya kuongoza mhimili namba mbili kati ya mihimili mitatu ya dola.
Pamoja na
mafanikio yote hayo, Makinda alikumbana na ukosoaji kila kona, kutoka kwa
wanasiasa na vyombo vya habari. Walimponda kuwa hatakuwa na uwezo wa kulimudu
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo lilishuhudiwa likikua kwa kasi
kati ya mwaka 2005 na 2010.
Na kwa
sababu Bunge la 10, ndilo lililoingiza wabunge wengi wa upinzani kuliko
yaliyotangulia kabla yake, iliaminika kuwa hoja zingekuwa nzito na
kupelekeshana kati ya serikali na wabunge wa CCM kwa upande mmoja dhidi ya wale
wa upinzani. Kila Makinda alipoangaliwa, alionekana asingeweza kumudu changamoto
za bunge kubwa, lenye wabunge wengi wa upinzani.
Waliponda
kuwa Uspika wa Bunge la 10 ulikuwa wa Sitta lakini Kamati Kuu ya CCM iliamua
kuliondoa jina lake kwa kile kilichoelezwa alikuwa mwiba wa mafisadi wakati wa
uongozi wake kwenye Bunge la Tisa. Kwamba msimamo huo, ulikuwa unakigharimu
chama kwa kupakwa matope kwamba Serikali ya CCM imejaa ufisadi.
Makinda
aliitwa Spika wa ufisadi, kwa maana watuhumiwa wa ufisadi ndiyo waliofanya
mpango ulioingia mpaka Kamati Kuu ya CCM, kuhakikisha jina la Sitta halirudi
bungeni. Kwamba hata kitendo cha Chenge kujitokeza kugombea Uspika wa Bunge,
haikuwa kwa dhati, ilikuwa ni njama ya kutaka matokeo ya “tukose wote”, kuwa
isionekane Sitta pekee ndiye jina lake limekatwa, kwani hata Chenge naye
alikuwemo katika waliopigwa palanja.
Wapondaji
hawakuishia hapo, waliongeza kuwa kuwa Spika Makinda ni spika wa viti maalum,
kwamba yeye mwenyewe kwa wasifu wake na uwezo wake wa kujieleza, asingeweza
kushawishi kupewa uspika wa bunge, mpaka pale aliposaidiwa na Kamati Kuu ya CCM
katika kukamilisha shabaha ya kumzuia Sitta kupenya.
Hata hivyo,
hayo yalikuwa ni maneno ya wapondaji, ni maneno tu ambayo wana wa Kiswahili
hurahisha njia ya mkato kwa kuyabeza yasipoteze muda kuwa “hata kwenye kanga
yapo”. Ni sawasawa tu na msemo kuwa kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa
maji. Pamoja na yote yaliyosemwa, ukweli ni kwamba Makinda alifanikiwa katika
miaka yake mitano ya kuliongoza bunge.
Kwa kufanyia
kazi maneno, unaweza kumnyima sifa njema Makinda ambazo anastahili kwa uongozi wake
makini ndani ya bunge. Alikuwa ni spika makini, aliyefanya kazi kwa uangalifu
mkubwa, huku akilinda heshima ya chombo hicho cha kutunga sheria. Zipo nyakati
aliingia kwenye changamoto na kutakiwa kuamua mijadala ya bunge kwa weledi
mkubwa na kweli hilo lilifanyika.
Sifa ya
kwanza ianzie jinsi ambavyo bunge lilingia kwenye mtego wa kugongana na
mahakama kuhusiana na sakata la uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta
Escrow. Ilitakiwa spika afanye uamuzi wa kiweledi bila kuchanganywa na maneno
ya kila upande. Wapo waliopiga kelele kuwa suala hilo lipo mahakamani,
lisiingiliwe, kuna waliosema bunge lipo huru na kwamba mahakama ndiyo
iliingilia bunge.
Hati ya zuio
la mahakama, kulitaka bunge lisitishe mjadala wa Tegeta Escrow iliwasilishwa
bungeni. Wingu zito likatanda, huku swali kama ripoti ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya miamala katika Akaunti
ya Tegeta Escrow, ingesomwa bungeni au la, likisumbua vichwa vya wengi. Kwa
hakika ulihitajika umahiri wa Makinda.
Suala la
ripoti ya Tegeta Escrow kusomwa bungeni, lilikuwa ni changamoto nzito kwa
Makinda kuwahi kutokea katika historia ya maisha yake akiwa Spika wa Bunge . Na
pengine lilikuwa zito kulikabili na kulitolea uamuzi katika maisha yake yote ya
kisiasa. Hata hivyo, kwa umakini na umahiri mkubwa, alilifanyia uamuzi mzuri
kabisa.
Kabla ya
kusomwa kwa ripoti, ilibidi amsimamishe Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.
Asha-Rose Mtengeti Migiro, asome kanuni za bunge, asome pia muongozo wa Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
katika maeneo yanayoonesha kuwa mahakama haina ubavu wa kulizuia bunge
kuendelea na mijadala yake ambayo ilishaianza. Aliishinda mahakama kwa hoja za
kisheria na kikanuni.
Huwezi
kusifu mafanikio ya mjadala wa Tegeta Escrow Novemba 2014, pasipo kutoa heko
zote kwa Makinda ambaye ndiye alikuwa na rungu la kuamua mjadala uendelee au
usitishwe. Angekuwa ni mla rushwa au mwoga, Tegeta Escrow ingesitishwa, lakini
aliangalia wapi yalipo maslahi ya Watanzania kwa upana wake, naye akapita
hukohuko.
Makinda ni
muwazi sana, maana ni yeye ndiye alikuwa wa kwanza kutoa tamko kuwa kwa jinsi
alivyoiona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kwamba kama
kusingekuwa na Bunge Maalum la Katiba mwaka jana, kuna mawaziri wangepoteza
kazi mapema.
Hiyo ni
kuonesha kuwa Makinda alikuwa anajua madudu yaliyokuwemo kwenye ripoti ya CAG
na kwamba ufisadi mkubwa ulitendeka. Kitendo cha kusimama kidete bila kuyumba
kuhakikisha ripoti ya CAG kuhusu miamala iliyofanyika Benki Kuu ya Tanzania
katika Akaunti ya Tegeta Escrow, inachambuliwa vizuri na PAC kisha inasomwa
bungeni kama ilivyoahidiwa na kama ilivyo utaratibu wa kibunge siku zote,
kilimpa hadhi kubwa katika usimamizi wake wa shughuli za bunge.
Kwa kuruhusu
uwazi zaidi uonekane, wakati Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alipokuwa anasoma
ripoti ya kamati yake baada ya kuichambua ripoti ya CAG, muda wake ulikuwa
dakika 30 tu, hata hivyo, Makinda aliona kuna vitu havitaeleweka, alimuongezea
muda Zitto asome uchambuzi wa kamati yake mpaka utakapoisha, siyo kwa
kurukaruka vipengele.
Alimwambia:
“Soma mpaka utakapomaliza.” Zitto akajibu: “Asante, asante sana mama.” Kila
kitu kilikuwa na uashirio mkubwa kuwa Makinda ameweza kuongoza bunge kisasa,
akikabili changamoto nzito na kupita kishujaa kabisa. Ni Bunge la 10 chini ya
Makinda, lililoweka rekodi ya kuwa bunge lililowajibisha mawaziri wengi kuliko
lolote lile katika historia ya Tanzania.
Kabla ya
kuangaza matukio mengine ambayo yalitokea bungeni wakati wa uongozi wa Makinda
na kuwajibisha mawaziri, vema kumpa heshima nyingine Makinda kwa namna
alivyohitimisha mjadala wa Tegeta Escrow. Baada ya hoja iliyojengwa na PAC
kupitia ripoti yake iliyosomwa bungeni, kulikuwa na kazi kubwa ya kuyaweka
mapendekezo ya PAC ili kuja kuwa maazimio ya bunge.
Katika
mapendekezo ya PAC, kulikuwa na lugha kali na hata kuingilia mihimili mingine.
Alitaka lazima kuwe na lugha laini ya kuishauri serikali badala ya kuiamrisha.
Kwa uzoefu na uelewa wake, alishaona kazi imetendeka na kila mtu ameona, hivyo
haikuhitaji lugha ya kuamrisha eti ndipo serikali ingefanya uamuzi.
Baada ya
bunge kuvurugika, Makinda hakutaka kufunika kombe mwanaharamu apite. Ikumbukwe
kuwa siku bunge lilipovurugika kutokana na hali ya kubishana kutokana na namna
ya mpangilio wa mapendekezo ili baadaye kuja kuwa maazimio ya bunge
(parliamentary resolutions), ilikuwa siku ya mwisho ya kuahirishwa kwa mkutano
wa 17 wa Bunge la 10.
Hata hivyo,
kwa kuwa aliona umuhimu wa suala la Tegeta Escrow kufika mwisho, Makinda
aliunda kamati ya maridhiano iliyokutanisha wajumbe wa PAC, wabunge wachache wa
CCM, upinzani na serikali, kisha kuunda mapendekezo ambayo yalipita na kufanywa
kuwa maazimio ya bunge ambayo ndiyo yalimfanya Rais Kikwete kuamua kumfuta kazi
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka.
Maazimio
hayo ya bunge ndiyo sababu ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema,
kujizulu kila mmoja kwa wakati wake, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini akisimamishwa kazi kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi.
Kuutambua
ubora wa Makinda ni lazima pia kukumbuka jinsi alivyoisimamia Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira, inayoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli,
iliyochunguza madudu yaliyotokea katika Oparesheni Tokomomeza Ujangili ambapo
mawaziri wanne walilamizimishwa na bunge kujiuzulu.
Waliokuwa
mawaziri, Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa), Mathayo David (Mifugo) na Balozi Hamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii), waliachia ngazi kutokana na kashfa ya Oparesheni
Tokomeza Ujangili kama ilivyosomwa bungeni.
Kuna
mawaziri nane walioachishwa kazi na Rais Kikwete Januari 2013, kutokana na
ripoti za kamati za bunge, hususan zile za mahesabu, iliyokuwa Kamati ya Hesabu
za Mashirika ya Umma (POAC), Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na
PAC. Mfumo wa Makinda wa kuliongoza bunge kwa misingi ya ukweli na uwazi,
imekuwa sababu ya mawaziri wasiowajibika ipasavyo kukiona cha moto.
Waliokuwa
mawaziri, Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), Cyril
Chami (Viwanda na Biashara) na wengine, walijikuta wakifunguliwa milango yaa
kutoka kwenye Baraza la Mawaziri kutokana na kazi ya kibunge chini ya uongozi
wa Spika Makinda. Huwezi kumnyima pongezi hizi.
Mara nyingi,
ilitokea kiti cha spika kinapokuwa kimekaliwa na naibu wake, Ndugai au
wenyeviti, hasa kipindi ambacho Sylvester Mabumba alikuwa mmoja wa wenyeviti wa
bunge, hali ilikuwa inachafuka, lakini anapokaa mwenyewe alikuwa akijua namna
ya kuwatuliza wabunge na kwenda nao sawa katika kujadili hoja za kibunge.
Kwa hakika,
Makinda alieweza kuifanya heshima yake kama Spika wa Bunge ikae kwenye mkondo
wake na kwa hili, waliokuwa wanaamini kuwa atavuja, walibaki kushangaa
alipomaliza miaka mitano ya uspika, akiwa na mafanikio mengi. Zaidi
aliwathibitishia hasi (proved wrong), wale wote waliokuwa wanaamini
angeshindwa.
Mwaka 2013,
bunge lilikumbwa na kashfa nzito kuelekea kusomwa kwa bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini. Uliibuka mjadala mzito kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Tanesco, walikiuka sheria
ya manunuzi kwa kuipa zabuni kampuni iliyoshindwa kwenye mchakato wa zabuni ya
ununuzi wa mafuta ghafi kwa ajili ya mitambo ya umeme.
Upande wa
pili, ikadaiwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
pamoja na wabunge wengine kadhaa, walikuwa wamehongwa na makampuni ya mafuta
ili kumtetea Mkurugenzi wa Tanesco aliyefukuzwa kazi, William Mhando. Kulikuwa
na pande mbili zilizokuwa zinashambuliana kwa maneno mazito, kwa hoja nzito.
Uamuzi wa
kwanza ambao Makinda aliufanya ni kuruhusu bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini isomwe, kisha akaivunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
halafu aliunda kamati ya kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli wa kashfa
hiyo. Kamati iliongozwa na Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi ambaye ni
mbunge wa Mlalo (CCM).
Ripoti
ilipotoka, ilibaini ukweli kwamba Maswi na waziri wake Muhongo, walilidanganya
bunge kwa kuwasingizia wabunge kuhongwa na kula rushwa. Alitoa onyo kali kwa
Maswi na Muhongo kwamba kama wangelidanganya bunge siku nyingine,
angewachukulia hatua hali za kinidhamu.
Hoja
inayojitosheleza hapa ni kuwa Makinda pamoja na uimara wake wa kusimamia vikao,
amekuwa akitoa fursa ya kila tuhuma kuchunguzwa kama inavyofika bungeni na
majibu kuwekwa wazi. Pale alipotoa uamuzi mbaya, alijisahihisha, mfano pale
alipoivunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, baada ya ripoti ya
Ngwilizi aliisafisha kwamba wajumbe wa kamati hiyo walisingiziwa.
Makinda
alikuwa mpingaji wa vitendo vya rushwa bungeni. Wakati anafunga mjadala wa
Tegeta Escrow bungeni, aliwaonya wabunge kuacha tamaa, kwa kile alichokiita
kuwa tamaa zao za kuchukua fedha ndogondogo itawaponza. Aliwasisitizia kuwa
kama hawataacha, kuna watakaoumbuka. Aliyasema hayo kipindi ambacho kulikuwa na
tuhuma kuwa wabunge huyumbisha mijadala inayoendelea bungeni kwa sababu ya
kuhongwa fedha.
Mwaka 2013,
wakati sakata la rushwa lilipoibuka wakati wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na
Madini, Makinda alisema: “Unakuta mtu anaongea kwa jazba kweli bungeni mpaka
mishipa inamtoka, unafikiri anaizungumzia nchi, kumbe mishipa inamtoka kwa
sababu anafanyia kazi fedha alizopewa.”
Chukua
viwango ambavyo alivionesha akiwa Spika wa Bunge, uzingatie kwamba alikuwa
Naibu Spika wa Bunge kabla hajafikia hatua hiyo. Ongeza uzoefu wake wote katika
siasa na utumishi wa serikali, utaona kwamba ni ‘mama mkubwa’ katika Taifa la
Tanzania.
Ni bahati mbaya
kuwa huwa hapewi sifa kwa namna alivyoliendesha Bunge la 10 ambalo lilikuwa na
matokeo mengi yenye kusisimua.
Bunge la 10
angalau lilijenga dhana ya woga kwa watendaji serikalini, kwamba wakifanya
ubadhirifu wanawajibishwa. Kongole sana Makinda!
Bunge la 10
lilipanua demokrasia ya kibunge. Liliongeza afya ya upinzani. Maana sauti za
wabunge wa vyama mbalimbali zilisikika hata kwa uchache wao. Makinda ni
mwana-demokrasia.
Pamoja na
dosari chache au maeneo machache yenye kuweza kukosolewa, bado Bunge la 10
liliweza kuonesha nguvu zake, kwa sehemu kubwa lilijipambanua kama mhimili huru
pasipo kujipendekeza kwa serikali.
Zipo nyakati
CCM kupitia wingi wao, waliweza kuzuia mijadala mikali ya wapinzani, hususan
ile iliyokuwa na sura ya kuiumbua serikali lakini kwa jumla, Makinda alisimama
kama kiongozi mkuu wa bunge na siyo mwakilishi wa chama.
MAKINDA
ALIPOTOKA
Mwaka 1975,
Makinda akiwa kijana mwenye umri wa miaka 26 tu, alimvutia Rais wa Awamu ya
Kwanza ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, akamteua kuwa Mbunge wa Kuteuliwa, nafasi hiyo aliendelea nayo kwa
miaka 10 mpaka pale Mwalimu Nyerere alipong’atuka mwaka 1985. Mbali na ubunge,
Makinda aliteuliwa na Mwalimu Nyerere kushika nyadhifa mbalimbali serikalini
ikiwemo uwaziri.
Ubora wa
Makinda, ulimvutia pia Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliyemteua
tena kuwa mbunge mpaka mwaka 1995 alipogombea Ubunge Jimbo la Njombe Kusini na
kushinda, kisha kuendelea kulishikilia jimbo hilo kila uchaguzi na bila
kupingwa mpaka mwaka 2015 alipotangaza kutogombea.
Ameshakamata
nyadhifa za uwaziri, ukuu wa mkoa pamoja na idara mbalimbali ndani ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kusahau ujumbe na ukurugenzi wa bodi
mbalimbali za mashirika ya umma.
Baada ya
Uchaguzi Mkuu 2015, Makinda aliamua kukaa pembeni, hakugombea tena uspika. Hii
inampambanua kama mtu asiye na uroho wa madaraka. Kijiti kimepokelewa na
Ndugai, ni zamu yake sasa. Ila naamini kuwa zitakuja nyakati ndani ya bunge
watu watamkumbuka Makinda ambaye alikuwa spika bora sana lakini hapewi thamani
yake.
0 comments :
Post a Comment